Na Muhidin Amri,Songea

JUMLA ya wanafunzi 62 wamehitimu masomo ya kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Wasichana FEO iliyopo Halmashauri ya Madaba wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.

Hii ni mara ya kwanza kwa shule hiyo kutoa wanafunzi wa kidato cha nne tangu ilipoanzishwa mwaka 2016 shule inayotajwa kuwa na mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia kuliko shule zote katika mkoa wa Ruvuma.

Wanafunzi wa shule hiyo katika risala yao iliyosomwa na Jackline Mgina walisema, walianza safari ya masomo ya sekondari mwaka 2016 wakiwa 78, hata hivyo wanafunzi wengine walishindwa kuendelea kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ugonjwa na wengine kuhama shule.

Aidha walisema, wahitimu wote 62 wamechukua mchepuo wa sayansi kwa kuzingatia sera ya nchi ya viwanda, na kumpongeza Rais Dkt John Magufuri kwa kazi kubwa anayofanya kuanzisha viwanda ambavyo vitakuwa mkombozi mkubwa wa kiuchumi hapa Nchini.

Walisema, tangu kuanzishwa kwake shule imeweza kufanikisha kuwa na matokeo mazuri kitaaluma kwa kidato cha pili kwa miaka miwili mfululizo 2017 ilishika nafasi ya kwanza kiwilaya na mkoa na mwaka 2018 ilishika nafasi ya kwanza kiwilaya na mkoa ilishika nafasi ya tatu.

Walisema, matokeo hayo mazuri kitaaluma yametokana na walimu kutoa mitihani ya kutosha kila wiki,mwezi,robo muhula na ya mwaka ya ndani na nje na kuwa na mazoezi ya kutosha madarasani.

Hata hivyo, wameuomba uongozi wa shule hiyo chini ya mmiliki na meneja wake Omari Msigwa kuanzisha kidato cha tano na sita ili wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne waweze kupata maarifa zaidi katika mchepuo wa sayansi na ndoto zao ziweze kutimia hata kwa wahitimu wengine wa kidato cha nne kwa manufaa ya Tanzania ya viwanda.

Mgeni rasmi katika mahafali hao Mtendaji Mkuu wa Benki ya TPB Sabasaba Moshingi amepongeza uwekezaji mkubwa uliofanyika katika shule hiyo hasa kwa kuwa na majengo ya kutosha na yenye ubora wa hali ya juu ambayo yanatoa fursa kwa wanafunzi kujisomea na walimu kufundisha vizuri.

Alisema,kuwepo kwa maabara za kisasa na zenye vifaa vya kutosha katika masomo ya sayansi vinawezesha wanafunzi kufanya mazoezi kwa vitendo ambapo Benki ya TPB imetoa msaada wa kompyuta 10 kwa shule hiyo ambazo zitawasaidia wanafunzi kuongeza maarifa na walimu kuandaa masomo.

Moshingi alisema, wazazi hawakufanya makosa kupeleka watoto wao katika shule hiyo ambayo ina mazingira rafiki inayowezesha wanafunzi kupenda na kufurahia masoma ikilinganisha na shule nyingine hapa nchini.

Moshingi,amewapongeza wanafunzi hao kwa matokeo mazuri waliyopata katika mitihani mbalimbali ya majaribio kwani yanatia matumaini ya kufanya vizuri zaidi kwenye mitihani ya kitaifa ya kidato cha nne.

Amewataka wahitimu hao, kuwa mfano mzuri kwa wazazi na jamii inayowazunguka, na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kukatisha ndoto zao wakati huu wanaposubiri matokeo ya mitihani yao.

Moshingi ambaye ni mlezi wa shule hiyo,amewaasa wazazi kwenda kuwalea vijana hao kwa maadili mema na nidhamu ya hali ya juu ili wale watakao chaguliwa kuingia kidato cha tano wakawe mabalozi wazuri wa shule ya FEO Girls kwa kufanya vizuri katika masomo yao.

Moshingi,amewataka wanafunzi na wazazi kuona umuhimu wa kutumia huduma ya benki ya TPB Tanzania ambayo imekuwa kimbilio la wananchi wengi kutokana na ubora wa huduma zake kama ,mikopo ambayo imewasaidia watu wengi kuanzisha na kukuza shughuli zao za kiuchumi na wanafunzi kuweka akiba kwa ajili ya kutimiza malengo yao katika masomo.

Kwa upande wake meneja wa shule hiyo Omari Msigwa, amewashukuru wazazi kwa kuiamini shule hiyo na kupeleka watoto wao bila kujali muda tangu ilipoanzishwa ambapo amehaidi kuendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ili wanafunzi na walimu wa shule hiyo kila upande uweze kutekeleza majukumu yake vizuri.

Msigwa alisema, malengo yaliyopo ni shule kufanya vizuri katika matokeo ya mitihani mbalimbali kuanzia ngazi ya wilaya,mkoa na Taifa ili iwe miongoni mwa shule kumi bora hapa nchini.

Alisema, ni matumaini yake kuwa wazazi kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania wataendelea kupeleka watoto katika shule hiyo kwa ajili ya kupata elimu bora na sio bora elimu hasa kwa kuzingatia uwekezaji mkubwa uliofanyika kama walimu wa kutosha na wenye uwezo,vifaa na miundombinu ya shule.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...