NA RIPOTA WETU, KISARAWE

KATIKA hali isiyo ya kawaida, idadi kubwa ya wanawake wilayani Kisarawe mkoa wa Pwani wamejitokeza kujisajili Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kupata Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) hatimaye watambulike kama walipakodi na waweze kufanya biashara zao kwa uhuru na halali.

Hali hiyo ilijitokeza wakati wa maadhimisho ya wiki ya huduma, elimu ya kodi na usajili wa walipakodi inayoendelea katika mkoa wa Pwani ambapo katika wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji idadi kubwa ya wanaume ndiyo iliyokuwa inajitokeza kupata TIN lakini hali imekuwa tofauti katika Wilaya ya Kisarawe ambapo idadi kubwa ya wanawake ndiyo iliyojitokeza.

Meneja wa Huduma kwa Mlipakodi kutoka TRA, Honesta Ndunguru amesema ni kweli kwamba idadi kubwa ya wanawake wamejitokeza kupata Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi katika Wilaya ya Kisarawe ukilinganisa na wilaya zingine za mkoa wa Pwani walikopita.

Ndunguru amesema, TRA imevutiwa na mwamko wa wananchi wa wilaya zote katika mkoa wa Pwani na kuwapongeza wale wote waliojitokeza kupata huduma, elimu pamoja na kujisajili kuwa walipakodi.

“Kwa mwitikio huu, inadhihirisha kwamba elimu ya kodi tunayoitoa inawafikia walengwa na wanafuata sheria ya kodi inayomtaka kila mfanyabiashara kujisajili na kupata Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi inayotolewa bure na TRA”, amesema Ndunguru.

Kwa mujibu wa Ndunguru kati ya wananchi 10 waliojitokeza kupata TIN 8 kati yao walikuwa wanawake, tofauti na wilaya nyingine ambapo idadi kubwa walikuwa wanaume.

Baadhi ya wanawake waliojitokeza katika viwanja vya stendi ya zamani ili kusajiliwa na kupata TIN hawakusita kueleza hisia zao ya kwamba wanawake wa wilaya ya Kisarawe wamepata mwamko wa kufuata sheria za nchi zikiwemo za kulipa kodi ili waweze kutumia fursa mbalimbali ambazo zionatokana na kutambulika na serikali kama vile kupata mikopo ya wajasiliamali na huduma zingine muhimu.

“Binafsi nimehamasika na kuja kupata Tin kwa sababu nimeelimishwa na maofisa wa TRA na nimeelewa umuhimu wa kujisajili kama mlipakodi na kulipa kodi kwa nchi yangu”, amesema Fatma Omari

Naye Sophia Ndume mkazi wa Kisarawe ameongeza kuwa wanawake wa Kisarawe ni wahangaikaji katika biashara ndiyo maana wamehamasika kwa wingi kuja kuchukua TIN ili wakafanya biashara zao kwa uhuru bila kubughudhiwa.Zainess Madeng’ha ambaye ni mmiliki wa saluni ya kike, amesema amehamasika kuchukua TIN baada ya kupata elimu kutoka kwa maofisa wa TRA na kwamba huduma hiyo imesogezwa karibu na inapatikana bure.

“Kwa kweli nimeona nitumie fursa hii kwa kuwa huduma imenifuata dukani kwangu na vile vile Napata huduma hii bure bila kulipia chochote”, alisema.
TRA inafanya wiki ya elimu kwa mlipakodi katika mikoa ya Pwani na Morogoro kwa lengo la kusogeza huduma za ulipaji kodi karibu na wananchi lakini pia kusajili walipakodi ili kuongeza idada ya walipakodi nchini.
Zainess Madeng'ha (kulia), mkazi wa Kisarawe mkoani Pwani akifurahia kupokea Cheti cha Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) kutoka kwa maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika wiki ya mlipakodi inayoendelea mkoa wa Pwani.
Afisa wa TRA akiwahudumia akina mama hawa kupata Vyeti vya Utambulisho wa Mlipa kodi yaani TIN, huko Kisarawe mkoani Pwani.
Wanawake wa wilaya ya Kisarawe wakichangamkia fursa ya kupata Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...