Wanafunzi pamoja na baadhi ya wananchi wakicheza ngoma ya asili ya Maasai wakati wa sherehe za Mahafali ya kumaliza kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Hocet, iliyopo Kata ya Shungubweni,wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani hivi karibuni. Kulia ni Mkurugenzi wa na Mwasisi wa Hocet, Hezekiah Mwalugaja.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Good For All (Washona Mahema), Askofu Edger Mwamfupe ambaye alikuwa mgeni rasmi, akijumuika pamoja na wanafunzi Angel Kiphutu na Tibet Eliya kukata keki wakati wa mahafali hayo.
Mkurugenzi wa Shule ya Sekondary Hocet, Hezekiah Mwalugaja akilishwa keki na mwanafunzi aliyemaliza kidato cha nne, Angel Kiphutu. 
Mkurugenzi wa Taasisi ya Good For All (Washona Mahema), Askofu Edger Mwamfupe, akilishwa keki na mwanafunzi Tibeti Eliya.

Na Richard Mwaikenda, Mkuranga.

MKURUGENZI wa Taasisi ya Hope For All (Washona Mahema), Edger Mwamfupe ameupongeza uongozi wa Shule ya Sekondari ya Hocet, kwa kuwanusuru Watoto Yatima kutoka kwenye hali ya mateso, kuwabadilisha tabia ya awali hadi kuwa na furaha ya maisha.

Kwa hatua nzuri waliyofikia, Mwamfupe aliutaka uongozi kuachana na mazoea ya wanafunzi hao kuwaita yatima au shule hiyo kuiita ya Yatima, bali iitwe ya shule maalumu kwa vile mambo mengi waliyofundishwa hapo yakiwemo ya ujasiriamali yameyatoa kwenye uyatima.

Mwamfupe ambaye alikuwa mgeni rasmi, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki alipokuwa akihutubia katika sherehe za mahafali ya Kidato cha Nne ya shule hiyo iliyopo wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani.

“Nawasihi kuanzia sasa muache kutumia jina Yatima, msiwarudishe watoto kwenye unyonge, kwani mmefanya kazi kubwa ya kuwafundisha mambo mbalimbali ya kujitegemea, hawa sasa si sawa na watu wanaotegemea kila kitu kutoka kwa watu wengine. Hawa ni tofauti wana uwezo wa kujitegemea, Hivyo nashauri shule hii iitwe ya wanafunzi maalumu si Yatima tena,” alisema Mwamfupe, huku akipigiwa makofi.

Alitoa ushauri kwa uongozi kushirikiana na Taasisi yake kuweka mpango maalumu wa kuwawezesha wahitimu kubaki shuleni hapo kwa kuendesha miradi ya ujasiriamali kwa kutumia elimu waliyopata badala ya kuwaachia kurudi mitaani walikotoka ambako ni rahisi kurudia tena katika hali waliyokuwa nayo awali ya maisha hatarishi..

Mkurugenzi wa shule hiyo, iliyoanzishwa mwaka 2007, Mchungaji Hezekiah Mwalugaja, alisema kuwa wanafunzi wanaojiunga na shule ni yatima pamoja na wanaoishi kwenye mazingira magumu ambapo huwabadilisha tabia na mwenendo na hatimaye kuwa na tabia nzuri.

Alisema hufundishwa masomo ya kawaida, stadi za kazi, ujasiriamali, kilimo cha mbogamboga, matunda na mazao mbalimbali ambayo baadhi hutumika shuleni hapo kwa mahitaji ya chakula.

Naye, Diwani wa Kata ya Shungubweni, Kamwiri Omari aliyekuwa mmoja wa wageni waalikwa katika mahafali hayo yaliyohudhuriwa pia na baadhi ya wananchi wa kata, alifurahia uwepo wa shule hiyo katika kata hiyo, ambapo aliahidi kutoa ushirikiano kutatua kero zinazoikabili. 

Alisema kuwa tayari amewasiliana na Wizara ya Nishati ili umeme wa Rea ufike shuleni hapo na kwamba nguzo zinaletwa na umeme unaweza kuwashwa kabla ya Januari mwakani. Hivi sasa shule inatumia umeme wa jua.

Pia, ameahidi kumpeleka shuleni hapo,Ofisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya hiyo, akawapatie wahitimu 43 elimu ya mikopo kuunda vikundi ili wawezeshwe kupata mikopo kwa ajili ya kuanzisha miradi mbalimbali.

Wahitimu Leila Mketo, Rahel Sarakikya na Fatuma Kalanje kila mmoja alikabidhiwa zawadi ya cherehani na kupata wasaa wa kuonesha kwa waalikwa nguo walizozishona.

Mahafali hayo yalihanikizwa kwa kwaya, ngoma za asili, shoo ya mitindo ya nguo na walioshinda michezo mbalimbali walizawadiwa ikiwemo mbuzi iliyotwaliwa na timu ya Shungubweni FC iliyoishinda timu ya Mamba FC. Zote kutoka kata hiyo ya Shungubweni.

Pia palifanyika michezo ya kuvuta kamba, kukimbia na yai likiwa kwenye kijiko mdomoni, kula apple zilizoning’inizwa kwenye kamba, Mr & Miss Hocet na mingineyo.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Good For All (Washona Mahema), Askofu Edger Mwamfupe akihutubia katika mahafali hayo.
Sehemu ya wageni waalikwa wakiwa katika hafla hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...