Meneja Mradi wa Shirikisho la Vyama vya magonjwa yasiyo ya kuambukizwa (TANCDA) Happy Nchimbi akizungumza leo jijini Dar es Salaam kwenye mkutano Mkuu wa Asasi ya kuelimisha jamii kuhusu magonjwa yasiyo ya kuambukiza
Waandishi wa habari wa Asasi ya kuelimisha jamii kuhusu magonjwa yasiyoambukiza wakifuatilia kwa makini
Mwenyekiti wa Asasi hiyo Leon Bahati akifafanua jambo wakati wa mkutano huo ambapo amettumia nafasi hiyo kuhamasisha waandishi wa habari kuandika habari zinazoelimisha kuhusu magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Mwanzilishi wa Taasisi ya kutoa elimu ya kisukari kwa jamii(DICOCO)Lucy Johnbosco akizungumza wakati wa mkutano huo ambapo amesisitiza umuhimuwa jamii kutambua umuhimu wa kupima afya zao kila wakati.Lucy amekuwa akiishi na ugonjwa wa kisukari kwa mwaka 19 sasa.
Makamu Mwenyekiti wa Asasi hiyo Exuper Kachenje (aliyesimama) akizungumza kwenye mkutano huo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya washiriki wa mkutano mkuu wa asasi ya kuelimisha jamii kuhusu magonjwa yasiyo ya kuambukiza wakifanya mazoezi ya kunyoosha viungo kabla ya kumalizika kwa mkutano huo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Na Said Mwishehe,Michuzi Globu ya
jamii
ASASI ya Kuelimisha jamii kuhusu
magonjwa yasiyoambukiza inayohusisha waandishi wa habari nchini(TOANCD),
imefanya mkutano Mkuu wa mwaka na kuazimia mambo mbalimbali yakiwemo ya
kuendelea kuandika habari zinazoelimisha kuhusu magonjwa hayo ambayo yamekuwa tishio
na kusababisha vifo vya Watanzania walio wengi.
Pamoja na mambo mengine asasi hiyo
imewahamasisha waandishi wengine nchini kujiunga nao kwa lengo la kuufikisha
elimu na habari zinazohusu magonjwa hayo kwa wananchi walio wengi ili
kuyatokomeza ambayo mengi yanatokana na staili ya maisha ambayo imekuwa chanzo
kikubwa cha magonywa yasiyo ya kuambukiza.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam
wakati wa mkutano huo mkuu wa mwaka, Mwenyekiti wa Asasi hiyo Leon Bahati
amesema ni jukumu la waandishi wenye utashi wa kuandika kuhusu habari
zinazohusu magonjwa hayo kutumia fursa waliyonayo kutoa elimu kwa jamii kwa
kuandika habari kwa wingi na hatimaye kuokoa jamii ya watanzania.
Amefafanua magonjwa yasiyoambukiza ni
magonjwa yasiyo na vimelea vinavyoweza kusambazwa na kutoa mfano wa magonjwa ya
moyo na mishipa ya damu, saratani, magonjwa sugu ya njia ya hewa, kisukari,
magonjwa ya akili na mengine ya kurithi kama vile selimundu.
"Magonjwa haya yanaongezeka kwa
kasi na kuathiri hata watu wenye umri mdogo wakiwemo watoto.Kutokana na uwepo
wa magonjwa haya kumeibuka utapeli mwingi, hivyo ni jukumu letu waandishi
kupitia asasi hii kuhakikisha tunahabarisha umma jinsi ya kujiepusha na
magonjwa haya na kwa wale ambayo tayari wanayo ni jinsi gani wanaweza kuwa na
mfumo ambao utawawezesha kuishi,"amesema Bahati.
Ameongeza waandishi ni kundi ambalo linaweza
kuwafikia watu wengi kwa urahisi zaidi kwa umoja wao wanaweza kuandaa vipindi
vya redio na vya tevisheni pamoja na kuandika makala mbalimbali ambazo
zitasaidia watu kubadilika.
Bahati amesema kwa mwaka 2016 watu
milioni 42 sawa ya asilimia 71 ya vifo vyote walifariki dunia kutokana na magonjwa
yasiyoambukizwa huku asilimia 75 ya vifo vyote vinavyohusu watu kwenye umri wa
miaka 30 hadi 70 husababisha magonjwa hayo.
Kwa upande wake Meneja Mradi wa
Shirikisho la Vyama vya magonjwa yasiyo ya kuambukizwa (TANCDA) Happy Nchimbi
amewakumbusha waandishi wa habari nchini na hasa walioko kwenye chama hicho kuendelea
kutoa elimu na vipindi mbalimbali kwa jamii kuhusu magonjwa yasiyoambukizwa
kwani yamekuwa tishio kutokana na mtindo wa maisha.
Amesema tayari kuna juhudi zinazoendelea
kufanyika na matokeo yanaonekana kwa jamii kwani watu wengi hivi sasa wamekuwa
wakipima afya zao, kufanya mazoezi pamoja na kubadilisha mitindo ya maisha
kutokana na mradi walionao wa uelimishaji kwa jamii.
Nchimbi amesema shirikisho hilo
tayari kwa mwaka jana limefanikiwa kuwafikia watu zaidi ya 1000 wakiwemo
wanafunzi wa kike 40 ambao wanao uwezo wa kusimama na kutoa elimu kwa wanafunzi
wenzao huku katika jamii takribani wakinamama 16 nao wamepewa elimu ya
masuala ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukizwa.
Amesema mradi huo umewafikia pia
wanafunzi wa Dar es Salaam na Arusha na wanaendelea na utoaji wa elimu kuhusu
magonjwa hayo , hivyo amesisitiza waandishi wa habari kutumia kalamu zao kutoa
elimu kwa jamii ya Watanzania.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...