Charles James, Michuzi TV

MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi leo amefanya ziara ya kukagua agizo alilolitoa kwa Makampuni ya Simu, NIDA na Idara ya Uhamiaji ya kuwataka kuhamishia ofisi zao kwa muda eneo la Nyerere Square kwa ajili ya kurahisisha zoezi la usajili wa line za simu.

DC Katambi amefika katika eneo hilo na kujionea namna ambavyo zoezi hilo linaendeshwa kwa kasi huku akizitaka taasisi zote zinazohusika na mchakato huo kuongeza idadi ya watumishi wao ili kuendana na wingi wa wananchi wanaojitokeza.

Pia amesema zoezi hilo litadumu hadi siku ya mwisho ya usajili Januari 20 iliyotangazwa na Mhe Rais Magufuli hivyo kuwataka wananchi wa Dodoma kujitokeza kwa wingi kusajili line zao kwa njia ya vidole.

Akizungumza baada ya ukaguzi huo DC Katambi amekiri kuridhishwa na namna zoezi hilo linavyoendeshwa kwa hali ya utulivu jambo ambalo anaamini kama wananchi wataendelea na muamko huo basi hakuna mkazi wa Dodoma ambaye line zake zitafungiwa.

" Kwa uzalendo mkubwa Mhe Rais alitoa siku 20 kwa ajili ya wale ambao walikua hawajakamilisha kuweza kukamilisha hivyo na sisi kama Wilaya tukaona tutenge eneo hili kwa watu wetu hawa.

Unajua kabla ya hapa niligundua wengi wanapata changamoto ya kutoka NIDA waende Uhamiaji kisha ndo waende kwa mawakala wa simu wakasajili sasa mlolongo ule sasa hivi hakuna wote wanaohusika na usajili wako sehemu moja hapa hivyo wananchi waje wasajili line zao," Amesema Katambi.

Nae mmoja wa wananchi waliojitokeza kusajili line zao eneo hilo la Nyerere wamempongeza DC Katambi kwa ubunifu ambao ameuonesha kwani umesaidia kuepusha usumbufu kwao kwa kumaliza mchakato wote ndani ya eneo moja.

" Kwa kweli DC amefanya jambo kubwa na la busara sana, wengi tulikua tunapata changamoto ya kwenda NIDA, Uhamiaji halafu ndio tukasajili, hawa wote kuwepo hapa ni faida kwetu kwani tunamaliza zoezi hili kwa haraka bila usumbufu, " Amesema Joseph Mazengo mmoja wa wananchi waliojitokeza kusajili line zao.
 Wataalamu kutoka Makampuni ya Simu, Uhamiaji na NIDA wakiendelea na zoezi la usajili wa wa wananchi wa line za simu kwa njia ya kidole jijini Dodoma.
 Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mh Patrobas Katambi akipokea maelezo kwa Afisa Usajili kutoka NIDA baada ya kufika eneo la Nyerere square kujionea zoezi la usajili wa line za simu kwa njia ya kidole baada ya kuagiza wanaohusika kuweka kambi sehemu moja kurahisisha zoezi hilo.
Wananchi kutoka sehemu mbalimbali za Jiji la Dodoma wakiwa wamejitokeza katika eneo la Nyerere square kusajili line zao za simu kwa njia ya kidole baada ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi kuagiza zoezi hilo kufanyika sehemu moja ili kurahisisha huduma hiyo kwa wananchi.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...