Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii
MAHAKAMA  ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kutoa uamuzi wa maombi yaliyowasilishwa na Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita anayeiomba mahakama hiyo itoe amri ya kusitisha mchakato wa kung'olewa madarakani kwenye nafasi yake hiyo hadi hapo maombi ya msingi yatakaposikilizwa.

Kabla ya kesi hiyo kuingia mahakamani, leo Januari 9,2020 kwa ajili ya kutolewa uamuzi,  askari walionekana kuimarisha ulinzi mahakamani hapo.

Hata hivyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Janeth Mtega anayesikiliza kesi hiyo, amesema bado hajamaliza kuandaa uamuzi dhidi ya kesi hiyo hivyo ameahirisha shauri hilo hadi kesho saa tano asubuhi.

Wakati kesi hiyo inaitwa mahakamani, upande wa wajibu maombi uliwakilishwa mahakamani hapo na jopo la mawakili wa serikali wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Joseph Tango huku upande wa mleta maombi ukiwakilishwa na Wakili Hekima Mwasipo na wenzake Wawili.
 Januari 8,2019 Mwita kupitia wakili wake Mwasipo aliwasilisha maombi hayo chini ya hati ya dharula dhidi ya Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda, Halmashauri ya Jiji hilo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katika maombi hayo, yanalenga kuwazuia Mkuu wa Mkoa na Halmashauri kujihusisha katika mchakato wa kumng'oa kwenye nafasi ya Umeya wa jiji hilo.

"Tunaomba mahakama izuie mchakato huo au hata kama kutakuwa na kikao chenye ajenda hiyo  isizungumziwe  na Mkuu wa Mkoa  pamoja na Halmashauri  wazuiliwe kufanya mchakato huo. Mahakama isipofanya hivyo mleta maombi (Mwita) hatapata haki yake ya kusikilizwa,"alidai Mwasipo.
Akijibu hoja hiyo, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Gabriel  Malata alidai kesi hiyo imekuja kusikilizwa chini ya hati ya dharura na kwamba ili haki ionekane imetendeka.

Alidai hawajui  kama kuna  kitu chochote kinachoweza kutokea kuhusu  kung'olewa kwa mleta maombi huyo hivyo, aliiomba mahakama kukataa maombi hayo  kwa gharama.

Alidai hakuna mazingira ya moja kwa moja yanayoashiria kwamba kwenye kikao kitakachofanyika kutakuwa na ajenda inayohusu kumtoa katika nafasi hiyo meya huyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...