Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, ametoa wito kwa wamiliki wa sehemu za kazi wa mkoa wa Mwanza kuipokea na kuitekeleza ipasavyo kampeni ya kutokomeza ajali na magonjwa katika sehemu za kazi ya Vision Zero.

Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa katika hafla ya kuzindua kampeni hiyo kwa mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Dkt. Phillis Nyimbi, amesema endapo wamiliki wa sehemu za kazi watapata mafunzo ya uhakika kuhusu utekelezaji kampeni hiyo, ni dhahiri kuwa uzalishaji utaongezeka na kuleta tija kwa serikali na wananchi wote kwa ujumla.

“Kwakweli kupitia kampeni na mafunzo haya, OSHA mmenirahisishia sana kazi kwani hata nisipopita mara kwa mara katika maeneo ya kazi kukagua naamini mafunzo haya yataenda kusafisha vitu vichache vilivyobakia, yataenda kujazia pale palikuwa pamepwaya na naamini kuwa mafunzo haya yataenda kuleta tija pia kwa watumishi na wafanyakazi katika maeneo mbali mbali ya kazi,” alisema Mkuu wa Wilaya.

Katika mohojiano baada ya kutoa semina kuhusu utekelezaji wa kampeni hiyo kwa waajiri hao ambao ni wanachama wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) wa mkoa wa Mwanza, Mkurugenzi wa Mafunzo, Tafiti na Takwimu wa OSHA, Bw. Joshua Matiko, amesema kupitia kampeni hiyo wataendelea kuwaelimisha waajiri ili waweze kuona umuhimu wa kuwekeza katika afya na usalama wa wafanyakazi wao.

“Kupitia kampeni hii tuliyoianzisha tunataka kuwadhihirishia waajiri kwamba wakiwekeza katika masuala ya usalama na afya kwa wafanyakazi hawatapata hasara bali itawaletea tija zaidi,” alifafanua Bw. Matiko.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TCCIA mkoa wa Mwanza, Dkt. Elibariki Mmari, amesema wanachama wa TCCIA wameipokea vizuri kampeni ya Vision Zero na wanashiriki katika mafunzo ili kuweza kutambua wajibu wao katika utekelezaji wa kampeni hiyo.

“Tumefurahi baada ya kuona OSHA na WCF wamekuja leo mkoani kwetu kutoa semina kuhusu kampeni ya Vision Zero ambapo mkakati huo ni wa kutaka kuhakikisha kwamba hali ya usalama na afya katika maeneo yetu ya kazi yawe ni kwenye viwanda, mahospitali na maeneo mengine ya kazi, vihatarishi vyake vinapungua hadi kufikia sifuri,” alisema Dkt. Mmari.

Naye Jane Masanja ambaye alishiriki katika semina hiyo kutoka Kampuni ya ONA FAMILY EYE CARE amesema amefurahishwa na kampeni hiyo na kuahidi kupeleka mrejesho katika taasisi yake ili kuanza kuitekeleza kampeni hiyo kwa vitendo.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa OSHA, Kanda ya Ziwa, Mjawa Mohamed, amesema wataendelea kutoa elimu na kufanya uhamasishaji zaidi katika mikoa yote ya Kanda ya Ziwa ili kufikia lengo la kampeni hiyo ambalo ni kutokomeza ajali na magonjwa katika maeneo yote ya kazi.

Dhana ya “Vision Zero” ilibuniwa na Shirikisho la Mashirika ya Hifadhi za Jamii Duniani (ISSA) na inatekelezwa na nchi mbali mbali duniani kwa namna fofauti kutegemeana na mazingira ya nchi husika.
 Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Dkt. Phillis Nyimba, akizungumza na washiriki wa semina ya kampeni ya kutokomeza ajali na magonjwa mahali pa kazi ya vision zero (hawako pichani), alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella katika hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo kwa mkoa wa Mwanza. Waliokaa (kutoka kulia) ni Mwenyekiti wa TCCIA Mwanza, Mkurugenzi wa Mafunzo, Utafiti na Takwimu wa OSHA, Joshua Matiko, na Kaimu Meneja wa OSHA Kanda ya Ziwa, Mjawa Mohamed.
Mkurugenzi wa Mafunzo, Utafiti na Takwimu wa OSHA, Joshua Matiko, akiwasilisha mada katika semina kuhusu kampeni ya kutokomeza ajali na magonjwa mahali pa kazi ya vision zero mkoani Mwanza.
Washiriki wa semina kuhusu kampeni ya kutokomeza ajali na magonjwa mahali pa kazi ya vision zero, wakifuatilia mada wakati wa uzinduzi kampeni hiyo katika mkoa wa Mwanza.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...