Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na watumishi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, akiwa katika siku ya pili ya ziara yake Zanzibar. Januari 18, 2020
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Makamu Mkuu wa Chuo cha State University of Zanzibar, Dkt. Zakia Mohammed Abubakar, wakati alipotembelea Chuo cha Kilimo Kizimbani, kilichopo katika Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar. Januari 18, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akipanda mti kwenye Chuo cha Kilimo Kizimbani, kilichopo katika Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar. Januari 18, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akikagua mradi wa maji, katika Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar. Januari 18, 2020
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa tanki la maji Mwera, katika Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar. Januari 18, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akikagua mradi wa ujenzi wa Terminal III, katika uwanja wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Zanzibar. Januari 18, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

…………………

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Viwanda Bw. Juma Hassan Reli ahakikishe anazuia utoaji wa vibali vya kuingiza sukari kutoka nje hadi sukari inayozalishwa na kiwanda cha sukari cha Zanzibar kilichopo Mahonda iishe.

Amesema haiwezekani kiwanda hicho cha pekee kinachozalisha tani 6,000 za sukari kwa mwaka kikakosa wateja wakati mahitaji ya sukari Zanzibar ni tani 36,000 kwa mwaka.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumamosi, Januari 18, 2020) wakati apotembelea kiwanda cha kuzalisha sukari cha Zanzibar kilichopo katika eneo la Mahonda wilaya ya Kaskazini ‘A’ mkoa wa Kaskazini Unguja.

Amesema ni vizuri wizara ikahahakikisha sukari inayozalishwa na kiwanda hicho inapewa kipaumbele cha kwanza kwa kununuliwa kwa sababu wanauhakika na ubora wake kwa kuwa wameshuhudia uzalishaji wake kuanzia hatua ya awali miwa ikiwa shambani.

“Wizara ya Viwanda lazima mbadilike na muweke utaratibu mzuri wa kusimamia uingizwaji wa sukari kutoka nje. Haiwezekani sukari inayozalishwa ndani ikakosa soko kutokana na uingizwaji wa sukari kutoka nje. Hatuwezi kumfurahisha mtu mmoja huku wengi wakiumia.”

Waziri Mkuu amesema Serikali imeamua kukuza uchumi kwa kupitia sekta ya viwanda hivyo ni lazima viwanda vya ndani vikalindwa. “Viwanda vinasaidia katika kuondoa tatizo la ajira, vinawapa wakulima soko la uhakika la mazao yao pamoja na Serikali kupata kodi ya uhakika.”

Amesema kitendo cha wizara hiyo kushindwa kuratibu vizuri suala la uingizwaji wa sukari kutoka nje ya nchi kutakwamisha uwekezaji jambo ambalo ni sawa na kuihujumu Serikali kwa kuwa itasababisha wananchi kupoteza ajira pamoja na Serikali kukosa mapato.

Waziri Mkuu amesema “haiwezekani sukari inayotengezwa na kiwanda hicho ambayo ubora wake umethibitishwa na Shirika la Viwango Zanzibar ikakosa soko hii haiwezekani tukashindwa kununua tani 6,000 huku mahitaji yetu ni tani 36,000.”

Amesema sera ya nchi inasisitiza umuhimu wa kulinda wazalishaji wa ndani ambao bidhaa zao zimethibitishwa na mamlaka husika. Hivyo, ni lazima kuwalinda wawekezaji kwa kuhakikisha wanapata masoko ya uhakika pamoja na kuhamasisha wananchi kutumia bidhaa hizo.

Awali, Mkurugenzi Mkaazi wa kiwanda cha Sukari Zanzibar, Bw. Rahim Bhaloo alisema kiwanda chao kinazalisha tani 6,000 kwa mwaka huku kikiwa na uwezo wa kuzalisha tani zaidi ya 20,000 kwa mwaka ila tatizo ni soko pamoja na ardhi ya kutosha kulima miwa.

Alisema kutokana na uhaba wa soko sukari waliyozalisha katika msimu wa mwaka 2010/2020 wameuza tani 2,800 tu na kiasi cha tani 3,200 bado kipo kiwandani hapo, hivyo ameiomba Serikali iwasaidie kwa kuwatafutia masoko pamoja na ardhi ili waweze kuongeza uzalishaji.

Mkurugenzi huyo aliiomba Serika iwe inazuia utoaji wa vibali vya uagizaji wa sukari kutoka nje hususani kipindi cha uzalishaji ili waweze kuuza sukari yao na itakapoisha ndio vibali hivyo vianze kutolewa. Kiwanda kimeajiri wafanyakazi 300, pia wakulima wa nje zaidi ya 800 wanauza miwa yao kiwandai hapo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar, Bw. Juma Hassan Reli amemhakikishia Waziri Mkuu kwamba sukari yote iliyopo kiwandani hapo itakuwa imeshanunuliwa ifikapo Februari mwaka huu. Pia maelekezo yote aliyoyatoa kuhusu utoaji wa vibali vya uagizaji wa sukari watayafanyia kazi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...