Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki Kingu

Na Dotto Mwaibale, Singida

WIZARA ya Kilimo imetuma timu ya wataalamu kwenda wilayani Ikungi mkoani Singida kuona wadudu wa haribifu wa mazo waitwao Silangwa ambao wameleta changamoto kubwa kwa wakulima.

Akizungumza na waandishi wa habari Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki Kingu alisema wataalamu hao wamewasili katika wilaya hiyo baada ya kuiomba wizara hiyo kufuatia wakulima kukabiliwa na changamoto ya wadudu hao.

"Wakulima wetu wamekuwa na changamoto kubwa ya mazao yao kushambuliwa na wadudu hao ndio maana kilio chao nilikipeleka wizarani na leo hii 'jana' wataalamu wamewasili hapa Ikungi kufanya utafiti wa wadudu hao" alisema Kingu.

Alisema wataalamu hao watatembelea kata na vijiji vyote vyenye changamoto ya wadudu hao ambapo katika Kata ya Minyughe vijiji vitakavyo fikiwa ni Misuke na Mayaha.

Alisema katika Kata ya Mtunduru vijiji vitakavyo tembelewa ni Masweya, Kipunda na kitongoji cha Ifyamahumbi ambapo katika Kata ya Ighombwe wataalamu hao watatembelea Kijiji cha Germany, Msosa na Makhonda.

Kingu alisema ugeni huo baada ya kuwasili utakwenda kuonana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo Justice Kijazi pamoja na Mkuu wa wilaya Edward Mpogolo na baada ya hapo wataongozana kwenda kwenye maeneo yaliyoathiriwa na wadudu hao.

Alisema baada ya kutembelea maeneo hayo na kuwabaini wadudu hao wizara hiyo itaomba kibali maalumu toka Wizara ya Maliasili na Utalii na kutumia mbinu mbadala kuwaangamiza wadudu hao.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo amewaomba wananchi maeneo watakayopita wataalamu hao kuwapa ushirikiano.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...