Afisa Msimamizi wa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Chama Siriwa akiwaelimisha wananchi wanaofanya shughuli zao katika fukwe ya bahari ya Ununio jijini Dar es Salaam wakati wa kampeni maalum ya kuelimisha wananchi kuhusu athari za magendo katika ukanda wa Bahari ya Hindi.
Afisa Msimamizi Mkuu wa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Rose Mahendeka akiwaelimisha wananchi wanaoishi jirani na fukwe ya Bahari ya Kunduchi jijini Dar es Salaam wakati wa kampeni maalum ya kuelimisha wananchi kuhusu athari za magendo katika ukanda wa Bahari ya Hindi.



****************************

Na Veronica Kazimoto
Dar es Salaam

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka wafanyabiashara na wachuuzi wanaoishi jirani na fukwe za Bahari ya Hindi kutojihusisha na biashara za magengo kwani kufanya hivyo ni kuisababishia nchi kukosa mapato yake stahiki kutokana na wahusika wa biashara hizo kukwepa kulipa kodi.

Akizungumza na wafanyabiashara hao katika fukwe za bahari za Msasani, Mbweni, Ununio, Beach kidimbwi na Kunduchi zilizopo jijini Dar es Salaam, Afisa Msimamizi  Mkuu wa Kodi, Rose Mahendeka, kutoka Mamlaka hiyo ameeleza kuwa, watakaobainika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja na kukamata bidhaa zote na kutaifisha vyombo vilivyohusika kubeba bidhaa hizo.

“Tumeamua kufanya kampeni maalum ya kuelimisha wananchi kuhusu athari za magendo katika ukanda wa Bahari ya Hindi na moja ya madhumuni ya kampeni hii ni kuwaonya wale wote wanaojihusisha na biashara za magengo kwani adhabu yake siyo tu kukamata bidhaa na kutaifisha vyombo bali pia kuchukuliwa hatua za kisheria
ikiwemo kufungwa jela,” alisema Mahendeka.

Ameongeza kuwa, mbali na wahusika hao wanaojihusisha na biashara za magendo kukwepa kulipa kodi ya Serikali, kuna uwekezekano wa kuwasababishia wananchi madhara ya kiafya kwa kuwa bidhaa zinazopita katika njia zisizo rasmi zinakuwa hazijathibitishwa na Mamlaka husika za Serikali.

“Ni muhimu tukumbuke kwamba, bidhaa zote zinazopita katika njia za vichochoro au bandari bubu hazipiti katika utaratibu rasmi na hivyo zinakuwa hazijakaguliwa wala kuthibitishwa kama ni salama au la na Mamlaka husika kama vile TBS, TMDA, Mkemia Mkuu wa Serikali na nyinginezo. Kwa mantiki hiyo, bidhaa hizo zinaweza kuhatarisha afya za walaji,” alieleza.

Kampeni ya kuelimisha wananchi kuhusu athari za magendo katika ukanda wa Bahari ya Hindi imeanzia mkoa wa Dar es Salaam na timu ya maafisa wa TRA wanaendelea
na kampeni hiyo katika mikoa ya Pwani, Tanga, Mtwara na Lindi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...