Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

USAFIRI wa pikipiki umekuwa maarufu zaidi barani Afrika hasa katika ukanda wa Afrika Mashariki hasa kwa nchi za Tanzania, Kenya na Uganda ambako nchini Tanzania hufahamika zaidi kwa jina la bodaboda huku Kenya wakiita pikipikis, Rwanda wakiita Moto na Nigeria wakiita Okada.

Pikipiki ni jina lililotokana na mlio/sauti  ya kifaa chenyewe 'Pikipiki' wengine huita 'Tukutuku' na umekuwa usafiri wa dharura kwa watu wengi pindi wanapochelewa mahali au wanapotaka kukwepa foleni katika miji yenye misongamano.

Ripoti zinaonesha kuwa nchi za Afrika Kusini, Nigeria, Tanzania, Kenya, Uganda, Misri, Morocco, Angola, Algeria na Ethiopia zina uwingi wa pikipiki zinazotumika  kusafirisha  abiria na bidhaa na hiyo ni kutokana na kupitika kwa urahisi katika barabara za nchi hizo huku madereva wa vyombo hivyo wakihusishwa na matukio ya kusababisha ajali, wizi na kuvunja sheria za barabara.

Kutokana na urahisi na masafa marefu ya kuvuka mipaka ambayo pikipiki inaweza kukatiza ndipo ulipoanzia msamiati wa bodaboda kwa maana ya "border to border"  nchini uganda pikipiki zilianza kuvuka mpaka kuelekea Kenya kupitia mji wa Busia katika miaka ya 1990 hapo ndio msamiati wa bodaboda ukashamiri zaidi.

Nchini Uganda kwa mujibu wa Shirika la utangazaji la BBC imeelezwa kuwa mwaka 2000 kulikuwa pikipiki nyingi kuliko matatu (daladala) ambazo zilizokuwa zikiendesha shughuli za usafirishaji wa watu na mizigo nchini humo.

Vijana wengi nchini Uganda wamejitengenezea ajira kupitia uendeshaji wa bodaboda pamoja na kuwa kivutio kwa watalii wanaokuja nchini humo.

Nchini Kenya imeelezwa kuwa zaidi ya pikipiki 16,000 husajiliwa kwa mwezi na inaelezwa kuwa hadi sasa kuna zaidi ya pikipiki milioni moja zinazofanya kazi.

Nchini Tanzania ripoti zinaonesha kuwa kwa mwaka 2010 kulikuwa na ongezeko la pikipiki hadi kufikia 1,047,659 na nyingi humilikiwa na vijana ikiwa ni sehemu ya kujitafutia ridhiki zao.

Katika maeneo mengi ya Miji usafiri wa bodaboda umekuwa maarufu na wenye ulazima katika kuharakisha safari, na hali ya kusimamia usalama wa madereva na abiria umewekewa mkazo hasa katika kuzingatia matumizi ya kofia ngumu (helmet,) kutobeba abiria zaidi ya mmoja na kutotumia pombe wakati wa kuendesha vyombo hivyo.

Licha ya kurahishisha usafiri bado bodaboda nchini Tanzania zinakupambana na changamoto mbalimbali ikiwemo vifo (3,468 kwa mwaka 2015) huku asilimia 60 ya wagonjwa wanaotibiwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili asilimia 60 ni majeruhi wa ajali za pikipiki.

Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia usafiri wa bodaboda umepanda hadhi, watumiaji wamekuwa wakitumia simu zao kupata usafiri wa bodaboda kupitia Uber au Taxify mahali popote.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...