Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Kagera

NI maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Kagera ambao wamejitokeza kwenye mkutano wa Kampeni za Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Dk.John Magufuli ambaye ametumia mkutano huo kuelekeza mambo ambayo amepanga kuyafanya katika Mkoa wa Kagera na Taifa kwa ujumla.

Hata hivyo amekumbusha kwamba mwaka 2015 akiwa mbele ya wananchi hao alitoa ahadi nyingi lakini kubwa kuliko yote ilikuwa ni kuimarisha ulinzi na usalama katika Mkoa wa Kagera na leo hii anayo furaha kuona hali ya usalama imekuwa shwari wakati wote.

"Kagera ni Mkoa ambao uko mpakani, Kagera pamekuwa na masuala ya ujambazi, wakati naomba kura , miaka michache iliyopita ilikuwa ni jambo gumu kusafiri usiku,ilikuwa ni ngumu kupita kwenye misitu inayozunguka mkoa huu unapotoka kwenda maeneo mengine.Wenyeji wa mkoa huu watakuwa wanakumbuka hali ilivyokuwa, huenda leo hii hali ni tofauti.

"Nampongeza Mkuu wa Mkoa, nawapongeza wananchi wa Kagera, navipongeza vyombo vya ulinzi na usalama.Usalama na amani ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015 hadi 2020 na hakika tumeitekeleza vizuri.Yale mapori yaliyokuwa tishio yamegeuzwa kuwa hifadhi ya Taifa.Tunayo Burigi Chato, Ibanda, Rumanyika kule Karagwe.

Akiendelea kuzungumza na maelfu ya wananchi hao, Dk.Magufuli amesema waliahidi kukuza sekta utalii ili kuongeza mapato na kuongeza utalii nchini , na kwamba kazi hiyo wameifanya vizuri kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

"Tunataka ukanda huu wa Kagera uwe wa utalii kama ilivyo kwenye maeneo mengine, sekta ya utalii ndio inatoa ajira nyingi, imetengeneza ajira milioni nne na imeingiza fedha za kigeni na imekuwa ya pili baada ya sekta ya madini, iliyochangia dola bilioni 2.7.Hivyo  utalii ukiimarishwa utasaidia kuongeza ajira na watu kutengeneza fedha na hicho ndicho tunakitaka.

"Leo tunatoa takwimu kwa yale ambayo yamefanyika ili tunapoomba kura watu wajue yaliyofanyika, katika madini tumeanzisha masoko, kuongeza maeneo ya wachimbaji wadogo, hapa Kagera kuna kiwanda cha madini.Tani 24.62 za bati au tini zimeuzwa pale Kyerwa, kwa upande wa dhahabu mgodi wa Stamigo nako uzalishaji umeongezeka. tumeanzisha soko la dhahabu , hatua hizo ndio zimeachangia kuipiku sekta ya utalii,"amesema Dk.Magufuli.

Hata hivyo amesema miaka mitano ijayo wamepanga kukuza zaidi sekta ya utalii na madini na malengo yaliyopo ni kuongeza fedha za kigeni kutokana na sekta hizo na matarajio yawe ni kupata dola bilioni sita katika kuchangia pato la Taifa."Tumejipanga na kuimarisha uchimbaji madini kwa wachimbaji wadogo na wakubwa pamoja na kuwapatia vifaa vya uchimbaji,

 Kuhusu miundombinu Dk.Magufuli amesema wamejitahidi kuimarisa miundombinu kwa Mkoa wa Kagera na ahadi yake aliyotoa miaka mitano iliyopita ilikuwa kuimarisha usafiri ukiwemo wa usafiri wa meli katika Ziwa Victoria.

"Ninyi  wana Bukoba mnafahamu na ni mashahidi, baada ya kuzama kwa MV Bukoba na usafiri wa meli ulisimama kwa miaka 10 na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wafanyabiashara.

"Meli ya MV Victoria Hapa Kazi Tu imeanza kufanya kazi, inaitwa Mama Koku, na meli hiyo imefanyiwa matengenezo ni kama imenunuliwa upya na Sh.bilioni 22 zimetumika kukarabati meli hiyo. Tunaendelea kufanya ukarabati wa meli nyingine na nyingine zimekuwa tayari,"amesema Dk.Magufuli.

Amesisitiza lengo la Serikali ni kuona usafiri wa meli katika Ziwa Victoria unakuwa wa uhakika na wafanyabiashara wanaweza kusafiri kutoka sehemu moja na nyinyine ikiwemo ya kwenda nchi jirani za Uganda na Kisumu.

"Tumeanza kutengeneza meli kubwa kwa gharama ya Sh.bilioni 90, ambayo itakuwa ni kubwa na itakuwa inabeba watu 1200 na tani 400 za mizigo. Tunataka wafanyabiashara wa ndizi hapa Kagera wawe wanasafirisha ndizi zao hata Ulaya , hiyo ndio dhana ya uchumi wa kisasa, hakuna mtu anayeweza kuja kutupa pesa."

Kuhusu usafiri wa anga, Dk.Magufuli amesema ukitaka kuendeleza sekta ya utalii lazima uwe na uwanja wa ndege, ndio maana uwanja wa ndege wa Kagera umekarabitiwa. Maana yake  mtalii anaweza kutoka Uwanja wa Ndege Kimataifa wa Kilimanjaro(KIA) na kisha kufika Kagera kwenda kutembelea maeneo ya vivutio vya utalii.

"Ndio maana katika miaka mitano tumeimarisha usafiri wa anga, mbali na kujenga viwanja na kukarabati  viwanja tumenunua ndege mpya 11, na kati hizo nane zimefika na nyingine zinaendelea kutengenezwa.Hapa Kagera usafiri wa ndege ulikuwa imefikia Sh.milioni 1.5 na leo baada ya kununua ndege gharama zimeshuka.

"Lakini kwenye Ilani ya uchaguzi mkuu mwaka huu inaagiza kununuliwa kwa ndege nyingine tano, hivyo ndege zitakuja kununua Samaki hapa Kagera.Pia tumeimarisha usafiri wa barabara ambapo Sh.bilioni 149.3 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara,"amesema Dk.Kagera.
Sehemu ya Wananchi wa mkoa wa Kagera waliokusanyika katika Viwanja vya Gymkhana kumsikiliza Mgombea Urais kupitia Tiketi ya Chama cha Mapinduzi CCM Rais Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 16 Septemba, 2020

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...