*Aanika mipango , mikakati iliyowekwa katika Ilani kuhusu maendeleo

*Azungumzia upanuzi wa barabara ya njia nane kutoka Kibaha-Chalinze

*Awapongeza kwa kuongoza kwa viwanda vingi kuliko mkoa wowote nchini

 Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Pwani

MAELFU ya wananchi wa Wilaya ya Bagomoyo mkoani Pwani wamejitokeza kwenye mkutano wa kampeni za gombea urais kwa tiketi ya CCM Dk.John Magufuli ambaye ametumia mkutano huo kuelezea maendeleo makubwa yanayokwenda kufanya mkoa humo ikiwemo ujenzi wa upanuzi wa  barabara ya njia nane kutoka Kibaha hadi Chalinze.

Akizungumza leo Oktoba 19,2020 mbele ya maelfu ya wananchi hao, Dk.Magufuli alianza kwa kumshukuru Rais mstaafu Jakaya kikwete ambaye amesema amemlea na amejifunza mengi kutoka kwake na wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais mwaka 2015 walikuwa wagombea 42 lakini chini ya Kikwete aliendesha uchaguzi vizuri mpaka kupatikana yeye kugombea urais.

"Ahsante, upendo wako hauna kifani, pamoja na kutambua kazi ya urais ni ngumu lakini nakushukuru kwa upendo mkubwa ambao umeonesha kwangu, pia nakishukuru Chama Cha Mapinduzi(CCM) kwa kuridhia kunipitisha kugombea tena urais kwa awamu ya pili.Nimekuja kuomba tena kura kwasababu kubwa mbili.

"Miaka miatano iliyopita tumeshirikiana vizuri na kupata maendeleo, ambayo kwa bahati nzuri wagombea ubunge na udiwani wamekuwa wakieleza vizuri.Tumetoa elimu bila malipo na hasa kutoka familia masikini, tumejenga shule, madarasa  , mabweni, na kuboresha shule kongwe tano kwa hapa Mkoa wa Pwani.Miaka mitano ijayo tutaendelea kutoa elimu bila malipo na tutaongeze fedha za mikopo ya elimu ya juu, hatutaki watoto wakose elimu kwasababu ya kutokuwa na fedha.

"Tumeboresha huduma za afya kwa kujenga hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati, tumefanya hivyo na hapa Mkoa wa Pwani.Pwani ina  magari ya wagonjwa 36, tumeajiri watumishi wa afya 8,96, miaka mitano ijayo  tutaendelea kuboresha huduma za afya.Katika maji tumetekeleza miradi mikubwa miwili, mradi wa Ruvu Chini uliogharim Sh.bilioni 183.4 na mradi wa maji wa Ruvu Juu uliogharimu Sh.Bilioni 105.5.

"Miradi hiyo imepunguza tatizo la maji katika mkoa huu, ingawa tunafahamu bado kuna changamoto ya upatikanaji maji lakini niwahakikishie wananchi tunakwenda kumaliza tatizo hilo.Kuhusu miundombinu tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa, tumejenga barabara nyingi za lami. Kwa hapa tunayo barabara ya Bagamoyo- Msata, siku hizi mabasi mengi ya kutoka Dar kwenda mikoa ya kaskazini yanapitia katika barabara hiyo.Mbali na ujenzi wa barabara hiyo tunaendelea na ujenzi wa daraja la Wami ambapo kiasi cha Sh.bilioni 67.8 zinatumika katika ujenzi huo.

"Tunaendelea na upanuzi wa barabara ya njia nane kutoka Kibaha -Dar es Salaam na miaka mitano ijayo tutapanua barabara hiyo kutoka Kibaha hadi Chalinze kilometa 75, tumejenga gati la Nyamsati na kivuko kiko hatua za mwisho kabisa kumalizwa ili kuondoa tatizo la uasafiri Mafya,tumepanga kukamilisha barabara ya Kisarawe -Mwanalumango kwa kiwango cha lami na fedha zipo.Barabara ya Makofia nayo itajengwa kwa lami,"amesema Dk.Magufuli.

Pia amesema ujenzi wa reli ya kisasa baadhi ya vituo vyake vinapita Mkoa wa Pwani na yote yako kwenye Ilani ya Uchaguzi mwaka 2020, barabara ya Utete -Nyamwage nayo itajengwa kwa lami kilometa 37 huku akifafanua katika miaka mitano wamejitahidi kushughulikia kero mbalimbali.

"Moja ya migogoro ilikuwa ya ardhi kati ya vijiji na hifadhi, kwa Bagamoyo tumerasimisha baadhi ya vijiji vikiwemo Kaole Ufundi, Kialaka, Mwaluhombo, Pongwe, Msungura, Kifureta, Vigwaza, Chamakweza, Ruvu Darajani, Kaloleni, Kwa Masanja, Mindu, Tulieni, Kizangu na Sadani ambayo baadhi ya vitongoji vitakuwa makazi ya wananchi,"amesema.

Hata hivyo amesema Dk.Magufuli amesema Bagamoyo lazima warudishe heshima yake, ilijukukana enzi na enzi na ndio ilikuwa makao makuu na kwamba Bagamoyo lazima iwe Bagamoyo. "Katika wilaya hii ya Bagamoyo na Mkoa wa Pwani viwanda vingi, nikichaguliwa nataka pale Chalinze iwe wilaya ili huduma ziende vizuri na miundombinu ipo, jukumu lenu  nileteeni wabunge na madiwani ili baada ya kuchagulia kikao cha kwanza kiwe cha kuangalia namna gani wataigawa Bagamoyo ili iende kwa spidi kubwa.

"Mtakumbuka moja ya ahadi kubwa nilizotoa mwaka 2015 ilikuwa kujenga uchumi wa viwanda, nawapongeza Pwani kwa kuitikia mwito wa Serikali , kwani hivi sasa kuna viwanda 1,236 wakati mwaka 2015 vilikuwa viwanda 305 .Mkoa wa Pwani ndio unaongoza kwa mikoa yote ya Tanzania kwa kujenga viwanda vingi, nawapongeza sana viongozi wote kwa kujenga viwanda vingi ambavyo vimetengeneza ajira 200,000 na kati ya hizo ajira 50,000 za moja kwa moja kwa moja na 150,000 ni zile ambazo sio za  moja kwa moja,"amesema Dk.Magufuli.

Ameongeza viwanda hivyo vimesaidia kupatikana kwa malighafi, kila mahali unakutana na majengo makubwa ya viwanda na kwamba usione vyaelea vimeundwa na waundaji ni wana Pwani.Amesema zamani matunda yalikuwa yanakosa soko mpaka mengine yanauzwa kwa bei ya kutupwa lakini baada ya Serikali kuhimiza viwanda kikiwemo cha Bakhera na kiwanda cha Sayona ambavyo vinanunua matunda sasa matunda yanasoko.

Hata hivyo amesema kuna taarifa matunda mengine yanafuatwa mikoa jirani, hivyo ni fursa kwa Pwani kulima mananasi kwa wingi kwani soko lipo, walitumie kutengeneza fedha."Kujengwa kwa viwanda kumepunguza fedha za kigeni, kwa mfano leo tunajenga reli yetu na vifaa vyote vinazalishwa hapa nchini, Pwani mmenifurahisha mno na ndio maana barabara ambazo nimeahidi nitajenga kwa lami ili viwanda viendelee kujengwa, ili Pwani hii iendelee kubadilika kweli kweli.

Kuhusu sekta ua uvuvi, Dk.Magufuli amesema Mkoa wa Pwani una wavuvi wengi na kuna changamoto ambazo zinawakabili , kupitia Ilani ya Uchaguzi Mkuu wameweka mkakati kuwasaidia na watanaka wavuvi wafaidike na uvuvi wao."Tunataka kufufua shirika letu la uvuvi, kuna mali ambazo zimechukuliwa na watu tumezirudisha.

"Hata hivyo tunao mpango wa kununua meli nane za uvuvi, meli nne zitakuwa Tanzania Visiwani na meli nne Tanzania Bara.Tumeanzisha sheria ya kusimamia uvuvi nchini ambayo ni nzuri na hivyo tunawakaribisha wawekezaji wa ndani na nje kuja kuwekeza katika uvuvi, tunataka siku moja Bagamoyo iwe na kiwanda cha kuchakata samaki,"amesema Dk.Magufuli.

Pia amesema kuna makakati wa kuendeleza katika utalii wa baharini na watahakikisha meli za utalii zinakuja hapa nchini ikiwemo wilayani Bagamoyo huku akielezea mipango iliyopo katika kuimarisha utalii wa mali kale ambao wamepanga ufanyike Bagamoyo.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...