Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw John Mongella amezindua rasmi usajili wa mbio za Rock City Marathon msimu wa 11 huku akitoa wito kwa wadau mbalimbali kutoka kanda Ziwa kushiriki kikamilifu katika kufanikisha maandalizi ya mbio.

Mbio hizo zinatarajiwa kufanyika Novemba 29 mwaka huu eneo la  Rock City Mall jijini humo.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa usajili wa mbio hizo iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Mwanza, Bw Mongella aliwaomba wadau mbalimbali wakiwemo washiriki na wadhamini kujitokeza kwa wingi ili kuunga mkono mbio hizo zenye agenda ya kutangaza utalii wa ndani katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Katika hafla hiyo ilishuhudiwa Mkuu huyo wa Mkoa pamoja na viongozi wengine waandamizi wakijisajili kwa ajili kushiriki katika mbio hizo.

“Nasisitiza ushiriki wa wadau kutoka Kanda ya Ziwa hususani katika Mkoa wa Mwanza kwasababu hizi ni mbio zetu haitapendeza sana kuona kwamba wadau wakuu wa mbio hizi wakiwemo wadhamini na hata washiriki wanatoka kwa wingi mikoa iliyo nje ya Kanda ya Ziwa.’’ Alisema Bw Mongella

Alitoa wito kwa mashirika na taasisi mbalimbali zikiwemo zile watu binafsi kujitokeza ili kuongeza nguvu katika kufanikisha mbio hizo.

Zaidi, Bw Mongella alizipongeza taasisi na mashirika mbalimbali ambayo tayari yamejitokeza kufanikisha mbio hizo ikiwemo kampuni za TIPER, Chuo cha Mtakatifu Agustino (SAUT), Pepsi, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Kampuni ya Ujenzi ya CRJE, Pigeon Hotel, CF Hospital, Hospitali ya Bugando, Garda World, The Cask.

Aidha aliziagiza halmashauri za Wilaya zote za mkoa huo kupitia maafisa michezo kuhakikisha wanahamasisha usajili wa washiriki wengi iwezekanavyo ili mkoa huo uweze kupata wawakilishi wa kutosha kiasi cha kuakisi uenyeji wa mkoa huo katika kuandaa mbio hizo.

“Hata hivyo Mkoa wa Mwanza una historia ya kutoa wanariadha wakubwa walioipatia nchi hii heshima kubwa katika mchezo wa riadha akiwemo Suleimani Nyambui. Tunahitaji kuendeleza heshima hiyo kupitia mbio hizi hivyo tusimame wote pamoja kufanikisha hili. Washiriki wajitokeze kwa wingi na pia wadhamini wajitokeze kwa wingi,’’ aliongeza.

Akizungumza kwenye hafla hiyo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT), Profesa Costa Mahalu alisema chuo hicho kimeguswa na mbio hizo kutokana na adhma yake ya kutangaza utalii wa kanda ya Ziwa mkakati ambao unakwenda sambamba na mpango wa chuo hicho wa kukuza na kutangaza utalii katika Kanda ya Ziwa.

“Ushiriki wa Chuo cha SAUT kwenye mbio hizi ni mkubwa sana na ushiriki huo hautaishia tu kwenye kushiriki mbio bali pia utahusisha ziara za kutembelea na kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo Kanda ya Ziwa.’’ Alisema

Katika hafla hiyo, mbali na usajili, Mratibu wa mbio hizo Bw Kasara Naftal alimkabidhi Mkuu huyo wa Mkoa moja ya fulana maalum zitakazotumika katika mbio hizo katika msimu huu huku akibainisha kuwa tayari maandalizi muhimu yameshafanyika ikiwemo suala zima la fulana za washiriki pamoja na medali huku akitaja mbio zitakazohusishwa kuwa ni  km 21, km 10 na Km 5.

Alisema usajili wa mbio hizo tayari umekwisha anza kwa njia ya mtandao kupitia tovuti ya mbio hizo pamoja na usajili wa kawaida kupitia vituo mbalimbali vilivyopo mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga, Dodoma, Arusha huku mikoa zaidi ikiendelea kuongezwa.

“Usajili unaendelea vizuri na mwitikio wa washiriki ni mkubwa. Lengo ni kukimbiza washiriki  wasiopungua 3000 yakiwemo makundi yote yaani wakimbiaji wa mbio za ushindani (Elite runners), washiriki wa mbio za kujifurahisha (Fun run) pamoja na wanafunzi.” Alisema.

 “Kuhusu zawadi,  pamoja na medali washindi wa kwanza wa mbio za kilomita 21 kwa wanaume na wanawake watajinyakulia sh. Mil 2 kila mmoja, sh.mil  1.3 /-  kwa washindi wa pili na sh. 700,000 kwa washindi wa tatu, huku washindi wanne hadi kumi nao pia wakiibuka na zawadi  za medali na pesa taslimu.’’

“Kwa upande wa mbio za  Kilomita 10 hatutakuwa na zawadi za fedha taslimu isipokuwa washiriki watajipatia medali na fulana . Kuhusu mbio za kilomita tano ambazo zitahusisha washiriki kutoka mashirika na taasisi mbalimbali (corporates) sambamba na washiriki wenye ualbino zawadi za fedha taslimu zitatolewa kwa washindi watatu wenye ualbino pekee.’’ Alitaja.

Mratibu wa mbio za Rock City Marathon Bw Kasara Naftal (kushoto) akionesha fomu ya usajili wa mbio hizo baada ya kujazwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw John Mongella (kulia) ambaye alithibitisha ushiriki wake kwenye mbio za km 21 wakati wa hafla ya uzinduzi wa usajili wa mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika Novemba 29 mwaka huu jijini Mwanza.


Mratibu wa mbio za Rock City Marathon Bw Kasara Naftal (kushoto) akikabidhi moja ya fulana itakayotumiwa na washiriki wa mbio hizo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw John Mongella (kulia) ambaye alithibitisha ushiriki wake kwenye mbio za km 21 wakati wa hafla ya uzinduzi wa usajili wa mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika Novemba 29 mwaka huu jijini Mwanza.


Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw John Mongella  akithibitisha ushiriki wake kwenye mbio za za Rock City Marathon 2020 kwa kusaini form ya kushiriki mbio hizo ambapo alithibitisha kushiriki mbio za KM 21.


Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw John Mongella (wa pili kushoto, walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau muhimu wa mbio hizo akiwemo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT), Profesa Costa Mahalu (wa kwanza kulia, walioketi). Wengine ni pamoja na waratibu na wadhamini wa mbio hizo.



Karibuni Rock City Marathon 2020! Ndivyo wanavyomaanisha wadau muhimu wa mbio hizo akiwemo Mratibu wa mbio hizo Kanda ya Ziwa Bi Magreth Laizer (Kulia) na Mwandishi wa habari kutoka Sahara Media ya jijini Mwanza Bw Bernard James.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...