Na Mwandishi Wetu,Michuzi TV

RAIS Mstaafu katika Serikali ya Awamu ya Nne Jakaya Kikwete amewaomba Watanzania kumhakikisha katika Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyiika Oktoba 28 mwaka huu wanamchagua mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Dk.John Magufuli ili aendelee na kazi ya kuleta maendeleo.

Kikwete amesema hayo leo wakati akihutubia maelfu ya wananchi alipokuwa akifanya mkutano mkubwa wa kampeni kuwanadi wagombea wa Chama Cha Mapinduzi katika viwanja vya Zakiem Mbagala jijini Dar es Salaam ambapo ametumia nafasi hiyo kufafanua mambo mbalimbali pamoja na kujibu hoja za wapinzani ambazo wamekuwa wakizitoa kwa ajili ya kuwadanganya wananchi.

Rais huyo mstaafu amefanya mkutano huo ikiwa ni matekelezo ya ombi la mgombea urais kupitia CCM Dk.Magufuli aliyemuomba kumsaidia kumuombea kura katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Dar es Salaam baada ya yeye kukamilisha ziara zake katika mkoa huo mapema Oktoba 14,2020.

Katika mkutano huo Kikwete amewaeleza wananchi wa Temeke na Mbagala kuwa sababu za kuichagua CCM kuwa ni ubora wa sera na utekelezaji wa Ilani uliotukuka wenye kuwaletea wananchi maendeleo na kutambua shida zao.

" CCM inayo Ilani inayogusa matatizo ya wananchi moja kwa moja na Ilani ya CCM hutoa ufumbuzi wa nini kifanyike ili kuboresha maisha ya watanzania, hivyo wananchi wanakila sababu ya kuichagua CCM" ameeleza Kikwete. "Umoja wa kitaifa, amani utekelezaji wa miradi ya afya, elimu, maji na kuwawezesha wananchi kiuchumi imefanyika kwa kiasi kikubwa chini ya usimamizi mzuri wa Rais Magufuli lakini bado changamoto ziko,hivyo CCM inaomba kuchaguliwa tena ili kukamilisha majukumu yaliyobakia,"amesema Kikwete.

Pia amewaambia wananchi hao kuwa CCM imewaleta wagombea wazuri kwao ambao wameaminiwa kuwa wanaweza kusimamia maendeleo katika jimbo la Temeke Dorothy Kilave na Mbagala Abdallah Chaulembo wanatosha hivyo wawachague.


Akihitimisha hotuba yake Kikwete aliwaomba wananchi kujitokeza siku ya kupiga kura 28 Oktoba pamoja na kudumisha amani kwa kukubaliana na matokeo ya uchaguzi.Akijibu kuhusu baadhi ya hoja wapinzani, Kikwete amesema kumekuwepo na maneno mengi yanayotolewa na wapinzani kutokana na uamuzi wa Serikali kujenga uwanja wa ndege mkoani Geita, ambapo amewataka wananchi kutambua viwanja vya ndege vimejengwa katika mikoa yote na sio katika mkoa huo peke yake.

Amefafanua jitihada kubwa zimefanyika katika ujenzi wa viwanja vya ndege nchini pamoja na ununuzi wa ndege mpya 11, lakini kuna watu wamekuwa na nongwa kweli kisa tu ujenzi wa uwanja wa ndege Chato."Kwa upande wa anga viwanja vya ndege vimejengwa vingi , karibu mikoa yote inaviwanja vya ndege ulibakia uwanja mmoja tu wa Geita sasa umejengwa nanga inapaa.

"hasa ninyi mnataka Geita wasipate uwanja?Tatizo kujengwa Chato? Wakati ule tunajenga barabara ya Bagamoyo -Msata bungeni kulikua na vurumai hujapata kuona, Rais anajenga barabara kwao, wakati ule nasikia na Spika wangu kalibebea bango tena wakiwamo na wabunge wa CCM.

"Barabara ile haikujengwa na mie, uamuzi ule haukuwa wangu, Mzee Mwinyi ndio alianza kutengeneza barabara, kwanza wakati ule zilizopo zilikuwa na mashimo makubwa, mkakati huo wa ujenzi wa barabara ukaendelea, Dar es Salaam ilikuwa na barabara moja tu ya Dar -Morogoro hivyo tunakawa na mkakati wa kuitafutia barabara ya pili ya Bagamoyo-Msata,"amesema Kikwete.Amefafanua Mzee Mkapa alipoingia alitenga fedha kwa ajili ya barabara hiyo, na yeye alipoingia kulikuwa na maneno dhidi ya Rais Dk.Magufuli wakati huo akiwa Waziri kwamba amejenga barabara kwao, hivyo yeye(Kikwete)

Aliamua kutafutwa fedha za kwenda kujengwa kwa barabara huko na baada ya kupatikana kwa fedha za kujenga barabara ya Msata maneno yakawa mengi lakini barabara hiyo inanufaisha wengi."Ujue haya mambo ni tafsiri tu, kama viwanja vimejengwa vingi tu, shirika la ndege limeimarishwa, hivi ninyi mnataka watu wote wasafiri kwa gari tu.Lakini haya ndio mambo ya uchaguzi , adui yako muombee njaa, na haya yote hayana msingi, kazi imefanyika nzuri sana."


Aidha Mkutano huo wa ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Jumuiya akiwemo Mwenyekiti wa UWT Taifa Mama Gaudentia M. Kabaka pamoja na Wagombea wa nafasi za Udiwani.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...