Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia kiatu kilichontengezwa kwa bidhaa ya ngozi kutoka Tanzania, wakati akikagua mabanda katika maonesho ya Tano ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania, yaliyofanyika kwenye Uwanja wa maonesho wa Julius Nyerere, Sabasaba jijini Dar es Salaam Leo Disemba 4, 2020 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa apewa maelezo na kuhusu dawa za tiba asili inayotibu sukari na Mkurugenzi wa Kliniki ya tiba asili ya Cornwell Tanzania, Dkt Elizabeth Lema, katika maonesho ya Tano ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania, yaliyofanyika kwenye Uwanja wa maonesho wa Julius Nyerere, Sabasaba jijini Dar es Salaam Leo Disemba 4, 2020 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia kifaa cha kusambazia mtandao ‘internet’ wakati alipotembelea banda la kampuni ya simu Tanzania (TTCL), kwenye maonesho ya Tano ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania, Leo Disemba 4, 2020 jijini Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipewa maelezo na Fundi Mitambo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Yahya Mohammed, kuhusu mashine ya kisasa ya kuchambulia mpunga katika maonesho ya Tano ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania, Leo Disemba 4, 2020 jijini Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipewa maelezo na Kijana Mbunifu kutoka SIDO, Joseph Taifa,  kuhusu gari kwa ajili ya walemavu wa miguu lililotengenezwa na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) katika maonesho ya Tano ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania, Leo Disemba 4, 2020 jijini Dar es Salaam.  (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

**********************************************

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameziagiza mamlaka zote za udhibiti zihakikishe kuwa bidhaa zinazoingizwa nchini kwa ajili maonesho mbalimbali zinakuwa na viwango vya kimataifa na pia bidhaa zisizo na viwango na bidhaa bandia hazipati nafasi ya kuingia kwenye soko la Tanzania.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka wamiliki wa viwanda wazalishe bidhaa kwa wingi na kwa kutumia malighafi zinazopatikana katika mbalimbali nchini jambo ambalo litawezesha kuwa na uzalishaji wenye gharama ndogo na kuwa na bei shindani katika soko. 

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Ijumaa, Desemba 4, 2020) baada ya kufungua Maonesho ya Tano ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania katika Uwanja wa Maonesho ya Biashara ya Kimataifa wa Mwalimu J. K. Nyerere, Dar-Es-Salaam.  Kaulimbiu ya maeneo hayo ni ‘Tumia Bidhaa za Tanzania, Jenga Tanzania.’

“Watanzania tuachane na fikra potofu kuwa bidhaa zinazotoka nje ya nchi ndizo zenye ubora kuliko za hapa nchini, kwani bidhaa zetu ni bora na zina viwango vinavyostahili. Hebu sote tununue bidhaa zetu ili kukuza ajira na pato la mtu binafsi na Taifa kwa ujumla. Sisi Watanzania tunazalisha vitu bora na vyenye uhalisia.”

Amesema uwekezaji unaofanywa lazima uzingatie uendelevu, ubora na tija kulingana na viwango vinavyokubalika Kitaifa na Kimataifa katika shughuli za uzalishaji ili kuhimili ushindani na hata kuweza kunufaika na fursa za masoko zinazoendelea kujitokeza. “Nina hakika tukijipanga tutaweza kuwa washindani mahiri na bidhaa zenu zitaingia na kuleta ushindani mkubwa kwenye soko.”

Pia, Waziri Mkuu amewataka wawekezaji na wazalishaji wote nchini wafanye biashara halali, walipe kodi kikamilifu na wahakikishe wanatunza kumbukumbu vizuri ili Serikali iweze kupata takwimu sahihi za biashara zinazofanyika ikiwemo na nchi jirani na kuweza kuandaa sera mahususi za kuwasaidia.

“Wizara ya Viwanda na Biashara hakikisheni wazalishaji wanatumia vizuri sheria za uasilia wa bidhaa ili kuweza kukidhi matakwa na kutumia fursa ya masoko ambayo Serikali yetu imesaini mikataba ya maridhiano hususani soko la Afrika Mashariki, SADC, AGOA na fursa nyingine za masoko ya pamoja.”

Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuziagiza Halmashauri zote nchini zihakikishe viwanda vilivyo katika mamlaka zao vinashiriki kuonesha bidhaa wanazozalisha ili bidhaa hizo ziweze kutafutiwa masoko katika nchi mbalimbali duniani zikwemo nchi za Ukanda wa EAC na SADC kwa lengo la kuongeza mauzo ya Tanzania nje ya nchi.

Pia, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara za Fedha na Mipango na Viwanda na Biashara ziendelee na mikakati ya kisera na kikodi ya namna ya kupunguza uagizaji wa baadhi ya bidhaa zinazozalishwa nje na kuongeza ununuzi wa bidhaa zinazozalishwa ndani ili kukuza viwanda vya ndani mfano; bidhaa za mbao, mafuta ya kula na saruji.

 

“SIDO kwa kushirikiana na VETA wekeni kipaumbele cha kutoa mafunzo na kubuni nyenzo zinazoendana na mahitaji makubwa yaliyomo katika jamii ikiwemo katika eneo la kuchakata mazao kama korosho, chikichi, ufuta, alizeti na matumizi ya TEHAMA katika kuboresha uzalishaji mali, ufanisi, viwango na kutafuta masoko.”

Pia, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kufanya maboresho katika uratibu wa maonesho mbalimbali ya Viwanda na Biashara ili yafanyike kwa kuzingatia kanda za uzalishaji nchini badala ya nguvu kubwa kuelekezwa Dar Es Salaam na miji mikubwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...