Na Mwandishi Wetu
Katika kuadhimisha miaka kumi tangu kuanzishwa kwake redio ya Voice of Africa yenye masafa ya 98.5 yenye ofisi zake wilaya ya Korogwe mkoani Tanga iliratibu na kushiriki zoezi la upandaji miti 100 katika hospitali mpya ya wilaya ya muheza.
Akizungumzia uamuzi huo,Mkurugenzi Mtendaji wa redio ya Voice of Africa Bi.Chemuye Ngosha amesema kwamba huo haukuwa uamuzi mgumu kuufanya kwani redio hiyo ni sehemu ya kuihudumia jamii na wakati huu ambapo imetimiza miaka kumi ulikuwa wakati muafaka wa kuweka alama katika jamii na hasa kwa kuyagusa mazingira kwa kupanda miti.
"Unaweza ukajiuliza kwanini miti hii 100 tumeamua kuipanda hapa hospitali,niseme tu kwamba licha ya kuwa itabaki kama alama ya kumbukumbu, mazingira na hali ya hewa hapa hospitali vitakuwa katika hali safi kabisa ya hewa na hivyo kufanyika chachu ya nafuu kwa wagonjwa na watu mbalimbali watakaofika hapa kwa ajili ya kupata huduma" Alisema Bi.Chemuye
Mbali na zoezi la upandaji miti, miaka kumi ya Voice of Africa iliadhimishwa kwa tamasha lililofanyika katika viwanja vya CCM Jitegemee Muheza na kupambwa na shughuli mbalimbali ikiwemo mazoezi,semina za kielimu kutoka taasisi mbalimbali zkiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Jeshi la Zimamoto, vipaji vya muziki pamoja na burudani za ngoma.
Akimwakilisha Mh.Mkuu wa Wilaya,Kaimu Mgeni Rasmi,Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Muheza Bw.Shaban Selemani Maghembe amekipongeza kituo cha redio cha Voice of Africa kwa kufikia miaka kumi ya utendaji wenye kuyagusa moja kwa moja maisha ya wananchi na kutoa rai kuwa kazi hii iendelee na iboreshwe zaidi na zaidi kwani mafanikio hayatakiwi kuwa chanzo cha kubweteka bali yafanyike chachu ya kuwa bora zaidi.
Aidha katika hotuba yake Mkurugenzi Mtendaji wa redio ya Voice of Africa ameishukuru Serikali kwa kuwapa vibali na ushauri na ushirikiano katika kipindi chote ambapo redio ipo hewani. Vilevile amewashukuru wadau wote wanaofanya kazi na redio hiyo zikiwemo kampuni na taasisi za ndani na nje ya nchi na kuahidi kuwa Voice of Africa itaendelea kuboresha huduma zake ili kuwafikia watu wengi zaidi hapa nchini.
Kituo cha redio cha Voice of Africa kilianzishwa Februari 25,mwaka 2011 katika Wilaya ya Muheza na Decemba 2014 kituo hicho kilihamishiwa wilayani Korogwe. Voice of Africa inasikika mkoa mzima wa Tanga kwa maana ya wilaya zote na katika mikoa jirani inasikika Morogoro, Dodoma Manyara Kilimanjaro, Pwani na Visiwa vya Pemba,Unguja,Visiwa vya Comoro na Mafia.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...