Na Daudi Manongi- MAELEZO

SERIKALI inafanya mapitio ya tozo za redio katika wilaya na maeneo ya pembezoni mwa nchi ili kuzipunguza kwa ajili ya kuongeza usikivu wa redio na kuwafikia wananchi nchini kote.

 

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile wakati wa uzinduzi wa studio za redio jamii 93.7 inayomilikiwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) iliyozinduliwa leo jijini Dodoma.

 

“Tumeshatoa zabuni za masafa na leseni za redio katika mikoa zaidi ya ishirini pamoja na wilaya ambazo ziko pembezoni na natoa rai kwa watanzania waende katika website ya TCRA au wafike katika ofisi hizo wataona wilaya ambazo tumezitangaza , tunaenda kupunguza gharama za leseni kwa redio katika ngazi ya wilaya, ngazi ya jamii na pembezoni,” amesema Ndugulile.

 

Ameongeza kuwa kwa kufanya hivyo wananchi wataondokana na kusikiliza redio kutoka nchi jirani na hivyo itasaidia kupata taarifa mbalimbali za maendeleo za nchini mwao.

 

Aidha, amesema wameshatoa zabuni ya mawasiliano ya simu katika maeneo ambayo yako pembezoni mwa nchi ili makampuni ya simu yaweze kufanya tathmini na kuwekeza katika kuboresha usikivu wa simu ili mawasiliano ya nchini lengo likiwa mawasiliano yote ya  nchini mwetu yawe ya simu za Tanzania na sio nchi jirani.

 

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul  aliyekuwa akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa amesema kuanzishwa kwa redio hiyo ni jambo la kihistoria kutokana na uhumimu wake kwa Taifa hasa katika kufikisha huduma za matangazo ya redio kwa wananchi wa makao makuu na mikoa ya jirani.

 

“Kituo hiki kinapokwenda kufunguliwa leo tunategemea masuala ya kawaida yanayowagusa watanzania  yanakwenda kuzungumzwa na burudani mbalimbali zinaenda kutolewa pamoja na vipindi vinavyokwenda kurushwa ni vya utalii, kilimo na ufugaji, michezo, vijana, michezo, muziki na mila na desturi.” Alisisitiza Waziri Gekul.

 

Aidha, ametoa wito kwa vyombo vya habari nchini kuzingatia weledi na kuhakikisha maudhui yanayokwenda kwa wananchi hayapotoshi na ni ya sahihi na kweli.

 

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Nchini (TBC), Dkt. Ayoub Rioba amesema radio hiyo ya jamii itakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa kanda ya kati na zitawezesha wananchi kufuatilia maudhui mbalimbali na pia wananchi watapata fursa ya kutembelea studio hizo na kuzungumza moja kwa moja.

 

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF), Bi.Justina Mahiba amesema ukarabati wa studio na ununuzi wa vifaa umegharimu bilioni 1.71.

 

“Tumeiwezesha TBC kusikika katika maeneo yote ya mipakani na mpaka hivi sasa tuna miradi 14 ambayo inaendelea katika utekelezaji.”Alisema Bi.Mahiba.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...