Raisa Said,Handeni.


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Handeni Mussa Mkombati amewataka Wananchi wa Mji huo kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa mchakato wa Sensa ya Watu na Makazi utakapoanza mwakani.

Akizungumza Wakati wa Ziara yake ya kukagua miradi ya maendele Kijiji cha Bondo kata ya Kwamagome ,Mkombati alisema suala la kuhesabiwa ni muhimu sababu Serikali haiwezi kutengeneza mipango ya maendeleo kwa wananchi wake bila kuwa na takwimu sahihi za wakazi wa eneo husika.

Akifafanua, Mkombati alieleza kuwa lengo la sensa hiyo ni kuisadia Serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025, mageuzi ya masuala ya afya na jamii, pamoja na ufuatiliaji wa ajenda za maendeleo za kimataifa.

Alisisitiza kuwa taarifa za idadi ya watu husaidia katika mamlaka za wilaya katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ambayo huakisi matakwa ya watu katika ngazi husika na kusaidia kwenye uwiano wa mgawanyo wa rasilimali

"Takwimu sahihi za Sensa zinahitajika kwa ajili ya ugawaji wa majimbo ya uchaguzi kwa ufanisi, kurekebisha mipaka ya kiutawala katika serikali za mitaa" Alieleza Mkombati

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepanga kufanya Sensa ya Watu na Makazi ifikapo mwezi Agosti 2022.

Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS), ipo kwenye maandalizi ya kufanya Sensa hiyo.

Sensa ya Watu na Makazi ni zoezi la kitaifa linalofanyika kila baada ya miaka 10 ambapo Sensa ya mwisho kufanyika nchini ni ile ya mwaka 2012.

Hivyo Sensa ya mwaka 2022 itakuwa ni sensa ya Sita kufanyika nchini baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964. Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...