BARUA YA WAZI KWA MWENYEKITI WA JUMUIYA YA WATANZANIA UINGEREZA

31.05.2007

Abubakar Faraji
Mwenyekiti
Jumuiya ya Watanzania Uingereza


Ndugu Mwenyekiti

YAH: USIMAMIZI WAKO WA KADHIA YA UKAGUZI WA MAGARI YAENDAYO TANZANIA

Nadhani barua hii itakukuta katikati ya shughuli za kawaida za kimaisha pamoja na kushughulikia masuala ya jumuiya.

Kama mmoja wa Watanzania waishio Uingereza napenda kukuandikia waraka huu kukuelezea masikitiko yangu juu ya namna unavyolishughulikia suala hili.

Nimelazimika kuchukua hatua hii licha ya ukweli kuwa na mimi ni mmoja wa wajumbe wa kamati mojawapo mpya zilizoundwa, hii ni kwa vile Mwenyekiti umeamua kulitolea kauli suala hili bila kufanya tafakuri na mtu yeyote ndani ya Jumuiya ya Watanzania waishio Uingereza.

Jitihada zangu za kukushawishi ujizuie kutoa tamko hadharani mpaka hapo utakapo kutana na wajumbe wenzako japo wa kamati ndogo ya Utendaji zimeshindikana, nimelazimika kuandika waraka huu kuelezea maoni yangu hadharani ili ieleweke wazi kwamba katika hili Mwenyekiti unaiongoza vibaya jumuiya.

Taarifa zako kuhusu kadhia ya WTM Utility Services na TBS zinaonyesha Mwenyekiti haupo katika upande WA Watanzania walio wengi, zinajikanganya na hazitoi picha halisi ya maumivu na dhulma ya dhahiri inayoonekana kufanywa kwa Watanzania:

Taarifa hii kuhusu mkataba huu usio na maslahi kwa Watanzania ilianza kujulikana kupitia tovuti yako binafsi
www.tzuk.com tarehe 26.05.2007 ambapo uliitoa kama habari tu. Kama Mwenyekiti wa Watanzania mwenye jukumu la kusimamia maslahi yetu tulitarajia kwamba ungetoa maelekezo haya hata katika tovuti ya Jumuiya www.tzcommunity.co.uk ili watanzania wajue kuwa kuna utaratibu mpya wa ukaguzi. Ni taarifa ambayo inawagusa watanzania walio wengi kama sio wote waishio nchini hapa, hukuona umuhimu wa kuweka taarifa hii katika tovuti ya Jumuiya badala yake ukaweka katika tovuti yako binafsi ambayo kama mmoja wa waandishi wa tovuti hiyo siku za nyuma,nafahamu kwamba inaendeshwa kibiashara…






Kuna maswali mengi hoja namba moja hapo juu:

- Je ulipokea malipo yoyote katika kutoa taarifa hii kwa Watanzania waishio Uingereza?
- Kama Mwenyekiti wa Watanzania hukuona umuhimu wa kutaka kujua zaidi na kuwasilisha maslahi ya watanzania ikiwa ni pamoja na kutaka kuhoji baadhi ya matatizo ya dhahiri ambayo yamejionyesha katika taarifa yenyewe?

Baada kufanya mawasiliano binafsi nawe, tarehe 28.05.07 ulikiri kuwa umepokea malalamiko mengi kutoka kwa Watanzania, lakini hukuona umuhimu wa kuitisha mkutano wa wajumbe wenzako kujadili hili? Badala yake tarehe 30.05.07 ulitoa tamko kuwajulisha watanzania kuwa umepokea malalamiko yao na kama Mwenyekiti unafanya jitihada za kutoa tamko, ndani ya siku tano baada ya kukusanya ushahidi toka pande zote. Siku ya pili 31.05.07 umekurupuka na kutoa tamko kuelezea yaliyojiri katika mazungumzo yako na TBS, pekee!

Ukweli ni kuwa katika mazungumzo yetu baada ya tamko la kwanza, ulisema kikubwa ulichoongea na wadau husika [TBS] waliotoa zabuni kwa kampuni moja tu kufanya ukaguzi huu wa magari ni kutaka kujua vigezo wanavyoangalia katika ukaguzi. Licha ya kuwa hukushariana [kwa mara ya pili na kiongozi yeyote mwenzio ndani ya jumuiya na licha ya kukusihi sana usiendelee kutolea tamko hili suala mpaka hapo umekutana na wenzako wote] na yeyote, kwenye maelezo yako marefu ya tarehe 31.05.07, Mwenyekiti kipengele hiki kikubwa kilichotawala mazungumzo yako na TBS hukukiweka kwenye taarifa!

Badala ya kutuelezea vigezo vinavyotumika kwenye ubora wa magari, Mwenyekiti taarifa yako imeelezea kwa kirefu historian na umuhimu wa ukaguzi huu bila kugusa maswali muhimu ya watanzania.
Ndugu Mwenyekiti kukusaidia katika kujua ubaya na uonevu wa dhahiri unaofanywa na TBS ikishirikiana na Kampuni hii changa isiyo na nyenzo za kufanya zoezi zito na kubwa kama hii nakuomba uzingatie maelezo niliyoyatoa katika blog yangu hapo jana: http://saidiyakubu.blogspot.com/2007/05/utaratibu-wa-mpya-wa-kukagua-magari.html

Natambua wazi kwa kueleza msimamo wangu hadharani, nitakuwa sitendei haki nadharia ya uwajibikaji wa pamoja [collective responsibility] lakini kabla hujanisuta kwa hili nakuomba urejee vitendo vyako binafsi kuhusu kadhia hii ambavyo bila shaka kabisa si tu vinakiuka nadharia hii bali pia kuna wasi wasi miongoni mwa watanzania kuwa huenda ni mgongano wa maslahi [conflict of interest] ambayo ni dhambi kubwa zaidi.

Lakini pia nadhani kwa kukaa kimya dhamira yangu ya kukubali kuwa mjumbe wa kuteuliwa kwenye kamati hii kwa maslahi ya watanzania wote itakuwa inanisuta, mimi nawe tumejuana kwa miaka takriban mitano sasa na tumetokea kuwa marafiki wa karibu lakini katika hili Mwenyekiti nimejikuta sina budi kuuweka urafiki wetu kando kuangalia maslahi ya wengi. Ni matumaini yangu Mwenyekiti utakuwa na nguvu na uelewa wa kutambua kuwa ni tofauti katika hili ndio zimetutetanganisha na iwapo tukijirekebisha na kufanya kazi kwa maslahi ya wengi hakuna kitakachoharibika

Tunakuomba Mwenyekiti ili kuendeleza Jumuiya hii changa utoe maelezo binafsi kujiweka kando na mkataba huu vinginevyo utakuwa unapoteza sifa ya kuwa msimamizi mzuri wa haki na maslahi ya watanzania wote kwani msimamo wako katika hili unaonekana kuyumba sana hususan ukionekana kuvutia upande mmoja ambao ni dhahiri sio unaopendelewa na watanzania walio wengi.

Ahsante Sana.

Saidi Yakubu
Mtanzania aishie Uingereza.


Nakala kwa:

BI MWANAIDI SINARE MAAJAR
BALOZI WA TANZANIA UINGEREZA NA MLEZI WA JUMUIYA YA WATANZANIA WAISHIO UINGEREZA.

WAJUMBE WA KAMATI YA UTENDAJI YA JUMUIYA YA WATANZANIA.

WATANZANIA WOTE WAISHIO UINGEREZA.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 43 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 31, 2007

    huyo mwenyekiti ajiuzulu! hafai kabsaa

    ReplyDelete
  2. Hivi wa-danganyika mtaacha majungu lini? Nadhani ndio maana NAOGOPA SANA East Africa Federation!!

    Mtabaki na majukungu siku zote!!!

    ReplyDelete
  3. AnonymousMay 31, 2007

    Good job. nakupa hongera na kingine nimefurahi ulivyoweka na jina lako. kweli wewe ni mtanzania halisi na hutafuti majungu ila unaeleza ukweli.

    jasho la mnyonge haliendi bure.

    Mimi sisishi UK lakini katika kusoma hii niliona kuwa hapa ni kazi ya kuwatajirisha tu wachache.

    Tenda inatolewa kwa kampuni moja tu. Je TBS walitangaza wapi na kuona ni nani au ni kampuni gani wanaweza kuja na bei nzuri zaidi kama ni muhimu kuwa na hiyo pre inspection huko UK?

    Je kama mnavyose hawa watu hawanaujuzi wala vifaa vya kufanya hii inspection ni jinsi gani walipata lincense?

    Watanzania inabidi tufungue macho sana. Tumechoshwa na hao wachache wanaochukua uongozi kwa manufaa yao wenyewe.

    Hii sio kwa UK tu.. bali nchini mwetu. Kinachonishangaza ni kuwa kiongozi anachaguliwa baada ya mwaka moja anakua na nyumba, magari na bishara zenye thamani ya mabilion. Inamaana mishahara ya hao viongozi wetu kwa mwaka ni mabilioni ya hela? kama sio ...Hizo hela zingine wanapata wapi?
    Kwa vile Tanzania hamna haja ya kuonyesha income yako unaipata wapi au vipi viongozi wengi tu wanajikusanyia utajiri sana kupitia migongo ya walala hoi.

    ReplyDelete
  4. AnonymousMay 31, 2007

    Siko UK, lakini hapa ni jazba (post-traumatic stress) kwa kwenda mbele.

    ReplyDelete
  5. AnonymousMay 31, 2007

    Unajua watu tumetoka kwenye ukiritimba uliokomaaa... yaani nchi za kiafrika ikiwemo tanzania ukiishi huko unaona kama mambo yanaenda sawa ila ukitoka ndio unaona tofauti..
    Hoja hapa ni kwamba nadhani wote twafahamu vyema ni jinsi gani vifaa vya kufanyia MOT ni vya kisasa na kitaalam, isitoshe ni jinsi gani labor charge huku ughaibuni ilivyo ghali, lakini kwa mchanganuo wote huo bado tumeona kuwa MOT ni £34 - £45 sasa kwa fununu nasikia ya kuwa hiyo inspection ni zaidi ya mara mbili ya price ya MOT nini mnataka kutueleza hapa ni kwamba hivyo vifaa ni vya gharama gani? na hao ma-engineer ni wakutoka wapi? nadhani ule msemo usemao ucan fool only one one person but not a group of person sasa unatimia..
    Naomba hao TBS na hao wanyonyaji wanaotaka kujaza matumbo yao kwa hela tuzipatazo kwa taabu muelewe kuwa wengi wetu tuishio huku tuna vitu vikuu vitatu muhimu 1;Education 2;Exposure 3;Expirience ya maisha yote ya kikazi na mazingira as well.
    Wito ni kwa serikali kuliangalia hili kwa ukaribu na lirekebishwe.

    ReplyDelete
  6. AnonymousMay 31, 2007

    wizi umezidi UK ndo maana mmeanzisha tawi la ccm, Good Job Yakubu! mi naona jumuiya ivunjwe na tawi lenu la wizi la ccm livunjwe pia muanze

    ReplyDelete
  7. AnonymousMay 31, 2007

    huyu mwenyekiti na kamati yake wanaboa, miezi mitatu sasa hakuna mkutano na watanzania, kisha tunaona wanaanza kulumbana,

    jambo dogo kama hili mwenyekiti anashindwa kulitolea tamko?

    ama kweli any thing is possible if you are a tanzanian...

    ReplyDelete
  8. AnonymousMay 31, 2007

    Saidi/Issa

    Ninapenda kukupeni mkono kuwezesha hili swala kulitoa katika blog yako. Hivi ndio tutaweza sisi wananchi ambao hatuna sauti kutoa maoni yetu na muono wetu juu wa mfumo mzima wa uanzishaji wa sheria hii bila kuzingatia maslahi ya wananchi wake.

    Hii inaonyesha dhahiri maamuzi yanayofanya na vyombo vya serikali hii, bila kujali msingi muhimu wa kuwatumikia, kuwashirikisha na hata kujali maslahi ya wananchi wake. Haya ni maswala ambayo yanaturudisha nyuma kimaendeleo hususan kwa wananchi na siyo vyenginevyo.

    Swala muhimu la kujiuliza na kuwauliza hawa waungwana, Je ni vipi tofauti ya MOT, in technical aspects, na hiyo taratibu watakazotumia hawa WTM utility services aka TBS.

    Vile vile ningependa watuonyeshe wazi hizo taratibu zao na standard zao, ambazo zinahitajika kwa gari kupasi kabla ya kusafirishwa. Hizi manifesto lazima zitakuwepo TBS, watuwekee wazi.

    kwa mfano acceptable wheel alignment, exhaust emission, na vinginevyo vingi, Je hivi vipengele vinapishana vipi na hivyo vya MOT.

    Je vipimo na viangalio vya TBS Tanzania ni bora zaidi, kuliko hivyo vya MOT-UK, au ni vyenye kulingana, au ni vipi vipi naomba tufahamishwe hilo.

    Nitakupeni hadithi moja NASA - National Aeronautics and Space Administration ya Marekani, walitumia karibuni milioni moja dola, kwa kufanya utafiti wa kalamu itakayotumika kwenye SPACE shuttle, wakati hawa astronauts watakua kwenye space ships zao. Russia waliamua kutumia PENCIL. Je hii habari inalingana na hii ??? Ni kitu cha kujiuliza.

    Na hizi mobile unit zao ambazo zitakuwepo kwenye hizi port, Je zina facility zote za mashine za kupandishia gari kucheki chini ya gari na vinginevyo vingi ambavyo vinatizamwa na MOT - UK. Kuna utata hapa.

    Halafu swala jengine la kujiuliza, hawa jamaa watapeleka vipi hizi mobile units zao kwenye Bandari, itakua ni kuendana kinyume kabisa sheria na taratibu nzima za Health and Safety issues, kwa mujibu wa serikali ya UK. Bandari ni sehemu ya kuhifadhia mizigo na kulay down mzigo uliongia port au unaokusudiwa kusafirishwa na siyo vyenginevyo.

    Na je kama unakusudia kupeleka gari kwa port ya Northen Ireland(kisiwani)-miongoni mwa nchi ndani ya UK, ambayo pia ni UK, hawa jamaa watapanda maferi na mobile unit zao kuja nazo port ya Northen Ireland.

    Hawa jamaa wanataka kufanya mambo yao kiholela bila kuendana na taratibu za sheria hapa UK.

    Watanzania unganeni muweze kulifikisha hili swala kweye serikali ya UK na Ministry of Transport, Kama serikali inasikia habari hizi, lazima watapandishwa Court, mimi nahisi hili swala ni lazima lipitishe kwenye vyombo husika vya UK.

    Kwa sababu ni mahisio yangu makubwa hawa jamaa ni matapeli, na inafaa sisi watanzania kutafuta Lawyer UK, na kuwapandisha Court.

    Na mwisho kabisa ni mahisio yetu hizi mobile unit, whatever the name they make call them ni MAVANI na JEKI. Utapeli wa wazi kabisa.

    By Mchangiaji

    ReplyDelete
  9. AnonymousMay 31, 2007

    MICHUZI FATILIA HII HALAFU UTULETEE PUMBA ZA HAO WATOTO WA MLIMANI:

    Chuo Kikuu Dar chaandaa warsha ya sheria ya uraia

    2007-05-31 09:47:24
    Na Erick Lema


    Taasisi ya Maendeleo ya Taaluma (IDS) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, imeandaa warsha ya siku moja juu ya sheria mpya ya uraia wa nchi mbili.

    Mratibu wa warsha hiyo, Dk. Colman Msoka alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa, warsha hiyo inalenga kujadili kwa kina juu ya sheria mpya ya uraia wa nchi mbili inayotarajiwa kuwasilishwa bungeni wakati wowote.

    Dk. Msoka alisema kwamba, katika warsha hiyo inayotarajiwa kuhudhuria na wasomi wengi akiwamo Ofisa Mwandamizi wa Ubalozi wa Marekani nchini, Robert Hannang, jamii ya chuo kikuu inatarajia kujadili juu ya sheria ya uraia wa nchi mbili. Watanzania wameombwa kujitokeza kutoa maoni yao juu ya sheria hiyo.

    ``Ni fursa ya pekee. Tuna wasemaji wengi wakiwamo hata ofisa wa ubalozi wa Marekani (Robert Hannang) atakayeshiriki na kuelezea uzoefu wake katika sheria za uraia wa nchi mbili.

    ``Tunadhani ni wakati mwafaka kwa Watanzania wengi, kushiriki kikamilifu katika kuujadili muswada huu wa sheria kwani sheria sii ya watu wachache bali ni ya watanzania wote.``

    Warsha hiyo inayotarajiwa kuhudhuriwa na wasomi wengi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na wadau wengine, inatarajiwa kuanza saa 3:00 katika ukumbi wa Baraza la Chuo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Sehemu ya Mlimani.

    ``Ni fursa pekee kwa taasisi yenye hadhi kama hii kuandaa mjadala unaowahusisha watu wa kada mbalimbali. Tunawakaribisha wote,`` alisema Dk. Msoka.

    Hatua ya IDS imekuja baada ya serikali kutangaza kuanza kwa mchakato wa kuwaruhusu Watanzania walioukana Utanzania wao kuwa na uraia wa nchi mbili.

    Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Nje, Benard Membe alihojiwa na Shirika la Habari la Uingereza na kusema kwamba, serikali imeona upo umuhimu wa kutunga sheria itakayowaruhusu wananchi hao kuwa na uraia wa nchi mbili ili waweze kushiriki kuleta maendeleo nyumbani.

    ``Tayari Rais Jakaya Kikwete ameagiza tuanze mchakato wa kuwapatia wananchi wetu uraia wa nchi mbili... tumegundua kuwa tukifanya hivyo wenzetu hao wanaweza kusaidia sana kuleta maendeleo nchini,`` alisema Membe ambaye pia ni Mbunge wa Mtama, mkoani Lindi.

    Sheria ya Tanzania inasema mtu akipewa uraia wa nchi nyingine atalazimika kuukana urai wa Tanzania na hivyo kukosa haki ya kuitwa Mtanzania.

    Membe alisema kwamba, dhana iliyokuwa imejengeka hapo awali kuwa wananchi wanaoukana uraia wa Tanzania ni wasaliti imepitwa na wakati kwa vile wengi wao hufanya hivyo kwa lengo la kujitafutia maisha bora.

    ``Watu hawa hasa waliofanikiwa kupata maisha bora ugenini wakijua kuwa bado wanayo haki nchini mwao lazima watarudi kuwasaidia shangazi na wajomba zao, hiyo itasaidia kuboresha maisha ya Watanzania,`` alisema Membe.

    Hata hivyo Waziri Membe hakueleza lini mchakato huo unatarajia kumalizika na hatimaye kuwa sheria inayowaruhusu wanaoukana uraia wa Tanzania kuwa na uraia wa nchi mbili.

    SOURCE: Nipashe

    ReplyDelete
  10. AnonymousMay 31, 2007

    Mlitakiwa kulisolve tatizo hili wenyewe huko UK, hatuna haja ya kujua matatizo yenu, anyways jumuiya nyingi za watanzania(sio zote) waishio nje (marekani na Uk zikiongoza) zina majungu majungu tu sana, watu kusemana hovyo, kuchunguzana na ushindani usio na msingi, kwnani mngeitana kikao chenu mkapata nafasi ya kulizungumzia hili suala ingekuwaje? basi tu tumeshawazoea lakini.

    ReplyDelete
  11. AnonymousMay 31, 2007

    safi sana mzee Yakubu kwani huyo mwenyekiti ana kitu anachotaka ndio maana anajidai eti anataka kuunganisha watanzania apa UK.

    ReplyDelete
  12. AnonymousMay 31, 2007

    Hii ni jazba na kujitafutia jina tu. Kwani tatizo ni nini? kama gari unayotaka kusafirisha ina viwango au ni mpya una wasiwasi wa nini? Nchi imechoka na taka taka mnazopeleka eti mnaita magari 5th hand, bora hata ingekuwa 2nd hand. Wewe nunua gari yako mpya, peleka uone kama watakuletea gumzo. Acheni ubabaishaji, na majungu. Fanyeji vitu vya uhakika, hapa inaonyesha dhahiri mna matarajio ya kupeleka mikweche Tz, hii ni kiboko yenu. Hiyo kampuni keep it up, waTanzania tutawa support.

    cheers

    ReplyDelete
  13. AnonymousMay 31, 2007

    Hamjiulizi kwa nini watoto wa wanasiasa na watu wa serikalini ndio hao hao wana kimbilia kuwania uongozi mbalimbali katika nchi kupitia vyama?

    Ni kwavile walivyoukua waliona baba zao wanatengenea good and easy money kwa kusema tu "Kidumu chama cha mapinduzi". Akitembelea kiwanda cha sukari ana gunia la sukari, akienda kiwanda cha mafuta ameondoka na debe la mafuta, akitembelea wafanya bishara ndio hivyo tena .....

    ReplyDelete
  14. AnonymousMay 31, 2007

    Mimi kama mdau wa biashara ya magari hapa UK london kwa miaka 10 nasikitishwa sana na uamuzi huo kwamfano ukiingiza gari hapa UK kutoka popote duniani inabidi ipasi MOT ndio isajiliwe hapa kama ni muhimu si basi wakafanyie hapo hapo Tanzania
    Halafu hiyo test wanayofanya ni standard ipi
    ikiwa bei ya MOT ni £35 sasa hi cost yao inatoka wapi if consumer XXXXxXXXXx

    ReplyDelete
  15. AnonymousMay 31, 2007

    Hii bwana ni kilaji cha ulaini sana TBS kama ni kiwango basi si wa improve clearance pale bandarini

    ReplyDelete
  16. AnonymousMay 31, 2007

    Kama mtanzania anyeishi hapa Uingereza suala hili naliona kama mwanzo wa ngoma...huyu ndugu Said Yakubu na mwenyekiti wa jumuia ya watanzania wanajuana kwa muda mrefu na wote ni viongozi au wajumbe ndani ya jumuiya!?

    Sikwenda kwenye uchaguzi wao kwani nilijua yote ni danganya toto hawawalishaamua nani awe nani na sisi tuweke muhuri tu.

    Sasa wanavaana wenyewe kwa wenyewe, niliona wakati JK alivyokuwa hapa watu wanavyojipendekeza kwake, mimi mtoto wa fulani, watu hawaangalii maslahi ya Taifa hata kidogo na TBS nao wanatia shaka.

    Huyo anayejiita mwenyekiti wa jumuiya na ajibu hizi tuhuma hapa michuzi blog kwani hii ni blog maarufu kabisa kwa watanzania wa nje.

    ReplyDelete
  17. AnonymousMay 31, 2007

    uchaguzi umekwisha watanzania wameshamchaGUA KIONGOZI WAO SIASA ZAKO ZA MZEE MADEVU HAZITA KUAPATIA UENYEKITI KAMWE

    ReplyDelete
  18. AnonymousMay 31, 2007

    UCHAGUZI UMEKWISHA NA WEWE ULISHINDWA KIDEMOKRASI SASA UMEANZA SIASA ZA MZEE MADEVU WATANZANIA TUMEMCHAGUA MWENYEKITI NA TUNA SUBURI TAMKO LAKE

    ReplyDelete
  19. AnonymousMay 31, 2007

    Mimi sioni kama kuwa na share au kumegewa mkate kuna hali ya utata kuwa mwenyekiti haina maana usifanye biashara mbona kule bongo mawaziri siku hizi wanakuwa wakurugenzi wa makampuni yao binafsi we need to change and focus badala ya kupondana pondana Tena sisi watanzania tumekalia majungu tu yaani hamna mshikamano wala nini kila mtu kivyake ukifanya kitu badala ya kupata saport utashambuliwa mpaka ukome ni lini tutabadilika na kuwa kitu kimoja? kinaeleweka kwamba Tanzania sasa imekuwa ya kurithishana mzee yuko sehemu nyeti basi anawapasia watoto wake hata miradi hivyo hivyo watu wanpeana kijamaa na kindugu Mzee wetu Nyerere akifufuka leo atalia na kuomba arudi huko huko kwenye amani ya milele.Kwa hawa jamaa zetu kama watakagua na dar gari yangu isikaguliwe tena hamna maneno ila kama ndio hapa na kule basi mimi nitasafirisha moja kwa moja wala sipitii kwao kwani hata dar watacheki ya n ini kuhangaika.

    ReplyDelete
  20. AnonymousMay 31, 2007

    Bora umeongea ukweli bro. Uk kumejaa majungu sana,hata huo umoja sijui, maana kila mtu anaongea lake kuhusu huu umoja, bora tubaki na viumoja vyetu vya mitaani, kazi kubwa ya umoja ni kuandaa Party tuuuuuuuu

    ReplyDelete
  21. AnonymousJune 01, 2007

    ACHENI KABISA KUTUUMIZA ICHWA KWA KUWEKA MASWALA BINAFSI YA HUKO UK. JAPO MNATAKA KUJIFANYA YANATUHUSU WOTE KWA STYLE YA PROPAGANDA. UKISOMA KWA MAKINI UJUMBE ULIOWEKWA JUU YA MALALAMIKO KWA MWENYEKITI WENU HUYO, UNAGUNDUA KUWA, ALIYEANDIKA ANA UGOMVI BINAFSI NA HUYO MWENYEKITI. SASA KATAFUTA UFA WA KUTOLEA KINYONGO CHAKE. WEWE UNAYEJIITA MJUMBE KATIKA UMOJA WA WATZ WA UK. UNASHINDWAJE KULIONGELEA HILI SWALA KATIKA VIKAO VYENU AU KUTUMA UJUMBE KWA NJIA YA BARUA PEPE KWA WATANZANIA WA UK KWANZA KABLA YA KUTUTUMIA WOTE KATIKA WEBSITE HII?????

    WEWE MNAFIKI MKUBWA. UNAJIFANYA ETI UMETUMA NAKALA KWA WATANZANIA WOTE WAISHIO UINGEREZA. ACHA KABISA KUFANYA WEWE NI EVERYTHING. HIVI UNAWEZAJE KUTUMA NAKALA KWA WATANZANIA WOTE WAISHIO UK KAMA SI KUJITAFUTIA UMAARUFU TU. MIMI NAISHI HAPA UK NA SI MWANACHAMA WA HUO UMOJA. CHA AJABU UNAZUNGUMZA AS IF WOTE TUMO KWENYE HUO UMOJA WENU MNAOGOMBANIA MASLAHI. ACHENI MAJUNGU NA FANYENI KAZI, OK?

    mk

    ReplyDelete
  22. AnonymousJune 01, 2007

    hIVI NA MIMI NILIOPO HUKU glasgow INABIDI NIPELEKE gari lANGU LIKATAZAMWE huko DAGENHAM kisha basi,

    Hii ni rushwa na najiuliza MAREHEMU alitoa kiasi gani mpaka hili dili likapitishwa

    TUNAOMBA SERIKALI ILIINGILE HILI

    sawa na Mwendazimu mmoja akisaidiwa na weendawazimu wengine kule TBS waamue kuwa GARI ZOTE TOKA USA lazima zikaguliwe SEATTLE regardless majimbo gani, kisha kila mmoja alipe DOLA MIAMBILI japo hizo gari zishapita kila sehemu kuwa ni safi na vyeti vyote vipo

    Mbona tunatafutiana Ubaya? mambo ya watu kutaka kushushwa MABUSHA haya

    ReplyDelete
  23. AnonymousJune 01, 2007

    WEZI WEZI WEZI WEZI WEZI HAOOOOOOOOOOOOOOOOOO KUANZIA KILA KITU NI WEZI WEZI TUMEWASHITUKIA AFADHALI UMMETOA HII HABARI YAANI HAIBU ETI NINI?! WANATOA HABARI KATIKA TOVUTI ZAO ILI KUFICHA UOZO WAO TZUK NI WEZI NA MWENYEKITI + TBS WOTE WEZI.

    TUNAWATAKA WATOE KAULI ZAO LA SIVYO JAMAA HAACHIE NGAZI NA ALIYE HUSIKA TBS PIA HAACHIE NGAZI.

    RUSHWA NA WIZI KUANZIA TANZANIA MPAKA UK HII HAIBU HAPO NDIO UAMINI YAANI TUKIJA KUBADILISHA NCHI KATI YA UK NA TANZANIA STILL TUTAKUWA MASIKINI ATA KAMA TUKIAMIA UK KUTOKANA NA WIZI WA WA WATANZANIA KAMA HAWA NA TBS.

    HAIBU MKILALA NA KUAMKA MUONE HAIBU NA WIZI WENU. RUSHWAAAAAAAAAAAAA, WEZI HAAAAAAAOOOOOOOO.

    MTANZANIA MWENYE UCHUNGU.

    ReplyDelete
  24. Kitendo cha kitendo cha Shirika la Ubora wa Viwango Tanzania (TBS) kutangaza (?) kwamba magari yote yanayoingizwa Tanzania toka Uingereza (kwanini Uingereza tu?) lazma yakaguliwe na kampuni waliyoichagua kinatia shaka sana.Kinaniacha na maswali mengi ya kujiuliza.

    (1) Magari yatayoingizwa Tanzania toka nchi nyingine (za dunia hii) ambazo hazipungui 200 yatakaguliwa wapi na nani na tangu lini?

    (2) Magari yatayoingizwa Tanzania na watu ambao sio watanzania (kutokea Uingereza) nayo yatapitia ktk ukaguzi wa kampuni twaja? Kama hapana: kwanini? sasa huo utakuwa ukaguzi wa magari au wa watu (watanzania v. wasio watanzania)?

    (3) Serikali ya Tanzania haikubaliani/hairidhishwi na ubora/umuhimu wa ukaguzi unaofanywa na serikali ya Uingereza kwa magari yaliyo Uingereza? Imeshawahi kutoa tamko la namna hiyo? Kwanini?

    (4) Kwanini serikali ya Tanzania isiweke kitengo/kituo/kampuni ya kukagua magari yote yaingizwayo toka nje ya nchi ktk ardhi ya Tanzania yenyewe?

    (5)Serikali haioni kuwa kitendo hiki ni uvunjaji wa ibara ya 13 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inatamka kwamba "watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria" (ibara ya 13(1))?

    Kwanini kunakuwa na double standards ktk sula hili la ukaguzi wa magari (ya watanzania kutoka Uingereza v. ya watanzania kutoka nchi nyingine duniani)?

    (6) Je, hiyo kampuni ilishinda zabuni kihalali? Ilitangazwa lini hiyo zabuni na ktk media gani? Kampuni ngapi ziliomba? Hii kampuni italipa mrahaba/kodi/ushuru serikalini wa pauni (kwasababu 'watakuwa wanapata pauni' huku Uingereza) ngapi/asilimia ngapi? Hiyo ni zabuni ya muda gani?

    Nina maswali mengi sana,sana ila nawaachia wenzangu nao maana najua wanayo kwa maelfu pia.Nitarudi tena Inshaallah.

    Ahsante Michuzi!

    ReplyDelete
  25. AnonymousJune 01, 2007

    Mimi siishi UK, lakini niko nje ya nchi kama WaTanzania wengine walio nje ya nchi. nimejitahidi kufuatilia swala zima la ukaguzi wa magari na bahati nzuri nimekuja kwenye blog hii na kukuta ujumbe huu wa kumlaumu mwenyekiti wa Jumuiya hii ya WaTz wa UK.

    Kwa kweli swala la mwenyekiti, nafiki ndugu Saidi ujaribu kulipeleka katika kamati yenu huko mjadiliane kuhusu msimamo wa mwenyekiti wenu hasa kuhusu msimamo wake juu ya swala hili la ukaguzi wa magari.

    Jambo la msingi ninaloliona hapa, ni swala zima la TBS kuamua kuipa kampuni ya nje ulaji wa kiuwazi kabisa. Mimi kwa akili yangu ndogo ninafikiri kwamba, kwa nchi changa kama Tanzania, TBS ingeweza kabisa kuweka viwango vinavyotakiwa kwa magari mapya yaingizwayo Tanzania. Halafu ingechagua kampuni pale Tanzania ya kukagua magari yanayoingizwa kwa kufuata viwango ilivyoweka. Magari yasiyotimiza viwango hivyo yasisajiliwe kabisa, kwa hiyo hasara ni kwa mletaji.

    Lakini pia, TBS ingechukua jukumu la kuwataarifa wananchi ndani na nje ya nchi, kwamba sasa hivi magari yote yanayoingia Tanzania lazima yatimize viwango hivi vilivyowekwa.

    Ninasema hivyo kwa sababu, kwanza, pesa inayoachwa UK sasa hivi ingeingizwa Tanzania na kusaidia kuendeleza nchi badala ya kuziacha zibaki UK.

    Pili hiyo au hizo kampuni za ukaguzi Tanzania zingesaidia kuongeza ajira kwa watu, badala ya kusaidia UK kupunguza unemployment problem zao.

    Halafu, magari yanatoka sehemu mbali mbali, ina maana TBS watachagua makampuni kila nchi ili kukagua magari yatokayo huko kwenda Tanzania? Kwa nini wasiwe na central location ya kukagua magari yote yaingiayo Tz badala ya kutafuta taabu ya kupitisha tender kila nchi.

    Nafikiri WaTanzania wengi sasa hivi tuna kaelimu fulani ka kutuwezesha kupambanua mambo, na tukatumie basi ili kuendelea kanchi ketu, tamaa za kibinafsi hazitatufikisha popote. Hakuna mtu aliyekufa na kuondoka na pesa hata kama zilikuwa ngapi. Na tufanye kitu cha kusaidia kanchi ketu, vinginevyo tutajikuta tegemezi wa nchi zilizoendelea mpaka mwisho wa dunia.

    Nisameheni kwa mawazo mafupi.

    Asante

    ReplyDelete
  26. AnonymousJune 01, 2007

    waTZ tulio nje tunapenda sana kuluumbana esp cc wa USA na UK watoto wa dallas huku kazi kupigana mashuti kutukanana ukiwa na hichi we malaya kama mwanamke kama mwanaume jambazi au drug dealer na ktk hivi vikundi ndo kabisaa vyama vimejaa chuki ubinafsi na watu kujitaftia umaarufu kama hawa wapuuzi wanavotuletea pumba zao hapa! TUMECHOKA NA WIZI WENUUU mambo yenu binafsi myatatue wenyewe na hivo vyama vyenu watu tutaacha kuhudhuria manake hamna chochote hamuoni wanigeria wakenya wanavopendana?????si tunakuwa utafkiri sio watu wa taifa moja????mpaka tunaona bora kujichanganya na wa niger...mmezidi!

    ReplyDelete
  27. AnonymousJune 01, 2007

    mimi lawama zangu nazielekeza kwako wewe michuzi na mapaparazi wenzio wote wa hapa Bongo. Juzi nimeona tangazo katika local paper kuhusu kuhusu huu ukaguzi. kwa maoni ya wengi inaonekana huu ni wizi wa mchana. kama hivyo ndivyo ilivyo na kwa kuzingatia kwamba media ndo watchdog yetu kwanini wanahabari wa hapa nyumbani Tanzania suala hili sijasikia mmelishikia bango,au mpaka amina chifupa afumaniwe ndo mmpate la kuandika?

    ReplyDelete
  28. AnonymousJune 01, 2007

    kwasababu muda wangu aunitoshi naenda kazini nitatoa hoja yangu baadae kwa ajili ya huyo MLAFI

    ReplyDelete
  29. AnonymousJune 01, 2007

    KUNA MIJITU VERY SELFISH HAPO JUU ETI HIZI NI ISSUE PERSONAL ZA UK HIVYO TUWEKEANE KIKAO HAPA.... HIVI MNATUMIA AKILI NYIE AU MNAONGEA ONGEA TUU KAMA WAJINGA...!! HII GLOB YA MICHUZI KWANZA NI BINAFSI PILI NI CHOMBO AMBACHO KINA SOMWA NA WATANZANIA WALIO WENGI HIVYO NI MAHALI AMBAPO ISSUE KAMA HII NA NYINGINEZO ZIKITOKEA ZINAPATA KUCHAMBULIWA IPASAVYO. MBONA HUKULALAMIKA KUHUSU WANAFUNZI WA RUSIA.. MBONA WATU WANATOA MATANGAZO YA MISIBA FROM KONA KIBAO, SIJUI MICHANGO NK .... PUMBAFU KABISA WEWE TUMIA AKILI SIO KUKURUPUKA NA KUANZA KUROPOKA ROPOKA AU NA WEWE UNAHUSIKA KATIKA HILI SAKATA HIVYO HUTAKI LIMWAGE HADHARANI??????????

    MICHUZI WEYE KILA MTU AKIKUANDIKIA ISSUE INAYOGUSA JAMII NA KUKUOMBA UIWEKE HADHARANI WE TUMWAGIE TUU MWANANGU.. KWANZA HATA HIVYO VIKAO VIKIWEKWA WENGINE HATUTAWEZA KWENDA KUTOKANA NA KUWA NJE YA LONDON NA MAJUKUMU MENGINE YA KUTAFUTA UNGA WA WATOTO...!!

    NAWAKILISHA

    ReplyDelete
  30. AnonymousJune 01, 2007

    Anoy 3.26 am either una akili ndogo sana au umelambwa ubongo na cobra. Issue hapa ni TBS na contract zake za kijinga.

    Si ajabu huna hata hela ya kupelega gari bongo ndio maana you don't care.

    Kama nigers ni wazuri kaa nao wazidi kukuchukulia kila kisenti unachokokoeza kwenye mabox huko TX. Like if we don't know them.

    Siku ukifa tusije tukasikia unaomba michango kwa watanzania, uwaambie hao niger wakuzike wako pumbafu sana wewe.

    ReplyDelete
  31. AnonymousJune 01, 2007

    Haya hao majimambo, mimi namshukuru Said Yakubu kutoa hii news, maaana hata siye tusioishi Uingereza tusingejua kuna kipi kinaendelea. Chanzo cha migogoro yote hii ni ukiritimba na masuala ya TEN pasenti, hakuna lolote. WaTZ muishio UK inabidi muwe macho maana kuna watu wanataka kuwapanda kwenye migongo yenu.

    GAZ

    ReplyDelete
  32. AnonymousJune 01, 2007

    ZAIDI YA HAYO KUNA HABRI KUWA CHAM CHA KIBAGUZI CHA BNP nacho kimeeingilia hili

    http://www.jamboforums.com/showthread.php?t=3079

    Ama kweli wana JAMBOFORUMS hamuna
    dogo,laini hii yote ni changamoto kwetu sisi wenyewe na naamini hata waheshimiwa huko serikalini wanaona na wanasoma hizo blogs

    Sme hiyo ya kushushana MABUSHA hiyo nadhani anon hapo juu anajua walengwa ni akina nani

    ReplyDelete
  33. AnonymousJune 01, 2007

    Kwanza Bro michu hana kosa hapa we anon uliyesema waandishi hawalivalii njuga hili swala, pili kwa taarifa yako tuna waandishi wachache Sana wenye ujuzi kule TZ kama unakumbuka MH mstaafa Mzee MKAPA alishawahi kuwaambia waandishi hawajui hata kuuliza maswali si siri kweli kabisa hawajui kufanya habari za uchunguzi na utafiti wa kina ukitaka kujua walivyo filisika kimawazo na kiuwezo wewe angalia vyombo vya habri kuanzia program za tv, radio na magazeti mengi yaandikwayo hau kutangazwa kila siku ni cheap story ambazo hazina hata msisimko. Ingekuwa wenzetu wa huku tayari walisha wavalia njuga hao TBS kwa kautafiti kangu kadogo inaonyesha mtu wa TBS na hawa jamaa wa uk wote jamaa zetu wa kule Bukoba sasa wategemea nini kama si kubebana, Ni kweli kwa jinsi wanavyokagua magari hapa UK hata kule Bongo hamna kitu na si rahisi kupeleka gari bovu na wote wanaorudi bongo si wajinga ni wasomi ambao wanafahamu ubora wa gari hawa jamaa waache kutufanya sisi watoto wadogo tunaelewa hako kamchezo kao kakijinga. Haya mambo ya jumuia ya watanzania ni ujinga jinga tu mtupu maana ni maugomvi kila siku humu watu hawaongei wao kwa wao na uwezo wa kufikiria mdogo ninachojua watu wanatumia nafasi hiyo kujitangaza kwa ajili ya kwenda kutafutia uongozi Bongo sasa nawaambia Bongo vipo vichwa si mchezo watu wameamka kule msije mkatoka na ushamba wenu wa ula kwenda kujifanya wajuaji kule mtaadhirika. Watanzania Mshikamano ni mwiko wivu umetujaa na hii inatokana na ulimbukeni na kutokwenda shule wengi wa hapo uk tunajua hamna hata vyeti vya kuoimbea kazi ya kufagia ofisini mmekaa miaka kibao kazi maboxi na pesa hamna sasa mnataka kupiga bao dakika za majeruhi sahauni kabisa tena mkome na huo upuuzi wenu. Ningefurahi kama huyu jama wa TBS angepunguzwa kazi maana hawa ndio wanturudisha nyuma.
    Nwakilisha kaka michu and keep it up

    ReplyDelete
  34. AnonymousJune 01, 2007

    anoy 7.57 mbona hueleweki...nasoma hata sikuelewi ulikua unatka kueleza nini. wew e unasema wenzako hawanavyeti lakini wanajua write and wrong wew sijui unasema nini na vyeti vyako

    ReplyDelete
  35. AnonymousJune 02, 2007

    Hawa TBS wangesema kuwa kila gari linalotoka UK liwe na MOT certificate mpya au ambayo sio zaidi ya 3 months old tangu itolewe.Hatuwezi kuwa na inspections 100 za gari moja.

    Ni ujinga ule ule wa kuweka bei ya visa kuwa ni £50.00 kwa UK, $50.00 kwa US, €50.00 kwa EU kama vile hizi pesa zote ni sawa value yake. Hakuna aliyeuliza, na watu wakalipa. Kwa watanzania walivyo watakubali tu!! Tutawaona!!!

    ReplyDelete
  36. AnonymousJune 02, 2007

    The rich get richer and the poor get children

    ReplyDelete
  37. AnonymousJune 03, 2007

    Mimi yakubu umenifurahisha sana zile zama za kuoneana haya zimepitwa na wakati. Kama mtu amekosea ni vema kumkosoa hadharani, watanzania wengi ni waoga sana sijui kwa nini tunapenda kuogopana. Umenifurahisha zaidi ulivyoweka jina lako, safi sana!!! Kuna mtu hapo juu ameongelea wakenya na wanigeria, wakenya sio waoga kama wa-tz wenzangu wangekuwa wao wasingekubali huu upuuzi wa TBS. Na huyu mwenyekiti hafai kabisa maana anatumia nafasi yake kuendeleza tzuk.

    ReplyDelete
  38. AnonymousJune 03, 2007

    Watanzania tuache kuwa selfish jamani especially watu wa US kuna mtu kaandika hapo juu kuwa haya mambo ya uk wao hayawahusu, ukiona mwenzio ananyolewa wewe tia maji, leo kwetu kesho kwenu. Ni lazima watanzania wote tulioko abroad tukemee huu ukandamizaji wa hali ya juu.
    Mimi nimeshatuma gari nyumbani before and it was so easy!! Sasa huu ukiritimba ni wa nini? It really is not fair on us!1 Nilikuwa naplan kutuma gari jingine soon lakini nimekatishwa tamaa sana kusikia hili zoezi maana i have just put an mot on my car and have spent alot on it moreover i dont think i will have time to go and do that test naona niahirishe tu kutuma hiyo gari.

    ReplyDelete
  39. AnonymousJune 03, 2007

    Does this mean TBS does not acknowledge the UK standards but trust a dodgy guy instead? All our cars have been tested at proper uk garages through a computer system does it mean that this guy have better equipments than the ones found at uk garages???
    Michuzi naomba nikuulize je yale matakataka yanayotoka Dubai na Japan yanachekiwa wapi, na nani? Maana migari yote inayotoka Japan ni uozo mtupu utakuta nyingi zina mileage 100,000 na kuendelea wakazi hizi za Uk nyingi zina mileage ndogo na pia ziko katika hali nzuri sana. Huu ni wizi na uonevu mkubwa sana kwa kweli.

    ReplyDelete
  40. AnonymousJune 03, 2007

    Habari Bro michuzi, mimi ninahitaji kujua je hii kampuni inaruhusiwa kufanya hili zoezi hapa UK? Na je wana yard ya kutosha ku-accomodate magari yote yanayotaka kutumwa? Mimi nataka kuwasiliana na Trading standards ya hapa kujua kama wameapprove hii business.
    Kuna mahali nimesoma kuwa hii company itakuwa mobile je wakija kufanya hii inspection nje ya nyumba yangu si tutaitiwa police? Maana nakaa jirani na vibibi vya kizungu vinoko sana!! And what do they really inspect?
    Kwa nini TBS wasilifanyie hili zoezi hukohuko bongo ama ndio mambo ya ulaji? Huu ni wizi mkubwa sana.It will be a very good idea if this is done in tz because people will not send old cars and incurr so many expenses and when it gets there to be told its not road worthy.

    ReplyDelete
  41. AnonymousJune 03, 2007

    It takes a real man to do what you have done Yakubu, well done we need guys like you in our society.

    ReplyDelete
  42. AnonymousJune 03, 2007

    Hiki chama walichaguana watu wachache wakajipanga nani awe nani, hakinisaidii chochote mimi mtanzania niishie uk!! Wanatumia majina yetu kwa manufaa yao hakuna wanachotusaidia. Sasa kama kuna website ya umoja kwa nini mwenyekiti anaweka tangazo linalohusu chama kwenye website yake binafsi? Wanataka kujijengea cv ili wakirudi bongo wakatafutie ubunge na vyeo vingine.
    Tumewagundua.

    ReplyDelete
  43. AnonymousJune 04, 2007

    Jamani wadau wapendwa, leo hii tumejaribu kuinvestigate hii address na hii WTM utility company kama iko Dagenham kama wanavyodai kwenye tovotu yao.

    Lakini tulivyojaribu kuisearch na kuigoggle kwenye Google Earth, nimeambukia kwamba hii Maybells Commercial Estate iko Barking, kwenye main road ya Ripple Road, kama inavyoonyesha hapo kwenye ramani,

    Tumejaribu kufuatilia kwa kupiga simu hiyo KAmpuni One Call Furniture ambao wao wako Unit 1 Maybells Commercial Estate, na WTM utility wako Unit 1a Maybells Commercial Estate, lakini kutokana na maeleozo ya mfanyakazi wa One Call Furniture ambae ufahamu ni jirani tu na WTM Utility anadai hafahamu kuwepo kwa WTM Utility katika Commercial State hiyo.

    Je WTM watakua wamekosea address yao, au wako sehemu tofauti kabisa na hiyo Maybells Commercial Estate, kama wanavyodai kwenye tovotu yao.

    http://www.wtmutilityservices.com/index.php?option=com_contact&ta

    Zaidi pitia blog hii, kwa maelezo zaidi
    http://tbswtmuncovered.blogspot.com/

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...