mh. dk. asha-rose migiro akitoka bungeni na manaibu wake baada ya kuwasilisha bajeti ya wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa jana naiti


Pssst...jana mshikaji wetu ameniletea nyuzi hii...



Tanzania Lawamani…



28/07/2006




Na Pascal Mayalla-Mutukula

Maofisa wa taasisi mbalimbali za Serikali waliopo eneo la Mtukula, mpakani kati ya Tanzania na Uganda washutumiwa kwa tuhuma za unyanyasaji na ukiukwaji wa haki za binadamu na kwa baadhi ya raia wa Tanzania kwa kuwafukuza nchini na kudai kuwa sio raia bila sababu za msingi.

Shutuma zimetolewa na Bi Ndasoro Haule (Asiye na Uraia) wa eneo hilo la mpakani katika Mkutano wa Hadhara wa Kamati ya Biashara, Uwekezaji na Mawasiliano ya Bunge la Afrika Mashariki, katika ziara ya kamati hiyo kutembelea vituo vya ushuru wa forodha vya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, kutathmini utekelezaji wa Ushuru wa Pamoja ulioanza mwezi Januari, 2005.

Akielezea mkasa wake, Ndasoro Haule ambaye alizaliwa Tanzania na mama wa Kitanzania lakini Baba wa Kiganda aliyemtelekeza yeye na mama yake, hivyo akakulia Tanzania na kuolewa na Mtanzania Joseph Haule (Siyo Profesa J-ambaye nae ni Joseph Haule) lakini ametimuliwa nchini kwa hati ya PI na kuelezwa sio raia.

Akielezea mkasa huo, huku akilengwa lengwa na machozi, Bibi Haule ameieleza kamati hiyo, chanzo cha matatizo yeke ni kisa kilichotokea Januari 2004 baada ya mtoto wake wa kiume kujihusisha na uhusiano wa mapenzi na mwanamke fulani bila kujua kuwa mwanamke huyo ni Bibi wa ofisa mmoja wa Idara ya Uhamiaji (jina tunalo) na ndipo ofisa huyo alipokwenda nyumbani kwake na kutoa vitisho vya “ watakiona cha mtema kuni.”

Aliendelea kueleza kuwa siku 4 baada ya tukio hiyo, alifuatwa nyumbani na Difenda ya Polisi, akapelekwa kituo cha polisi cha Rusumo, ambako alisachiwa kila sehemu za mwili wake na askari wa kiume na baada ya hapo, alitiwa ndani na mwanae na kutakiwa kusaini karatasi ambayo hakujua imeandikwa nini kutokana na yeye kutojua kusoma wala kuandika.

Anasema alisita kusaini na kuomba kwanza aelezwe karatasi hiyo imeandikwa nini, anasema kilichofuatia hapo na kipigo toka maofisa wa polisi, hali iliyopelekea kukubali kusaini hiyo karatasi na kesho yake yeye na mwanae walichukuliwa na gari ya polisi wa Tanzania na kukabidhiwa kituo cha polisi cha Uganda eneo la Mutukula na ndipo alipoeleza kuwa hati aliyosaini ni PI na kuelezwa kuwa yeye ni mtu asiyetakiwa Tanzania kwa sababu siyo raia.

Uganda nako walishindwa kumpokea kufuatia kutomjua ndugu yake yoyote wa baba yake na hivyo kumuhesabu kama Mtanzania, kwa kuzaliwa na hata kwa kuolewa na vyeti vyote kuanzia cha ndoa na vya kuzaliwa watoto vinaonyesha wote ni Watanzania lakini juhudi zote za kueleza kuwa anafanyiwa visa, hazikuza matunda.

Ndipo mume wake, Mzee, Joseph Haule, alipolivalia njuga suala la mke wake kwa kulifikisha ngazi za juu serikalini ikiwemo mpaka kuja Dar es Salaam kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ambapo ombi lake lilikataliwa kwa sababu ambazo hazikuelezwa.

Amemalizia kueleza kuwa mpaka sasa, anaishi eneo la Uganda akiwa hana uraia wa nchi yoyote na hivyo kuwaomba waheshimiwa wa Bunge la Afrika Mashariki, wakifikishe kilio chake na cha cha mamia wengine ambao hawajapata pa kusemea na kusisitiza ni raia halali wa kuzaliwa na kuolewa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Biashara, Uwekezaji na Mawasiliano ya Bunge la Afrika Mashariki, Mhe. George Nangale, (Tanzania) ,amesema, ingawa mkasa huo, sio madhumuni ya ziara yao, lakini kutokana na uzito wa shutuma na tuhuma mbalimbali za unyanyasaji zinazodaiwa kufanywa na maofisa wa Forodha, Uhamiaji na Polisi, wao watayafikisha malalamiko hayo katika ngazi zinazohusika ili yafanyiwe kazi.

Kisa kama hicho, pia kimewahi kumkumba aliyekuwa Mwenyekiti wa Habari Corparation, Jenerali Ulimwengu, ambaye alinyan’ganywa uraia wa Tanzania na kujikuta ni mtu asiye na uraia wowote kabla ya kurejeshewa uraia wake.

Sheria za Tanzania, zinatoa mamlaka ya kisheria na kumnyan’ganya uraia mtu yoyote ambaye uraia wake unatiliwa mashaka kwa kumpa hati ya P.I (Personal Non Granta-mtu siyetakiwa) ambapo hufuatiwa na mtu huyo kusindikizwa chini ya ulinzi mkali mpaka mpakani mwa nchi yoyote atakaichagua.

Sheria hiyo ya P.I. inatoa mamlaka kwa Serikali kutoa hati hiyo ama na kutoa sababu za kufukuzwa nchini ama bila kutoa sababu za kufukuzwa nchini ambapo ni Mahakama Kuu tuu nchini, yenye uwezo wa kuzuia utekelezaji wa P.I. Sheria hiyo ya P.I ni miongoni mwa Sheria 40 za Ukandamizaji, ambazo Tume ya Nyalali alipendekezwa zifutwe na kwa upande wa P.I. serikali ilizimishwe kutoa sababu za kutoa P.I.

Ziara hiyo ya Kamati ya Biashara, Uwekezaji na Mawasiliano ya Bunge la Afrika Mashariki, iliyodhaminiwa na Shirika la Frriedrich Ebert Stiftung, kesho inaingia siku yake ya 10 kwa kutembelea mpaka ya Tanzania na Kenya, eneo la Namanga.-End. Hii Story ina picha.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 31, 2006

    hivi jamani unyanyasaji tanzania utaisha lini?kuna wakimbizi waliingia tanzania tangu miaka ya 1965 na 70,na wengi tumekua nao tumesoma nao tulikua nao jkt,na tukawa nao maofisini na hata leo ndo waalimu na manesi,sasa ni miaka 40 kama si 35,na bado serikali ya tanzania haiwatambui na wala haitaki kuwatambua kama watanzania,kwa nini serikali isiwape tu uraia?kama ndugu zetu nchi zilizoendelea,watu wameamua kuwa wasomali na warundi nasiwanyamwezi tena,na baada ya miaka mitatu wanawapa uraia??

    ReplyDelete
  2. Habari za siku nyingi Mr. P Mayalla?
    Ndugu yangu Michael Mapalala hajambo?
    Salaam nyngi saana kutoka kwangu John Rupia hapa Boston.
    Endellea na kazi njema.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...