Wafuasi wa Felix Tshisekedi awali walikusanyika nje ya makao makuu ya chama chake Limete, Kinshasa Jumatano


Felix Tshisekedi ameshinda uchaguzi wa urais nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, tume ya uchaguzi imesema.

Matokeo ya awali yanaonyesha mgombea huyo wa upinzani amemshinda mgombea mwingine wa upinzani Martin Fayulu, pamoja na mgombea aliyekuwa anaungwa mkono na serikali Emmanuel Shadary.

Mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Ceni) Corneille Nangaa, alisema mapema Alhamisi kwamba Bw Tshisekedi alipata asilimia 38.57 ya kura zilizopigwa na "anatangazwa mshindi wa urais mteule."

Tshisekedi alipata zaidi ya kura 7 milioni naye bw Fayulu akapata kura takriban 6.4 milioni, huku mgombea wa serikali Emmanuel Ramazani Shadary akipata takriban kura 4.4 milioni.

Iwapo matokeo hayo yatathibitishwa, Bw Tshisekedi atakuwa mgombea wa kwanza kabisa wa upinzani kushinda uchaguzi wa urais tangu DRC ilipojipatia uhuru.

Bw Tshisekedi yuko kwenye muungano wa kisiasa aliyekuwa mgombea wa chama cha UNC (Union for the Congolese Nation) Vital Kamerhe UNC ambapo walikuwa wamekubaliana kwamba Tshiskedi atagombea wadhifa wa rais naye Kamerhe awe waziri mkuu iwapo muungano wao utashinda urais.

Rais Joseph Kabila anatarajiwa kuondoka madarakani baada ya kuongoza kwa miaka 18.Mgombea wake aliyemteua kuwakilisha muungano tawala Emmanuel Ramazani Shadary amemaliza wa tatu.

Martin Fayulu ambaye awali alikuwa mgombea wa pamoja wa muungano wa upinzani kabla ya Tshisekedi na mgombea wa chama cha UNC (Union for the Congolese Nation) Vital Kamerhe kujiondoa kutoka kwenye muungano huo na kuunda muungano wao wawili, alimaliza akiwa nafasi ya pili.

CHANZO BBC Swahili.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...