Mwenyekiti wa
Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Mbeya, Leonard Manyesha (aliyesimama),
akiongea wakati wa Mkutano wa viongozi wa wachimbaji wa madini ya
dhahabu Wilaya ya Chunya na viongozi kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia
Mkuu wa Serikali ambao ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi na Mkemia
Mkuu wa Serikali (hawapo pichani).
Mkemia Mkuu wa
Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko (aliyesimama), akiongea na viongozi hao
wa wachimbaji wa madini ya dhahabu Wilaya ya Chunya (hawapo Pichani)
katika Mkutano huo uliofanyika wilayani Chunya.
Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa
Esther Hellen Jason (wa pili kulia) akiongea na viongozi wa wachimbaji
wa dhahabu katika migodi ya Chunya (hawapo pichani). Mwenyekiti wa Bodi
na Mkemia Mkuu wa Serikali (wa tatu kulia), walikutana na wadau hao kwa
lengo la kuwasikiliza maoni waliyonayo juu ya huduma zinazotolewa na
Mamlaka hiyo
Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi, Profesa Esther Hellen Jason (aliyekaa katikati), Mkemia
Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko (wa pili kushoto), wakiwa
pamoja na Mwenyekiti wa Wachimbaji wa Dhahabu Mkoa wa Mbeya, Leonard
Manyesha (wa pili kulia), Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia
Mkuu wa Serikali, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Gaspar Mushi (kulia) na
viongozi wengine wa wachimbaji na wamiliki migodi ya dhahabu iliyopo
katika Wilaya ya Chunya.
*****************************
Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof.
Esther Hellen Jason amewataka wachimbaji wa madini ya dhahabu wa Chunya
kuzingatia matumizi salama ya kemikali wanazozitumia katika shughuli zao
za uchimbaji kwa lengo la kulinda afya na mazingira.
Prof. Esther Hellen Jason ameyasema hayo wilayani Chunya wakati
akiongea na viongozi wa wachimbaji na wamiliki wa migodi ya madini ya
dhahabu.
“Ndugu zangu tuzingatie matumizi salama ya kemikali kwa lengo la
kulinda mazingira, afya zetu na vizazi vyetu, tunatambua sekta ya
madini ni moja ya sekta muhimu sana katika kukuza uchumi wa nchi kwa
sababu dhahabu inaingiza mapato ndani ya Serikali lakini huwezi kuipata
dhahabu bila kutumia baadhi ya kemikali.” Alisema Prof. Jason.
Ameongeza kuwa, kukutana na wadau na kujadiliana namna bora ya
kuimarisha mahusiano ya kikazi ni njia sahihi ya kutatua changamoto na
kuboresha utendaji kazi wa pande zote katika shughuli hizi za uchimbaji
na uchenjuaji wa dhahabu.
Hivyo changamoto zenu
mlizowasilisha leo tunazichukua kwa uzito mkubwa na tutayafanyia kazi
ili kuboresha zaidi utendaji wetu na shughuli zenu.
“Kwa zile zilizo ndani ya
uwezo wa Bodi ya Wakurugenzi tutazifanyia kazi kwa lengo la kurahisisha
utendaji wenu na zinayohitaji maamuzi ya juu zaidi tutayawasilisha ili
kupatiwa ufumbuzi maana zikitatuliwa changamoto hizi tunaamini
hazitakuwa kwa faida ya Chunya tu bali kwa wachimbaji wa Tanzania nzima
wanaotumia kemikali.” Alimalizia
Kwa upande wake, Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice
Mafumiko, alisema mkutano huo ni mwanzo wa ushirikiano wa Mamlaka na
wachimbaji hao wenye lengo la kutatua changamoto na kuzifanya kuwa fursa
za kuboresha utendaji na kuwezesha wadau hao wa Chunya na maeneo
mengine ya migodi nchini.
Akiongea kwa niaba ya wachimbaji, Mwenyekiti wa Wachimbaji wa
dhahabu Mkoa wa Mbeya, Leonard Manyesha, alisema anashukuru kwa mkutano
huo na anaamini mazuri yaliyojadiliwa yataleta tija yakifanyiwa kazi.
“Nimefurahishwa na mkutano huu na naamini tuliyojadili
yakifanyiwa kazi yataleta tija kwenye kazi zetu za uchimbaji wa dhahabu.
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wamekuwa karibu sana
kwetu hasa kwenye mafunzo ya matumizi salama ya kemikali na kutatua
changamoto zetu pale tunapoziwasilisha.” Alisema Manyesha.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...