Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe . Kassim Majaliwa amefanya ufunguzi wa njia ya reli ya Tanga mpaka Moshi / Kilimanjaro katika hafla iliyofanyika mjini Moshi , Kilimanjaro Julai 20, 2019, iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wa vyama pamoja na wa dini.

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amelipongeza Shirika la Reli Tanzania -TRC kwa Kurejesha njia ya Tanga-Moshi ambayo takribani zaidi ya miaka 12 ilikuwa haifanyi kazi. Waziri Mkuu amesema kuwa mafanikio haya ni utekelezaji wa sera ya kitaifa na Mkakati wa Nchi kuinua sekta mbalimbali za kimkakati ili inchi ya Tanzania ifikie Uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Waziri mkuu aliongeza kuwa juhudi na kujitoa kulikofanyika kurejesha njia ya reli kuanzia Dar es Salaam hadi Tanga na kisha kuelekea Moshi ,Kilimanjaro ni uamuzi wa busara uliokuja kwa wakati na unaoshamirisha azima yetu ya kuchochea ukuaji wa uchumi lakini na kuyabadili maisha ya wananchi kupitia huduma bora za usafiri na uchukuzi .

“ Kamwe hatuwezi kufikia hadhi hiyo muhimu kiuchumi bila kuwa na miundombinu imara ikiwemo ya reli “ amesema Mhe. Kassim Majaliwa.

Aidha Waziri Mkuu amebainisha kuwa Tanzania inapakana na nchi zaidi ya tano ambazo zinategemea sana miundombinu ya nchi ya Tanzania ya usafirishaji na uchukuzi ndani ya nchi ili kupitisha bidhaa. Pia aligusia juu ya mradi mkubwa wa kihistoria wa SGR unaoendelea kuanzia Dar es Salaam hadi Mokutopola na kusema kuwa Serikali ya awamu ya tano imewekeza takribani Shilingi Bilioni 7.2 fedha za walipa kodi kutekeleza mradi huo .

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Atashasta Nditiye ameipongeza Serikali ya awamu ya tano kwa kutoa fedha pia amepongeza bodi na uongozi wa Shirika la Reli Tanzania katika ufuatiliaji na utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya ufufuaji wa Shirika na njia mbalimbali za reli zilizokufa kwa miaka mingi hapa nchini. Hata hivyo Naibu Waziri ametoa rai kwa wafanyazi wa Shirika la Reli na watanzania kwa ujumla kuwa walizi wa miundombinu ya reli ambayo ni kichocheo kikubwa cha uchumi wa nchi yetu.

“TRC limepewa dhamana na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kusimamia uhuishaji na utendaji wa shirika pamoja na kuboresha huduma za reli “ amesema Mhe . Nditiye .

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania ndugu Masanja Kungu Kadogosa ametoa Shukrani za dhati kwa Waziri Mkuu kuitikia wito wa ufunguzi wa reli hiyo ya Tanga hadi Moshi / Kilimanjaro ulioambatana na uzinduzi wa safari za treni za mizigo kutoka bandari za Dar es Salaam na Tanga kuelekea Moshi Kilimanjaro. Ndugu Kadogosa aliwapongeza wafanyakazi wa Shirika la Reli kwa uzalendo na juhudi kubwa walizofanya katika mradi wa ufufuaji wa njia ya reli kutoka Tanga hadi Moshi.

“Timu ya kutekeleza mradi huu ilijumuisha wafanyakazi wapatao 525 kutoka TRC , kati ya hao vibarua ni 466, wahandisi 12 na mafundi wa reli na nyanja nyingine 47 “ amesema Ndugu Masanja Kungu Kadogosa.

Hata hivyo Mkurugenzi Mkuu alibainisha kua juhudi za Serikali na kujituma kwa wafanyakazi wa TRC kutafungua fursa mpya katika usafirishaji na uchukuzi katika ukanda wa Kilimanjaro ambapo historia inaonesha 12 iliyopita Shirika lilikuwa na uwezo wa kusafirisha mazao mbalimbali tani elfu 70 kwa mwaka kutoka Tanga, tani Laki moja za mbolea kwa mwaka na maharage mabehewa 144 kwa mwaka.

“ Ningependa kuihakikishia serikali kuwa Shirika la Reli Tanzania litaendelea kusimamia miradi yote ya kuboresha huduma za Shirika, utendaji na miundombinu kwa kasi na ubunifu unaopaswa ili kufikia malengo ya Serikali ya awamu ya tano” alizungumza Mkurugenzi Mkuu.


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza mbele ya Wageni waalikwa mbalimbali (hawapo pichani) wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa treni ya mizigo katika reli ya Kaskazini uliyofanyika katika stesheni ya reli Moshi, Julai 20.2019.
Muonekano wa Treni ya Mizigo iliyozinduliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Wananchi wa Moshi, wakipokea treni ya mizigo kwa furaha kubwa, wakati ikiwasili tokea Tanga, Julai 20.2019.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwapungia mikono wananchi waliyofika kushuhudia uzinduzi wa treni ya mizigo katika reli ya Kaskazini uliyofanyika katika stesheni ya reli Moshi, Julai 20.2019.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...