Charles James, Michuzi TV

UJENZI wa Reli ya Kisasa, ufufuaji wa Shirika la Ndege nchini, usimamizi makini wa ulipaji kodi, elimu bure kuanzia shule ya Msingi hadi kidato cha nne, vituo bora vya afya ni sababu ambazo zinatajwa kuipa ushindi wa kishindo Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi unaokuja wa Serikali za Mitaa.

Hayo yamesemwa na Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Mh Elibariki Kingu wakati akihutubia wananchi waliojitokeza kuupokea Mwenge wa Uhuru katika eneo la Sepuka wilayani Ikungi, Singida.

Mhe Kingu amesema tangu Rais Dk John Magufuli aingie madarakani amefanya mambo makubwa kwa Watanzania wakiwemo wananchi wake wa Singida Magharibi ambapo amepeleka miradi mingi ya maendeleo ndani ya kipindi cha muda mfupi.

Amesema wananchi wa Jimbo lake wamenufaika na miradi ya ujenzi wa Kituo kikubwa cha Afya cha Sepuka kilichozinduliwa jana na Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Mzee Mkongea Ally ambacho kinakwenda kumaliza adha iliyokua ikiwasumbua kwa muda mrefu.

" Sisi watu wa Singida Magharibi na Wilaya ya Ikungi tuna mengi ya kumshukuru Rais Magufuli kwa namna alivyotukarimu, miradi mikubwa ya Afya ukiachilia mbali Kituo hiki cha Sepuka lakini pia tumeshapokea takribani Milioni 500 kwa ajili ya Kituo kingine cha Ihumba.

" Kwenye maji huko ndio usiseme kila Kijiji tumepanga kuhakikisha kinakua na Maji ya kutosha lengo likiwa ni kuakisi kwa vitendo Sera ya Rais Magufuli ya kumtua Mama ndoo, ndio maana tunaanza ujenzi wa miradi 14 ya maji na tayari tumeshanunua mitambo miwili ya Kisasa kwa ajili ya kumaliza changamoto ya maji pia, " amesema Mh Kingu.

Amesema yeye kama Mbunge anaetokana na CCM ni lazima ahakikishe anasimamia Sera ya Elimu bure kwa kuhakikisha anasimamia ujenzi wa vyumba vya madarasa na Hostel ambavyo vyote viko mbioni kukamilika.
Amesema miradi yote hiyo imeweza kutekelezwa kutokana na namna Rais Magufuli anavyosimamia kwa uadilifu ukusanyaji wa kodi za Watanzania ambazo zimekua zikitumika kwenye miradi ya maendeleo.

" Kwa haya makubwa ambayo Rais Magufuli anatutendea njia pekee ya kumpa shukrani zetu ni kuhakikisha tunachagua wenyeviti wa CCM katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hilo ndilo deni letu kwake," amesema Mh Kingu.

Aidha amesema Jumatatu ya Wiki ijayo wanatarajia kupokea Fedha za mfuko wa Jimbo takribani Milioni 46 ambazo zote zitaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.
 Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Mhe Elibariki Kingu (kushoto) akiwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Mzee Mkongea Ally wakati wa ukaguzi wa miradi ya maendeleo wilayani Ikungi, Dodoma.
Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Mh Elibariki Kingu akihutubia wananchi waliojitokeza kuupokea Mwenge wa Uhuru katika eneo la Puma wilayani Ikungi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...