Mwakilishi Msaidizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) nchini Tanzania, Charles Tulahi, amesema walimu na wazazi wana mchango mkubwa katika kutambua na kukuza vipaji vya wanafunzi, akiwahimiza kuendelea kuwaunga mkono watoto ili waweze kutumia uwezo wao kuchangia maendeleo ya taifa.

Akizungumza Oktoba 14, 2026, katika mashindano ya uchoraji yaliyoandaliwa na FAO katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, jijini Tanga, ndani ya maonesho ya Siku ya Chakula Duniani, Tulahi amesema wanafunzi wanapaswa kuendelea kukuza vipaji vyao na kuwa mabalozi wa kuhamasisha ubunifu katika masuala ya chakula na lishe.

Amesema mashindano hayo ni fursa kwa wanafunzi kuonesha uwezo wao na kujifunza umuhimu wa ubunifu katika kuchangia upatikanaji wa chakula na kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050, ameongeza kuwa ubunifu huo unapaswa kuendelea hata baada ya mashindano, ili ujumbe wake uweze kuwafikia watu wengi zaidi nchini.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Muheza na Mgeni rasmi wa Mashindano hayo Ayubu Sebabile, amewahimiza wanafunzi kutumia vipaji vyao kuibua mawazo yatakayosaidia kuimarisha uzalishaji wa chakula nchini na kuchangia azma ya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa uzalishaji wa chakula barani Afrika na duniani.

Sebabile amesema anatarajia wanafunzi kuwasilisha kazi za ubunifu zinazoendana na ujumbe wa mashindano hayo, huku akieleza kuwa washiriki wameandaliwa zawadi na washindi watano watakabidhiwa zawadi maalumu Oktoba 16, 2026, siku ya kilele cha maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani jijini Tanga.

Akizungumzia mashindano hayo msimamizi kutoka FAO amesema yanalenga kuwajengea wanafunzi uelewa wa kaulimbiu ya mwaka huu kwa kuhakikisha wanaitambua na kuitumia kama msingi wa michoro yao, ili kuonesha uhusiano kati ya ubunifu, chakula na lishe pamoja na malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.

Amesema kazi za wanafunzi zitapitiwa na wataalamu na washindi watano watakabidhiwa zawadi Oktoba 16, 2026, wakati wa kilele cha maadhimisho hayo.

Mashindano hayo ni sehemu ya shughuli za kuelekea Siku ya Chakula Duniani, inayolenga kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa chakula, lishe na ubunifu katika kuboresha uzalishaji na upatikanaji wa chakula.



Benki ya Absa Tanzania imezindua kampeni iliyopewa jina la “Mkwanja Kilaini na Kadi ya Absa”, ikiwa na na lengo la kuhamasisha matumizi ya huduma za kibenki kwa njia za kidigitali huku ikitenga jumla ya Shilingi milioni 60 kama zawadi za fedha taslimu kwa wateja wanaotumia kadi zake za malipo na mikopo katika miamala yao ya kila siku.

Kupitia kampeni hiyo itakayodumu kwa muda wa miezi mitatu itashuhudia washindi watatu wa kila mwezi wakijishinda pesa taslimu ambapo mshindi wa kwanza Shilingi milioni 5, mshindi wa pili Shilingi milioni 3 na mshindi wa tatu Shilingi milioni 2.

Jumla ya washindi tisa watapatikana katika kampeni hiyo ambapo zawadi kuu ya Shilingi milioni 30 itatolewa kwa mshindi mmoja mwishoni mwa kampeni, na kufanya jumla ya zawadi zote kufikia Shilingi milioni 60.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo wakati wa uzinduzi huo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Wateja Binafsi, Mkuu Mikakati na Bidhaa za Wateja Binafsi wa benki hiyo, Heristraton Genesis, alisema kampeni hiyo inaakisi dhamira ya benki ya kuwazawadia wateja wake huku ikihamasisha matumizi ya huduma za kibenki zilizo salama na rahisi zaidi.

“Katika Absa, tunaendelea kutafuta njia bunifu za kuwazawadia wateja wetu huku tukihamasisha tabia bora za kifedha. Kupitia kampeni ya ‘Mkwanja Kilaini, na Kadi ya Absa’, wateja wanachotakiwa kufanya ni kutumia kadi zao za Absa za malipo au mikopo katika manunuzi na miamala yao ya kila siku ili kupata nafasi ya kushinda zawadi za fedha taslimu zinazoweza kuleta mabadiliko makubwa katika maisha yao,” alisema.

Genesis aliongeza kuwa kadiri wateja wanavyofanya miamala mingi zaidi inayokidhi vigezo vya kampeni hiyo, ndivyo wanavyoongeza nafasi zao za kushiriki katika droo za bahati nasibu na kushinda zawadi.

Alibainisha kuwa malipo kwa kutumia kadi yana faida mbalimbali, zikiwemo urahisi wa matumizi, usalama ulioimarishwa, kukubalika katika maeneo mbalimbali duniani na kurahisisha upatikanaji wa huduma za biashara za kidijitali. Alisema faida hizo zinaifanya njia hiyo kuwa chaguo linalofaa zaidi katika uchumi wa kisasa unaozidi kutegemea teknolojia.

Kampeni hiyo inawahusu wateja waliopo na wapya wa Absa wenye umri wa miaka 18 na kuendelea ambao wanamiliki kadi za benki za malipo au mikopo za Absa. Wateja wanapaswa kufanya miamala inayokidhi vigezo vya kampeni kwa kutumia kadi zao na njia za huduma za kibenki za kidijitali zinazostahili ndani ya kipindi cha kampeni.

Washindi watapatikana kupitia droo za bahati nasibu zitakazofanyika kila mwezi chini ya usimamizi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania.

Kwa upande wake, Meneja Huduma za Jamii wa Benki ya Absa Tanzania, Abigail Lukuvi, alisema kampeni hiyo inasisitiza dhamira ya benki hiyo ya kuwaweka wateja katika kiini cha shughuli zake zote.

Alisema mpango huo unafuatia Wiki ya Huduma kwa Wateja, lakini unaonyesha kuwa juhudi za benki hiyo za kutambua na kuthamini wateja wake zinaendelea hata baada ya maadhimisho hayo ya kila mwaka.

“Wateja wetu ndio kiini cha biashara yetu, na kampeni ya ‘Mkwanja Kilaini, na Kadi ya Absa’ ni fursa nyingine kwetu ya kuwatambua, kuwazawadia na kuthamini imani wanayoendelea kutupatia kila siku,” alisema Abigail.

Aliongeza kuwa Absa imekuwa ikiendesha kampeni za kuwazawadia wateja kwa miaka mitatu mfululizo, huku kampeni zilizotangulia zikiwa na zawadi kubwa za fedha taslimu pamoja na zawadi nyingine zenye thamani, zikiwemo magari.

Kwa mujibu wa Abigail, kampeni hizo zinaunga mkono dhamira ya benki hiyo ya “Kuiwezesha Afrika ya Kesho pamoja… Hatua moja baada ya nyingine”, kwa kutambua wateja wake na kuwasaidia kufikia malengo yenye umuhimu katika maisha yao.

Kampeni hiyo mpya pia ni sehemu ya mkakati mpana wa Absa wa kuongeza matumizi ya huduma za kibenki za kidijitali na kuhamasisha malipo yasiyotumia fedha taslimu katika matumizi ya kila siku, manunuzi ya mtandaoni na miamala ya biashara.
01: Mkuu wa Mikakati na Bidhaa za Wateja Binafsi wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Heristraton Genesis (kushoto), akizungumza jijini Dar es Saaam leo, wakati wa uzinduzi rasmi wa Kampeni ya ‘Mkwanja Kiulaini na Kadi ya Absa’ yenye lengo la kuhamasisha matumizi ya huduma za kibenki kwa njia za kidigitali. Absa imetenga zawadi za pesa taslimu kiasi cha shs milioni 60 katika kampeni hiyo itakayodumu kwa muda wa miezi mitatu. Kulia ni Meneja Bidhaa za Kadi, Bi. Erica Mwaipopo.

Meneja Bidhaa za Kadi wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Erica Mwaipopo (kulia), akizungumza jijini Dar es Salaam leo, katika uzinduzi rasmi wa Kampeni ya ‘Mkwanja Kiulaini na Kadi ya Absa’ yenye lengo la kuhamasisha matumizi ya huduma za kibenki kwa njia za kidigitali. Absa imetenga zawadi za pesa taslimu kiasi cha shs milioni 60 katika kampeni hiyo itkayodumu kwa muda wa miezi mitatu. Kulia kwake ni Mkuu wa Mikakati na Bidhaa za Wateja Binafsi, Bw. Heristraton Genesis na wafanyakazi wengine wa benki hiyo.

Mkuu wa Mikakati na Bidhaa za Wateja Binafsi wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Heristraton Genesis (wa nne kutoka kushoto, waliokaa), pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Absa, wakipozi mbele ya wapigapicha, wakati wa uzinduzi rasmi wa Kampeni ya ‘Mkwanja Kiulaini na Kadi ya Absa’ yenye lengo la kuhamasisha matumizi ya huduma za kibenki kwa njia za kidigitali. Absa imetenga zawadi za pesa taslimu kiasi cha shs milioni 60 katika kampeni hiyo itkayodumu kwa muda wa miezi mitatu.


Benki ya Stanbic Tanzania imewafuata wafanyabiashara wa Kariakoo katika maeneo yao ya biashara kuwahamasisha kutumia huduma inayowawezesha kulipia bidhaa kutoka China kwa yuan moja kwa moja kutoka kwenye akaunti zao za shilingi, hatua inayolenga kupunguza gharama za miamala na kurahisisha biashara kati ya nchi hizo.

Huduma hiyo inatumia mfumo wa malipo wa China wa Cross-Border Interbank Payment System (CIPS), unaowawezesha wafanyabiashara kulipa wasambazaji wao nchini China kwa yuan kutoka kwenye akaunti zao za shilingi bila kulazimika kubadilisha fedha hizo kwanza kuwa dola za Marekani.

Akizungumza wakati wa kuhamasisha matumizi ya huduma hiyo Kariakoo, Oktoba 13, 2026, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, alisema kupunguza gharama za malipo ya kimataifa kunaweza kusaidia wafanyabiashara kuelekeza fedha zaidi katika kuongeza bidhaa, ajira na kukuza biashara zao.

“Serikali inataka kila biashara ya Mtanzania, kuanzia wazalishaji wakubwa hadi wafanyabiashara wa Kariakoo, ifanye biashara na dunia kwa gharama ndogo iwezekanavyo. Kila shilingi inayookolewa kwenye malipo ni shilingi inayoweza kurejeshwa kwenye bidhaa, ajira na ukuaji,” alisema.

Kapinga aliipongeza Stanbic kwa kuwafikia wafanyabiashara katika maeneo yao ya kazi na kuwataka kutumia njia rasmi na zinazosimamiwa kisheria wanapolipa wasambazaji wao.

Alisema China imefungua soko lake kwa baadhi ya bidhaa za Tanzania bila ushuru, akisisitiza umuhimu wa nchi kuongeza mauzo yake katika soko hilo badala ya kutegemea zaidi uagizaji wa bidhaa kutoka China.

Kwa mujibu wa Stanbic, huduma hiyo ilizinduliwa Agosti 12, 2026, na kuifanya benki hiyo kuwa ya kwanza nchini kutoa malipo ya moja kwa moja kutoka shilingi kwenda yuan kupitia mfumo wa CIPS.

Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Stanbic Bank Tanzania, Jonathan Ngoma, alisema huduma hiyo inalenga kurahisisha biashara kwa kuwapa wafanyabiashara njia ya kufanya malipo ya kimataifa kwa urahisi zaidi.

“Kariakoo ni mojawapo ya vitovu vikubwa vya biashara nchini, kinachowaunganisha maelfu ya wafanyabiashara na wasambazaji na masoko ya kimataifa. Tumewafuata hapa ili kuwaonesha kwamba sasa wanaweza kuwalipa wasambazaji wao wa China kwa urahisi zaidi, kupunguza gharama za miamala na kuelekeza nguvu zaidi katika kukuza biashara zao,” alisema

China imekuwa mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa Tanzania kwa miaka 10 mfululizo. Kwa mujibu wa taarifa ya benki hiyo, biashara kati ya nchi hizo ilifikia dola za Marekani bilioni 11.28 mwaka 2025, ikiwa ni mara ya kwanza kuvuka kiwango cha dola bilioni 10.

Katika miezi sita ya kwanza ya mwaka 2026, thamani ya biashara kati ya Tanzania na China ilifikia dola bilioni 6.48.

Sehemu ya bidhaa zinazoagizwa kutoka China, zikiwemo vifaa vya kielektroniki, nguo, vifaa vya ujenzi na bidhaa za nyumbani, hupitia Kariakoo kabla ya kusambazwa kwa wateja nchini Tanzania na nchi jirani.

Stanbic imesema malipo yanayokidhi masharti ya benki yanaweza kukamilika ndani ya dakika chache, kutegemea taratibu za kawaida za kibenki na saa za kazi.

Benki hiyo pia imesema haitatoza ada ya uhamisho wa fedha kwa malipo ya moja kwa moja ya yuan hadi Desemba 31, 2026. Huduma hiyo inapatikana katika matawi yote ya benki hiyo kwa wafanyabiashara binafsi, biashara ndogo na kampuni kubwa.

Aidha, wafanyabiashara wanaweza kutumia mikataba ya kubainisha kiwango cha ubadilishaji fedha mapema ili kupunguza athari za mabadiliko ya viwango kati ya kuagiza bidhaa na kufanya malipo.

Mkuu wa kitengo cha wafanyabiashara wadogo na wa kati, Stanbic Bank Tanzania, Fatma Ahmed, alisema huduma hiyo inaweza pia kurahisisha malipo kwa wafanyabiashara wa Tanzania wanaouza bidhaa zao nchini China.

Alisema tangu Mei 1, 2026, China imeondoa ushuru kwa bidhaa kutoka nchi 53 za Afrika, zikiwemo Tanzania, hatua inayofungua fursa kwa bidhaa za Tanzania kama ufuta, korosho, parachichi na kahawa.

“Msafirishaji anaweza sasa kupokea Shilingi moja kwa moja kwenye akaunti ya Stanbic na kujua kwa uhakika kiasi ambacho mzigo wake utazalisha kabla haujaondoka bandarini. Jukumu letu ni kuhakikisha biashara za Tanzania zinauza China kwa kujiamini kama zinavyonunua kutoka huko,” alisema.

Kwa upande wake, mmiliki wa Mwangaza Home Supplies, Asha Mwakalinga, biashara ya bidhaa za nyumbani iliyopo Kariakoo, alisema huduma hiyo inaweza kupunguza changamoto za ucheleweshaji wa malipo na mabadiliko ya viwango vya ubadilishaji fedha.

“Unapoendesha biashara kama yetu, bidhaa nyingi zinatoka China, hivyo kufanya malipo kwa wasambazaji ni jambo tunalolifanya mara kwa mara. Wakati mwingine mchakato huchukua muda mrefu kuliko inavyotarajiwa, na viwango vya kubadilisha fedha huathiri kiasi tunachotumia,” alisema.

Aliongeza kuwa huduma inayomwezesha mfanyabiashara kulipa moja kwa moja kwa yuan kutoka kwenye akaunti ya shilingi inaweza kurahisisha malipo na kusaidia kudhibiti gharama za uendeshaji.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Salvio Kapinga (kulia), akizungumza na Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Stanbic Bank Tanzania, Jonathan Ngoma (katikati kushoto), huku Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo (katikati kulia), akishuhudia wakati wa ziara yake katika banda la benki hiyo Kariakoo, jijini Dar es Salaam, Oktoba 13, 2026. Ziara hiyo ilikuwa sehemu ya kampeni ya Stanbic ya kuwafikia wafanyabiashara na kuwaelimisha kuhusu huduma ya kulipia bidhaa kutoka China moja kwa moja kwa yuan kupitia mfumo wa CIPS, bila kulazimika kubadilisha shilingi kwenda dola za Marekani kwanza.








Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratias John Ndejembi, amezitaka Wizara na Taasisi za Serikali kuhakikisha mifumo yao inasomana na kubadilishana taarifa ili kuondoa urasimu na kurahisisha upatikanaji wa huduma na fursa kwa wananchi, hususan vijana.

Akizungumza katika kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2026, kilichofanyika katika Viwanja vya CCM Nelson Mandela, Sumbawanga mkoani Rukwa, Ndejembi amesema agizo hilo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuunganisha mifumo ya Serikali ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.

Ametolea mfano Wizara mbili zinazoshughulikia masuala ya vijana, ambazo zimebuni mifumo tofauti isiyosomana, na kuzitaka kushirikiana kuhakikisha vijana wananufaika na fursa za ajira, mafunzo ya vitendo na uwezeshaji wa kiuchumi.

Aidha, Makamu wa Rais amesisitiza kuendelezwa kwa mapambano dhidi ya rushwa, dawa za kulevya, VVU na UKIMWI pamoja na umaskini, huku akiwaagiza viongozi kusimamia kwa uadilifu miradi ya maendeleo iliyopitiwa na Mwenge wa Uhuru ili kuhakikisha thamani ya fedha za umma.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka Watanzania kuendelea kuenzi misingi ya amani, umoja, uzalendo na uwajibikaji iliyoasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Nanauka, amesema Mbio za Mwenge wa Uhuru zimeendelea kuhamasisha maendeleo na ushiriki wa vijana katika shughuli za kiuchumi, huku Kiongozi wa Mbio hizo Kitaifa, Wazo Mwang’onda, akieleza kuwa wananchi wamepongeza utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuomba kuongezwa kwa fursa za uwezeshaji wa vijana na wanawake.

Makamu wa Rais amehitimisha mbio hizo akimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika maadhimisho yaliyoenda sambamba na kumbukizi ya miaka 27 ya kifo cha Baba wa Taifa na Maonesho ya 26 ya Wiki ya Vijana Kitaifa.









Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jeremiah Wambura, amesisitiza umuhimu wa kuwaenzi maveterani wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kwa kutambua mchango wao katika harakati za kudai uhuru wa Tanganyika.

Wambura, aliyewahi kuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la Wazazi Taifa, amesema maveterani hao wana historia muhimu katika ujenzi wa taifa inayopaswa kutambuliwa, kuhifadhiwa na kuendelezwa kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Ameyasema hayo leo, Oktoba 14, 2026, wakati wa kumbukizi ya miaka 27 ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, iliyoandaliwa na maveterani wa UVCCM Mkoa wa Dar es Salaam.

Kumbukizi hiyo imefanyika katika Ofisi za UVCCM Taifa, Mkoa wa Dar es Salaam, ikiwakutanisha maveterani kutoka wilaya mbalimbali za mkoa huo kwa ajili ya kufanya dua na kumuenzi Baba wa Taifa kupitia hotuba zake na simulizi za maisha yake wakati wa uhai wake.

Wambura, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mazingira na Ufugaji Tanzania (CHAMAUTA), amesema kumbukizi ya Mwalimu Nyerere, aliyekuwa mwasisi wa taifa na kiongozi wa harakati za ukombozi, ni fursa ya kutafakari mchango wa viongozi na vijana waliojitolea katika kupigania uhuru na maendeleo ya nchi.

Amesisitiza kuwa maveterani hao wanastahili kutambuliwa na kuenziwa kwa mchango wao, ikiwemo kushirikishwa katika shughuli za kitaifa zinazohusu kumbukizi na heshima kwa mashujaa wa taifa.

Katika kuunga mkono juhudi za maveterani hao, Wambura amekabidhi Shilingi 200,000 kwa ajili ya kufungua akaunti maalumu ya maveterani wa UVCCM itakayowasaidia kuratibu na kuendesha shughuli zao kwa urahisi na ufanisi.

Aidha, amewataka viongozi wa maveterani kuhakikisha akaunti hiyo inafunguliwa haraka, huku akiahidi kuwakatia bima ya afya maveterani walio hai walioshiriki katika harakati za kudai uhuru ili waweze kupata huduma za afya kwa urahisi.

“Pia nitajitolea kuandaa mkutano wa maveterani wa UVCCM wa kitaifa,” amesema Wambura.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Stanley Mkandawile, amewataka maveterani na viongozi wa chama kuendelea kutoa elimu kwa vijana kuhusu umuhimu wa kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, huku wakikemea udini na migawanyiko inayoweza kuhatarisha umoja wa Watanzania.

Mkandawile amesema Mwalimu Nyerere aliacha urithi wa amani, upendo na umoja uliowawezesha Watanzania wenye makabila na tamaduni tofauti kuishi pamoja kama familia moja.

Ameeleza kuwa misingi hiyo imechangia kujenga taifa lenye lugha ya pamoja ya Kiswahili na Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar, hivyo akasisitiza wajibu wa Watanzania wote kuuenzi na kuulinda.

Ameongeza kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa mtetezi wa haki za wanyonge na aliunga mkono harakati za ukombozi katika nchi mbalimbali za Afrika. Kutokana na mchango huo, amewataka Watanzania kuendeleza misingi ya upendo, haki, umoja na mshikamano ili kudumisha amani nchini.

Naye Katibu wa Maveterani wa UVCCM, Yahya Ngoma, amesema vijana waliojitolea kukitumikia chama na kushiriki katika harakati za kudai uhuru hawakulipwa mishahara, bali walifanya hivyo kwa uzalendo na dhamira ya kuona Tanganyika inapata uhuru.

Ngoma amewataka vijana wa sasa kujifunza kutoka kwa maveterani hao kwa kuheshimu maadili, kulinda misingi ya taifa na kuepuka makundi yanayoweza kuhatarisha amani na mshikamano wa nchi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Maveterani wa UVCCM Wilaya ya Kinondoni, Ahmad Mhando, amesema vijana wanapaswa kuwasikiliza wazee kutokana na uzoefu wao wa maisha, ambao unaweza kuwa mwongozo muhimu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alizaliwa mwaka 1922 na kufariki dunia Oktoba 14, 1999.






Na Mwandishi Wetu, Rukwa

‎Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesisitiza umuhimu wa kuunganisha mifumo ya kidijitali ya Serikali inayotoa taarifa za ajira na fursa kwa vijana kisimana ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo.

‎Amesema hayo baada ya kutembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano pamoja na Taasisi zake katika Maonesho ya Wiki ya Vijana yanayoendelea katika viwanja vya Shule ya Msingi Ndua, Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa.

‎Mhe. Ndejembi amesema kuwa Serikali ni moja, hivyo ni muhimu mifumo ya Serikali iliyopo katika Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano na Ofisi ya Rais - Maendeleo ya Vijana kuunganishwa ili iweze kusomana na kubadilishana taarifa kwa urahisi.

‎“Serikali ni moja, tunatakiwa mifumo ya wizara zote isomane ili fursa zote tuzikusanye pamoja na kisha tuzipeleke kwa vijana wa Kitanzania,” amesema Mhe. Ndejembi.

‎Halikadhalika Mhe. Ndejembi, amesema kuwa muda alioutoa kwa ajili ya kutekeleza maelekezo aliyoyatoa jijini Arusha Septemba 28, 2026, kuhusu kuunganisha mifumo hiyo umepita. Hivyo, Serikali itaziita wizara zenye dhamana ya masuala hayo kwa ajili ya kikao cha pamoja kitakacholenga kujadili namna ya kupata suluhisho.

‎Amesisitiza kuwa hatua hiyo inalenga kuweka utaratibu utakaowezesha fursa za ajira na maendeleo ya vijana kukusanywa katika sehemu moja, ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa na kuhakikisha vijana wa Kitanzania wanazifikia fursa hizo kwa urahisi na kwa wakati.




Na Mwandishi Wetu, Mirerani

WAKAZI 57,000 wa Tarafa ya Moipo, wilayani Simanjiro, mkoani Manyara, wanatarajiwa kunufaika na mradi wa maji wa mji mdogo wa Mirerani unaotekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA).

Mkurugenzi Mtendaji wa AUWSA, Mhandisi Idd Msuya, amesema hayo wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Fadhili Rajab Maganya, alipotembelea mradi huo katika mji mdogo wa Mirerani.

Amesema mradi huo utakapokamilika utahudumia wakazi wa kata nne za Tarafa ya Moipo ambazo ni Mirerani, Endiamtu, Naisinyai na Shambarai.

Kwa mujibu wa Mhandisi Msuya, mradi huo unagharimu Sh bilioni 4.3, ambapo hadi sasa Sh bilioni 2.5 zimetumika katika utekelezaji wake.

Kwa upande wake, Maganya ameitaka AUWSA kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati ili kuwawezesha wananchi wa eneo hilo kupata huduma ya maji safi na salama.

“Ninatambua utendaji kazi wako, Mhandisi Idd Msuya. Nilipofika kwenye mradi sikufurahi, lakini nimepata faraja kukuona hapa,” amesema Maganya.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Mkoa wa Manyara, Janes Darabe, amesema Mhandisi Msuya aliwahi kufanya kazi katika Mamlaka ya Maji Babati (BAWASA), hivyo ana imani na uwajibikaji wake katika kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.

Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Manyara (MAREMA), Elisha Nelson Mnyawi, amesema kampuni ya God Charity imejitolea kutoa kisima kimoja kilichopo katika machimbo ya madini ya Tanzanite ili kiwahudumie wachimbaji wa madini hayo.



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu (Watatu kulia), akipokea mfuko wenye machapisho mbalimbali yahusuyo utekelezaji wa majukumu ya Mfuko wa PSSSF, kutoka kwa Afisa Uhusiano wa Mfuko huo, Bi. Zaituni Hemed, alipotembelea banda la Mfuko katika Maonesho ya Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa, yanayofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Ndua, Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa. Maonesho hayo yanafikia kilele leo, Oktoba 14, 2026.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa PSSSF alipotembelea banda la Mfuko huo katika Maonesho ya Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa, yanayofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Ndua, Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa. Maonesho hayo yanafikia kilele leo, Oktoba 14, 2026.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, akisaini kitabu cha wageni alipotembelea banda la PSSSF katika Maonesho ya Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanayofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Ndua, Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa.

Mwanachama wa PSSSF akipatiwa huduma na mtumishi wa Mfuko huo katika banda la PSSSF wakati wa Maonesho ya Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanayofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Ndua, Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa.

Mwanachama wa PSSSF akipatiwa huduma na mtumishi wa Mfuko huo katika banda la PSSSF wakati wa Maonesho ya Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanayofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Ndua, Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa.

Mwanachama wa PSSSF akipatiwa huduma na mtumishi wa Mfuko huo katika banda la PSSSF wakati wa Maonesho ya Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanayofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Ndua, Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa.

Mwanachama wa PSSSF akipatiwa huduma na mtumishi wa Mfuko huo katika banda la PSSSF wakati wa Maonesho ya Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanayofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Ndua, Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa.


Na Mwandishi Wetu, Sumbawanga

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, ameupongeza Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa juhudi zinazofanywa katika kuboresha huduma na kuhakikisha wanachama na wastaafu wanapata mafao yao kwa wakati.

Mhe. Sangu ametoa pongezi hizo Oktoba 13, 2026, alipotembelea banda la PSSSF katika Maonesho ya Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa, yanayofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Ndua, Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa. Maonesho hayo yanafikia kilele leo, Oktoba 14, 2026.

“Hongereni, mnafanya kazi nzuri sana, endeleeni hivyo hivyo. Kabla ya kuja hapa, nilifungua semina ya wastaafu watarajiwa wa PSSSF na kuwaeleza kuwa chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mfuko umeimarika na unaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, ikiwemo kulipa mafao kwa wakati. Hivyo, endeleeni kufanya kazi nzuri ili wastaafu wetu waendelee kufurahia huduma za Mfuko wao,” alisema Mhe. Sangu.

Aidha, Mhe. Sangu alielezwa kuwa PSSSF inashiriki maonesho hayo kwa lengo la kuwafikia wanachama na wananchi kwa ujumla, kutoa elimu kuhusu hifadhi ya jamii na kuwahudumia wanachama, wakiwemo wastaafu.

Kupitia maonesho hayo, PSSSF inaendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa hifadhi ya jamii, maandalizi ya kustaafu na huduma mbalimbali zinazotolewa na Mfuko. Vilevile, maonesho hayo yanatoa fursa kwa wananchi kufahamu maboresho yaliyofanyika katika mifumo ya utoaji huduma na mafao, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wanachama.

Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA) imeendelea kutoa elimu na kusimamia hatua mbalimbali za kulinda afya ya mimea, kudhibiti visumbufu na kuhakikisha mazao yanayozalishwa na kuingia nchini yanakuwa salama kwa matumizi ya binadamu.

Akizungumza jijini Tanga katika maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani yanayoendelea kuanzia Oktoba 10 hadi 16, Saumu Zuberi Mwessongo, Afisa Kilimo kutoka TPHPA, Kitengo cha Usafi wa Mimea na Karantini, amesema mamlaka hiyo hukagua mazao yanayoingia na kutoka nchini ili kuzuia kuenea kwa wadudu na magonjwa vamizi ambayo hayapo nchini.

Mwessongo amesema TPHPA hutumia teknolojia mbalimbali, ikiwemo ndege nyuki (drone), kufuatilia mashamba na kubaini maeneo yaliyoathirika na wadudu au magonjwa ya mimea. Aidha, mamlaka hiyo hutoa elimu kwa wakulima kuhusu uchaguzi na matumizi sahihi ya viuatilifu vilivyosajiliwa ili kulinda mazao na afya za walaji.

Ameeleza kuwa mamlaka hiyo pia hutoa vibali vya usafi wa mimea kwa mazao yanayoingizwa nchini na yale yanayosafirishwa kwenda nje ya nchi. Amesema kupitia ukaguzi wa shehena za mazao, TPHPA huchukua hatua za kuzuia kuingia nchini kwa mazao yaliyobainika kuwa na wadudu au magonjwa vamizi, huku ikitoa maelekezo ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa pale changamoto zinapobainika.

Kwa upande wake, Letan Kurenia Mollel, mtaalamu kutoka Kitengo cha Hifadhi ya Taifa ya Mimea (National Herbarium of Tanzania), amesema kitengo hicho hukusanya sampuli za mimea na kufanya utambuzi wa kisayansi ili kubaini aina zake, hasa mimea isiyofahamika ambayo inaweza kuwa vamizi.

Mollel amesema mimea vamizi inaweza kuenea kwa kasi na kuathiri uzalishaji wa mazao kwa kushindana na mimea ya chakula, hali inayoweza kupunguza mavuno ya wakulima. Pia, mimea hiyo inaweza kuathiri maeneo ya malisho kwa kuenea na kuchukua nafasi ya mimea inayoliwa na mifugo na wanyamapori, hivyo kuathiri upatikanaji wa chakula cha mifugo.

Amesema utambuzi wa mapema wa mimea vamizi ni muhimu ili kuwezesha hatua za udhibiti kuchukuliwa kabla haijaenea na kusababisha madhara makubwa kwa kilimo na mazingira. Juhudi hizo zina mchango katika kulinda uzalishaji wa chakula na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

Naye, Mapulish D. Hebel kutoka Kitengo cha Teknolojia za Vinyunyizi vya Viuatilifu cha TPHPA amesema mamlaka hiyo husimamia usajili na ukaguzi wa vifaa vya kunyunyizia viuatilifu vinavyoingia nchini ili kuhakikisha vinakidhi vigezo vya ubora na vinafaa kwa matumizi ya kilimo.

Hebel amesema mamlaka hiyo pia hutoa mafunzo kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi na salama ya viuatilifu, namna ya kudhibiti visumbufu vya mimea na mbinu bora za kunyunyizia dawa. Ameeleza kuwa mafunzo hayo yanalenga kupunguza gharama za uzalishaji, kuongeza tija na kupunguza madhara ya viuatilifu kwa afya ya binadamu na mazingira.

Kwa upande wake, Masoud Matimbwa kutoka Kitengo cha Kudhibiti Visumbufu vya Mlipuko cha TPHPA amesema mamlaka hiyo imefanikiwa kudhibiti kwelea kwelea kwa kiwango kikubwa katika maeneo ya Babati, Moshi, Pwani na Kilosa, hatua inayosaidia kulinda mazao ya wakulima na kuongeza kipato chao.

Matimbwa amewataka wakulima kukagua mashamba yao mara kwa mara na kutoa taarifa mapema wanapobaini dalili za uvamizi wa visumbufu vya mimea ili hatua za udhibiti zichukuliwe kabla havijasababisha uharibifu mkubwa wa mazao. Amesema utambuzi wa mapema utasaidia kuokoa mazao na kuongeza tija katika uzalishaji wa chakula.

Akizungumza, Alfred Kiraho, mtaalamu kutoka Idara ya Usimamizi wa Viuatilifu ya TPHPA, amewashauri wafanyabiashara wanaosafirisha mazao nje ya nchi kupeleka sampuli maabara kupima masalia ya viuatilifu kabla ya kusafirisha, na hatua hiyo husaidia kuhakikisha mazao yanakidhi viwango vya usalama vinavyotakiwa katika masoko ya kimataifa, huku majibu ya maabara hiyo yakiaminika na kukubalika duniani.






Taasisi ya Kuendeleza Kilimo Hai Tanzania (TOAM) imeitaka Serikali kuimarisha usambazaji wa taarifa kuhusu mbolea na viuatilifu vya kilimo hai vilivyosajiliwa, ili kuwawezesha maafisa ugani na wakulima kupata elimu sahihi ya pembejeo zinazofaa, kuongeza tija na kuepuka hasara zinazotokana na matumizi yasiyofaa ya viuatilifu.

Akizungumza Jijini Tanga, katika mwendelezo wa maadhimisho ya siku ya Chakula Duniani yaliyoanza Oktoba 10 hadi 16, Afisa Ushawishi na Utetezi wa TOAM, Paul Chilewa, amesema licha ya kuwepo kwa mbolea na viuatilifu vya kilimo hai vilivyosajiliwa na mamlaka husika, taarifa zake bado hazijawafikia ipasavyo maafisa ugani na wakulima wanaohitaji kuzitumia katika uzalishaji.

Amesema hali hiyo inaweza kuathiri wakulima wanaolenga masoko ya nje, akitoa mfano wa wakulima wa parachichi ambao mazao yao yanaweza kukataliwa katika masoko hayo kutokana na kubainika kwa mabaki ya viuatilifu, ameeleza kuwa changamoto hiyo inaweza kupunguzwa kwa kuwapatia wakulima elimu na taarifa sahihi kuhusu matumizi ya pembejeo zinazofaa tangu hatua za uzalishaji.

Chilewa amesema TOAM imeandaa orodha ya mbolea zilizosajiliwa ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa zake, huku akibainisha kuwa bado kuna haja ya kuandaa na kusambaza taarifa za viuatilifu vilivyosajiliwa kwa maafisa ugani na wakulima nchini, Juhudi hizo ni sehemu ya kuunga mkono utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Kilimo Ikolojia Hai wa mwaka 2023–2030, na wamekuwa wakishirikiana kwa ukaribu na TFRA pamoja na TPHPA.