"MAHAKAMA"
Showing posts with label MAHAKAMA. Show all posts

MKAZI wa Ubungo jijini Dar es Salaam, Monica Mujungu ameliomba Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Kinondoni kutenda haki kwani wakili wa mpinzani wake, Benjamin Karume anatumia taaluma yake ya Sheri kuishawishi mahakama imnyime haki yake.

Monica alidai hayo mbele ya Hakimu Joaquine Cheng'a wakati pingamizi alilowasilisha kwamba anayemdai gharama za kesi takribani Sh milioni 10 hajawahi kushtakiana naye mahakamani likisikilizwa.

Monica aliwasilisha pingamizi dhidi ya Adon Christian Hajayandi akidai hajawahi kushtakiana naye mahakamani, aliyeshtakiana naye ni Hajayandi Adon.

Wakili wa Hajayandi, Benjamin Karume alidai mteja wake aliwahi kufunguliwa kesi ya mgogoro wa mpaka katika eneo lililopo Kimara Temboni na Monica iliyosikilizwa upande mmoja na kumpa ushindi Monica .

Alidai aliwasilisha maombi ya kutengua hukumu hiyo na ilitenguliwa Septemba 3, 2021 na akaamuliwa Monica kuwasilisha maombi mengine.

Wakili Karume alidai aliwasilisha maombi mapya Mei 25,2026 Ili upande wao wawasilishe majibu ya utetezi,

majina yakiwa Monica Kalibona Mujungu dhidi ya Adon Christian Hajayandi, shauri hilo pia likafutwa Julai 2 mwaka huu kwa gharama.

"Mheshimiwa akisema hajafanya kesi na Adon ni kujichanganya mwenyewe, hoja haina mashiko tuendelee na shauri la gharama za kesi,"anadai Wakili Karume.

Akijibu Monica anadai hajawahi kuwasikisha maombi ya Mei mwaka huu dhidi ya Adon na kwamba kesi iliisha mwaka 2021.

"Mheshimiwa Wakili anatumia ujuzi wake kuishawishi Mahakama kwa sababu kesi iliisha 2021 na hukumu ipo, nilikazia hukumu na kukabidhiwa eneo.

"Mwaka 2022 alifaili kesi namba 130, alidai kesi ilisikilizwa upande mmoja, hajahudhuria ikafutwa, alidai ni mfanyakazi wa Ikulu alihamishwa mkoa, akaomba kesi ianze upya.

"Wakati huo Baraza la Ardhi Ubungo lilishaanza nikaomba kesi yangu ihamie huko Hakimu aliyekuwa akisikiliza awali alinikatalia.

"Kesi iliendeshwa kwa jina la Hajayandi Adon, mwanzoni nilimfahamu kwa jina la Adon Christian Hajayandi, nilipompelekea hati ya wito wa mahakama alikataa akidai si jina lake, alidai jina lake sahihi ni Hajayandi Adon,"anadai Monica na kuongezea kwamba hata kesi alizowasilisha aliandika Hajayandi Adon

"Anachokifanya ni kutaka kunisumbua, naomba mahakama itambue anatumia ujuzi wake kuninyanyasa, kesi tulifanya na Hajayandi Adon sio Adon Christian Hajayandi, naomba maombi yake ya gharama yatupiliwe mbali.

"Alipewa ushindi ambao sielewi, naomba nipate haki yangu, kesi itupiliwe mbali, niliyowasilisha isikilizwe,"anadai Monica.


Na Karama Kenyunko, Michuzi TV

DAR ES SALAAM — Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ameiambia Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, kuwa shauri la uhaini linalomkabili ni la kwanza katika historia ya Tanzania ambapo mshtakiwa ni mmoja na shtaka hilo halihusiani na kumuua Rais wala kuipindua Serikali.

Lissu ameyasema hayo wakati akiendelea kutoa majumuisho yake ya mwisho mbele ya jopo la majaji watatu, wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiwa na Jaji James Karayemaha na Jaji Ferdinand Kiwonde.

Amesema kesi hiyo ni ya tatu ya uhaini katika historia ya Tanzania, akitaja kesi za Grey Likungu Mataka na wenzake ya mwaka 1970 na Khatibu Ghandi na wenzake ya mwaka 1983.

Kwa mujibu wa Lissu, kesi hizo mbili zilizotangulia zilihusu madai ya mipango ya kumuua Rais na kuipindua Serikali kwa kutumia silaha, tofauti na kesi inayomkabili ambayo imefunguliwa chini ya kifungu cha 39(2)(d) cha Kanuni ya Adhabu, kinachohusu uhaini kwa kuitishia Serikali.

“Tofauti na hizo kesi mbili za mwanzo, hii ya kwangu imefunguliwa chini ya kifungu cha 39(2)(d) na uhaini wa hapa ni wa kuitishia Serikali. Hakuna kumuua Rais wala kuipindua Serikali. Hii ni kesi ya kwanza,” amesema Lissu.

Amesema uamuzi utakaotolewa na Mahakama katika shauri hilo utaweka msingi wa kisheria kuhusu dhana ya uhaini kwa kuitishia Serikali na unaweza kuwa rejea katika kesi zijazo.
“Vyovyote vile mtakavyoamua, mtaweka msingi wa kisheria kuhusu uhaini wa kuitishia Serikali. Waheshimiwa Majaji, mtaweka precedent ambayo itaongoza Mahakama zetu kwa miaka mingi ijayo,” amesema.

Lissu amesema majaji hawataamua tu hatma ya mshtakiwa mmoja, bali pia wataweka msingi wa kisheria utakaoweza kutumika katika kuamua masuala kama hayo kwa miaka ijayo.

“Kwahiyo Majaji, hamtahukumu mtu mmoja, kwahiyo mtaweka utaratibu wa kisheria utakaofuatwa miaka mingi ijayo. Waheshimiwa Majaji wangu, sihitaji kuwakumbusha uzito wa huo mzigo mliobebeshwa. Hamuamui guilt ya mtu mmoja, bali mzigo wa kisheria kwa masuala haya for many years to come,” amesema.

Lissu amesema utetezi wake tangu mwanzo haukuwa wa kukanusha maneno aliyoyasema, bali ulikuwa ukilenga kuieleza Mahakama msingi wa kisheria kwamba, kwa mtazamo wake, kauli za kisiasa hazijawahi kutengeneza kosa la uhaini.

Akiifafanua dhana hiyo ya kisheria, Lissu ametaja hoja sita anazodai zinapaswa kuthibitishwa ili kosa hilo liweze kutengenezwa, ikiwemo kuwepo kwa nia madhubuti (mens rea), uchochezi unaolenga mtu au kundi maalumu la watu, pamoja na matokeo yanayoonekana kwa mujibu wa kifungu cha 10(2) cha Kanuni ya Adhabu.

Amedai kuwa pale sheria inapohitaji kuwepo kwa nia katika kosa, ni lazima matokeo ya nia hiyo yaonekane na kuthibitika. Kwa mtazamo wake, iwapo hakuna matokeo yaliyotokea, maana yake ni kwamba nia hiyo haikutimia na hivyo kosa la uhaini haliwezi kuwepo.

Aidha, Lissu amesema baada ya Mahakama kusikiliza mashahidi 17 wa upande wa mashtaka na kupokea vielelezo 16 vya utetezi, bila kuwepo kwa kielelezo cha Jamhuri, kesi ya Serikali imekuwa dhaifu zaidi ikilinganishwa na ilivyokuwa wakati ilipowasilishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Katika hatua nyingine ya majumuisho yake, Lissu ameiomba Mahakama kutathmini iwapo yeye ndiye aliyeitisha mkutano huo na kuwaalika wanahabari, pamoja na iwapo alikuwa na nia ya kuchochea kundi la watu kuzuia uchaguzi kwa lengo la kuitishia Serikali.

Kesi hiyo bado inaendelea, huku Lissu akiendelea kuwasilisha majumuisho yake ya mwisho mbele ya Mahakama.



MKURUGENZI wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Kamishna wa Polisi Ramadhani Kingai, amegoma kutoa ushahidi kwa upande wa utetezi wa Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, anayekabiliwa na mashtaka ya uhaini katika Mahakama Kuu Masijala Ndogo Dar es Salaam.

Hatua hiyo imempelekea mshtakiwa Lissu, ambaye anajitetea mwenyewe katika kesi hiyo, kufunga ushahidi wa upande wa utetezi.

Kesi hiyo leo, Septemba 18, 2026, iliitwa mahakamani hapo kwa ajili ya kuendelea na ushahidi wa upande wa utetezi, ambapo DCI Kingai alitarajiwa kutoa ushahidi.

Akizungumza mbele ya Jopo la Majaji linaloongozwa na Jaji Dustun Ndunguru, Lissu amedai amekutana na DCI Kingai, ambaye alikuwa amependekeza awe shahidi wake wa leo, ndani ya chumba cha mahakama na kuzungumza naye kwa kina kuhusu suala la kutoa ushahidi kwa upande wa utetezi.

Amedai kuwa baada ya kumweleza Kingai maeneo ambayo angependa ayatolee ushahidi, shahidi huyo alimweleza kuwa hawezi na hayuko tayari kutoa ushahidi kwa upande wa utetezi.

“Mimi nimemuelewa kama hayuko tayari, siwezi kumlazimisha kutoa ushahidi ambao hayupo tayari kuutoa,” amedai Lissu.

Amedai Kingai amemweleza kuwa yeye yuko upande wa watu wanaoomba na watakaoshangilia endapo atapatikana na hatia, hivyo hayuko tayari kutoa ushahidi kwa niaba yake.

“Yeye yuko upande wa wale wanaoomba na watakaoshangilia nikipatikana na hatia, kwa hiyo amesema hayuko tayari kuja kutoa ushahidi kwa niaba yangu,” amedai Lissu.

Amedai Kingai pia amemweleza kuhusu mashahidi wengine wawili ambao ni Mkuu wa Majeshi, CDF Jacob Nkunda, na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Camilius Wambura, ambao pia mahakama iliamuru wapelekewe wito, kuwa nao watakaporejea nchini na kupata wito wa mahakama, msimamo wao utakuwa kama wake.

“Kwamba na wao hawatakuwa tayari kutoa ushahidi kwa upande wa utetezi, hawawezi kwa sababu ile ile ya wale wanaoombea na watakaoshangilia nikipatikana na hatia,” amedai Lissu.

Kutokana na hali hiyo, Lissu amesema hana mashahidi wengine wa kuwaita na hivyo ameomba kufunga ushahidi wa upande wa utetezi.

Baada ya kusikiliza maelezo hayo, kesi hiyo sasa imefungwa kwa pande zote mbili na kuomba kupangiwa siku ya kuwasilisha hoja za mwisho.

Upande wa utetezi umeeleza kuwa ratiba ya kikao cha mahakama inaishia Septemba 25, hivyo kubaki siku saba za kuandaa hoja za mwisho.

Lissu amesema yuko tayari kuwasilisha hoja hizo Jumatano, huku akieleza kuwa mwenendo wa kesi una hoja zaidi ya kurasa 1,000.

Upande wa Jamhuri umekubaliana na Lissu kuhusu tarehe hiyo na kueleza kuwa utakuwa tayari kwa ajili ya kuwasilisha hoja za mwisho.

Kesi imeahirishwa hadi Septemba 23, 2026. 







Na HABIBA MBARUKU, Mahakama-Dodoma

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju amesema kuwa, Haki Jinai si mali ya Taasisi moja bali ni mfumo wenye Taasisi nyingi, wenye lengo la kuhakikisha haki inapatikana mapema ipasavyo kwa usawa, uadilifu na kwa kuzingatia Katiba na Sheria za nchi huku akieleza kuwa wadau wote wanapaswa kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha haki haicheleweshwi bila sababu za msingi.

Mhe. Masaju ameyasema hayo wakati wa kufunga Mkutano wa Mahakama na Wadau wa Haki Kuhusu Ushirikiano na Mahusiano katika Utekelezaji Majukumu ya Utoaji Haki Mahakamani leo tarehe 17 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

“Haki jinai ni mfumo mmoja wenye taasisi nyingi lakini wenye lengo moja, yaani kuhakikisha kuwa haki inapatikana mapema ipasavyo tunapaswa kuzungumza kuhusu mfumo mzima kwa sababu udhaifu wa kiungo kimoja katika mnyororo wa haki jinai unaweza kuchelewesha haki kwa mfumo mzima,” amesema Jaji Mkuu.

Mhe. Masaju ametoa mfano wa Mtume Paulo anapozungumza kuhusu kanisa ambapo amesema, “ni kama mwili wa binadamu, kama ambavyo kuna mikono, macho, miguu, lakini hivyo vyote ndiyo vinakamilisha mwili. Yaani macho hayawezi kujifanya yenyewe ni bora kuliko mguu na vile viungo vilivyoonekana kama ni dhaifu, hivyo Mungu alivifanya kuwa vya maana zaidi lakini ukweli hapa wote hakuna kiungo dhaifu, hizi Taasisi zote ni muhimu.”

Ameongeza kuwa, jukumu la kwanza la sheria duniani kote ni kusimamia utawala wa sheria, amani na usalama katika jamii na jukumu la pili ni kukusanya kodi kwa ajili ya maendeleo mbalimbali na kuongeza kuwa hata Mwenyezi Mungu huko mbinguni aliweka sheria, na aliyekwenda kinyume na sheria aliwajibika kama ambavyo Lucifer alivyowajibika.

“Kwa hiyo, mkishakuwa zaidi ya mtu mmoja tu lazima mjiwekee sheria namna ya kufanya mambo yenu na kwetu Tanzania utawala wa sheria unapatikana katika Ibara ya 26 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mfumo wowote lazima uwe unaongozwa na utawala wa sheria, hata Mwenyezi Mungu kule mbinguni aliweka sheria, na bwana mkubwa yule akiitwa Lucifer alipoasi akawajibika” amesema Mhe. Masaju.

Katika hatua nyingine Jaji Mkuu amefafanua kuwa, Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050 inasisitiza juu ya amani, usalama na utulivu, ulinzi wa haki, uhuru wa msingi, uimara wa Taasisi na utawala wa sheria ambao ni kipengele muhimu cha utawala bora kinachosaidia kujenga jamii yenye usawa, uwajibikaji, haki na kuaminiana.

Aidha, ameeleza kuwa, mashauri ya jinai hayaanzii mahakamani wala polisi pekee kwa kuwa vyombo hivyo vyote haviwi sehemu na wakati ambapo matukio hayo ya kihalifu yanatokea hivyo, wadau wote wanapaswa kuungana na kufanya kazi kwa pamoja kama ambavyo viungo katika mwili vinavyofanya kazi kwa pamoja na kutegemeana.

“Kesi ya jinai inaanza kwenye jamii huko tukio linapotokea, inaenda kwenye vyombo vya uchunguzi iwe ni Polisi, ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, ni Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, inaenda Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, hatimaye kama kuna ushahidi inaenda mahakamani, na waliohusika kumkamata mshukiwa wanakuja kutoa ushahidi mahakamani kama amepatikana na hatia anarudi gerezani kwa ajili ya reform, utaona kwamba huu mnyororo ni mpana ni mnyororo mrefu lakini mnyororo imara, ” ameeleza Mhe. Masaju.

Katika hatua nyingine, amesema kuwa, ni vema kukawa na mtiririko mzuri wa kimfumo wa usimamizi wa mashauri ya jinai ili kuondoa changamoto zinazokwamisha mashauri kumalizika na kuongeza kuwa Mahakama haiwezi kuwa na ufanisi wa asilimia 100, ikiwa hatua zilizotangulia hazifanyi kazi mapema ipasavyo na kwa ufanisi na kwamba kunaweza kuwa na Mahakama yenye uwezo wa kusikiliza Mashauri Majaji na Mahakimu wenye uwezo lakini kama uchunguzi haujakamilika au kuwepo kwa changamoto yoyote shauri haliwezi kuendelea.

“Mahakama haiwezi kuwa na ufanisi wa asilimia 100 ikiwa hatua zilizotangulia Mahakama hazifanyi kazi mapema ipasavyo na kwa ufanisi. Tunaweza kuwa na Mahakama yenye uwezo wa kusikiliza mashauri, Majaji na Mahakimu wenye uwezo, na mifumo ya kielektroniki au miundombinu, lakini pia ni waadilifu. Lakini kama uchunguzi haujakamilika, jalada halijawasilishwa, mashahidi hawapatikani, maelezo hayajakamilika, hati za mashtaka zina kasoro, mshtakiwa hajaletwa mahakamani, au nyaraka muhimu hazijafikishwa mahakamani mapema, katika mtiririko kama huu kesi haiwezi kwenda mbele, hivyo ni vema kukawa na ile systematic flow ya criminal justice ya case management ili kuondoa hizo changamoto” amesisitiza Jaji Mkuu.

Akizungumza kuhusu uwajibikaji na kujituma, Mhe. Masaju amesema kuwa, kila Taasisi ya Haki Jinai inapaswa kuwajibika ipasavyo ili kuondoa ucheleweshaji wa mashauri bila kusubiri shauri lifike mahakamani huku akirejea Ibara ya 25 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inasisitiza juu ya uwajibikaji na kujituma katika kila kazi kwa kufahamu chanzo cha kukwama kwa shauri, wapi lilipofikia katika utekelezaji, imefikia hatua zipi za ushahidi, jambo litakalosaidia mnyororo mzima wa haki jinai kufanya kazi vizuri.

Kadhalika, Mhe. Masaju amewakumbusha wadau wa Haki Jinai kwamba, mfumo unahitaji ushirikiano thabiti, mawasiliano ya karibu na uratibu mzuri ambayo ndio nguzo ya mafanikio hivyo, taasisi zote zifanye kazi bila kujitenga.

“Ni vyema tukumbuke kuwa, mfumo wetu wa haki jinai unahitaji ushirikiano thabiti (cooperation), mawasiliano ya karibu (communication), na uratibu mzuri (coordination). Hivi vitu vitatu yaani Cooperation, Communication, and Coordination ndivyo nguzo kuu za mafanikio yetu katika usimamizi wa haki jinai. Kama taasisi moja inafanya kazi kwa kujitenga au bila kutoa taarifa kwa nyingine, ni wazi kuwa, kutakuwa na kukwama kwa mashauri au kuchelewa kwa haki,” amesisitiza Jaji Mkuu.

Kadhalika, Mhe. Masaju amezitaka Taasisi za mnyororo wa Haki Jinai kuzingatia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kuhakikisha mifumo inasomana ili kurahisisha mchakato mzima wa kuhakikisha haki inapatikana mapema ipasavyo bila kucheleweshwa na sababu zisizo na msingi.

Akihitimisha hotuba yake. Mhe. Masaju amezitaka Taasisi za mnyororo wa Haki Jinai kuchukua tahadhari juu ya uwepo wa mvua za El nino kwa kuhakikisha wanaweka miundombinu imara itakayowawezesha kufanya kazi pindi mvua hizo zitakapoanza kunyesha.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Majaji, Viongozi na Watumishi wa Mahakama pamoja na Wadau wa Haki Jinai wakati wa Mkutano wa Mahakama na Wadau wa Haki Kuhusu Ushirikiano na Mahusiano katika Utekelezaji Majukumu ya Utoaji Haki Mahakamani uliofanyika tarehe 17 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. Aliyeketi kushoto ni Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Amir Mruma na kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga.

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akitoa hotuba ya kufunga Mkutano wa Mahakama na Wadau wa Haki Kuhusu Ushirikiano na Mahusiano katika Utekelezaji Majukumu ya Utoaji Haki Mahakamani uliofanyika tarehe 17 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.





Baadhi ya Viongozi, Watumishi wa Mahakama pamoja na Wadau wa Haki Jinai wakisikiliza hotuba ya Jaji Mkuu alipokuwa akifunga Mkutano wa Mahakama na Wadau wa Haki Kuhusu Ushirikiano na Mahusiano katika Utekelezaji Majukumu ya Utoaji Haki Mahakamani uliofanyika tarehe 17 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Amir Mruma akitoa neno wakati wa kufunga Mkutano wa Mahakama na Wadau wa Haki Kuhusu Ushirikiano na Mahusiano katika Utekelezaji Majukumu ya Utoaji Haki Mahakamani uliofanyika tarehe 17 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.


Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya akitoa taarifa ya utekelezaji wa mikakati kwa upande wa Mahakama wakati wa Mkutano kati ya Mahakama na Wadau wa Haki Kuhusu Ushirikiano na Mahusiano katika Utekelezaji Majukumu ya Utoaji Haki Mahakamani uliofanyika tarehe 17 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.


(Picha na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania imeamuru kutolewa kwa wito (summons) kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), ili kutoa ushahidi katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.

Uamuzi huo umetolewa leo na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dustan Ndunguru baada ya Mahakama kusikiliza hoja za upande wa mashtaka na utetezi kuhusu ombi la Lissu la kuwaita mashahidi hao pamoja na viongozi wengine wa Serikali.

Mahakama imesema, kwa kuzingatia kifungu cha 314 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), ina hiari ya kuruhusu mashahidi kuitwa kwa kuangalia umuhimu wa ushahidi wao katika shauri.

Katika uamuzi huo, Mahakama imesema imeridhika kuwa ushahidi wa IGP, CDF na DCI ni muhimu katika kesi hiyo, hivyo imeamuru summons zitolewe ili waje kutoa ushahidi upande wa utetezi.

Hata hivyo, Mahakama imekataa ombi la kuwaita baadhi ya mashahidi waliotajwa na Lissu, akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu wa zamani Kassim Majaliwa, ikisema ushahidi wao hauhusiani na kesi hiyo kwa upande wa utetezi.

Mahakama pia imekubaliana na hoja ya upande wa mashtaka kwamba mashahidi ambao hawakutajwa wakati wa committal proceedings hawawezi kutajwa baadaye wakati wa usikilizwaji wa hoja za awali (PH).

Jaji Ndunguru amesema kifungu cha 281 cha CPA kinaeleza kuwa msajili atatoa summons kwa mashahidi waliotajwa wakati wa committal proceedings, huku Mahakama ikibaini kuwa katika mwenendo wa kesi hiyo hakukuwa na orodha ya mashahidi waliotajwa.

Kuhusu hoja ya kumuita Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Mahakama imesema mfano wa kesi ya Khatibu Ghandi hauwezi kutumika moja kwa moja kwa kuwa katika kesi hiyo shahidi huyo aliitwa na upande wa mashtaka na pia sheria ya sasa ya Usalama wa Taifa haikuwepo wakati huo.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho saa tatu asubuhi kwa ajili ya kuendelea na hatua ya utetezi.


Na Karama Kenyunko - Michuzi tv

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeelezwa kuwa Mwenyekiti CHADEMA, Tundu Lissu, hakuwa na ufahamu wa uwepo wa waandishi wa habari katika mkutano wa chama hicho na watia nia uliofanyika Aprili 3, 2025.

Shahidi wa nne wa utetezi, Brenda Rupia, ambaye ni Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, amedai hayo leo Septemba 7, 2026 mbele ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru akisaidiana na jaji Fednand Kiwonde na James Karayemaha alipokuwa akitoa ushahidi katika kesi ya uhaini inayomkabili Lissu.

Brenda amedai kuwa, Lissu hakuwa ameandaa mkutano huo wala aliyealika vyombo vya habari, akieleza kuwa jukumu hilo lilifanywa na Sekretarieti ya CHADEMA chini ya Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika.

Amesema yeye ndiye aliyeandika taarifa kwa umma na watia nia kuhusu mkutano huo Machi 27, 2025, na kuiweka katika kurasa za chama kwenye mitandao ya kijamii, huku waandishi wa habari wakialikwa kufanya coverage ya mkutano huo.

Kwa mujibu wa Brenda, takribani watu 250 walihudhuria mkutano huo, wakiwemo watia nia, wajumbe wa Sekretarieti, viongozi wakuu wa CHADEMA pamoja na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali, akiwemo Jambo TV.

Brenda amedai Lissu alikuwa mzungumzaji mkuu katika mkutano huo na alitoa hotuba kuhusu msimamo wa chama wa “No Reforms, No Election”, huku akisisitiza kuwa hakumuona akifanya jukumu lingine lolote katika mkutano huo.

Kuhusu maudhui yaliyorushwa na Jambo TV, shahidi huyo amesema yaliyorekodiwa na chombo hicho yalikuwa mali ya Jambo TV na kwamba Lissu hakuwa mfanyakazi wa chombo hicho wala hakuhusika na kurusha matangazo hayo.

Baada ya ushahidi huo, Mahakama iliahirisha kesi hadi kesho saa tatu asubuhi huku Jaji Dustan Ndunguru akieleza kuwa kesi hiyo imeongezewa siku 14 kuanzia leo kwa ajili ya kukamilisha mwenendo wake.


Na Janeth Raphael - MichuziTv

Upande wa Jamhuri umefunga ushahidi wake baada ya kuwasilisha ushahidi wa mashahidi 17 katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.

Hatua hiyo imefikiwa leo Jumatatu, Agosti 17, 2026, katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo, Dar es Salaam, wakati kesi hiyo ikiendelea kusikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu.

Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, ameieleza Mahakama kuwa baada ya upande wa Jamhuri kupitia kwa kina ushahidi uliotolewa na mashahidi wake pamoja na hoja mbalimbali zilizowasilishwa wakati wa usikilizwaji wa kesi, umefikia uamuzi kuwa ushahidi uliopo unatosheleza.

Kwa mujibu wa Katuga, uchambuzi wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani umeifanya Jamhuri kuona hakuna ulazima wa kuongeza mashahidi wengine, hivyo upande huo umefunga rasmi ushahidi wake.

“Baada ya kupitia ushahidi uliowasilishwa hapa mahakamani na kuangalia ushahidi wa mashahidi waliobakia, tumechambua na kuangalia hoja zilizowasilishwa mahakamani hapa. Hata hivyo, upande wa Jamhuri tunaona ushahidi ambao tumeutoa ni ushahidi toshelezi zaidi kuleta mashahidi wengine,” amesema Katuga.

Uamuzi huo unaweka kesi hiyo katika hatua muhimu, baada ya upande wa mashtaka kukamilisha uwasilishaji wa ushahidi wake kupitia mashahidi 17.

Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiwa na Jaji James Karayemaha na Jaji Ferdinand Kiwonde.

Kufungwa kwa ushahidi wa Jamhuri kunafungua hatua nyingine ya kisheria katika mwenendo wa kesi hiyo, huku taratibu za mahakama zikiendelea kuamua hatua zinazofuata.



Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ameiomba Mahakama ya Rufani kutupilia mbali maombi ya marejeo yaliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), akidai hayana msingi wa kisheria na yanalenga kuchelewesha usikilizwaji wa kesi ya tuhuma za uhaini inayomkabili.

Lissu alidai hayo mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani baada ya Jamhuri kufungua shauri la mapitio kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu uliotupilia mbali notisi ya Jamhuri ya kuwasilisha ushahidi mpya katika kesi hiyo.

Alidai uamuzi wa Mahakama Kuu wa Februari 24, 2026 haukumaliza kesi ya msingi ya uhaini, hivyo ni uamuzi mdogo usioruhusiwa kukatiwa rufaa wala kuwasilishwa maombi ya marejeo kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Rufani.

Lissu pia alidai DPP hakupaswa kuwasilisha maombi hayo moja kwa moja Mahakama ya Rufani bali alitakiwa kwanza kuandika barua rasmi kwa Jaji Mkuu.

Kwa upande wa Jamhuri, Wakili wa Serikali Mkuu Nassoro Katuga na Job Mrema waliieleza Mahakama kuwa Lissu ametegemea kanuni za mashauri ya madai badala ya jinai na kwamba maombi ya DPP yamewasilishwa kwa mujibu wa Sheria ya Mahakama ya Rufani na Kanuni zake.

Katuga alidai Mahakama Kuu ilikataa ushahidi huo kabla haujapokelewa na kupimwa, jambo ambalo lilinyima Jamhuri haki ya kusikilizwa kikamilifu, huku akisisitiza kuwa Mahakama ilipaswa kuangalia uhalali wa notisi ya kuongeza ushahidi.

Mrema naye alidai pingamizi la awali la Lissu halina uwezo wa kuondoa shauri lote na kwamba halijazingatia sheria ya sasa kwa kuwa linahusu mashauri ya madai.

Katika majibu yake, Lissu aliiomba Mahakama itupilie mbali maombi hayo na iamuru DPP amlipe fidia kwa kile alichodai ni ucheleweshaji wa makusudi wa shauri lake, akisema amekaa gerezani kwa mwaka mmoja na miezi mitatu huku kesi ikicheleweshwa kwa siku 139.

Katuga alipinga madai hayo akieleza kuwa maombi hayo hayajalenga kuchelewesha kesi na kwamba Mahakama ya Rufani ina mamlaka ya kuhakikisha mwenendo wa Mahakama Kuu unafuata sheria.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Mahakama iliahirisha shauri hilo hadi itakapotoa uamuzi wake kwa tarehe ambayo pande zote zitajulishwa.






Na Janeth Raphael MichuziTv Bungeni - Dodoma

Mbunge wa Korogwe Vijijini, Timotheo Mnzava, ameishauri Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuharakisha uimarishaji na usambazaji wa mfumo wa kidijitali wa usimamizi wa ardhi nchini ili kupunguza migogoro ya ardhi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Akizungumza bungeni leo wakati akichangia mjadala wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka wa fedha 2026/27, Mnzava amesema kuwa licha ya Serikali kuanza hatua za matumizi ya mifumo ya kidijitali katika usimamizi wa ardhi, bado halmashauri chache pekee ndizo zimefanikiwa kufikiwa na mfumo huo, jambo linalochangia kuendelea kuwepo kwa migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema mfumo huo unapaswa kusambazwa katika halmashauri zote nchini ili kurahisisha usimamizi wa taarifa za ardhi, kuongeza uwazi katika umiliki wa maeneo na kusaidia wananchi kupata huduma kwa haraka zaidi.

“Mpaka sasa ni halmashauri chache sana ambazo zimefanikiwa kupata mfumo wa kidijitali wa usimamizi wa ardhi. Serikali inapaswa kuhakikisha mfumo huu unasambazwa nchi nzima ili kupunguza migogoro ya ardhi na kuongeza ufanisi katika sekta hii muhimu,” amwsema Mzava.

Mbunge huyo alikiri kuwa utekelezaji wa mpango huo unahitaji fedha nyingi, lakini akasisitiza kuwa umuhimu wa sekta ya ardhi kwa uchumi wa taifa unapaswa kupewa kipaumbele maalum.

Amesema mapato yanayotokana na kodi na pango la ardhi yanaweza kutumika kusaidia kuendeleza mifumo hiyo ya kisasa, huku akiishauri Serikali kuhakikisha sehemu ya fedha zinazokusanywa na Wizara ya Ardhi zinabaki wizara hiyo ili kusaidia kuimarisha mifumo ya usimamizi na kuongeza uwezo wa ukusanyaji wa mapato zaidi.

“Kazi ya kusambaza mfumo huu nchi nzima siyo ndogo, ninafahamu kutakuwa na changamoto ya upatikanaji wa fedha. Lakini kutokana na umuhimu wa sekta ya ardhi, naiomba Serikali mapato yanayotokana na kodi na pango la ardhi yarudishwe kwa kiwango kikubwa zaidi wizara husika ili waweze kuendelea kutengeneza mifumo na kuboresha ukusanyaji wa mapato,” amesisitiza.

Mnzava ameeleza kuwa katika baadhi ya nchi zilizoendelea, sekta ya ardhi imekuwa chanzo kikubwa cha mapato ya Serikali kupitia kodi mbalimbali zinazotokana na umiliki na matumizi ya ardhi, hivyo Tanzania nayo inaweza kunufaika zaidi iwapo itawekeza vya kutosha katika mifumo ya kisasa ya usimamizi wa ardhi.

Aidha, ameipongeza Wizara ya Ardhi kwa juhudi zake za kuongeza makusanyo ya mapato na kuendelea kuboresha huduma kwa wananchi, huku akiitaka Serikali kuendelea kuiwezesha wizara hiyo ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.

“Tunaona kazi kubwa inayofanywa na Wizara ya Ardhi katika kuongeza makusanyo ya Serikali. Sasa ni wakati wa Serikali kuendelea kupeleka fedha zaidi kwa wizara hiyo ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi na kuendelea kulitumikia taifa,” alisema.

Kauli ya mbunge huyo imekuja wakati ambapo Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za umma, ikiwa ni pamoja na usimamizi wa ardhi na upangaji wa matumizi bora ya maeneo nchini.


Na Karama Kenyunko - Michuzi Tv

Wafanyabiashara watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni wakikabiliwa na tuhuma za makosa ya Uhujumu Uchumi, wakidaiwa kutoa taarifa za uongo kwa maofisa wa forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kusababisha mamlaka hiyo hasara ya zaidi ya Sh milioni 120.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutekeleza makosa hayo katika mipaka ya Sirari mkoani Mara, Mkenda na Kawale mkoani Ruvuma, kwa lengo la kujipatia vibali vya muda vya matumizi ya magari yaliyokuwa yamesajiliwa kwa namba za Afrika Kusini.

Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani na Wakili wa Serikali, Godfrey Nugu akisaidiana na Rozalia Rutagwerela, washtakiwa hao wametajwa kuwa ni George Kaiza (35), Hosiana Sanga (31) na Hamu Sanga (26).

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhani Rugemarila, upande wa mashtaka ulidai kuwa katika kesi namba 11588/2026 inayomkabili George Kaiza pekee, mshtakiwa huyo anakabiliwa na mashtaka saba.

Inadaiwa kuwa Machi 27, 2026 katika mpaka wa Mkenda na Kawale mkoani Ruvuma, Kaiza alitoa taarifa za uongo kwa maofisa wa forodha wa TRA ili kuingiza nchini gari aina ya Toyota Fortuner lenye namba za usajili za Afrika Kusini kwa lengo la kupata kibali cha muda.

Aidha, Februari 25, 2026 katika mpaka wa Sirari mkoani Mara, Kaiza anadaiwa kutoa taarifa za uongo kwa maofisa wa TRA wakati akiingiza nchini gari aina ya Ford Ranger lenye namba za usajili za Afrika Kusini kwa lengo la kujipatia kibali cha muda kwa njia ya udanganyifu.

Upande wa mashtaka ulidai pia kuwa Kaiza aliuza magari hayo kinyume cha sheria huku akijua kuwa yalikuwa yamepewa vibali vya muda na TRA.

Wakili Nugu alidai kuwa Machi 27, 2026 katika mpaka wa Mkenda na Kawale mkoani Ruvuma, Kaiza alikwepa kwa makusudi kulipa ushuru wa zaidi ya Sh milioni 84 kwa magari mawili ambayo ni Toyota Fortuner na Ford Ranger yaliyokuwa na namba za usajili za Afrika Kusini, jambo ambalo alifahamu kuwa ni kinyume na sheria.

Hata hivyo, Kaiza hakutakiwa kujibu chochote mahakamani kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za Uhujumu Uchumi. Upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Kwa upande wa washtakiwa Hosiana na Hamu, wanadaiwa kuwa Januari 25, 2026 katika eneo la Tunduma mkoani Songwe walitoa taarifa za uongo ili kujipatia kibali cha muda na kuingiza nchini gari aina ya Ford Ranger lenye namba za usajili za Afrika Kusini.

Inadaiwa kuwa kwa kufanya hivyo, waliisababishia TRA hasara ya Sh milioni 35.5 kutokana na kukwepa kulipa ushuru wa uingizaji wa gari hilo huku wakijua kuwa kitendo hicho ni kinyume cha sheria.

Licha ya dhamana kuwa wazi, hadi wakati Michuzi Blog inaondoka mahakamani, washtakiwa wote walikuwa bado wamerudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyotaka kila mmoja kuwa na wadhamini wawili, kuweka fedha taslimu sawa na nusu ya kiasi cha hasara kinachodaiwa kusababishwa au kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 9, 2026 kwa ajili ya kutajwa.