"AFYA"
Showing posts with label AFYA. Show all posts

Na John Mapepele, Mafia

Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa amemtaka Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dkt. Grace Magembe kuunda Kamati ya uchunguzi ili kuchunguza utolewaji wa huduma katika Hospitali ya  Wilaya ya Mafia ili kuboresha huduma katika hospitali hiyo.

Mhe. Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo Novemba 16, 2026  baada ya kufanya ziara ya kikazi na kukagua maeneo mbalimbali ya Hospitali hiyo ambapo hakuridhishwa na utendaji kazi.

Ninamuelekeza Katibu Mkuu kuunda timu kuja kufanya uchunguzi na kubaini changamoto ili kuja na suluhisho la maboresho ya kudumu katika hospitali

Amesema dhamira ya Serikali kwa sasa  ni kuifanya hospitali hiyo kutoa huduma za afya kwa kiwango cha kisasa na kuachana na mazoea.

amefafanua sababu za kuifanya Hospitali hiyo kutoa huduma kwa kiwango cha kisasa kuwa ni pamoja na sehemu ya kisiwa hicho  kuwa na Hifadhi ya Bahari ambayo huleta wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali duniani.

"Sote tunajua eneo hili la mafia ni eneo la kimkakati katika nchi yetu lina Hifadhi ya Bahari ambayo inatembelewa na watalii wengi hivyo pindi wanapopata shida za kiafya lazima tuwe na hospitali inayoweza kutoa huduma ya uhakika tofauti na sasa". Ameongeza Mhe. Mchengerwa

Aidha, ameitaja sababu nyingine kuwa kisiwa cha Mafia kipo pembeni mwa Tanzania bara na bado hakuna usafiri wa uhakika hivyo ni muhimu kuwa na huduma zilizoboreka.

Ametoa wiki mbili kwa uongozi wa hospitali hiyo kufunga mashine za kisasa  za  X-ray ambazo imepelekwa kwenye zahanati ya Chole.

"Naelekeza ile X-ray Mashine ya kisasa ambayo haijafungwa kwenye zahanati ya Chole sasa ije ifungwe hapa kwa kuwa hapa kuna uhitaji zaidi kuliko kule." amesisitiza Mhe. Waziri Mchengerwa.

Katika ziara hiyo ambayo aliambatana na Mkurugenzi wa Idara Kinga Dkt. Hamad Nyembea alipata fursa ya kuongea na wagonjwa waliofika kutibiwa.










Mwalimu wa elimu maalum na mzazi wa mtoto aliyezaliwa njiti, Dkt. Silvia Rwambo akizungumza katika maadhimisho hayo, yaliyoandaliwa na Dorice Mollel Foundation Jijini Dar es Salaam, Novemba 15,2026.





Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
KUELEKEA Siku ya Mtoto Njiti Duniani inayoadhimishwa Novemba 17 kila mwaka, wazazi wenye watoto waliozaliwa kabla ya wakati wameiomba Serikali na wadau wa afya kuboresha mazingira ya hospitali kwa ajili ya watoto hao na wazazi wao, ikiwamo kuweka huduma za ushauri nasaha na msaada wa kisaikolojia.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, yaliyoandaliwa na Dorice Mollel Foundation Jijini Dar es Salaam, Novemba 15,2026, mwalimu wa elimu maalum na mzazi wa mtoto aliyezaliwa njiti, Dkt. Silvia Rwambo, amesema wazazi wengi hupitia msongo mkubwa wa mawazo, hofu na wakati mwingine huzuni kutokana na changamoto wanazokutana nazo wakati watoto wao wanapokuwa wodini.

Amesema baadhi ya wazazi hupoteza watoto wakiwa hospitalini, huku wengine wakiwa na watoto zaidi ya mmoja wanaohitaji huduma maalum, hali inayofanya umuhimu wa kupata msaada wa kisaikolojia na kijamii kuwa mkubwa ili wazazi hao waweze kukabiliana na hali hiyo.

Dkt. Rwambo amesema pia kuna umuhimu wa kuwapatia wazazi taarifa sahihi kuhusu watoto njiti pamoja na kuwaunganisha na wazazi wengine ambao tayari wamepitia hali hiyo, kwa kuwa uzoefu wa mzazi aliyewahi kulea mtoto njiti unaweza kuwa msaada mkubwa kwa mzazi anayekabiliwa na hali hiyo kwa mara ya kwanza.

Amesema Mtandao wa Wazazi wenye Watoto Njiti Tanzania, uliozinduliwa rasmi mwaka 2022 na kuwa na zaidi ya wazazi 200 kutoka maeneo mbalimbali nchini, umekuwa ukitembelea watoto njiti waliolazwa hospitalini, kuwafariji wazazi na kutoa msaada kulingana na mahitaji yao, ikiwamo kuchangisha fedha kwa familia zinazokabiliwa na changamoto.

“Tunatamani mama anayejifungua mtoto njiti apate taarifa sahihi na apate wenzake wa kumtia moyo na kumweleza. Tunajua mtoto njiti anaweza kumletea mzazi hofu, hasa anapomuona mtoto akiwa mdogo sana na akiwa kwenye mashine za kumsaidia kupumua,” amesema.

Aidha, amesema wazazi wanahitaji mazingira rafiki hospitalini, yakiwamo sehemu salama za kula, kupumzika, kuoga, kukamua na kuhifadhi maziwa ya mtoto, pamoja na sehemu za ibada na faragha kwa ajili ya kupata ushauri au kukabiliana na changamoto za kihisia wanazopitia wakati wa kukaa hospitalini.

Amesema pia ni muhimu kuwepo maeneo maalum ambayo wazazi wanaweza kukutana na ndugu zao bila kulazimika kutoka wodini au kukutana nao kwenye korido, huku akisisitiza umuhimu wa kuboresha mazingira ya hospitali kwa ujumla ili yaweze kumhudumia mzazi na mtoto kwa pamoja.

“Tunatamani vitu hivi vyote viwe chini ya jengo moja, lakini katika maeneo tofauti, ili mzazi aweze kukaa kwa amani na kumlea mtoto wake vizuri. Haya si mahitaji yanayohitaji gharama kubwa pekee, bali yanahitaji utashi, utayari na kusikiliza kile ambacho wazazi tunakisema,” amesema.

Dkt. Rwambo amesema wazazi wa watoto njiti huenda wasiwe wataalamu wa kubuni majengo, miundombinu ya hospitali, udaktari au uuguzi, lakini wana uzoefu wa moja kwa moja wa changamoto wanazopitia wao na watoto wao, hivyo maoni yao yanapaswa kuzingatiwa katika uboreshaji wa huduma kwa watoto njiti nchini.


Na Mwandishi Wetu
HUDUMA za afya kwa watoto njiti na wanaozaliwa wakiwa na changamoto mbalimbali zimeonyesha mafanikio makubwa katika Wilaya ya Kwimba, Mwanza, baada ya kuanzishwa kwa Kitengo cha Huduma kwa Mama na Mtoto, hatua iliyosaidia kupunguza kwa asilimia 64 kiwango cha vifo vya watoto wanaolazwa katika kituo hicho.

Akizungumza Novemba 15, 2026, Muuguzi Daraja la II na Mkuu wa Wodi ya Watoto Wachanga katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba, Ernest John Kibona, amesema katika miezi tisa ya kwanza tangu kitengo hicho kuanza kufanya kazi, jumla ya watoto 542 wenye matatizo mbalimbali ya kiafya wamehudumiwa, ikilinganishwa na watoto 183 waliopatiwa huduma katika kipindi kama hicho kabla ya kuanzishwa kwa kitengo hicho.

Kibona amesema kati ya watoto 542 waliolazwa tangu kitengo hicho kilipoanza kufanya kazi Februari 26, 2026, watoto 250 sawa na asilimia 46 walikuwa wamezaliwa kabla ya wakati, huku watoto 66 sawa na takribani asilimia 12 ya waliolazwa wakifariki. Amesema hali hiyo ni tofauti na kipindi cha miezi tisa iliyotangulia, ambapo kati ya watoto 183 waliolazwa, 63 walifariki, sawa na asilimia 34.

Amesema takwimu hizo zinaonyesha kupungua kwa takribani asilimia 64 kwa uwiano wa vifo vya watoto waliolazwa, licha ya kuongezeka kwa kiasi kikubwa kwa idadi ya watoto wanaopatiwa matibabu katika kituo hicho.

Mbali na kuongeza upatikanaji wa huduma za matibabu, kuanzishwa kwa kitengo hicho kumepunguza pia ulazima wa familia kusafiri nje ya wilaya kutafuta huduma maalumu kwa watoto wachanga, hususan katika Jiji la Mwanza ambako hospitali za rufaa ziko zaidi ya kilomita 90 kutoka Kwimba.

Kabla ya kuanzishwa kwa kitengo hicho, watoto wachanga waliohitaji huduma maalumu walikuwa wakipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou Toure na Bugando Medical Centre. Safari hizo ziliongeza gharama na changamoto za usafiri kwa familia, huku Kibona akisema idadi ya rufaa kwenda hospitali za Mwanza imepungua kwa zaidi ya asilimia 67, wakati kitengo hicho sasa kinahudumia pia wagonjwa kutoka wilaya tano jirani.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Doris Mollel Foundation, Doris Mollel, kabla ya huduma hizo kusogezwa karibu na wananchi, baadhi ya mama walilazimika kupitia hatua kadhaa za rufaa kabla ya watoto wao kupata huduma stahiki. Amesema mama anaweza kuanza safari ya kujifungua katika zahanati, lakini mtoto akizaliwa njiti huhitaji kupelekwa kituo cha afya kwa huduma maalumu, huku baadhi ya vituo hivyo vikiwa umbali wa hadi saa mbili kutoka Hospitali ya Wilaya ya Kwimba.

Amesema iwapo kituo cha afya hakina uwezo wa kutoa huduma inayohitajika, mtoto hulazimika kupewa rufaa nyingine kwenda hospitali ya mkoa, hali ambayo huongeza hatari kwa mtoto pamoja na mzigo wa kifedha na kimazingira kwa familia. Kwa hiyo, amesema kuanzishwa kwa Kitengo cha Huduma kwa Mama na Mtoto, kwa msaada wa Doris Mollel Foundation, kumechangia kusogeza huduma za watoto wachanga karibu na jamii na kupunguza safari ndefu za kutafuta matibabu.

Mafanikio hayo yanakuja wakati Tanzania ikiendelea kukabiliwa na changamoto ya vifo vya watoto wachanga, hasa ndani ya siku 28 za kwanza baada ya kuzaliwa. Kwa mujibu wa Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto pamoja na Viashiria vya Malaria Tanzania wa mwaka 2022, kiwango cha vifo vya watoto wachanga nchini kilikuwa vifo 24 kwa kila vizazi hai 1,000, kutoka vifo 25 kwa kila vizazi hai 1,000 vilivyorekodiwa katika utafiti wa mwaka 2015/16.

Hata hivyo, Kibona amesema kitengo hicho bado kinakabiliwa na changamoto za uhaba wa wataalamu na vifaa muhimu vya matibabu, hali inayopunguza uwezo wa kutoa huduma kamili kwa idadi inayoongezeka ya watoto wanaohitaji matibabu. Amesema kuna uhitaji wa mtaalamu wa huduma za watoto wachanga, madaktari zaidi pamoja na wauguzi wa kuongeza nguvu katika kitengo hicho.

Amesema pia kitengo hakina kiwanda cha kuzalisha oksijeni na kinahitaji vifaa zaidi, ikiwamo radiant warmers kwa ajili ya kudhibiti joto la mwili wa watoto wachanga pamoja na mashine za phototherapy zinazotumika kutibu manjano kwa watoto wachanga. Changamoto hizo zinaonyesha umuhimu wa kuambatana kwa uwekezaji katika miundombinu ya afya na uwezeshaji wa kutosha kwa wataalamu, vifaa na dawa ili huduma ziendelee kuwa bora.

Wakati huo huo, katika kuadhimisha Siku ya Watoto Njiti Duniani mwaka huu, Doris Mollel Foundation imeandaa hafla ya jioni jijini Dar es Salaam, ambapo vitabu vitatu vinavyolenga kuongeza uelewa kuhusu watoto njiti, ushiriki wa wazazi na huduma kwa watoto wachanga vinatarajiwa kuzinduliwa.

Machapisho hayo ni My Baby Is Born Too Soon. What Do I Do? (Nimezaa Njiti, Nifanyeje?), kinachotoa mwongozo kwa wazazi na walezi; How We Want Neonatal Care Units to Look Like, kilichoandaliwa na Tanzania Preterm Family Network; pamoja na mwongozo kuhusu utoaji wa huduma na msaada wa kisaikolojia kwa mama walio na watoto njiti.

Machapisho hayo yanalenga kushughulikia mahitaji ya kitabibu, kihisia na kisaikolojia ya familia zinazokumbwa na changamoto ya kujifungua watoto njiti, sambamba na kutoa mwongozo kwa wahudumu wa afya na wadau wanaohusika na upangaji na uendelezaji wa vituo vya huduma za watoto wachanga. Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence George Samizi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepanga kutumia uzoefu wa Tanzania katika kuimarisha huduma za watoto njiti kuhamasisha nchi nyingine za Afrika kuwekeza katika ujenzi wa wodi maalumu za watoto wachanga, huku akichangia ujenzi wa wodi hizo katika baadhi ya nchi za Bara la Afrika.

Hayo yameelezwa Novemba 11, 2026, na Mshauri wa Rais wa Masuala ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto na Mkuu wa Sekretarieti ya Kinara wa Umoja wa Afrika wa Masuala ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa ziara katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza, ambako amejionea mafanikio ya wodi maalumu ya watoto njiti.

“Rais Dkt. Samia amepewa dhamana na Wakuu wa nchi 55 na Viongozi wanachama wa Umoja wa Afrika kuwa Kinara wa masuala ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto barani humo, amedhamiria kuendeleza uwekezaji katika huduma zinazookoa maisha ya wanawake na watoto, ndani na nje ya Tanzania” amesema Mhe. Ummy Mwalimu

Amesema wodi hiyo ni mfano wa uwekezaji ambao Tanzania kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo ya Sekta ya Afya wanakusudia kuutumia kuhamasisha nchi nyingine za Afrika kuongeza uwekezaji katika huduma za kuokoa maisha ya watoto wachanga.

Akifafanua namna uzoefu wa Kwimba utakavyotumika katika kuhamasisha nchi nyingine za Afrika, Mhe. Ummy amesema Tanzania itatumia mfumo wa kuhamasisha uwekezaji kwa vitendo, ambapo Rais Samia atatoa mchango wa kujenga wodi katika nchi nyingine pamoja na kusomesha wataalam wa Afya ya Mama na Mtoto huku akiendelea kuzihamasisha Serikali za. nchi husika kuongeza uwekezaji katika miundombinu na rasilimali watu.

Katika hatua nyingine, Mhe. Ummy amebainisha kuwa Rais Dkt. Samia ametoa ahadi ya kuchangia Shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya wazazi katika hospitali hiyo ili kuendelea kuimarisha huduma za afya ya uzazi Wilayani Kwimba.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Watoto Wachanga, Watoto na Vijana kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Felix Bundala, amesema katika kipindi cha miezi tisa baada ya kuanzishwa kwa wodi hiyo katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba, idadi ya watoto waliopata huduma imeongezeka kutoka 183 hadi 542, huku rufaa zikipungua kwa asilimia 70 na vifo vya watoto waliolazwa vikishuka kutoka asilimia 34 hadi asilimia 12.

Amesema mafanikio hayo yanaunga mkono mpango wa Serikali wa kujenga wodi maalumu za watoto njiti zisizopungua 60 ifikapo mwaka 2028, kwa lengo la kupunguza vifo vya watoto wachanga na kufikia lengo la vifo 12 au chini ya hapo kwa kila vizazi hai 1,000 ifikapo mwaka 2030.

“Uwekezaji huu ni sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya Rais Samia, Kinara wa Umoja wa Afrika (AU) wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, inayolenga kufikia malengo makuu matatu ya sifuri: sifuri ya uzazi wa nyumbani, sifuri ya vifo vinavyoweza kuzuilika vya kina mama na watoto wachanga, na sifuri ya watoto wasiopata chanjo” amefafanua Dkt. Bundala.

Wodi ya kwanza na ya kisasa nchini kwa ajili ya watoto njiti imejengwa na taasisi ya Doris Mollel kwa kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine wa maendeleo ya Sekta ya Afya ni kielelezo hai cha namna ushirikiano kwenye maendeleo ya Sekta ya Afya unavyoweza kuleta tija katika upatikanaji wa Huduma za Afya.













Na FARIDA MANGUBE, MOROGORO

Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Hamis Taletale maarufu Babu Tale, amegaramia huduma za matibabu ya kibingwa bure kwa wananchi kupitia kambi maalumu ya afya inayoendelea katika Tarafa ya Ngerengere.

Kambi hiyo ya siku 10, iliyoanza Novemba 10 hadi 20, 2026, imeandaliwa kwa ushirikiano na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), ikilenga kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi uliofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Queen Sendiga, Babu Tale amesema wananchi watapata vipimo, matibabu na dawa bila malipo, ili kuhakikisha hakuna anayekosa huduma kwa sababu ya ukosefu wa fedha.

Huduma zinazotolewa ni pamoja na uchunguzi wa moyo kwa teknolojia za ECHO na ECG, ushauri wa madaktari bingwa pamoja na matibabu kulingana na mahitaji ya wagonjwa.

Aidha, Babu Tale ametangaza mpango wa kutoa bima za afya bure kwa kaya maskini 150 ndani ya jimbo hilo, hatua inayolenga kuwasaidia wananchi wenye kipato duni kupata huduma za afya.

Kambi hiyo inatarajiwa kunufaisha wakazi wa Ngerengere na maeneo jirani kwa kuwawezesha kupata huduma za kibingwa ambazo awali zilikuwa changamoto kutokana na gharama na umbali wa vituo vya matibabu.








Ujenzi wa Ghala Jipya la Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Kagera lililopo Chato, mkoani Geita, umefikia asilimia 97 ya utekelezaji, hatua inayotarajiwa kuongeza uwezo wa taasisi hiyo kuhifadhi bidhaa za afya kwa ufanisi zaidi katika mikoa ya Kagera, Geita na maeneo jirani pindi litakapoanza kutumika.

Ghala hilo lenye ukubwa wa mita za mraba 4,800 na kugharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 19 linatarajiwa kuwa kitovu muhimu cha kuhifadhi na kusambaza bidhaa za afya, huku likiongeza wigo wa huduma kutoka halmashauri 11 zinazohudumiwa sasa hadi Halmashauri 17.

Meneja wa MSD Kanda ya Kagera, Kalendero Masatu, amesema kukamilika kwa ghala hilo kutawawezesha kuongeza uwezo wa kuhifadhi bidhaa nyingi zaidi katika ubora unaohitajika na kupanua huduma kwa wateja wake.

“Tunatoa huduma kutokea ofisi zetu zilizopo Wilaya ya  Muleba, Mkoa wa Kagera katika mazingira magumu kutokana na ufinyu wa nafasi ya kuhifadhi bidhaa pamoja na changamoto za hali ya hewa, hususan mvua nyingi zinazonyesha katika eneo hilo” amesema Masatu.

Ameeleza kuwa kupitia ghala jipya la Chato, Kanda hiyo itaongeza maeneo ya huduma kwa kujumuisha halmashauri zilizokuwa zikihudumiwa na Kanda ya Mwanza, pamoja na kuongeza halmashauri nyingine mbili kutoka Mkoa wa Kigoma, zilizokuwa zikihudumiwa na Kanda ya Tabora.

“Kwa uwepo wa ghala hili sasa tunaenda kutunza mzigo mkubwa na hivyo tutaweza kuwahudumia wateja wetu kwa upana zaidi. Pia, maeneo haya yako karibu nasi, hivyo tutarahisisha usambazaji na kupunguza gharama ambazo taasisi ilikuwa ikitumia,” amesema Masatu.

Kwa upande wa utekelezaji wa mradi, Mhandisi wa Kampuni ya HAINAN International Ltd, Patrick Laibo, amesema ujenzi ulianza Agosti 20, 2025 na ulipangwa kutekelezwa kwa kipindi cha miezi 14.

Amesema kwa sasa jengo la ofisi limefikia asilimia 99 ya utekelezaji, ghala kuu likiwa katika asilimia 96 kutokana na kazi za mwisho za ufungaji na ukamilishaji wa mfumo wa viyoyozi (AC), huku miundombinu ya nje ikiwa karibu kukamilika kwa asilimia 100.

Ameongeza kuwa kwa ujumla mradi umefikia asilimia 97 na kazi zilizobaki ni za ukamilishaji wa mifumo na maeneo machache ya mradi.

Mbali na kuimarisha miundombinu ya MSD, mradi huo umekuwa chanzo cha ajira kwa wananchi wa Chato, ambapo zaidi ya vijana 100 wamepata fursa za ajira kupitia utekelezaji wake. Mhandisi Laibo amesema mradi huo umechangia pia kuwajengea vijana uwezo na uzoefu wa kitaalamu kupitia ushiriki wao katika shughuli mbalimbali za ujenzi.

Akizungumzia mazingira ya kazi katika ghala hilo, Afisa Huduma kwa Wateja wa MSD Kagera, Julieth Msele, amesema jengo hilo lina nafasi kubwa na mazingira mazuri yatakayorahisisha utoaji wa huduma kwa wateja pamoja na uhifadhi wa bidhaa mbalimbali za afya.

Naye Fundi wa Mifumo ya Njia ya Hewa, Joseph Mwatoine, amesema mradi huo umekuwa fursa muhimu kwa vijana kupata ajira, kujiongezea kipato na kupata uzoefu wa kitaalamu kupitia ushiriki wao katika utekelezaji wa kazi mbalimbali za ujenzi.

Bi. Hellen Juma, mkazi wa Chato ameishukuru Serikali kwa kuleta mradi huo katika eneo hilo, akieleza kuwa mbali na kutoa ajira kwa wananchi, uwepo wa ghala hilo utarahisisha upatikanaji wa dawa kwa vituo vya kutolea huduma za afya vilivyopo maeneo ya jirani.












Na Mwandishi Wetu
BANDARI SACCOS, kwa kushirikiana na Bandari Foundation, imeendelea kuimarisha ushirikiano na jamii kupitia shughuli za uchangiaji damu, upimaji wa afya bila malipo na utoaji wa elimu ya afya. Shughuli hizo ni sehemu ya juhudi za kuboresha ustawi wa wananchi na kuwasaidia kupata huduma muhimu za kijamii.

Akizungumza katika viwanja vya Mwembeyanga jijini Dar Es Salaam leo Oktoba 26, 2026 kuhusu shughuli hizo, Mtendaji Mkuu wa Bandari SACCOS na mjumbe wa Bandari Foundation, Godfrey Rwehumbiza, amesema taasisi hizo zimejipanga kuhamasisha wananchi kujitokeza kuchangia damu, huku zikiendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa zoezi hilo, vigezo vinavyopaswa kuzingatiwa na mchango wa uchangiaji damu katika kuwasaidia wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.

Rwehumbiza amesema shughuli hizo pia zinahusisha upimaji wa afya bila malipo, kwa kushirikiana na wadau wa afya, wakiwamo Hospitali ya Bandari na Hospitali ya Temeke, ili kuwawezesha wananchi kufahamu hali zao za kiafya na kupata ushauri kutoka kwa wataalamu.

Kwa upande wake, Mwanachama wa Bandarini Saccos na mwanachama pia wa Bandarini Foundation, Juhudi Nyambuka amesema wananchi watapata elimu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza, yakiwamo magonjwa ya moyo na kisukari, pamoja na umuhimu wa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kubaini changamoto zinazoweza kujitokeza na kuchukua hatua stahiki mapema.

Nyambuka amesisitiza kuwa huduma hizo hazilengi watu wanaotaka kuchangia damu pekee, bali pia wananchi wanaohitaji kupima afya zao na kupata ushauri wa kitaalamu. Hivyo, amewahimiza wananchi kutumia fursa hiyo kujifunza zaidi kuhusu afya zao na namna ya kujikinga na magonjwa mbalimbali.

Aidha, amesema waandaaji wameweka utaratibu wa kufikisha huduma za uchangiaji damu katika maeneo mbalimbali ili kurahisisha upatikanaji wake. Taasisi, vikundi na maeneo yenye watu wasiopungua 10 wanaohitaji huduma hiyo yanaweza kutoa taarifa kwa waandaaji ili timu ya wataalamu ifike walipo na kutekeleza zoezi hilo.

Amesema utaratibu huo unalenga kuwafikia wananchi ambao wanaweza kushindwa kufika katika kituo kikuu cha shughuli hizo, huku akieleza kuwa huduma hizo zitapatikana katika maeneo yatakayopangwa kwa kushirikiana na waandaaji.

Kwa mujibu wa wazungumzaji hao, shughuli hizo zinatarajiwa kuendelea hadi Oktoba 19, huku wananchi wakihimizwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchangiaji damu na kutumia huduma za afya zinazotolewa.

Mbali na huduma za afya, Bandari SACCOS na Bandari Foundation zinaendelea kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kutoa elimu ya fedha kwa jamii. Wananchi pia watapata fursa ya kufahamu huduma na masharti ya kujiunga na Bandari SACCOS, ikiwa ni sehemu ya juhudi za taasisi hizo kuimarisha ustawi wa jamii.




NA DENIS MLOWE, IRINGA


SERIKALI imeombwa kuhakikisha watoto wenye ulemavu na yatima wanaotoka katika familia zenye hali duni ya kiuchumi wanapewa kipaumbele katika upatikanaji wa bima ya afya, ili kuwawezesha kupata matibabu kwa wakati bila kuathiri hali ya kiuchumi ya familia zao.

Ombi hilo limetolewa na Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Lebao’s Kids Foundation (BKF), Theophil Muyinga, wakati wa zoezi la kugawa bima za afya kwa watoto wenye ulemavu wanaohudumiwa na taasisi hiyo pamoja na watoto yatima kutoka kituo cha kulelea watoto yatima kilichopo Migoli, mkoani Iringa.

Zoezi hilo limeandaliwa na BKF kwa kushirikiana na Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii (CHF), ikiwa ni sehemu ya juhudi za kusaidia watoto wenye uhitaji kupata huduma za afya na kupunguza changamoto zinazowakabili wanapohitaji matibabu.

Muyinga amesema familia nyingi za watoto hao zinakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi, jambo linalozifanya kushindwa kumudu gharama za matibabu, hivyo umuhimu wa Serikali kuweka utaratibu utakaohakikisha watoto hao wanapata bima ya afya kwa kuzingatia mahitaji yao maalumu.

Amesema upatikanaji wa bima ya afya kwa watoto wenye ulemavu na yatima ni hatua muhimu katika kulinda afya zao na kuhakikisha changamoto za kifedha hazigeuki kuwa kikwazo cha kupata huduma za matibabu wanapougua.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwenza wa BKF, Catherine Moreno, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza juhudi za kusaidia watoto wenye uhitaji, akieleza kuwa upatikanaji wa huduma za afya ni miongoni mwa mahitaji muhimu yanayopaswa kuzingatiwa katika ustawi wa watoto hao.

Akijibu ombi hilo, Afisa Uandikishaji wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) katika Manispaa ya Iringa, Kokwiliza Katemana, amesema Serikali ina jukumu la kulinda afya za wananchi wake, huku watoto wakiwa miongoni mwa makundi yanayohitaji kupewa kipaumbele katika upatikanaji wa huduma za afya.

Katemana amesema katika awamu hii, Serikali imeweka mkazo katika kuwafikia watu wa makundi maalumu pamoja na kaya zisizo na uwezo wa kiuchumi, ili kuhakikisha nao wanapata fursa ya kunufaika na huduma za bima ya afya.

Amesema juhudi hizo zinalenga kupanua wigo wa wananchi wanaofikiwa na huduma za bima ya afya, hususan wale ambao hali zao za kiuchumi zinawafanya washindwe kugharamia matibabu wanapougua.

Utoaji wa bima hizo unatarajiwa kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa watoto hao na familia zao, huku ukiwapa nafasi ya kupata huduma za afya kwa urahisi zaidi wanapokabiliwa na changamoto za kiafya.

Hatua hiyo inaendana na juhudi za Serikali za kutekeleza awamu ya pili ya mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, unaolenga kupanua upatikanaji wa huduma za afya na kupunguza gharama za matibabu zinazobebwa na wananchi.

Kwa watoto wenye ulemavu na yatima kutoka familia zenye kipato cha chini, upatikanaji wa bima ya afya ni sehemu muhimu ya kuhakikisha wanapata huduma za matibabu bila kubaguliwa kutokana na hali zao za kiuchumi.