▪️︎ Ataka maandalizi ya eneo la ekari 50 kwa shughuli za kiuchumi za vijana yaharakishwe

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameagiza kukamilishwa haraka kwa uthamini wa maeneo yanayohitajika kwa uwekezaji katika Eneo Maalumu la Kiuchumi la Bagamoyo ili wananchi walipwe fidia na miradi iendelee bila migogoro.

Ametoa maelekezo hayo leo, Ijumaa, Oktoba 16, 2026, alipokagua maendeleo ya ujenzi wa kongani ya viwanda ya kampuni ya Hongwang Tanzania (HWTZ SEZ Limited), wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani.

Dkt. Mwigulu ameelekeza Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na uongozi wa mkoa na wilaya kukamilisha uthamini huo. Amesema serikali imeweka chanzo mahususi cha fedha za kulipa fidia kwa wananchi wanaopisha miradi ya maendeleo.

“Fanyeni uthamini, wanaoachia maeneo kupisha uwekezaji walipwe haki yao,” amesema.

Amesisitiza kuwa baada ya malipo ya fidia, maeneo hayo yapatiwe hati za kisheria na kuwekewa mipaka inayoeleweka ili kuzuia uvamizi. Akijibu maelezo kuwa uthamini ulisimama kutokana na tahadhari za mvua za El Niño, ameagiza kazi iendelee huku tahadhari zikizingatiwa.

“Tuchukue tahadhari huku tukiendelea na kazi,” amesema.

Kuhusu vijana, Waziri Mkuu ameagiza kuharakishwa kwa maandalizi ya eneo la ekari 50 lililotengwa kwa ajili ya mabanda ya viwanda na kituo cha mauzo ya nje. Amesema upatikanaji wa maeneo ya uzalishaji na biashara ni muhimu katika kuwawezesha vijana kushiriki katika uchumi na kutengeneza ajira.

Dkt. Mwigulu amesema kufikia malengo ya Dira ya Taifa 2050 kunahitaji ushiriki mpana wa wananchi na sekta binafsi imara. Amehimiza kuanzishwa kwa shughuli mpya za uzalishaji zitakazopanua ajira na vyanzo vya mapato ya serikali, huku akisisitiza kuwa utatuzi wa migogoro ya ardhi kwa wakati unalinda haki za wananchi na kuwezesha uwekezaji kufanyika kwa amani.

Aidha, amepongeza maendeleo ya kongani hiyo, akisema yanaonesha hatua za utekelezaji wa maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kujenga uchumi wa uzalishaji.

Awali, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Fred Msemwa, amesema uwekezaji wa ndani na nje una mchango muhimu katika kukuza uchumi kupitia ajira kwa vijana, mauzo ya nje, upatikanaji wa fedha za kigeni na teknolojia za kisasa.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Anna Limo, amesema Eneo Maalumu la Kiuchumi la Bagamoyo lina wawekezaji 36, wakiwemo wapya 25 waliopewa maeneo kuanzia Desemba 2025. Amesema eneo la hekta 5,135.22 bado halijalipiwa fidia, huku sehemu yake ikiwa ilifanyiwa uthamini mwaka 2009.

Kuhusu eneo la vijana, amesema mpango huo unalenga kuwapatia mabanda ya viwanda kwa gharama nafuu, miundombinu ya msingi, usaidizi wa leseni na vibali, pamoja na masoko ya bidhaa ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hongwang Tanzania, Sophia Su, amesema kampuni hiyo imepanga kutumia dola za Marekani milioni 150 katika awamu ya kwanza ya ujenzi wa miundombinu na uendelezaji wa eneo, huku karibu dola za Marekani milioni 30 zikiwa zimetumika hadi Oktoba 2026. Amesema kiwanda cha kuunganisha malori kinatarajiwa kuanza uzalishaji wa kibiashara kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Ameongeza kuwa mradi umetoa ajira 170 kwa Watanzania na unatarajia kufikisha takribani ajira 400 ifikapo mwisho wa mwaka, huku kampuni ikitoa kipaumbele kwa wazabuni wa ndani. Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanislaus Nyongo, amesema mkoa utaendelea kushughulikia uvamizi wa ardhi na kuimarisha miundombinu ili kuweka mazingira bora kwa wawekezaji.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema dhamira ya kimataifa ya kulinda bioanuai lazima iambatane na hatua halisi, fedha endelevu na ushiriki wa jamii ili kuhakikisha mifumo ya ikolojia inalindwa, inarejeshwa na kutumiwa kwa njia endelevu.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 16 Oktoba 2026, Jijini Yerevan, Armenia, alipohutubia Mkutano wa Viongozi kuhusu Bioanuai (Leaders’ Summit on Biodiversity) COP17, akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Amesema Tanzania imeandaa Mkakati na Mpango Kazi wa Taifa wa Bioanuai wa mwaka 2025–2030, unaolenga kuimarisha uhifadhi, urejeshaji wa mifumo ya ikolojia na matumizi endelevu ya rasilimali za kibiolojia.

Akieleza hatua zilizofikiwa Zanzibar, Rais Dkt. Mwinyi amesema maeneo ya hifadhi za bahari yameongezeka kutoka matano hadi saba, huku eneo linalosimamiwa kwa uhifadhi likiongezeka kutoka takriban kilomita za mraba 2,400 hadi zaidi ya 3,600, hatua inayochangia kulinda rasilimali za bahari na kukuza maendeleo endelevu.

Katika mkutano huo, Tanzania imeeleza kuunga mkono matokeo madhubuti ya kisiasa na utekelezaji wa malengo ya kimataifa ya bioanuai kuelekea mwaka 2030, ikiwemo lengo la kuhifadhi asilimia 30 ya maeneo ya ardhi na bahari ifikapo mwaka huo.

Katika ujumbe wa Tanzania, Rais Dkt. Mwinyi ameambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. James Kinyasi Millya; Balozi wa Tanzania nchini Urusi anayewakilisha pia Armenia, Mhe. Fredrick Ibrahim Kibuta; pamoja na viongozi na maafisa mbalimbali wa Serikali.



Azma ya Tanzania ya kufikia uchumi wenye thamani ya Dola za Marekani trilioni 1 ifikapo mwaka 2050 inahitaji ushirikiano wa kimkakati utakaounganisha mitaji ya kimataifa na fursa zenye uwezo wa kuleta mageuzi katika uzalishaji wa nchi na kuimarisha mustakabali wake wa kiuchumi wa muda mrefu.

Katika Jukwaa la Uwekezaji la Tanzania (Tanzania Investment Forum) lililofanyika jijini London hivi karibuni, Benki ya Stanbic Tanzania ilikutana na wawekezaji wa kimataifa kujadili fursa zinazoibuka katika sekta mbalimbali za uchumi, sambamba na kufanya mazungumzo ya ngazi ya juu pembezoni mwa jukwaa hilo na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, kuhusu namna ya kuhamasisha uwekezaji ili kufanikisha malengo ya maendeleo ya nchi.

Katika jukwaa hilo, Benki ya Stanbic Tanzania iliwezesha majadiliano ya kimkakati kati ya wawekezaji wa kimataifa na Serikali ya Tanzania, ikiwasilisha miradi ya kipaumbele ya Taasisi na Mashirika ya Umma, pamoja na kuainisha fursa za ushiriki wa mitaji ya sekta binafsi.

Ujumbe wa Stanbic, ukiungwa mkono na Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mhe. Balozi Mbelwa Kairuki, pia ulipata fursa ya kukutana na viongozi waandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wakiongozwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, pamoja na Mawaziri wenye dhamana ya Fedha na Uwekezaji kutoka pande zote mbili za Muungano.

Mazungumzo hayo yalijikita katika kuharakisha upatikanaji wa mitaji ya kimataifa kwa ajili ya miradi ya kipaumbele ya maendeleo nchini, kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na taasisi za fedha, pamoja na kusukuma mbele malengo mapana ya maendeleo ya Taifa.

Waziri Mkuu alisisitiza nafasi muhimu ya taasisi za fedha kama Stanbic katika kuhamasisha mitaji, kuwezesha uwekezaji na kujenga ushirikiano imara zaidi kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, ili kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akizungumza kwa niaba ya Benki ya Stanbic Tanzania, Mkuu wa Kitengo cha Uwekezaji (Investment Banking), Sarah Mkiramweni, alisisitiza dhamira ya Benki ya kuunga mkono malengo ya maendeleo ya Serikali kwa kuendelea kuhamasisha mitaji ya ndani na ya kimataifa kwa ajili ya miradi ya kimkakati ya kitaifa.

Alibainisha rekodi ya Stanbic katika eneo hili, ambapo Benki imewezesha upatikanaji wa takriban Dola za Marekani bilioni 3 katika kipindi cha miaka minne iliyopita, hatua inayodhihirisha dhamira endelevu ya Benki katika kuunganisha miradi ya kipaumbele ya Tanzania na vyanzo stahiki vya mitaji.

“Kufikia azma ya Tanzania ya kuwa na uchumi wa Dola za Marekani trilioni 1 ifikapo mwaka 2050 kutahitaji uwekezaji mkubwa na ushirikiano imara. Katika Benki ya Stanbic, jukumu letu ni kusaidia kuhamasisha mitaji inayohitajika ili kufanikisha azma hii, kwa kuiunganisha Tanzania na wawekezaji wa kimataifa na kuandaa mifumo ya ufadhili inayowezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.

Lengo letu ni kuhakikisha uwekezaji huu unaleta manufaa halisi ya kiuchumi, kuanzia kuboreshwa kwa miundombinu ya nishati na uchukuzi hadi ukuaji wa viwanda na upatikanaji wa ajira. Tunajivunia hatua zilizopigwa kwa kushirikiana na Serikali, na tunaendelea kujizatiti kuunga mkono mageuzi ya kiuchumi ya muda mrefu ya Tanzania,” alisema Mkiramweni.

Ikiwa sehemu ya Kundi la Standard Bank (Standard Bank Group), benki kubwa zaidi barani Afrika, Stanbic inaunganisha uelewa wa kina wa soko la ndani na mtandao mpana wa kikanda, pamoja na uwezo wa kufikia masoko ya fedha ya kimataifa. Tuko katika nafasi madhubuti ya kuwaunganisha wawekezaji na fursa zilizopo, na kuandaa mifumo ya ufadhili katika sekta za miundombinu, nishati, usafirishaji, ujenzi wa uchumi wa viwanda pamoja na sekta nyingine za kimkakati.

Dhamira yetu ni kusaidia kuugeuza uwezo mkubwa wa uwekezaji ulionao Tanzania kuwa matokeo halisi: biashara na makampuni yenye tija, fursa za ajira, na ukuaji endelevu wa uchumi.

Tanzania ni nyumbani kwetu. Tunachochea ukuaji wake.
Mkuu wa Kitengo cha Uwekezaji (Investment Banking) wa Benki ya Stanbic Tanzania, Sarah Mkiramweni, akiwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, pembezoni mwa Jukwaa la Uwekezaji la Tanzania (Tanzania Investment Forum) lililofanyika jijini London, Uingereza hivi karibuni.








Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo Oktoba 15, 2026 imesaini makubaliano ya kuimarisha nafasi yake kama kituo cha mafunzo ya tiba ya Interventional Radiology barani Afrika, hatua inayolenga kuongeza idadi ya wataalamu wenye ujuzi wa kutoa huduma hizo kwa kutumia teknolojia za kisasa.


Makubaliano hayo yamesainiwa sambamba na Mkutano wa Tano wa Afrika wa Interventional Radiology, uliofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency Dar es Salaam na kuwashirikisha wataalamu kutoka nchi mbalimbali za Afrika.

Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dkt. Delilah Kimambo, amesema tangu programu ya mafunzo ilipoanza mwaka 2018, hospitali hiyo imewafundisha wataalamu 22 kutoka Tanzania, Kenya, Cameroon, Nigeria na Uganda. Kati yao, 14 ni Watanzania.

Amesema makubaliano hayo yataimarisha mafunzo ya kibingwa na ushirikiano wa kitaalamu, huku yakipanua fursa kwa wataalamu wengi zaidi kupata ujuzi wa tiba hiyo inayowezesha kuchunguza na kutibu magonjwa kwa kutumia teknolojia za picha za kitabibu, mara nyingi bila kuhitaji upasuaji wa kawaida.






 


DENIS MLOWE, IRINGA

MKUU wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amewatangazia wananchi kuhusu ziara ya kikazi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, inayotarajiwa kufanyika mkoani humo Oktoba 18, 2026, ambapo atakagua miradi ya maendeleo ya elimu ya juu na miundombinu ya usafiri wa anga.

Akizungumza na waandishi wa habari, James alisema Makamu wa Rais atatembelea Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE), ambako atakagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi saba yenye thamani ya Sh bilioni 30.4.

Alisema miongoni mwa miradi hiyo ni Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), wenye thamani ya Sh bilioni 14.8, ujenzi wa maabara ya Fizikia na hosteli ya wanafunzi unaogharimu Sh bilioni saba, pamoja na ujenzi wa jengo la Sayansi na jengo la Midia Anuwai na Elimu Maalum unaogharimu Sh bilioni 7.8.

James alisema miradi hiyo inalenga kuboresha miundombinu ya elimu ya juu na mazingira ya kufundishia na kujifunzia, hatua itakayochangia kuimarisha utoaji wa elimu na kukuza maendeleo ya kiuchumi.

Aidha, Makamu wa Rais atatembelea Uwanja wa Ndege wa Iringa uliopo Nduli kukagua ujenzi wa jengo la abiria na maegesho ya magari, mradi wenye thamani ya Sh bilioni 41.06.

Kheri James alisema uwekezaji huo unalenga kuboresha huduma za usafiri wa anga na kuongeza fursa za biashara na shughuli za kiuchumi mkoani Iringa.

Alitumia fursa hiyo kuwaomba wananchi wa Manispaa ya Iringa na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki katika shughuli za ziara hiyo, akieleza kuwa ni nafasi ya kushuhudia maendeleo ya miradi inayotekelezwa mkoani humo.

Rc James aliongeza kuwa Makamu wa Rais anatarajiwa kufika Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa saa 2:00 asubuhi na baadaye kutembelea Uwanja wa Ndege wa Nduli kwa ajili ya kukagua mradi wa jengo la abiria na maegesho ya magari.

James alisema wananchi wanatarajiwa kushiriki katika mapokezi na shughuli zitakazofanyika katika maeneo hayo, huku Makamu wa Rais akitarajiwa pia kuzungumza na wananchi wa Mkoa wa Iringa.

Kwa ujumla miradi saba ya MUCE ina thamani ya Sh bilioni 30.4, huku mradi wa Uwanja wa Ndege wa Nduli ukiwa na thamani ya Sh bilioni 41.06, hivyo kufanya jumla ya uwekezaji katika miradi hiyo kuwa Sh bilioni 71.46.




‎Wanging’ombe, Njombe


‎Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilaya ya Wanging'ombe mkoani Njombe imekamilisha ujenzi wa madaraja mawili, daraja la Wanging'ombe lenye urefu wa mita 30 katika barabara ya Wanging'ombe- Wangutwa pamoja na daraja la Ukomola lenye urefu wa mita 26.1 katika barabara ya Ukomola-Ipwani.

‎Akizungumzia utekelezaji wa miradi hiyo, Meneja wa TARURA wilaya ya Wanging’ombe, Mhandisi Selemani Mziray amesema ujenzi wa madaraja hayo umetokana na changamoto kubwa zilizokuwa zikiwakabili wananchi wa maeneo hayo ambapo kipindi cha mvua maji yalikuwa yakikata mawasiliano na kuzuia shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

‎Amesema hali hiyo ilisababisha wananchi kushindwa kusafiri kutoka eneo moja kwenda jingine huku baadhi ya wanafunzi wakikosa fursa ya kufika shuleni kutokana na ugumu wa kuvuka maeneo hayo.

‎"Ujenzi wa madaraja haya mawili umetokana na kero kubwa iliyokuwa ikiwakabili wananchi hasa kipindi cha mvua walishindwa kutoka eneo moja kwenda jingine hali iliyosababisha hata watoto kushindwa kufika shuleni", amesema Mhandisi Mziray.

‎Aidha, Mhandisi Mziray ameeleza kuwa sambamba na ujenzi wa madaraja hayo, TARURA imeboresha mitaro ya kupitisha maji ili kuhakikisha maji yanapita katika njia zake bila kuathiri miundombinu ya barabara hususan katika kipindi hiki ambacho tahadhari ya mvua kubwa imetolewa.

‎Kwa upande wake, mkazi wa Wanging’ombe, Bw. Alex Benedict ameipongeza serikali kupitia TARURA kwa kukamilisha miradi hiyo akisema madaraja hayo yana umuhimu mkubwa katika kuimarisha shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa maeneo yanayohudumiwa na barabara hizo.

‎"Kipindi cha mvua tulishindwa kuvusha mazao na hata shughuli mbalimbali za kijamii zilisimama lakini kukamilika kwa miradi hii barabara zinapitika kipindi chote cha mwaka jambo litakalotusaidia kuendeleza shughuli zetu za kila siku", amesema Bw. Benedict.

‎Naye, Bw. Leonard Kayagala, mkazi wa Wanging’ombe amesema kukamilika kwa madaraja hayo kumetoa suluhisho kwa changamoto zilizokuwa zikiwakabili wananchi zikiwemo wanafunzi kushindwa kufika shuleni na wananchi kupata ugumu wa kufikia huduma muhimu za kijamii hususan huduma za afya.

‎Ameeleza kuwa miundombinu hiyo ni muhimu kwa kuwa inarahisisha usafiri na usafirishaji, inaongeza fursa za kiuchumi na kuwawezesha wananchi kupata huduma muhimu kwa wakati bila vikwazo.




Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amewataka viongozi na watendaji wa Sekta ya Maji kuhakikisha Mradi wa Kimkakati wa Maji kutoka Mto Kiwira, wenye thamani ya Shilingi bilioni 119, unatekelezwa kwa kasi na ufanisi ili kufikia Julai 2027 wananchi wa Mkoa wa Mbeya waondokane na changamoto za upatikanaji wa majisafi.

Makamu wa Rais ametoa agizo hilo leo, Oktoba 16, 2026, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo katika eneo la Forest Mpya, Jijini Mbeya, ambako Serikali inajenga tenki kubwa lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni tano za maji.

Akizungumza na viongozi na wananchi, Mhe. Ndejembi amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kubadilisha maisha ya Watanzania kwa kuhakikisha huduma muhimu za kijamii, ikiwemo majisafi, zinapatikana kwa uhakika.

Amesisitiza kuwa Mbeya ni mkoa wa kimkakati katika uchumi wa Taifa, hivyo upatikanaji wa maji ya uhakika ni jambo la msingi katika kuchochea shughuli za uzalishaji, biashara na maendeleo ya wananchi.

Aidha, Makamu wa Rais amewataka watendaji wa Serikali kusimamia kikamilifu fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, akisisitiza maelekezo ya Rais Samia ya kuhakikisha kila shilingi inayowekezwa inaleta thamani halisi na matokeo yanayoonekana kwa wananchi.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso, amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa Wizara itaendelea kuhakikisha utekelezaji wa mradi huo haukwamishwi, huku akiwataka watendaji na wataalamu kuongeza kasi na kuimarisha usimamizi ili mradi ukamilike kwa ubora na wakati.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya UWSA), mradi huo umefikia asilimia 49 ya utekelezaji, ambapo ujenzi wa banio la maji umefikia asilimia 98, tenki la kuhifadhi maji katika eneo la Forest Mpya asilimia 80, huku ulazaji wa bomba kuu la kusafirisha maji ukifikia asilimia 15.

Mradi huo unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa maji kwa lita milioni 116 kwa siku, na hivyo kupandisha uwezo wa jumla wa uzalishaji kutoka lita milioni 78 hadi milioni 195 kwa siku, hatua itakayowezesha kuhudumia wananchi wengi zaidi ifikapo mwaka 2045.

Kukamilika kwake kunatarajiwa kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya majisafi kutoka asilimia 90 hadi asilimia 100, pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata maji kwa saa 24 kwa siku, hivyo kuimarisha ustawi wa jamii na kuchochea ukuaji wa uchumi katika Jiji la Mbeya, Mji wa Mbalizi na maeneo jirani.