Timu ya Mamlaka ya hifadhi ya eneo la Ngorongoro imeagwa leo tarehe 4 Novemba, 2026 kuelekea mkoani Morogoro kushiriki mashindano ya Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi Tanzania (SHIMMUTA) ambapo imesafiri ikiwa na  ari ya kurudi na ushindi mnono kupitia michezo ya mpira wa Miguu, Netbali, Vollebal, Kamba na Michezo ya Jadi na Kuahidi kurudi na vikombe.

Akizungumza kwa niaba ya kamishna wa Uhifadhi wakati akiwaaga wachezaji hao, Naibu Kamishna huduma za Shirika, Bw. Aidan Makala , amewaasa washiriki kuzingatia nidhamu ya hali ya juu katika kipindi chote cha mashindano, akisisitiza kuwa nidhamu, umoja na ushirikiano ni msingi muhimu wa mafanikio katika michezo.

“Mnapoenda kushiriki michezo mnaitangaza Ngorongoro kupitia utalii wa michezo, ni mategeo yangu kuwa  mtakuwa mabalozi wa Ngorongoro, kuzingatia nidhamu, maadili na sheria za nchi na kuhakikisha kuwa timu yetu inarudi na vikombe vya kutosha”amesisitiza Makala.






Na Mwandishi Wetu, Addis Ababa

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Ndugu Aggrey Mwanri, ametembelea Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ethiopia, jijini Addis Ababa, leo Novemba 4, 2026, na kusaini kitabu cha wageni.

Akiwa ubalozini hapo, Mwanri alikutana na kufanya mazungumzo na maafisa wa ubalozi kuhusu masuala mbalimbali ya uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano kati ya Tanzania na Ethiopia, pamoja na nafasi ya Tanzania katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa.

Katika mazungumzo hayo, aliipongeza ofisi ya ubalozi kwa juhudi zake za kudumisha uhusiano wa kidiplomasia, urafiki na ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili.

Pia alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha shughuli za kidiplomasia na ushirikiano wa kimataifa na kikanda kwa manufaa ya nchi hizo.

Mwanri yupo nchini Ethiopia kumwakilisha Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Asha-Rose Migiro, katika Mkutano Maalumu wa Vyama vya Siasa Barani Afrika na Taasisi za Kimataifa, unaotarajiwa kufanyika jijini Addis Ababa kuanzia Novemba 5 hadi 7, 2026.

Mkutano huo unawakutanisha viongozi wa vyama vya siasa na wadau kutoka taasisi mbalimbali za kimataifa kujadili mustakabali wa Afrika, utawala bora, ushirikiano wa kisiasa na fursa za kukuza maendeleo ya kiuchumi barani humo.






NA JANE MWAKYOMA

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Rukwa imefanikiwa kurejesha Sh milioni 7.8 zilizotokana na ubadhirifu wa mapato ya ndani ya halmashauri na fedha za fidia ya mradi wa umeme, katika kipindi cha Aprili hadi Septemba 2026.

Fedha hizo zimerudishwa kufuatia hatua za ufuatiliaji na uchunguzi uliofanywa na taasisi hiyo baada ya kubaini matumizi yasiyo sahihi ya fedha za umma katika baadhi ya maeneo, ikiwemo Halmashauri za Manispaa ya Sumbawanga na Wilaya ya Kalambo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Sumbawanga, Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Rukwa, James Mbungano, alisema miongoni mwa fedha zilizorejeshwa ni Sh milioni 4, zilizokuwa sehemu ya Sh milioni 12.29 zilizolipwa kama fidia kwa mradi wa ujenzi wa njia ya umeme katika Shule ya Sekondari Makuzani, Manispaa ya Sumbawanga.

Alisema pia Sh milioni 1.365 zilizokusanywa kupitia mashine za POS na kutowasilishwa benki na aliyekuwa Afisa Mtendaji wa Kata ya Mpwapwa, Paschal Saanne, zimefanikiwa kurejeshwa. Fedha hizo zilihusisha kipindi cha Julai 2025 hadi Januari 2026.

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, TAKUKURU iliwezesha kurejeshwa kwa Sh milioni 2.44 zilizokusanywa kupitia mashine za POS lakini hazikuingizwa benki. Kati ya fedha hizo, Sh 898,600 zilihusishwa na ubadhirifu wa Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Kalemsha, Tarcisius Victor, katika kipindi cha Novemba 2019 hadi Januari 2023, huku Sh milioni 1.54 zikihusishwa na Afisa Kilimo Msaidizi wa Kijiji cha Mikonko, Hamis Mkenda Hamis, katika kipindi cha Februari 2024 hadi Mei 2026.

Kuhusu fedha za fidia za Shule ya Sekondari Makuzani, Mbungano alisema baadhi ya viongozi wa shule walizitumia kwa manufaa binafsi baada ya fedha hizo kulipwa na TANESCO kupitia Serikali ya Kijiji. Alisema TAKUKURU inaendelea kufuatilia urejeshaji wa fedha zilizobaki katika akaunti ya shule na kwamba hatua stahiki zitachukuliwa dhidi ya watuhumiwa.

Katika hatua nyingine, alisema taasisi hiyo ilifanya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha katika miradi 13 ya maendeleo yenye thamani ya Sh bilioni 3.19, ambapo ilitoa mapendekezo 34 kwa taasisi husika na yote yalipatiwa majibu.

Alisema mafanikio mengine ni kuongezeka kwa wananchi waliofikiwa na elimu ya mapambano dhidi ya rushwa kutoka 4,887 katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026 hadi 17,355 ndani ya kipindi cha miezi sita, kupitia semina 48, mikutano ya hadhara 58, maonesho sita, uimarishaji wa klabu 147 za wapinga rushwa, kuanzishwa kwa klabu moja mpya na vipindi 14 vya redio.

Aidha, TAKUKURU ilipokea malalamiko 120 katika kipindi hicho, ambapo 68 sawa na asilimia 57 yalihusu rushwa na 52 sawa na asilimia 43 hayakuhusu rushwa. Malalamiko yasiyohusu rushwa yalishughulikiwa kwa kuwashauri walalamikaji, huku uchunguzi ukiendelea kwa yale yanayohusu rushwa.

Katika upande wa mashauri ya mahakamani, Mbungano alisema kesi mpya tatu zilifunguliwa, kesi nne ziliendelea kusikilizwa na kesi mbili zilitolewa maamuzi, ambapo Jamhuri ilishinda kesi moja.

Alisema pia taasisi hiyo ilifanya uchambuzi wa mifumo mitatu katika sekta za afya, elimu na miundombinu, ikiwemo mfumo wa utoaji huduma za afya kwa makundi maalumu katika vituo vya umma wilayani Sumbawanga.

Alifafanua kuwa uchambuzi huo umewezesha kuboreshwa kwa mifumo ya kupokea malalamiko na mrejesho wa wananchi kupitia uanzishwaji wa namba maalumu za simu pamoja na kuboreshwa kwa masanduku ya maoni yatakayokaguliwa na timu huru nje ya idara husika.

Kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2026, alisema TAKUKURU imeweka mikakati ya kuendelea kufuatilia matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo, kutoa elimu kwa umma, kushirikisha wadau na kuchunguza vitendo vya rushwa ili kuhakikisha wanaohusika wanachukuliwa hatua za kisheria.

Alitoa wito kwa wananchi kuepuka vitendo vya rushwa na kuendelea kutoa taarifa kwa TAKUKURU ili kulinda rasilimali za umma na kuhakikisha fedha za maendeleo zinawanufaisha wananchi.


 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi ameshiriki katika zoezi la kupiga kura kumchagua Mbunge wa Jimbo la Chamwino, katika Uchaguzi mdogo unaofanyika leo tarehe 04 Novemba 2026.

Makamu wa Rais amepiga kura katika kituo namba Tano kilichopo Ofisi ya Kijiji cha Chamwino Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma. 

Awali,Mheshimiwa Deogratius Ndejembi, alikuwa Mbunge wa Jimbo hilo, kabla ya kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwezi Agosti 2026.






Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Prof. Neema Mori, na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Abdulmajid Nsekela, wameongoza ujumbe wa Benki ya CRDB katika mazungumzo na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Mhe. Judith Suminwa Tuluka, yaliyofanyika leo jijini Dar es Salaam.

Mazungumzo hayo ni sehemu ya juhudi za kimkakati za Benki ya CRDB katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda, kuunganisha masoko na kufungua fursa mpya za biashara, uwekezaji na maendeleo kati ya Tanzania na DRC, na kwa upana zaidi, katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Mhe. Judith Suminwa Tuluka ameeleza utayari wa Serikali ya DRC kushirikiana na Benki ya CRDB katika maeneo mbalimbali ya kimkakati, akitambua nafasi ya sekta ya fedha katika kuharakisha maendeleo, kurahisisha biashara na kuchochea uwekezaji wenye tija kwa wananchi wa nchi hizo mbili.

Kwa upande wake, Uongozi wa Benki ya CRDB umesisitiza dhamira ya Benki kuwa mshirika wa kimkakati katika utekelezaji wa ajenda za maendeleo ya kikanda, ikiwemo kutumia fursa zinazotokana na Ushoroba wa Kati na Ushoroba wa Lobito kuimarisha biashara, uwekezaji na miunganiko ya kiuchumi. Juhudi hizi pia zitalenga kupanua wigo wa uwezeshaji kwa vijana, wanawake na biashara ndogo na za kati (SMEs).

Sambamba na hilo, Benki imethibitisha dhamira yake ya kuendelea kuwekeza nchini DRC na kupanua wigo wa huduma zake nje ya Lubumbashi na Kinshasa, hatua itakayoiwezesha kuwafikia wateja wengi zaidi na kushiriki kikamilifu katika fursa zinazochochewa na ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo.

Kupitia uwepo wake Tanzania, Burundi na DRC, Benki ya CRDB inazidi kujijenga kama taasisi ya kifedha yenye mtazamo na ushawishi wa kikanda, inayokwenda zaidi ya kutoa huduma za kibenki na kuchukua nafasi ya kuunganisha mitaji, biashara, wawekezaji na fursa za maendeleo katika Afrika Mashariki na Kati.

Kwa CRDB, mipaka si kikwazo cha fursa, bali ni daraja la kuunganisha uchumi, masoko na mustakabali wa maendeleo ya kikanda.

#CRDBBank
#MshirikaWaKimkakati



Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) tarehe 3 Novemba, 2026, imekabidhi Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kituo cha mwitikio wa haraka kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu kilichojengwa  katika Kijiji cha Naalarami, Wilaya ya Monduli, Mkoani Arusha.

Akizungumza wakati wa kukabidhi kituo hicho Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayesimamia Huduma za Shirika Ngorongoro Aidan Makala amesema kuwa ujenzi wa vituo vya askari wa wanyamapori kwa ajili ya kutoa mwitikio wa haraka kwa matukio yanayohusisha wanyamapori wakali na waharibifu ni sehemu ya mchango wa Mamlaka katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kukabiliana na changamoto  hiyo.

Amesema lengo la Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia taasisi zake ni kuimarisha usalama wa wananchi, ambapo tayari Ngorongoro imejenga vituo hivyo Monduli, Babati, Same, Korogwe na Rufiji.

Msimamizi wa Ujenzi wa Kituo hicho Mhandisi Faraja Sembua ameeleza kuwa mradi wa ujenzi wa kituo hicho uliofanyika kwa kipindi cha miezi mitano na kugharimu shilingi milioni 102 ambapo kituo kinajumuisha ofisi, vyumba vya kulala, na sehemu za kuhifadhi silaha, choo na bafu pamoja na miundombinu mingine muhimu.

Akipokea kituo hicho Kamishna Msaidizi Mwandamizi kutoka TAWA  P.M Kasisi ametoa shukrani kwa Ngorongoro kuunga mkono juhudi za kudhibiti migangano ya wanyamapori wakali na waharibifu kwa mali za wananchi na kuahidi kusimamia  kituo hicho  ili kiwe na manufaa kwa wananchi .










NA: DK. REUBENI LUMBAGALA

Mkoa wa Tanga ni maarufu kwa uzalishaji wa matunda nchini. Machungwa ni miongoni mwa matunda yanayozalishwa kwa wingi katika wilaya za Muheza, Korogwe na Handeni mkoani humo.

Wakulima wa zao hili hufanya jitihada kubwa za uzalishaji, lakini bado hawajafaidi vya kutosha jasho lao. Wakulima hutegemea baada ya kuvuna, wauze machungwa kwa bei nzuri ambayo itarejesha gharama za uendeshaji.

Aidha, wakulima hao hutegemea kupata faida kwani kwao kilimo hicho ni ajira kwa ajili ya kuendesha maisha yao na kufanya mambo mengine ya maendeleo kama kusomesha watoto, kujenga nyumba, kufungua biashara, kununua vyombo vya moto za usafiri, kutaja kwa uchache.

Miongoni mwa changamoto katika kilimo cha machungwa ni bei ndogo na kukosa soko la uhakika. Hili limesababisha wakulima kuuza machungwa yao mashambani kwa madalali.

Kwa kufanya hivyo, wakulima wamejikuta wakiuza machungwa yao kwa bei ndogo huku madalali wakinufaika pasi na kumwaga jasho kama walivyomwaga wakulima.

Kutokana na changamoto hizi, serikali ya mkoa wa Tanga chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa, Balozi Dk. Batilda Buriani, umejizatiti kuinua zao hili ili libadili hali za maisha ya wakulima na kuchangia katika maendeleo.

Novemba 1, 2026, katika kikao cha viongozi wa mkoa na wilaya, Dk. Buriani alisema, mkoa wa Tanga huzalisha asilimia 60 ya machungwa yote nchini, hivyo ni muhimu kuweka mazingira mazuri ya biashara hiyo ili iwanufaishe wakulima.

"Tumepiga marufuku madalali kununua machungwa mashambani, machungwa yatauzwa katika vituo maalum, hii itasaidia machungwa kuuzwa kwa bei nzuri," amesema Dk. Buriani.

Katika hatua nyingine, Dk. Buriani amesema, serikali mkoani humo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), watajenga vituo vinne ambapo wanunuzi wa machungwa watakwenda kununua moja kwa moja katika vituo hivyo kwa bei elekezi.

Kimsingi, ujenzi wa vituo hivi na kuwa na bei elekezi ya machungwa ni mkakati mzuri wa kuinua zao hili. Ni wakati muafaka sasa kwa wakulima kufaidi jasho lao na kuona fahari kulima machungwa kwani sasa kilimo hicho kitalipa na chenchi itabaki.



ZAIDI ya tani 175,000 za korosho ghafi zimeuzwa kwa thamani ya Sh.bilioni 682 ndani ya wiki tatu za minada ya msimu wa 2026/27, huku zaidi ya tani 200,000 zikiwa zimekusanywa kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Bw. Asangye Bangu, ameyasema hayo leo, Novemba 3, 2026 jijini Dodoma kwenye Maonesho ya kuelekea uzinduzi wa sera ya maendeleo endelevu ya viwanda ya mwaka 2025 na sera ya maendeleo ya wajasiriamali wadogo na wa kati ya mwaka 2003 toleo la mwaka 2025

Bw. Bangu amesema tangu kuanza kwa msimu huo Oktoba 12, mwaka huu hadi leo minada 20 ya korosho imefanyika kupitia mfumo huo ambao umeendelea kuwaunganisha wakulima na wanunuzi, kurahisisha upatikanaji wa masoko na kuwezesha biashara ya mazao kufanyika kwa uwazi na ushindani.

"Hadi Novemba 1, 2026 tani za korosho 175,000 zenye thamani ya zaidi ya Sh.Bilioni 682 zimeuzwa kupitia Mfumo wa Stakabadhi za ghala kati ya tani 200,000 ambazo zimekusanywa kwa kipindi hicho,"amesema.

Aidha, ameeleza kuwa mafanikio mengine ya mfumo huo yameendelea kuonekana pia katika mazao mengine ambapo ndani ya miezi minne kuanzia Julai mosi, 2026 mfumo huo umewezesha kupokelewa na kuuzwa kwa tani 217,000 za mbaazi, zaidi ya tani 164,000 za dengu, zaidi ya tani 26,000 za ufuta, tani 8,700 za kahawa na tani 8,252 za kakao.

Amesisitiza kuwa mfumo huo una mchango mkubwa katika kuchochea maendeleo ya viwanda nchini kwa kuwezesha uhifadhi wa mazao katika ghala zenye leseni, usimamizi wa ubora na usalama wa bidhaa.




Na Mwandishi Wetu

Serikali imesema inaendelea kuchukua hatua za kupunguza makali ya ongezeko la bei za mafuta nchini, ikiwemo kutoa ruzuku ili kulinda watumiaji na kupunguzaathari za gharama za mafuta kwa shughuli za kiuchumi.

Hatua hizo zinalenga kuhakikisha kuwa, pamoja nachangamoto zinazoendelea katika soko la dunia, wananchi wanaendelea kupata mafuta kwa uhakika nakwa bei himilivu.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), bei za mafuta nchinizimeongezeka kwa mwezi Novemba 2026 kutokana nakuongezeka kwa gharama za usafirishaji na bima, kulikosababishwa na kuendelea kwa mgogoro waMashariki ya Kati, ambako Tanzania huagiza sehemukubwa ya mafuta yake.

Hali hiyo imejitokeza licha ya bei za mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia kupungua kidogo mwezi Oktoba ikilinganishwa na Septemba 2026.

Katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imefanya jitihada za kuweka ruzuku kwa lengo la kupunguza mzigo wa gharama kwa watumiaji wa mafuta na uchumi kwa ujumla, huku ikiendelea kuchukua hatua za kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa bidhaa hizo nchini.

EWURA imetangaza bei kikomo za mafuta zitakazoanza kutumika tarehe 4 Novemba 2026, ambapo kwa Dar es Salaam, petroli itauzwa kwa bei isiyozidi Shilingi 4,083 kwa lita, dizeli Shilingi 4,128 na mafuta ya taa Shilingi 4,117.

Licha ya ongezeko hilo, bei za mafuta hayo nchini ziko chini zikilinganishwa na baadhi ya nchi jirani katika ukanda wa Afrika Mashariki (EAC) na zile za Kusini mwa Afrika (SADC).

Serikali imeeleza kuwa itaendelea kufuatilia mwenendo wa soko la mafuta duniani na kuchukua hatua za kupunguza athari zake kwa wananchi na shughuli za uzalishaji, usafirishaji na uchumi kwa ujumla.

Kwa mujibu wa taarifa ya EWURA, kipaumbele cha serikali ni kuhakikisha mafuta yanaendelea kupatikanakwa uhakika nchini, huku gharama zake zikiendeleakuwa himilivu kwa wananchi na uchumi.

Kampuni ya TotalEnergies imeendelea kutoa elimu kwa watumiaji wa bidhaa za nishati na vyombo vya usafiri kuhusu matumizi sahihi ya vilainishi, gesi ya kupikia na mifumo ya malipo ya kidijitali, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu huduma hizo.

Elimu hiyo inatolewa kupitia banda la kampuni hiyo katika Maonesho ya Viwanda na Biashara yanayoendelea katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete (JKCC), jijini Dodoma, kuelekea uzinduzi wa sera ya maendeleo ya viwanda na sera ya Jasiriamali ndogo na za Kati ya mwaka 2003 Toleo la mwaka 2025, ambako wananchi wanapata fursa ya kufahamu aina mbalimbali za vilainishi na matumizi yake kulingana na aina ya injini, vilainishi vinavyotambulishwa ni Quartz kwa magari yanayotumia petroli, Rubia kwa magari ya dizeli na Hi-Perf kwa pikipiki.

Akizungumza katika maonesho hayo, Meneja Masoko wa TotalEnergies, Caroline Kakwezi, amesema matumizi ya vilainishi vinavyoendana na aina ya injini ni muhimu katika kuhakikisha vyombo vya usafiri vinapata huduma inayostahili, huku akieleza kuwa kampuni hiyo pia inasambaza gesi ya kupikia ya kilo sita na 13 kupitia vituo vyake na mawakala walioidhinishwa.

Katika eneo la huduma za malipo, Kakwezi amesema TotalEnergies imeboresha mifumo yake ya kidijitali inayowawezesha wateja kufanya miamala kwa kutumia kadi, namba za simu na misimbo ya OTP, pamoja na programu ya Mobility, mifumo hiyo inalenga kuongeza urahisi katika kufanya malipo na kupanua njia ambazo wateja wanaweza kutumia kupata huduma.

Amesema ushiriki wa kampuni hiyo katika maonesho hayo unatoa nafasi ya kukutana moja kwa moja na watumiaji wa bidhaa na huduma zake, kupata maoni yao na kubaini mahitaji yanayopaswa kuzingatiwa katika kuboresha huduma, ameongeza kuwa ushiriki wa sekta binafsi katika majukwaa hayo ni muhimu katika kuimarisha uhusiano kati ya wazalishaji, watoa huduma na wananchi.

Maonesho hayo pia yanatoa fursa kwa wananchi kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kuhusu bidhaa zinazotumika katika maisha ya kila siku, hususan matumizi ya vilainishi na gesi ya kupikia pamoja na njia za malipo, elimu hiyo ni muhimu katika kuwawezesha watumiaji kufanya maamuzi sahihi wanaponunua na kutumia bidhaa hizo.





Na Janeth Raphael - MichuziTv 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Jumatano, Novemba 4, 2026, ameshiriki Uchaguzi Mdogo wa Ubunge wa Jimbo la Chamwino baada ya kupiga kura katika Kituo cha Kupigia Kura cha Ofisi ya Kijiji cha Chamwino, mkoani Dodoma.

Rais Samia alifika katika kituo hicho kushiriki zoezi la uchaguzi linalofanyika kwa ajili ya kumpata Mbunge mpya wa Jimbo la Chamwino, nafasi iliyokuwa wazi kufuatia aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Mhe. Deogratius Ndejembi, kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ushiriki wa Rais Samia katika zoezi hilo unaonesha umuhimu wa wananchi kutumia haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka kuwawakilisha katika vyombo vya maamuzi.

Uchaguzi Mdogo wa Chamwino unawapa wapiga kura wa jimbo hilo fursa ya kuchagua mwakilishi mpya atakayechukua nafasi ya Ndejembi na kuendelea kusimamia masuala ya maendeleo pamoja na kuwakilisha wananchi wa Chamwino bungeni.

Ndejembi alikuwa Mbunge wa Jimbo la Chamwino kabla ya kuteuliwa kushika nafasi ya Makamu wa Rais, hatua iliyosababisha nafasi ya ubunge wa jimbo hilo kuwa wazi na hivyo kuhitajika kufanyika kwa Uchaguzi Mdogo.

Wananchi waliojiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wanashiriki katika uchaguzi huo kwa kutekeleza wajibu wao wa kuchagua kiongozi watakayempa dhamana ya kuwawakilisha kwa mujibu wa taratibu za uchaguzi.

Matokeo ya Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Chamwino yanatarajiwa kutoa Mbunge mpya ambaye atarithi nafasi hiyo na kuendeleza uwakilishi wa wananchi wa jimbo hilo katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akipiga kura kwenye Kituo cha kupigia kura cha Ofisi ya Kijiji cha Chamwino mkoani Dodoma, tarehe 04 Novemba, 2026 katika Uchaguzi mdogo wa Ubunge wa Jimbo la Chamwino. Uchaguzi huo unafanyika kufuatia aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Mhe. Deogratius Ndejembi kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.



Na Mwandishi Wetu
SERIKALI ya Mkoa wa Pwani imesema iko tayari kutoa ushirikiano katika kuimarisha Bandari Kavu ya Kwala na kuongeza matumizi ya reli katika usafirishaji wa makasha ya mizigo, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, wakati wa mazungumzo yake na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), iliyofanya ziara mkoani humo kwa lengo la kukagua miundombinu ya reli na huduma za usafirishaji wa makasha kwenda Bandari Kavu ya Kwala.

Nyongo amesema kuimarishwa kwa Bandari Kavu ya Kwala pamoja na kuongeza uwezo wa usafirishaji wa mizigo kupitia reli kutasaidia kupunguza msongamano wa magari makubwa na foleni katika Jiji la Dar es Salaam.

Amesema Mkoa wa Pwani kwa sasa unapokea wawekezaji wengi wanaokuja kuwekeza katika sekta ya viwanda, hali inayochochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kuongeza mahitaji ya huduma bora za usafirishaji.

Amesema kutokana na kasi hiyo ya maendeleo, kuna umuhimu wa kuimarisha miundombinu ya barabara na reli ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo na kukidhi mahitaji yanayoongezeka.

Aidha, amelitaka Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuendelea kuimarisha uwezo wake wa kusafirisha makasha na shehena nyingine kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Bandari Kavu ya Kwala, ili wafanyabiashara na wasafirishaji waweze kuchukua mizigo yao Kwala na kuisafirisha kwenda maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi.

Amesema matumizi makubwa ya reli katika usafirishaji wa mizigo yatapunguza idadi ya magari makubwa yanayoingia na kutoka Dar es Salaam, hivyo kupunguza msongamano na kuongeza ufanisi wa shughuli za usafirishaji.

Nyongo amesema uanzishwaji na uimarishaji wa Bandari Kavu ya Kwala ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kukuza uchumi na kuboresha huduma za usafirishaji nchini.

“Tunataka watendaji waumize vichwa katika kuhakikisha miundombinu ya reli inatumika kikamilifu na kuleta tija iliyokusudiwa. Changamoto zinapojitokeza, watendaji wanapaswa kuwa wa kwanza kuzishughulikia,” amesema Nyongo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Uwakala wa Meli (TASAC) Nahodha Mussa Mandia, amesema ziara hiyo imelenga kukagua miundombinu ya bandari kavu iliyopo mkoani Pwani ili kutathmini hali yake, uwezo wa kuhudumia shehena na mchango wake katika kurahisisha shughuli za usafirishaji na biashara.

Amesema ziara hiyo pia inalenga kubaini fursa zilizopo katika bandari Kavu ya Kwala, katika kupunguza msongamano wa shehena na magari katika Bandari ya Dar es Salaam,

Amesema kuondosha mizigo na makasha katika Bandari ya Dar es Salaam kunaongeza ufanisi wa huduma wa katika kuhudumia Meli

Naye, Meneja wa Stesheni ya Ruvu wa TRC, Dawa Onyango, amesema shirika hilo linaendelea kuboresha huduma za reli, ambapo kwa sasa reli hiyo ina uwezo wa kuhudumia makasha 100 ya mizigo kutoka Bandari za Tanga na Dar es Salaam.