Na Byera Deus, BUKOBA

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera imefanikiwa kurejesha Sh milioni 277.8 zilizokuwa zimepotea kutokana na ubadhirifu na matumizi yasiyo sahihi ya fedha za umma katika kipindi cha Aprili hadi Septemba 2026.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera, Hajinas Onesphory, amesema mafanikio hayo yametokana na ushindi wa kesi 45 kati ya 50 zilizofikishwa mahakamani kwa lengo la kulinda na kurejesha fedha za wananchi.

Amesema miongoni mwa fedha zilizorejeshwa ni Sh milioni 100 kutoka Kampuni ya STC Construction zilizohusishwa na ubadhirifu wa fedha za mradi wa maji katika Kijiji cha Katare, Halmashauri ya Bukoba.

Fedha nyingine ni Sh milioni 25.8 zilizorejeshwa na mzabuni pamoja na mtumishi wa TANESCO Wilaya ya Kyerwa, Sh milioni 35.6 kutoka kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Ngara Farmers, Sh milioni 26.1 zilizorejeshwa na karani wa Kyamulaile AMCOs na Sh milioni 15 zilizorejeshwa na viongozi wa Kijiji cha Rwinyana, Ngara.

Aidha, amesema TAKUKURU imekagua na kufuatilia miradi 67 yenye thamani ya Sh bilioni 8.9 kwa lengo la kubaini mapungufu na kutoa ushauri wa kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa.

Katika kipindi hicho, taasisi hiyo ilipokea taarifa 252, ambapo 131 zilihusu vitendo vya rushwa na 121 hazikuhusu rushwa. Pia, mashauri 85 yanaendelea kusikilizwa mahakamani.







Na Seif Mangwangi, Michuzi TV, Arusha


TANZANIA imetajwa kuwa miongoni mwa nchi nne za Afrika zilizoondoa utaratibu uliokuwa ukiwaruhusu wananchi wake kufikisha mashauri moja kwa moja katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR), hali inayotajwa kuwa miongoni mwa changamoto zinazoathiri upatikanaji wa haki kupitia taasisi hiyo inayotimiza miaka 20 tangu kuanzishwa kwake.

Wakili Bahame Tom Nyanduga kutoka Dar es Salaam, Tanzania, amesema hatua hiyo pamoja na changamoto za upungufu wa rasilimali watu na fedha ni miongoni mwa vikwazo vinavyoweza kudhoofisha uwezo wa mahakama hiyo kutekeleza majukumu yake ya kulinda haki za binadamu barani Afrika.

Akizungumza katika kongamano la maadhimisho ya miaka 20 ya mahakama hiyo lililofanyika Arusha, Nyanduga amesema licha ya taasisi hiyo kufanikiwa kuwepo kwa kipindi hicho, bado inahitaji ushirikiano wa dhati kutoka kwa nchi wanachama ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Amesema katika kipindi cha miaka mitano hadi kumi ya mwanzo wa uendeshaji wa mahakama hiyo, kati ya nchi 34 zilizokuwa zimeridhia mkataba wake, ni nchi 10 pekee zilizokuwa zimekubali wananchi wake kuwasilisha mashauri moja kwa moja mahakamani hapo.

Ameeleza kuwa hali hiyo ilikuwa changamoto kubwa ikizingatiwa kuwa bara la Afrika lina nchi 55, hivyo ushiriki mdogo wa nchi wanachama katika kuruhusu wananchi kutumia mahakama hiyo uliathiri wigo wa upatikanaji wa haki.

Nyanduga amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi nne zilizoondoa tamko maalumu lililokuwa likiruhusu wananchi na taasisi zisizo za kiserikali kuwasilisha mashauri moja kwa moja mahakamani hapo, huku nyingine zikiwa ni Rwanda, Tunisia na Ivory Coast.

Amesema msingi wa kuanzishwa kwa mahakama hiyo ulikuwa ni kuhakikisha wananchi wa Afrika wanapata fursa ya kutafuta haki katika ngazi ya bara pale wanaposhindwa kupata suluhisho kupitia mifumo ya mahakama za ndani ya nchi zao.

Hata hivyo, pamoja na changamoto hizo, Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu imeendelea kupata mafanikio katika kipindi cha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2006, ikiwa ni pamoja na kupokea zaidi ya mashauri 350 yaliyohusu ukiukwaji wa haki za binadamu katika nchi mbalimbali za Afrika.

Akizungumza katika kongamano hilo, Rais mstaafu wa mahakama hiyo, Jaji Imani Aboud, amesema taasisi hiyo imepiga hatua kubwa katika kipindi hicho, hususan katika kupokea na kushughulikia mashauri yanayohusu ukiukwaji wa haki za msingi za wananchi.

Jaji Aboud amesema kati ya mashauri zaidi ya 350 yaliyowasilishwa mahakamani hapo, takribani 200 tayari yamefanyiwa maamuzi, huku mengine yakiendelea kushughulikiwa, hatua inayoonesha mchango wa taasisi hiyo katika kuimarisha mifumo ya haki barani Afrika.

Amesema mahakama hiyo ilipoanza kazi ilikuwa na nchi 12 zilizokuwa zimekubali kutambua mamlaka yake kupitia matamko maalumu yaliyowezesha wananchi kupata haki moja kwa moja katika mahakama hiyo.

Ameongeza kuwa licha ya baadhi ya nchi kuondoa matamko hayo, mahakama inaendelea kutekeleza wajibu wake kwa kupokea mashauri yanayowasilishwa kwa mujibu wa taratibu na mamlaka iliyowekwa kisheria.

Kwa upande wake, Msajili wa mahakama hiyo, Dkt. Robert Eno, amesema taasisi hiyo imepata mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka 20, licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa watumishi.

Dkt. Eno amesema tathmini ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa mwaka 2021 hadi 2025 imeonesha ongezeko la asilimia 27 la mashauri yaliyokamilishwa, jambo linaloonesha kuimarika kwa uwezo wa mahakama katika kushughulikia mashauri yanayofikishwa mbele yake.

Amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano kati ya majaji, watumishi wa Ofisi ya Usajili, nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, asasi za kiraia, taasisi za kitaaluma na washirika wa maendeleo.

Ameeleza kuwa katika kipindi cha mwaka 2026 hadi 2030, mahakama hiyo imejipanga kuongeza upatikanaji wa haki, kuimarisha matumizi ya teknolojia, kujenga uwezo wa kitaasisi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na wadau wa sekta ya sheria.

Akizungumza katika ufunguzi wa kongamano hilo, Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Jaji Blaise Tchikaya, amesema ana imani na mustakabali wa taasisi hiyo, akieleza kuwa uwezo wa Afrika kuweka na kutekeleza malengo yake ni msingi muhimu wa kuimarisha ulinzi wa haki za binadamu katika bara hilo.

Jaji Tchikaya amesema anaamini mahakama hiyo itaendelea kufanya kazi kwa mafanikio katika miaka 40 ijayo na kufikisha miaka 60 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2006.

Amesema kongamano hilo si maadhimisho ya kawaida pekee, bali ni fursa kwa majaji, wataalamu wa sheria, viongozi wa taasisi na wadau mbalimbali kutathmini mafanikio yaliyopatikana, kujadili changamoto zilizopo na kuweka mikakati ya kuimarisha ulinzi wa haki za binadamu na watu barani Afrika.


▪️ Awataka mawaziri watatu kupitia muundo wa tozo

▪️ Aagiza usanifu wa barabara Ushetu uharakishwe ili kuwahi bajeti

▪️ Aitaka TANESCO kuunganisha umeme vijijini kwa sh. 27,000


WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewaelekeza mawaziri wenye dhamana ya TAMISEMI, Fedha na Kilimo kupitia upya muundo wa tozo zinazohusiana na pembejeo, baada ya kuelezwa kuwa gharama za mikopo zinapunguza mapato ya wakulima wa tumbaku.

Amesema mapitio hayo yafanyike kwa kuangalia tozo moja baada ya nyingine ili kupata ufumbuzi wa mzigo unaowakabili wakulima.

Dkt. Mwigulu ametoa maelekezo hayo leo (Jumatano, Novemba 11, 2026), akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Stendi ya Nyamilangano, Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, mkoani Shinyanga.

“Niwaelekeze Waziri wa TAMISEMI, Waziri wa Fedha, pamoja na Waziri wa Kilimo, wakae waangalie upya huu muundo wa hizi tozo,” amesema.

Maelekezo hayo yamefuatia hoja ya Mbunge wa Ushetu, Emmanuel Peter Cherehani, aliyelalamikia gharama za mikopo katika mfumo wa upatikanaji wa pembejeo za tumbaku.

Cherehani amesema msambazaji anapokopa kununua pembejeo anatozwa riba, na chama cha msingi kinapokopa kumlipa msambazaji nacho kinatozwa riba, huku mzigo huo ukimwathiri mkulima.

Waziri Mkuu amesema atakaa na mawaziri hao pamoja na wabunge wa maeneo yanayoathiriwa na changamoto hiyo ili kupata ufumbuzi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amemwelekeza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Shinyanga, Ntuli Mwaikokesye, kuharakisha usanifu wa kina wa barabara iliyotajwa na Mbunge wa Ushetu, ili ukamilike kabla ya maandalizi ya bajeti mpya.

Mwaikokesye alipoeleza kuwa usanifu unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi minne, Waziri Mkuu amemtaka kupunguza muda huo ili mradi uwe tayari kuzingatiwa Serikali itakapoanza kupokea miradi mipya ya barabara.

“Fanyeni kazi usiku na mchana, tumalize hiyo detailed design,” amesema.

Kuhusu umeme, Waziri Mkuu ameielekeza TANESCO kuzingatia hali halisi ya maeneo ya vijijini badala ya kutumia majina ya kiutawala ya miji kuwatoza wananchi gharama kubwa za kuunganishiwa huduma hiyo.

Amesema wananchi wa maeneo hayo waunganishiwe umeme kwa shilingi 27,000, bila kutozwa gharama kubwa kwa kigezo cha maeneo yao kuitwa miji kiutawala.

Aidha, amepokea ombi la kujengwa kwa chuo cha ufundi stadi Ushetu, akisema Serikali itapanga utekelezaji wake kwa kuzingatia uamuzi wa kila halmashauri kuwa na chuo cha VETA.












Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman (wapili kulia), akipokea mkoba wenye machapisho yanayohusu utekelezaji wa majukumu ya Mfuko wa PSSSF, kutoka kwa Meneja wa Mfuko huo Ofisi ya Zanzibar, Bi. Mariam Saleh, alipotembelea Banda la PSSSF kwenye Maonesho yanayofanyika sambamba na Mkutano wa 11 wa Mtandao wa Wasimamizi wa Rasilimaliwatu katika Taasisi za Umma Barani Afrika ( APS-HRMnet) mjini Unguja, Zanzibar Novemba 10, 2026.



Meneja Rasilimali Watu Bi. Gloria Mboya kulia, akiwa na Meneja wa Ofisi ya PSSSF Zanzibar, Bi. Mariam Saleh, wakitoa huduma kwa mwanachama katika banda la Maonesho ya Mkutano wa 11 wa APS-HRMnet (11th APS-HRMnet Annual Conference Delegates) unaoendelea Verde Hoteli, Zanzibar.


Meneja wa Utawala Bi. Fatma Chondo wa kwanza kulia akiwa na Afisa utekelezaji Bi. Zakia Mohamed, wakitoa huduma kwa wanachama wakati wa Maonesho ya Mkutano wa 11wa Mwaka wa APS-HRMnet (11th APS-HRMnet Annual Conference Delegates) Verde Hotel, Zanzibar. Novemba 10,2026.



Makamu wa Kwanza wa Rais, Mhe.Othman Masoud Othman, akimsikiliza Meneja wa Ofisi ya Zanzibar ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Bi. Mariam Saleh alipotembelea banda la mfuko huo kwenye Maonesho ya Mkutano wa 11 wa Mwaka wa APS-HRMnet (11th APS-HRMnet Annual Conference Delegates) Hotel Verde, Zanzibar. Novemba 10, 2026.




Novemba 10, 2026. Zanzibar


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, ameipongeza PSSSF kwa matumizi ya kidijitali katika kutoa huduma, amesema kwamba imechangia kwa kiasi kikubwa kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wanachama na kuwaondolea usumbufu wa kufika mara kwa mara katika ofisi za Mfuko kufuata huduma.

Mhe. Othman ameyasema hayo leo, Novemba 10, 2026, alipotembelea banda la PSSSF katika Maonesho ya Mkutano wa 11 wa Mwaka wa APS-HRMnet (11th APS-HRMnet Annual Conference Delegates) yaliyofanyika Zanzibar.

Akizungumza baada ya kupata maelezo kuhusu huduma zinazotolewa na Mfuko, Mhe. Othman alisema kuwa matumizi ya mifumo ya kidijitali yameleta urahisi mkubwa kwa wanachama.

Mhe. Othman, alimuwakilisha Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi kufungua mkutano huo, katika Banda la PSSSF alipokelewa na Meneja wa PSSSF Ofisi ya Zanzibar, Bi. Mariam Saleh aliyemueleza namna Mfuko ulivyoendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa kutumia ambapo sasa huduma zote zinapatikana kidijitali ili kuongeza ufanisi na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wanachama.

Aidha, alielezwa kaulimbiu mpya ya Mfuko isemayo 'Tunalipa Jana', inayosisitiza dhamira ya PSSSF ya kuhakikisha wanachama wanapata mafao yao kwa wakati na kwa ufanisi zaidi ikiwemo kuimarisha mifumo ya usimamizi na ufuatiliaji wa michango ili kuwezesha ulipaji wa mafao kwa wakati.
-Programu inayoungwa mkono na Serikali ya Uswisi yaingia awamu ya tatu, ikiwa na msisitizo wa kuziandaa biashara kuvutia uwekezaji, kuongeza ajira na kuwapa wanawake fursa zaidi.

Westerwelle Startup Haus Arusha (WSHA) imeadhimisha miaka minne ya kuwaunga mkono wajasiriamali kaskazini mwa Tanzania kwa kuzindua awamu ya tatu ya programu ya AfroGreen. Programu hiyo ya miezi tisa imewakutanisha wafanyabiashara 20 wa Kitanzania wanaoendesha biashara zinazotengeneza suluhisho za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

AfroGreen inafadhiliwa na Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania pamoja na Westerwelle Foundation ya Ujerumani. Inalenga biashara zinazojihusisha na nishati jadidifu, uchumi mzunguko, kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi, kukabiliana na athari za tabianchi pamoja na minyororo endelevu ya thamani. Kati ya biashara zilizochaguliwa, nane ambazo ni sawa na asilimia 40, zinaongozwa na wanawake. Biashara 15 zipo Arusha, huku nyingine tano zikitoka mikoa ya Dar es Salaam na Iringa.

Awamu hii mpya imekuja baada ya matokeo mazuri ya awamu mbili zilizopita, zilizosaidia biashara changa 30, kuchangia upatikanaji wa ajira 42 na kuvutia fedha za uwekezaji zilizozidi Euro 132,000. Kupitia awamu hii, biashara zote 20 zitasaidiwa kujiandaa kutafuta mitaji na kupima mchango wa biashara zao katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Programu pia inalenga kuchangia upatikanaji wa ajira mpya zisizopungua 40 na kupata uwekezaji mpya.

Kwa WSHA, programu hii inaonesha namna ambavyo msaada kwa wajasiriamali unavyoendelea kupanuka, ukiweka mkazo zaidi katika kuzisaidia biashara kukua na kuvutia uwekezaji.

“Miaka minne iliyopita tulipoanzisha WSHA, tulikuwa na lengo la kuwaunganisha wajasiriamali wa Kitanzania na mtandao wa kimataifa wa Westerwelle Foundation. Wengi wa wajasiriamali tuliowaunga mkono wakati huo wamepiga hatua na sasa wanahitaji msaada wa kiwango kingine. Mpango wetu hadi mwaka 2030 unaangazia mahitaji yao mapya, ikiwemo kuwaandaa kuvutia uwekezaji, kuwaunganisha na fursa za kimataifa na kujenga ushirikiano wa karibu zaidi na wafanyabiashara wa Arusha ili kupata ushauri, fursa za biashara na mitaji. AfroGreen ni sehemu ya utekelezaji wa mpango huo, kwa kuunga mkono biashara zinazotengeneza ajira na kusaidia jamii kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” amesema Isaack Shayo, Mkurugenzi wa Westerwelle Foundation Tanzania.

Ukuaji wa biashara hizo pia unahitaji ushirikiano unaowawezesha wajasiriamali kupata rasilimali na utaalamu wanaouhitaji. Serikali ya Uswisi inaunga mkono AfroGreen kwa mara ya pili, ikitambua umuhimu wa msaada huo katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

“Mabadiliko ya tabianchi ni mojawapo ya changamoto kubwa za wakati wetu. Yanagusa karibu kila eneo la maisha yetu, na Tanzania haiko nje ya changamoto hii. Upatikanaji wa mitaji, utaalamu wa kiufundi, mitandao ya kibiashara na msaada sahihi kwa wafanyabiashara unaweza kuleta tofauti kubwa. Hii ndiyo sababu hasa inayotufanya Serikali ya Uswisi kuendelea kuunga mkono programu ya AfroGreen kwa mara ya pili,” amesema Andrea Inglin, Mkuu wa Kitengo cha Ajira na Kipato katika Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania.

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2022, WSHA imewafikia wajasiriamali 809, wakiwemo waanzilishi wa biashara changa 309, huku wanawake wakichangia asilimia 55 ya wote waliofikiwa. Maadhimisho ya miaka minne ya taasisi hiyo yaliwakutanisha wajasiriamali, wawekezaji, wadau wa maendeleo na wawakilishi wa Serikali. Miongoni mwao alikuwa Evodius Cleophace, Afisa Vijana wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, aliyezungumzia mchango wa programu kama hizi katika kupanua fursa kwa vijana.

“Nawapongeza kwa kutimiza miaka minne. Kazi mnayoifanya ni muhimu sana na inakamilisha juhudi za Serikali. Kupitia programu zenu, mnawafikia na kuwapa msaada wajasiriamali ambao pengine ingekuwa vigumu kuwafikia kwa njia nyingine. Nawashukuru kwa mchango huu. Pia ninawahimiza vijana kutumia fursa zilizopo.

 Katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/27, Halmashauri imetoa mikopo ya jumla ya Shilingi bilioni mbili kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, ambapo vijana wamekopeshwa Shilingi 578,702,420. 

Aidha, kampuni ya Himan Investment, iliyoshiriki katika awamu iliyopita ya AfroGreen, imekopeshwa zaidi ya Shilingi milioni 130 kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana (YDF). Ninawasihi vijana wajasiriamali watafute fursa hizi na wazitumie vizuri,” amesema.

Ushiriki wa kampuni ya Himan Investment katika awamu iliyopita ni mfano wa namna biashara zinavyoweza kunufaika na fursa hizo. Naye Collins Kimaro, mjumbe wa bodi ya WSHA na mwanzilishi mwenza wa Obuntu Hub, ambayo ilikuja kuwa WSHA kupitia ushirikiano wake na Westerwelle Foundation, amewahimiza washiriki wapya kuamini uwezo wao na kutambua hatua wanazoweza kufikia.

“Kama sisi tuliweza kukua na kufika hapa tulipo, ninyi mnaweza kufikia wapi?” aliwauliza washiriki.

Kwa wajasiriamali waliojiunga na kundi jipya, AfroGreen ni fursa ya kuendeleza uwezo huo na kuziandaa biashara zao kwa hatua inayofuata ya ukuaji.

“AfroGreen ni fursa kwetu kukuza biashara zetu na kuweka mifumo sahihi itakayotuwezesha kuvutia uwekezaji. Tunatarajia kumaliza programu hii tukiwa tumejiandaa vizuri kupata mitaji, tukiwa na ujuzi na mahusiano yatakayotusaidia kupata fedha za kukuza biashara zetu,” amesema Fortunatus Fungatwende, Mwanzilishi wa Innolif Aquaculture Group.

Washiriki watapata mafunzo ya biashara, ushauri wa karibu wa kitaalamu na mwongozo wa kuziandaa biashara zao kuvutia wawekezaji, pamoja na fursa ya kuunganishwa na mtandao wa wawekezaji binafsi. Programu itahitimishwa kwa siku maalumu ya kuwasilisha mawazo na mipango ya biashara kwa wawekezaji (Demo Day), itakayofanyika tarehe 28 Mei 2027.

WSHA inapoingia mwaka wake wa tano, itaendelea kuwaunga mkono wajasiriamali wa Kitanzania kuimarisha biashara zao, kuvutia uwekezaji na kuongeza ajira, huku wakichangia kutafuta suluhisho za changamoto za mabadiliko ya tabianchi.




 Mfanyabiashara Peter Mwambo wa jijini Arusha amekuwa mshindi wa kwanza kujishindia pikipiki katika kampeni ya kukuza utamaduni wa kuweka akiba ya Benki ya Letshego Faidika, inayojulikana kama  “Weka. Tukuwekee!”

Mwambo amejishindia pikipiki hiyo kupitia mpango wa zawadi za kila mwezi wa kampeni hiyo ya wiki 12, ambayo ilizinduliwa Oktoba 5, 2026, ikiwa na lengo la kuwahamasisha Watanzania kuongeza akiba zao na kutumia huduma rasmi za kibenki.

Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi hiyo, Meneja wa Tawi la Benki ya  Letshego Faidika la Arusha, Neema Malisa, alisema benki hiyo imefurahi kumpata mshindi wake wa kwanza wa pikipiki tangu kuanza kwa kampeni hiyo.

Malisa alimpongeza Mwambo kwa ushindi huo na kuwahimiza wakazi wa Arusha pamoja na mikoa jirani kutumia huduma za benki hiyo kwa kuweka akiba na kupata fursa ya kushiriki katika kampeni zinazoandaliwa na kufaidika nazo.

Alisema kampeni ya  ‘Weka. Tukuwekee’ imekusudiwa kufanya uwekaji wa akiba kuwa rahisi, wenye manufaa na unaoweza kumwezesha kila Mtanzania kujenga utamaduni wa kuweka fedha kwa ajili ya mahitaji na mipango yake ya baadaye.

Aliongeza kuwa benki hiyo inaendelea kuboresha huduma zake ili kuwafikia wateja wengi zaidi, huku akieleza kuwa akaunti zake za akiba zinawapa wateja fursa ya kuweka fedha na kunufaika na huduma mbalimbali za kibenki.

Kwa upande wake, Meneja wa Masoko na Mawasiliano wa Letshego Faidika Bank, Kenneth Misigaro, alisema kampeni hiyo ni sehemu ya dhamira ya benki hiyo ya kuifanya huduma ya kuweka akiba iwe rahisi, yenye thamani na inayopatikana kwa Watanzania wengi zaidi.

Misigaro alisema benki inaendelea kupanua njia za uwekaji fedha na kusogeza huduma karibu na wananchi ili kuondoa vikwazo vinavyoweza kuwazuia kutumia huduma rasmi za kifedha.

Alisema wateja wanaweza kuweka fedha katika akaunti zao za LetsGo kupitia matawi na vituo vya benki hiyo, mawakala wake pamoja na mitandao ya simu ya M-Pesa, Airtel Money, Tigo Pesa na HaloPesa.

Pia, wateja wanaweza kuhamisha fedha kutoka benki nyingine kwenda kwenye akaunti zao za Letshego. Benki hiyo imepanua zaidi mtandao wake kwa kuruhusu wateja kuweka fedha kupitia mawakala wa CRDB na matawi ya Tanzania Commercial Bank (TCB), bila gharama za ziada za huduma hiyo.

Kampeni hiyo itakayohitimishwa Desemba 27, 2026, inatekelezwa katika kanda tano za benki hiyo nchini ambazo ni Kaskazini, Kati, Kusini, Magharibi na Ziwa.

Kupitia kampeni hiyo, wateja wanaoweka fedha katika akaunti za LetsGo wanashindanishwa katika makundi matatu kulingana na kiasi cha amana wanachoweka.

Katika kundi la Wathubutu, linalohusisha wateja wanaoweka hadi Sh50,000, mshindi wa kila wiki anapata Sh50,000. Kundi la Wajenzi, lenye amana za kati ya Sh50,000 na Sh500,000, linatoa zawadi ya Sh100,000, huku kundi la Wakubwa, kwa wanaoweka zaidi ya Sh500,000, likiwa na zawadi ya Sh200,000 kwa mshindi wa wiki.

Mbali na zawadi hizo za fedha, mteja atakayekuwa ameweka amana kubwa zaidi kila mwezi anajishindia pikipiki mpya, huku mteja atakayekuwa na jumla kubwa zaidi ya amana katika kipindi chote cha kampeni akitarajiwa kupata zawadi kuu ya guta la mizigo.

Akizungumzia ushindi wake, Mbwambo alisema hakutarajia kupata zawadi hiyo licha ya kuwa na utaratibu wa kuweka akiba katika benki mbalimbali.

Alisema ushindi huo ni wa kipekee kwake kwa kuwa hajawahi kupata zawadi ya aina hiyo kutokana na utaratibu wake wa kuweka akiba.

"Ni zawadi kubwa sana kwangu. Nitaiboresha biashara yangu kwa kuitumia pikipiki hii katika shughuli za usafirishaji na kuwafikia wateja wangu. Awali nilikuwa nikitumia pikipiki za kukodi, lakini sasa nitakuwa na yangu mwenyewe," alisema Mwambo.

Meneja wa Tawi la Benki ya  Letshego Faidika la Arusha, Neema Malisa (kulia) akikabidhi funguo ya pikipiki kwa mshindi wa kwanza wa kampeni ya Weka Tukuwekee, Peter Mwambo ambaye ni mfanyabiashara wa mkoa wa Arusha.Kampeni hiyo itakayodumu kwa wiki 12, imeanza tangu Oktoba 5 na inatarajiwa kumalizika Desemba 27, 2026, ikiwa inatekelezwa katika kanda tano nchini ambazo ni Kanda, Kati, Kusini, Magharibi, Ziwa na Kaskazini

Meneja wa Tawi la Benki ya  Letshego Faidika la Arusha, Neema Malisa (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na mshindi wa pikipiki wa droo ya kwanza ya kampeni ya kampeni ya Weka Tukuwekee, Peter Mwambo ambaye ni mfanyabiashara wa mkoa wa Arusha. Wa kwanza kulia ni meneja wa Amana wa Benki ya Letshego Faidika. Neema Soka.Kampeni hiyo itakayodumu kwa wiki 12, imeanza tangu Oktoba 5 na inatarajiwa kumalizika Desemba 27, 2026, ikiwa inatekelezwa katika kanda tano nchini ambazo ni Kanda, Kati, Kusini, Magharibi, Ziwa na Kaskazini.

Wafanyakazi wa benki ya Letshego Faidika na wadau wakiwa katika picha ya pamoja na mshindi wa pikipiki wa droo ya kwanza ya kampeni ya kampeni ya Weka Tukuwekee, Peter Mwambo (wa saba kutoka kulia) mara baada ya zoezi la kumkabishi zawadi yake ya kuwa mshindi wa kwanza wa kampeni ya Weka Tukuwekee. Kampeni hiyo itakayodumu kwa wiki 12, imeanza tangu Oktoba 5 na inatarajiwa kumalizika Desemba 27, 2026, ikiwa inatekelezwa katika kanda tano nchini ambazo ni Kanda, Kati, Kusini, Magharibi, Ziwa na Kaskazini.

MAKUNDI ya wasichana na wanawake vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 35 katika Manispaa ya Kibaha Mkoa wa Pwani na maeneo ya jirani wanatarajiwa kunufaika na mradi wa mwaka mmoja wa uwezeshaji kiuchumi unaolenga kukuza ajira, kujitambua na tija kwa jamii.

Mradi huo ujulikanao kama ' Girls Round Table- Season 12', utatekelezwa kwa pamoja na shirka lisilo la lissrikali la Nuruyetu Foundation na Serikali kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii na mamlaka za serikali za mitaa katika maeneo ya mradi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi katika Shule ya Msingi Sofu, Manispaa ya Kibaha hivi karibuni, Afisa Mtendaji wa Kata ya Sofu, Bi Aloysia Nyeto, alisema mradi huo unatarajiwa kubadilisha maisha ya wasichana na wanawake vijana ambao wamepoteza mwelekeo wa maisha, huku pia ukijenga uwezo wa jamii katika masuala mbalimbali ya maendeleo.

“Mradi huu utawafikia wasichana wetu na mabinti zetu, wengi wao waliokosa fursa za kufikia ndoto zao. Sambamba na hilo, jamii ambazo walengwa hawa wanatoka pia zitanufaika kwa namna moja ama nyingine kupitia programu za mradi huu. Tunashukuru sana Serikali kwa kutoa vibali kwa wadau mbalimbali wa maendeleo kufanya kazi na makundi mbalimbali ya watu katika maeneo yetu, na hii inaonesha dhahiri dhana ya utekelezaji wa malengo ya Dira ya 2050,” alisema.

Aliongeza kuwa, kupitia uwezeshaji wa kiuwezo na mtaji utakaotolewa kupitia mradi huo kwa walengwa hao, jamii katika maeneo husika zitajifunza umuhimu wa kuyajali makundi ya wanawake na wasichana kwa faida ya familia na jamii nzima.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Nuruyetu Foundation, Bi Zauja Mohamed, alisema wanawake vijana na wasichana kutoka maeneo ya Picha ya Ndege, Kwamfipa, Visiga na Sofu watanufaika katika awamu ya kwanza ya mradi huo, ambao unafadhiliwa kwa pamoja na Global Affairs Canada na Cuso International.

Akifafanua mradi huo, alisema walengwa watapata fursa ya kujifunza ujuzi wa kidijitali na fedha, utengenezaji wa kazi za mikono na ujuzi wa ujasiriamali.

“Tutaendelea kutafuta fursa mbalimbali kwa walengwa wa mradi huu kadri muda unavyokwenda. Lengo ni kuwawezesha kunufaika kulingana na uwezo wao wa kutumia ujuzi watakaoujifunza,” alisema.

Aliongeza kuwa mwishoni mwa mradi, walengwa watapewa vifaa vya kuanzishia biashara ili kuanzisha biashara zao wenyewe.

Alisema shirika hilo pia litaunga mkono Serikali katika kuimarisha masomo ya ufundi stadi kwa wasichana katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam, kama sehemu ya mradi huo.

Wakizungumza kwa niaba ya walengwa wengine, Olpa George wa Visiga na Rahma Hatibu wa Picha ya Ndege wote walionyesha matarajio makubwa ya mafanikio watakayoyapata kupitia mradi huo.
11-11- 2026, Dar es salaam
RAIS wa Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT), Ndg. Lukelo Willilo, ameteuliwa kuwa Kaimu Katibu Mkuu wa African Boxing, Shirikisho la Ngumi Barani Afrika.

Uteuzi huo ulifanywa rasmi na Rais wa African Boxing, Mheshimiwa Solomon Kargbo, na kuthibitishwa na Bodi ya Wakurugenzi katika kikao kilichofanyika tarehe 2-11-2026. Willilo alianza rasmi kutekeleza majukumu yake mapya tarehe 9-11-2026.

Mbali na nafasi hiyo mpya, Willilo pia ni mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya African Boxing na Mwenyekiti wa Kamati ya Mchezo na Mashindano ya Shirikisho hilo.

African Boxing ni chombo kinachosimamia na kuendeleza mchezo wa ngumi za mtindo wa Olimpiki katika bara la Afrika, na ni mshirika wa World Boxing.

Uteuzi huu unaifanya Tanzania kupata nafasi muhimu zaidi katika uongozi wa mchezo wa ngumi barani Afrika.

✍🏽 Mawasiliano BFT

Makamu  wa  Rais wa Kwanza Othman Masoud Othman akizungumza katika mkutano wa Maafisa Utumishi ulioendana na uzinduzi wa Mfumo wa Bima ya Maisha uliunganishwa Watumishi Portal
Mkurugenzi Mtendaji wa NIC Insurance Kaimu Mkeyenge akimsikiliza Makamu  wa  Rais wa Kwanza Othman Masoud Othman  katika mkutano wa Maafisa Utumishi ulioendana na uzinduzi wa Mfumo wa Bima ya Maisha uliunganishwa Watumishi Portal.
Maafisa utumimishi wakifatilia Mada ya Bima ya Maisha inayoyolewa na NIC Insurance

ZANZIBAR. Watumishi wa umma sasa wanaweza kujiunga na bima ya maisha ya Shirika la Bima la Taifa (NIC) kupitia Watumishi Portal (ESS), mfumo wanaoutumia kupata huduma za kiutumishi. Kwa kuweka huduma hiyo kwenye mfumo huo, NIC inalenga kurahisisha usajili na kupunguza matumizi ya fomu za karatasi.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, alizindua huduma hiyo Jumanne, tarehe 10 Novemba 2026, wakati wa Mkutano Mkuu wa 11 wa Mtandao wa Wasimamizi wa Rasilimali Watu katika Sekta ya Umma Barani Afrika (APS-HRMNet), uliofanyika Zanzibar. Othman pia alifungua mkutano huo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa NIC, Kaimu Abdi Mkeyenge, alisema huduma hiyo ni sehemu ya juhudi za shirika za kuwafikia wateja katika maeneo mbalimbali nchini. Hatua hiyo inaendana na msisitizo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, wa kutumia teknolojia kuboresha utoaji wa huduma katika taasisi za umma.

Katika mkakati wake wa matumizi ya teknolojia, NIC imeongeza njia ambazo mteja anaweza kutumia kupata taarifa, kununua bima na kufuatilia madai kupitia tovuti rasmi ya www.nicinsurance.co.tz, App ya NIC Kiganjani, na NIC Customer Portal. Shirika pia linatoa huduma kupitia NIC Rafiki kwenye WhatsApp.

Kupitia njia hizo, NIC inalenga kukidhi mahitaji ya wateja na kupanua upatikanaji wa ulinzi wa bima kwa watu binafsi, familia, taasisi na jamii kwa ujumla.

Kutoa huduma ya bima kupitia mfumo ambao watumishi tayari wanautumia kunaendana na Lengo la Nne la Dira 2050, linalohimiza matumizi ya teknolojia za kidigitali kuchochea ubunifu. Miongoni mwa shabaha za lengo hilo ni kuhakikisha zaidi ya asilimia 80 ya huduma za Serikali zinapatikana kupitia mifumo ya kidigitali iliyo salama na jumuishi.

Kwa mtumishi wa umma, urahisi wa kujiunga na bima ya maisha unatoa nafasi ya kupanga mapema ulinzi wa kifedha wa familia yake. Kwa kurahisisha hatua hiyo, NIC inalenga kuimarisha utamaduni wa kutumia bima kama sehemu ya mipango ya kifedha ya familia.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, leo tarehe 11 Novemba 2026 amekagua mradi wa ujenzi wa Stendi ya Mabasi ya Namtumbo, akiwa ziarani mkoani Ruvuma.

Mradi huo unaotekelezwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 8.4 unatarajiwa kuwa na Jengo la kisasa la utawala, Mgahawa, Kituo cha Polisi, Maduka pamoja na Barabara za ndani.

Stendi hiyo itaboresha huduma za usafiri kwa wananchi, kuongeza mapato ya halmashauri na kufungua fursa za ajira na biashara kwa vijana na wajasiriamali.

Akiwa katika eneo hilo, Mhe. Ndejembi ameielekeza Halmashauri hiyo kuwa na uhalisia katika kuzingatia mud ana fedha wakati wa kusaini mikataba ya ujenzi ili kuipunguzia Serikali mzigo wa malimbikizo ya madeni kwa wakandarasi.








 

KwaZulu-Natal, Afrika Kusini 

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imewapeleka nchini Afrika Kusini watumishi wake wanne kupata mafunzo ya wiki moja kuhusiana na Uhifadhi wa faru katika hifadhi ya Phinda  Private game Reserve  iliyopo Kwazulu Natal.

Mafunzo hayo yanatokana na ushirikiano wa karibu uliopo baina ya Hifadhi ya Ngorongoro na Phinda private Game Reserve ambapo hifadhi hizi zimekuwa zikishirikiana katika kufanikisha kuwalinda wanyama hao.

Kiongozi wa Ujumbe huo, Kanali Fikiri Machibya ambaye ni mshauri wa Jeshi la Uhifadhi ameeleza kuwa mafunzo hayo yameendelea kuwasaidia kujua mbinu ambazo hifadhi ya Phinda wanazotumia kulinda, kuhifadhi,kuzuia uharibifu, kufuatilia miendendo ya wanyamapori, mimea na matumizi ya teknolojia kama njia ya kisasa na imara kwenye ulinzi katika maeneo yenye changamoto.

Afisa Mhifadhi Mwandamizi ambaye ni mratibu wa Faru Ngorongoro Deogratius Maige ameeleza kuwa; "Ili nchi au  taasisi ifanikiwe kuwahifadhi Wanyama adimu kama  Faru ni muhimu  kuwajengea uzoefu kwa vitendo  watumishi kwenye nchi  ambazo zina uzoefu mkubwa wa kuwahifadhi na kuwalinda Wanyama hao, 

Mafunzo hayo pia yamekuwa ni  sehemu ya kubadilishana uzoefu kuhusu uhifadhi shirikishi kwa jamii zinazozunguka hifadhi, wajibu wa kutoa kwa jamii (CSR), uchomaji moto maeneo ya hifadhi kuimarisha malisho, kudhibiti uvamizi wa mimea na utoaji wa ajira za muda mfupi na mrefu kwa jamii zinazosaidia shughuli za uhifadhi.

Hifadhi ya Wanyamapori Binafsi ya Phinda iliyopo Jimbo la KwaZulu-Natal Nchini Afrika kusini ina ukubwa wa hekta 29,866 na moja ya maajabu ya dunia ikijumuisha wanyama mbalimbali wakiwepo Big Five (simba, chui, tembo, faru na nyati) na zaidi ya spishi 436 za ndege na kuifanya kuwa moja ya maeneo yanayoongoza kwa wanyamapori wengi Afrika Kusini.



Wananchi wa kijiji  cha Makhoromba wilayani Karatu hivi karibuni wanatarajiwa kupumua baada ya kumalizika kwa ujenzi wa uzio wa umeme unaofanywa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro  ambapo kwa sasa mradi huo  umefikia asilimia 72  ili uweze kukamilika.

Lengo la ujenzi wa uzio huo ni kuondoa migogoro baina ya wanyamapori wakali na waharibifu dhidi ya wananchi ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya CCM inayosisitiza umuhimu wa wananchi kulindwa.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Mamlaka  ya Hifadhi ya Ngorongoro Victoria Shayo, amesema ujenzi huo unafanyika ili wananchi katika eneo hilo na mali zao waweze kuwa salama.

Ziara hiyo imehitimishwa kwa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika kulinda na kutunza mazingira pamoja na kuhakikisha mradi huo unakuwa endelevu kwani uwepo wake utawazuia wanyamapori wakali kutotoka ndani ya hifadhi  ya Ngorongoro.