-Yawasogezea madereva wa bodaboda, bajaji na magari huduma za malipo ya kidijitali, bima na huduma za kibenki zinazolenga kulinda vyanzo vyao vya kipato.

Dar es Salaam, 14 Novemba 2026: Benki ya Exim Tanzania imetumia tamasha la Twende BBM Festival 2026 kuwasogezea madereva wa bodaboda, bajaji na magari huduma za kifedha zinazolenga kurahisisha shughuli zao za kila siku na kulinda vyanzo vyao vya kipato, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uhusiano na wadau wa sekta ya usafiri nchini.

Ikiwa mdhamini wa tamasha hilo, Exim Bank ilitumia fursa hiyo kuwafikia madereva wanaohusishwa na jukwaa la Twende. Jukwaa la Twende linahusisha madereva takribani 12,000 na jumuiya pana ya zaidi ya watumiaji 46,000 wa huduma zake. Kupitia tamasha hilo, Benki ya Exim ilipata fursa ya kukutana na kuwafahamisha madereva kuhusu huduma za kifedha zinazoweza kuwasaidia katika shughuli zao za kila siku.

Katika tamasha hilo, Benki ya Exim iliendeleza ujumbe wa kampeni “Exim Inalinda Hustle Yako” kwa kutambulisha huduma nne zinazolenga mahitaji ya madereva katika shughuli zao za kila siku. Huduma hizo ni Exim Lipa ChapChap, Tumaini Health Insurance, Motor Insurance na Exim Quick Account. Kwa pamoja, huduma hizi zinalenga kurahisisha upatikanaji wa malipo, kuwawezesha madereva kupata ulinzi wa afya na kulinda vyombo vya usafiri wanavyotegemea kujipatia kipato.

Akizungumza wakati wa tamasha hilo, Andrew Lyimo, Mkuu wa Kitengo cha Wateje Binafsi na Wakati wa Benki ya Exim Tanzania alisema benki inatambua mchango wa madereva katika kurahisisha usafiri na shughuli za kiuchumi, hivyo inaendelea kuwasogezea huduma zinazowasaidia kusimamia shughuli zao na kulinda vipato vyao.

“Kwa madereva wengi, bodaboda, bajaji na magari si vyombo vya usafiri pekee, bali ni nyenzo muhimu za kujipatia kipato na kutunza familia zao. Tunatambua changamoto na mahitaji yanayoambatana na kazi zao za kila siku. Ndiyo maana kupitia huduma zetu, tunalenga kurahisisha upatikanaji wa malipo, kuwapatia fursa ya kupata ulinzi wa afya na vyombo vyao vya usafiri, pamoja na huduma za kibenki zinazowawezesha kusimamia fedha zao kwa urahisi zaidi. Hii ndiyo maana halisi ya ujumbe wetu, Exim Inalinda Hustle Yako,” alisema Lyimo.

Kupitia Exim Lipa ChapChap, madereva wanaweza kurahisisha upokeaji na ufanyaji wa malipo. Tumaini Health Insurance inawawezesha kupata ulinzi wa bima ya afya, huku Motor Insurance ikitoa ulinzi wa bima kwa vyombo vya usafiri wanavyotumia katika shughuli zao za kila siku. Kw aupande wa Exim Quick Account, inawapa fursa ya kufungua akaunti na kutumia huduma za kibenki za Exim.

Xxxxxxx Mmoja wa madereva walioshiriki tamasha hilo, alisema ushiriki wa Exim Bank umewapa madereva fursa ya kufahamu huduma za kifedha zinazoweza kuwasaidia katika kusimamia na kulinda shughuli zao za kila siku.

“Ni jambo zuri kuona taasisi za kifedha zikija karibu nasi na kutuletea huduma zinazozingatia mahitaji yetu. Kazi yetu ya kila siku inategemea vyombo vyetu vya usafiri na uwezo wetu wa kuendelea kufanya kazi ili kupata kipato. Kwa hiyo, kufahamu huduma za malipo na bima zinazoweza kutusaidia kulinda kazi zetu ni jambo lenye umuhimu mkubwa kwetu,” alisema.

Kupitia ushiriki wake katika Twende BBM Festival 2026, Exim Bank imelenga kuongeza idadi ya watumiaji wa Exim Lipa ChapChap, kuwafikia wateja wapya wa Tumaini Health Insurance na Motor Insurance, pamoja na kuongeza idadi ya akaunti za Exim Quick Account zinazofunguliwa. Benki pia inalenga kujenga mahusiano ya muda mrefu na madereva, vikundi vyao na wadau wengine wa sekta ya usafiri kwa ajili ya fursa za ushirikiano wa baadaye.

Benki ya Exim inawaalika madereva, abiria na wadau wengine wa sekta ya usafiri kutembelea matawi yake nchini kote ili kupata maelezo zaidi kuhusu huduma hizo, kujisajili na kufungua akaunti. Kupitia huduma hizo, benki inalenga kuwasaidia wateja kurahisisha miamala yao, kupata ulinzi wa bima ya afya na vyombo vya usafiri, pamoja na kusimamia fedha zao kwa urahisi.








WIZARA ya Kilimo imefanya kikao kazi cha ushirikiano na wataalamu wa sheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria, tarehe 20 Novemba 2026, jijini Dodoma kwa lengo la kutathmini mapendekezo ya kutungwa kwa Sheria ya Ulinzi na Maendeleo ya Kilimo 2027.

Kikao kazi kimeongozwa na Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Kilimo, Bi. Angela K. Anatory, ambapo pamoja na masuala mengine ya kisheria, kikao pia kimejadili mapungufu katika mifumo ya sasa ya kisera, kisheria na kitaasisi inayosimamia sekta ya kilimo, pamoja na kuweka msingi wa kuimarisha ulinzi wa ardhi ya kilimo, kilimo cha mkataba, zana za kilimo na uratibu wa kisekta na kitaasisi.

Tathmini hiyo inalenga kuimarisha mazingira ya kisheria yatakayolinda rasilimali za kilimo, kuongeza uzalishaji, pamoja na kuhakikisha sekta ya kilimo inakuwa endelevu na yenye mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Hatua hiyo ni sehemu ya maandalizi ya kitaalamu ya kuimarisha mazingira ya kisheria na kitaasisi ya sekta ya kilimo, sambamba na Mwelekeo wa Maendeleo na Mageuzi ya Kilimo chini ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
















KAIMU Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Athumani Kilundumya, 
amesema kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha utekelezaji wa Azimio la Kampala chini ya Mpango Kabambe wa Maendeleo ya Kilimo Barani Afrika (CAADP), kwa lengo la kuongeza uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula, kukuza ajira na kuongeza mchango wa Sekta ya Kilimo katika uchumi wa Taifa.

Akizungumza wakati wa hitimisho la Ziara ya Uhamasishaji wa Utekelezaji wa Azimio la Kampala, tarehe 20 Novemba 2026 katika Hoteli ya Best Western jijini Dodoma, Mhandisi Kilundumya amesisitiza kuwa azimio hilo linaendana na vipaumbele vya Serikali vya kuleta mageuzi katika Sekta ya Kilimo kupitia sera, mikakati na uwekezaji unaolenga kuongeza tija na ushindani wa mazao ya kilimo.

Mhandisi Kilundumya, ambaye amemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli, amewashukuru wajumbe kutoka Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC), Sekretarieti ya SADC, Serikali ya Sudan Kusini, Wizara mbalimbali za Serikali, Taasisi za Umma, Sekta Binafsi, Mashirika yasiyo ya Kiserikali pamoja na Wadau wa Maendeleo kwa ushirikiano na michango yao iliyochangia mafanikio ya ziara hiyo.

Alieleza kuwa ziara hiyo imeongeza uelewa kuhusu malengo ya Azimio la Kampala na kutoa fursa kwa wadau kujadili hatua za kuharakisha utekelezaji wa ajenda ya mageuzi ya kilimo inayolenga uzalishaji wenye tija, biashara ya mazao, maendeleo ya viwanda vinavyotegemea kilimo, pamoja na kuimarisha mifumo himilivu ya chakula na lishe.

Aidha, amebainisha kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutekeleza agenda ya CAADP kwa kuimarisha uwekezaji katika umwagiliaji, matumizi ya zana na teknolojia za kisasa za kilimo, upatikanaji wa masoko na huduma za ugani, hatua ambazo ni muhimu katika kufikia malengo ya maendeleo ya Sekta ya Kilimo na ustawi wa wananchi.

Azimio la Kampala linatoa dira mpya ya maendeleo ya kilimo barani Afrika kwa kuhimiza nchi wanachama kuongeza kasi ya mageuzi ya Sekta hiyo ili kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira kwa vijana na wanawake, kuhakikisha usalama wa chakula na kujenga mifumo endelevu ya uzalishaji wa kilimo inayostahimili mabadiliko ya tabianchi.












Na Pamela Mollel, Arusha

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametunuku kamisheni kwa maafisa wanafunzi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kutoka kundi la 07/23 la Shahada ya Sayansi ya Kijeshi na kundi la 73/25 Regular, hafla iliyofanyika leo, Novemba 21, 2026, katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli, wilayani Monduli, Mkoani Arusha

Maafisa hao wanatunukiwa kamisheni baada ya kukamilisha mafunzo yao ya kijeshi na kupangiwa kuanza utumishi katika cheo cha Luteni Usu,Kwa mujibu wa taarifa ya Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli, kundi la 07/23 la Shahada ya Sayansi ya Kijeshi limepata mafunzo kwa muda wa miaka mitatu, huku kundi la 73/25 Regular likipata mafunzo kwa mwaka mmoja

Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli, Meja Jenerali Jackson Jairos Mwaseba, anabainisha kuwa baadhi ya maafisa wanafunzi wamepata mafunzo katika nchi rafiki ndani na nje ya bara la Afrika

Mafunzo hayo ni sehemu ya maandalizi ya maafisa hao katika kutekeleza majukumu yao ya kijeshi kwa weledi na kuzingatia misingi ya utumishi

Katika hafla hiyo, maafisa wanafunzi waliofanya vizuri katika maeneo mbalimbali ya mafunzo wanatambuliwa na kukabidhiwa zawadi na Rais Samia

Kwa kundi la 07/23, Afisa Mwanafunzi Nelson Kisomba anafanya vizuri zaidi katika fani zote kwa ujumla, Abdul-Halim Mohamed Othman anafanya vizuri zaidi katika taaluma, huku Jaquiline Kassian akifanya vizuri zaidi katika medani

Kwa upande wa kundi la 73/25 Regular, Afisa Mwanafunzi Steven Stanley Ubamba anatambuliwa kwa kufanya vizuri zaidi katika fani zote kwa ujumla, Vincent Benedict Mwakalila akifanya vizuri zaidi katika medani, huku Renatha Renatus Masunde akifanya vizuri zaidi katika taaluma

Aidha, Afisa Mwanafunzi Wickliffe Otiato Abeta kutoka Jamhuri ya Kenya anatambuliwa kwa kufanya vizuri zaidi miongoni mwa maafisa wanafunzi kutoka nchi rafiki

Hafla hiyo inahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na Jeshi, akiwemo Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho; Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob John Mkunda pamoja na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi, Luteni Jenerali Salum Haji Othman huku viongozi wengine ni makamanda, maafisa waandamizi wa JWTZ, wawakilishi wa nchi rafiki na wazazi pamoja na walezi wa maafisa wanafunzi

Kukamilika kwa mafunzo hayo na kutunukiwa kamisheni kwa maafisa wapya ni hatua muhimu katika kuwaandaa kutekeleza majukumu yao ndani ya JWTZ

Aidha Ujuzi na maarifa waliyopata vinatarajiwa kuwa msingi wa utendaji wao katika kulitumikia taifa kwa nidhamu, uzalendo, uadilifu na uwajibikaji, kwa kuzingatia majukumu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania katika kulinda uhuru na usalama wa nchi.
















▪️ Aonya dhidi ya kujichukulia sheria mikononi na kuuza ardhi kinyemela

▪️ Serikali yakamilisha usanifu wa barabara ya njia sita kutoka Picha ya Ndege hadi Chalinze


WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amekemea tabia ya watu kujichukulia sheria mkononi na kuonya kuwa Serikali haiungi mkono uvunjaji wa sheria wa makusudi.

“Tusiruhusu uvunjifu wa sheria wa makusudi kwa sababu utaua udugu wetu uliokuwepo kwa miaka mingi. Lazima tuzingatie utawala wa sheria, tuache utaratibu wa uvunjifu wa sheria na kujichukulia sheria mkononi,” amesisitiza.

Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Viwanja vya Polisi, wilayani Chalinze, mkoani Pwani, jana jioni (Jumamosi, Novemba 21, 2026), Waziri Mkuu alisema mmomonyoko wa utawala wa sheria unaalika visasi na makovu yasiyopona.

“Tusibaguane au kuchukiana kwa sababu ya ardhi kwani yenyewe haiongezeki lakini mahitaji ya ardhi yanaongezeka. Tunatakiwa tuweke nguvu kubwa katika kupanga matumizi bora ya ardhi na tuheshimu sheria,” alisisitiza.

Dkt. Mwigulu alisema Serikali haitavumilia vitendo vinavyofanywa na baadhi ya watu vya kulisha mifugo kwenye mashamba ya watu wengine kwa makusudi, kujeruhi mifugo au kushambulia watu kwa kulipiza kisasi.

“Kama mifugo yako inapenda kula mazao ya mashambani, basi lima mashamba yako kisha uingize mifugo yako shambani mwako. Mambo ya kuchukua chukua sheria mkononi yanaalika visasi. Na damu ikimwagika katika ardhi inaleta laana,” alisema.

Aliwaagiza viongozi wa wilaya na vijiji washughulikie migogoro hiyo kwa mujibu wa sheria, huku akikemea uuzaji wa ardhi kinyemela na kusisitiza kuwa kosa la mtu mmoja halipaswi kugeuzwa kuwa kosa la jamii nzima.

Kwa upande wake, Mbunge wa Chalinze ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, alisema uchunguzi wa mgogoro wa mipaka kati ya vijiji vya Pingo na Chamakweza umekamilika na taarifa yake iko tayari kwa hatua zinazofuata.

Alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kupeleka miradi mingi kwenye Halmashauri ya Wilaya hiyo, ikiwemo ya maji, elimu, afya na barabara.

“Wakati naanza ubunge, hatukuwa na Hospitali ya Wilaya lakini hivi sasa tumekamilisha ujenzi wake na tumepata shilingi bilioni tatu za ujenzi wa ICU,” alisema.

Alisema zamani, pakitokea ajali yoyote kati ya Kabuku (Tanga) na Chalinze (Pwani), walikuwa wakikimbilia Hospitali ya Tumbi ili kupeleka majeruhi huko, lakini kwa sasa hawatalazimika kuitegemea tena hospitali hiyo kwani wamepata kitengo cha wagonjwa wa dharura (EMD) cha kisasa kabisa.

Naye, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kaspar Mmuya, alisema vijiji hivyo ni miongoni mwa vijiji 16 vilivyopangwa kuandaliwa mipango bora ya matumizi ya ardhi mwaka huu ili kusaidia kutatua migogoro iliyodumu kwenye maeneo hayo.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, alisema Serikali imekamilisha usanifu wa barabara ya njia sita yenye urefu wa kilometa 74, kutoka Picha ya Ndege hadi Chalinze, inayotarajiwa kutekelezwa kupitia ubia kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP).

Alisema uthamini wa maeneo yanayohitajika kwa ajili ya mradi huo unaendelea, huku Serikali pia ikipanga kuboresha barabara iliyopo ya Dar es Salaam–Kibaha–Mlandizi–Chalinze ili kupunguza msongamano wa magari.