Na Oscar Assenga, TANGA

WAKALA wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Tanga unatarajia kufanya ukarabati wa madaraja ya Hale na Maguzoni yaliyopo katika barabara kuu ya Tanga–Segera, kwa lengo la kuimarisha usalama na kulinda miundombinu hiyo dhidi ya athari za mvua kubwa.

Hatua hiyo imekuja baada ya wataalamu wa TANROADS kufanya ukaguzi wa barabara na madaraja mkoani humo kufuatia taarifa za uwepo wa mvua nyingi za El Niño nchini, ambapo walibaini changamoto zinazohitaji kushughulikiwa katika madaraja hayo.

Akizungumzia hatua hiyo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tanga, Mhandisi Msama K Msama alisema ukarabati huo utahusisha maeneo ya chini ya madaraja yanayopitisha maji pamoja na vyuma vilivyopo katika sehemu za juu za madaraja ambavyo vimeathiriwa na kutu.

Alisema wamebaini kuwa maji ya mvua yanapita katika baadhi ya maeneo ya madaraja na kusababisha vyuma kupata kutu na kuharibika, hali inayohitaji hatua za haraka ili kuzuia uharibifu zaidi na kuhakikisha madaraja yanaendelea kutekeleza majukumu yake.



Alisema ukarabati huo unalenga kuimarisha uimara wa madaraja hayo na kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara, wakiwemo wasafiri na wasafirishaji wanaotumia njia hiyo muhimu.

Alifafanua kuwa ili kuruhusu kazi hiyo kufanyika kwa ufanisi na kwa muda uliopangwa, barabara ya Tanga–Segera itafungwa kwa muda wa saa nne, kuanzia asubuhi hadi saa sita mchana, Jumanne, Oktoba 20.

Alisema TANROADS imejipanga kuhakikisha mitambo na vifaa vinavyohitajika vinafika eneo la kazi ili ukarabati ukamilike ndani ya muda uliopangwa na kuruhusu magari kuendelea na safari zake.


Meneja huyo aliwataka wasafiri na wasafirishaji kupanga safari zao mapema kwa kuzingatia muda wa kufungwa kwa barabara hiyo ili kupunguza usumbufu unaoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa kazi hizo.

Barabara ya Tanga–Segera ni kiunganishi muhimu cha usafiri na usafirishaji, inayohudumia magari yanayotoka Dar es Salaam kupitia Chalinze kuelekea Segera na kuendelea Tanga, pamoja na magari yanayotoka mikoa ya Singida, Arusha na Kilimanjaro.


Aidha, barabara hiyo hutumiwa na magari yanayohudumia shughuli za Bandari ya Tanga pamoja na usafirishaji unaotoka eneo la Horohoro mpakani mwa Tanzania na Kenya.

Kosani alisema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha madaraja na barabara vinaendelea kuwa salama kwa matumizi ya wananchi na wadau wa usafirishaji.




Na Byera Deus, Ngara

NAIBU Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Andrew Mathew, amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua za kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa Kata ya Kabanga, wilayani Ngara, mkoani Kagera, ikiwemo kutafuta chanzo kipya cha maji ili kukidhi mahitaji ya wananchi.

Akizungumza na wananchi wa Kabanga, Mhandisi Kundo amesema Serikali imepeleka mradi wa maji wenye thamani ya Sh milioni 120 katika kata hiyo, huku mradi mwingine wenye thamani ya Sh milioni 300 ukiwa sehemu ya juhudi za kuimarisha upatikanaji wa huduma hiyo muhimu.

Amesema Serikali pia itafanyia kazi changamoto ya mabomba chakavu yanayopasuka na kusababisha upotevu wa maji, akisisitiza umuhimu wa kuboresha miundombinu ya usambazaji ili wananchi wanufaike na huduma hiyo kwa uhakika.

Aidha, amewataka wananchi kushirikiana na Serikali katika kulinda miundombinu na vyanzo vya maji ili kuhakikisha miradi inayotekelezwa inadumu na kutoa huduma kwa muda mrefu.

Amesema fedha zinazotumika kutekeleza miradi ya maendeleo zinatokana na kodi za wananchi, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kulinda na kutunza miradi hiyo kwa manufaa ya jamii.

Mhandisi Kundo ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya maji katika vijiji mbalimbali vya Wilaya ya Ngara kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi na kuchochea shughuli za kiuchumi, zikiwemo biashara na shughuli za kila siku za kaya.










  Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam 


Serikali imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na madhehebu ya dini nchini, ikitambua mchango wake katika malezi ya kiroho, utoaji wa huduma za kijamii na kuimarisha amani na mshikamano wa kitaifa.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, aliyemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika ibada takatifu ya kumweka wakfu Askofu John Jumanne Wambura wa Kanisa la Mennonite Tanzania (KMT), iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Oktoba 18, 2026.

Akizungumza katika ibada hiyo, Mhe. Sangu amesema viongozi wa dini wameendelea kuwa nguzo muhimu katika kutoa mafundisho, ushauri na malezi bora, pamoja na kuwahudumia wananchi wenye mahitaji maalumu, wakiwemo yatima, wajane na watu wenye ulemavu.

Amesema Serikali inatambua mchango wa taasisi za dini katika sekta za afya, elimu na huduma nyingine za kijamii, hususan katika maeneo ya pembezoni, na kwamba ushirikiano huo ni muhimu katika kuharakisha maendeleo ya wananchi. Aidha, amewataka viongozi wa dini kuendelea kuliombea Taifa na kuhamasisha jamii kulinda amani iliyopo nchini, akisisitiza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu iko tayari kushirikiana na wadau wote katika kuimarisha mshikamano na maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Mennonite Tanzania, Nelson Kisare, amewataka viongozi kutumia nafasi walizopewa kwa manufaa ya watu wanaowaongoza na jamii kwa ujumla, badala ya kujinufaisha binafsi. Amesema viongozi wanapaswa kuwa vielelezo vya maadili mema na matendo yanayojenga jamii. Huku Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, amelishukuru Kanisa la Mennonite kwa kuendelea kuliombea Taifa na kuchangia juhudi za kudumisha amani nchini.










Tume ya Taifa ya UNESCO yakutana na BAKITA, BAKIZA na TATAKI kujadili ushirikiano wa maendeleo ya Kiswahili

Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekutana na viongozi na wataalamu kutoka Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA) na Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI), kwa lengo la kuimarisha uratibu na ushirikiano wa kitaasisi katika kukuza nafasi ya lugha ya Kiswahili katika ngazi ya kikanda na kimataifa.

Kikao hicho cha pamoja cha kiofisi kimewakutanisha wawakilishi wa taasisi hizo nne kwa ajili ya kuimarisha mawasiliano na ushirikiano katika masuala yanayohusu maendeleo ya Kiswahili, kwa kuzingatia umuhimu wa kuunganisha juhudi za kitaifa na kutumia fursa zinazopatikana katika majukwaa ya kimataifa.


Katika mazingira ambayo lugha zina nafasi muhimu katika mawasiliano, utamaduni na ubadilishanaji wa maarifa, uratibu wa kitaifa ni nyenzo muhimu katika kuendeleza nafasi ya Kiswahili na kuongeza mwonekano wake katika majukwaa mbalimbali ya kikanda na kimataifa.

Kupitia kikao hicho, washiriki walikubaliana kuendelea kutumia mifumo na fursa zilizopo za kidiplomasia na ushirikiano wa kimataifa katika kuendeleza nafasi ya Kiswahili, sambamba na kuzingatia misingi rasmi ya usanifishaji na maendeleo ya lugha hiyo.

Ushirikiano kati ya Tume ya Taifa ya UNESCO, BAKITA, BAKIZA na TATAKI unaunganisha majukumu na utaalamu wa taasisi hizo katika masuala ya lugha, taaluma, utafiti na maendeleo ya Kiswahili. Ushirikiano huo ni muhimu katika kuweka msingi wa uratibu wa pamoja kuhusu fursa zinazoweza kuchangia kukuza lugha hiyo katika ngazi ya kimataifa.

Aidha, hatua hiyo inaonesha umuhimu wa ushirikiano wa taasisi za kitaifa katika kuendeleza Kiswahili kama lugha ya mawasiliano, maarifa na utamaduni, huku ikiimarisha juhudi za kuhakikisha lugha hiyo inaendelea kupata nafasi katika mazingira yanayozidi kuunganishwa kupitia mawasiliano ya kimataifa.

Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kushirikiana na wadau wa kitaifa katika kutekeleza majukumu yake yanayohusiana na maeneo ya UNESCO, ikiwemo mawasiliano na taarifa, kwa kuzingatia fursa za ushirikiano wa kikanda na kimataifa.

Tume ya Taifa ya UNESCO — Kuimarisha ushirikiano wa kitaifa kwa maendeleo ya lugha, maarifa na utamaduni.
Na Byera Deus, Biharamulo

WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) umetakiwa kuhakikisha mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji wa Nyakanazi–Nyakafundikwa, wilayani Biharamulo, mkoani Kagera, analipwa Sh milioni 600 ifikapo Desemba mwaka huu ili kuharakisha ukamilishaji wa mradi huo unaotarajiwa kunufaisha wananchi wapatao 42,000.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Maji, Kundo Mathew, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo wenye thamani ya Sh bilioni 2.9, ambao hadi sasa umefikia asilimia 78 ya utekelezaji.

Amesema kazi kubwa za ujenzi zimekamilika, huku shughuli zilizobaki zikihusisha kukamilisha vituo vya kuchotea maji ili kuwezesha wananchi kuanza kupata huduma hiyo ifikapo Desemba mwaka huu, endapo malipo kwa mkandarasi yatafanyika kwa wakati.

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji inayoukabili mji wa Nyakanazi, ambao unaendelea kukua kwa kasi na kuwa na mahitaji makubwa ya huduma za kijamii na kiuchumi.

Ameeleza kuwa Nyakanazi ni eneo muhimu kiuchumi na kijiografia, likiwa lango la wageni wanaoingia na kutoka katika nchi jirani za Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), hivyo upatikanaji wa maji ya uhakika ni muhimu kwa wakazi na wageni wanaopita katika eneo hilo.

Naibu Waziri huyo amesisitiza kuwa malipo ya wakandarasi kwa wakati ni muhimu katika kuhakikisha miradi ya maji inakamilika kwa mujibu wa malengo yaliyowekwa, akilitaka RUWASA kuhakikisha wakandarasi wa ndani wanaotekeleza miradi hiyo hawakwami kutokana na ucheleweshaji wa malipo.

Kwa upande wake, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Biharamulo, Mhandisi Lucas Matina, amesema kazi zilizotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa chanzo cha maji na miundombinu mingine ya mradi, huku kazi iliyobaki ikiwa ni kukamilisha vituo vya kuchotea maji ili huduma iweze kutolewa kwa wananchi wa Nyakanazi na maeneo jirani.

Amesema licha ya mradi kufikia asilimia 78 ya utekelezaji, mkandarasi amelipwa Sh milioni 700 pekee kati ya gharama zote za mradi, huku akiwa anadai zaidi ya Sh bilioni 1.4, hali inayohitaji hatua za haraka ili kukamilisha kazi zilizobaki.

Naye Mkurugenzi wa Mipango wa RUWASA Makao Makuu, Mhandisi Enock Wagala, amesema wakala huo unafanyia kazi agizo la Naibu Waziri, huku Sh milioni 600 zikitarajiwa kulipwa ifikapo Desemba mwaka huu ili kuharakisha ukamilishaji wa mradi.

Amesema RUWASA inatambua umuhimu wa mradi wa Nyakanazi–Nyakafundikwa katika kutatua changamoto ya maji safi na salama kwa maelfu ya wananchi, kutokana na ukuaji wa mji huo na ongezeko la mahitaji ya huduma za kijamii na kiuchumi.







Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Deogratius Ndejembi, ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa majengo mapya ya Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE), mkoani Iringa, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya elimu ya juu kupitia uwekezaji wa kimkakati unaolenga kupanua fursa za elimu, kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuzalisha wataalamu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya maendeleo ya taifa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu wa Rais amesema Serikali, kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, imewekeza zaidi ya dola za Marekani milioni 425, sawa na takribani shilingi trilioni moja, katika kuimarisha elimu ya juu nchini kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), huku Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa kikinufaika na uwekezaji wa zaidi ya shilingi bilioni 30.

Amesema uwekezaji huo ni kielelezo cha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha ongezeko la wanafunzi wanaohitimu elimu ya msingi na sekondari linaendana na upatikanaji wa nafasi za elimu ya juu, akibainisha kuwa tangu mwaka wa fedha 2021/2022, Mkoa wa Iringa umepokea zaidi ya shilingi bilioni 175 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu katika ngazi hizo.

Katika kuhakikisha uwekezaji huo unaleta matokeo yaliyokusudiwa, Mheshimiwa Ndejembi ameuagiza uongozi wa Chuo hicho kusimamia kwa umakini, uwazi na uadilifu fedha zote zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, huku akisisitiza umuhimu wa kukamilisha ujenzi kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya ubora. Amesema Serikali haitavumilia matumizi yasiyo sahihi ya fedha za umma, kwani kila shilingi inayowekezwa katika elimu inapaswa kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa Watanzania.

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Profesa Adolf Mkenda, akizungumza wakati wa kumkaribisha Makamu wa Rais, ameipongeza na kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kufanya uwekezaji mkubwa na wa kihistoria katika sekta ya elimu ya juu, akieleza kuwa kupitia Mradi wa HEET, jumla ya Taasisi 20 za elimu ya juu nchini zimenufaika na ujenzi wa maabara 309, hosteli 26, maktaba, kafeteria na ofisi 1,177, pamoja na ukarabati wa majengo 48, hatua inayofungua ukurasa mpya katika kuboresha mazingira ya ufundishaji, ujifunzaji, tafiti na ubunifu nchini.

Profesa Mkenda amesema mafanikio hayo hayaishii katika ujenzi wa majengo pekee, bali yameambatana na upanuzi wa wigo wa elimu ya juu kwa kuanzishwa kwa kampasi mpya katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo mikoa ya Manyara, Kagera, Lindi, Njombe, Katavi, Kigoma, Mwanza, Rukwa, Simiyu, Shinyanga, Tabora, Tanga, Singida, Mara na Ruvuma pamoja na Zanzibar. Amesema hatua hiyo inalenga kusogeza huduma za elimu ya juu karibu na wananchi, kupunguza changamoto ya umbali na gharama za masomo, pamoja na kutoa fursa zaidi kwa vijana kupata elimu na ujuzi utakaowawezesha kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa Taifa.

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa, amesema chuo hicho kimeendelea kupiga hatua kubwa katika kuimarisha miundombinu ya elimu kupitia utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa majengo saba yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 30.4, inayojumuisha majengo ya sayansi, maabara ya fizikia, midia anuwai na elimu maalumu, hosteli za wanafunzi pamoja na maktaba. Ameeleza kuwa hadi kufikia Septemba 30, 2026, ujenzi wa majengo manne yanayofadhiliwa kupitia Mradi wa HEET ulikuwa umekamilika kwa asilimia 100, hatua inayotarajiwa kuongeza uwezo wa chuo kupokea wanafunzi wengi zaidi na kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa.

Mkwawa ni miongoni mwa vyuo muhimu vinavyoandaa walimu wa sayansi na masomo mengine hapa nchini. Kuongezeka kwa mabweni, maabara na madarasa ya kisasa kutaongeza idadi ya wanafunzi wanaoweza kudahiliwa na kuimarisha mafunzo ya vitendo kwa walimu watakaofundisha vizazi vijavyo






















Na. Joseph Mahumi, Bangkok, Thailand

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ameishukuru Benki ya Dunia kwa mchango wake katika kuimarisha ushirikiano wa maendeleo na Tanzania, hususan katika ufadhili wa miradi ya kimkakati, maendeleo ya rasilimali watu, nishati na miundombinu ya usafirishaji, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano huo kwa manufaa ya wananchi na ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la Kwanza la Afrika la nchi wanachama wa Benki hiyo anayemaliza muda wake, Dkt. Zarau Kibwe, kando ya Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Kundi la Benki ya Dunia, jijini Bangkok, Thailand.

Mhe. Balozi Omar aliishukuru Benki ya Dunia kwa mchango wake katika maendeleo ya sekta ya nishati, akibainisha kuwa ushirikiano huo umechangia juhudi za kupanua upatikanaji wa umeme na kuimarisha miundombinu ya nishati, sambamba na mpango wa Mission 300 unaolenga kuongeza upatikanaji wa umeme barani Afrika.

“Tanzania imenufaika na ufadhili wa IDA-20 wa karibu dola bilioni sita za Marekani, huku chini ya IDA-21 tukipangiwa dola bilioni 2.54 za Marekani na ahadi za ufadhili zinazozidi dola milioni 760, huku miradi mingine ikiendelea kuandaliwa kwa ajili ya utekelezaji” alisema Mhe. Balozi Omar

Akizungumzia ukubwa wa ushirikiano wa sasa kati ya Tanzania na Benki ya Dunia, Mhe. Balozi Omar amesema kuwa thamani ya miradi 33 inayotekelezwa kupitia ushirikiano huo imefikia zaidi ya dola bilioni 8.8 za Marekani, ambapo miradi 30 ni ya kitaifa na mitatu ni ya kikanda, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha miundombinu na kuifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha shughuli za kiuchumi na usafirishaji Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Katika eneo la usafirishaji, Mhe. Balozi Omar alisema Serikali inaendelea kushirikiana na Benki ya Dunia katika kuboresha Ushoroba wa Kati (Central Corridor), kwa kuzingatia umuhimu wa kuunganisha bandari, reli na miundombinu mingine ya usafirishaji ili kurahisisha biashara na kuongeza fursa za uwekezaji.

“Serikali inalenga kuubadilisha Ushoroba wa Kati kutoka njia ya usafirishaji na kuufanya kuwa Ushoroba wa Maendeleo na Ustawi wa Kiuchumi (Economic Prosperity Corridor), kwa kutambua na kuendeleza fursa za uwekezaji, kuongeza ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi katika maeneo yanayopitiwa na miundombinu hiyo.” alisema Mhe. Balozi Omar.

Aliongeza kuwa Tanzania inathamini mchango wa Dkt. Kibwe katika kufanikisha majukwaa muhimu ya kimataifa yaliyofanyika nchini, yakiwemo Mkutano wa Wakuu wa Nchi kuhusu Rasilimali Watu (Human Capital Summit) uliofanyika Dar es Salaam mwezi Julai 2023, pamoja na Mkutano wa Mapitio ya Katikati ya Kipindi cha Mfuko wa Maendeleo wa Kimataifa (IDA) uliofanyika Zanzibar mwezi Desemba 2024.

Ameeleza kuwa mikutano hiyo imeipa Tanzania fursa ya kuimarisha nafasi yake katika mijadala ya maendeleo ya Afrika na kimataifa, hususan katika kuboresha rasilimali watu, ambayo ni nguzo muhimu katika kukuza uchumi na kukabiliana na changamoto za maendeleo barani Afrika.

Mhe. Balozi Omar alieleza matumaini ya Tanzania kuendelea kuimarisha ushirikiano na Mkurugenzi mpya atakayechukua nafasi hiyo Bi. Lonkhululeko Magagula, atakayechukua nafasi hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la Kwanza la Afrika la nchi wanachama wa Benki hiyo anayemaliza muda wake, Dkt. Zarau Kibwe, ameipongeza Tanzania kwa hatua zilizopigwa katika kuimarisha ushirikiano wake na Benki ya Dunia, akibainisha kuwa thamani ya miradi ya maendeleo kati ya pande hizo imeongezeka kutoka takribani dola bilioni nne alipokuwa akianza majukumu yake hadi kufikia kiwango cha sasa.

Alisema mafanikio hayo yanaonesha hatua kubwa iliyofikiwa katika kuimarisha ushirikiano na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, huku akieleza kuwa akiwa Benki ya Dunia, anajivunia kushuhudia Tanzania ikifikia hadhi ya nchi yenye uchumi wa kipato cha kati.

Dkt. Kibwe alisisitiza umuhimu wa Tanzania kuendelea kutumia fursa za uwekezaji katika miundombinu na maendeleo ya sekta ya madini, akieleza kuwa nchi hiyo ni miongoni mwa nchi 30 zinazozingatiwa katika mpango wa Benki ya Dunia unaolenga kuimarisha maendeleo ya sekta ya madini na rasilimali zake.

“Mpango huu unajumuisha maeneo muhimu matatu ambayo ni kuimarisha utawala na usimamizi wa sekta ya madini, kuendeleza miundombinu inayowezesha uchimbaji na usafirishaji wa madini, pamoja na kuongeza upatikanaji wa mitaji na uwekezaji katika sekta hiyo” alisema Dkt. Kibwe.

Mazungumzo hayo yameonesha dhamira ya Tanzania ya kuendeleza ushirikiano na washirika wake wa maendeleo ili kutumia fursa za ufadhili, uwekezaji na utaalamu katika kutekeleza miradi ya kimkakati na kufikia malengo ya maendeleo ya taifa.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Waziri wa Fedha-Zanzibar, Mhe. Dkt Juma Malik Akil, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Tausi Kida, na maafisa wengine waandamizi wa Serikali na Benki ya Dunia.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (Kushoto) akiwa katika picha na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la Kwanza la Afrika la nchi wanachama wa Benki ya Dunia anayemaliza muda wake, Dkt. Zarau Kibwe, walipokutana na kufanya mazungumzo, kando ya Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Kundi la Benki ya Dunia, jijini Bangkok, Thailand.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (wa tatu kushoto), Waziri wa Fedha-Zanzibar, Mhe. Dkt Juma Malik Akil (wa pili kushoto), Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba (wa tatu kulia), Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Tausi Kida (kulia), Mkurugenzi wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la Kwanza la Afrika la nchi wanachama wa Benki hiyo anayemaliza muda wake, Dkt. Zarau Kibwe (wa pili kulia), Mkurugenzi Mbadala wa Kundi la Kwanza la Afrika la nchi wanachama wa Benki ya Dunia, Bi. Lonkhululeko Magagula, wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya mazungumzo yao, kando ya Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Kundi la Benki ya Dunia, jijini Bangkok, Thailand.


Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akiongoza kikao na ujumbe wa Benki ya Dunia ukiongozwa na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la Kwanza la Afrika la nchi wanachama wa Benki hiyo anayemaliza muda wake, Dkt. Zarau Kibwe, walipokutana na kufanya mazungumzo kando ya Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Kundi la Benki ya Dunia, jijini Bangkok, Thailand.


(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, jijini Bangkok, nchini Thailand)



Na Mwandishi Wetu, Pwani

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa ofisi ya CCM Kata ya Kimanzichana Kusini, wilayani Mkuranga, mkoani Pwani, na kuchangia Sh milioni tano kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo.

Ujenzi wa ofisi hiyo unatarajiwa kugharimu jumla ya Sh milioni 34 hadi kukamilika kwake, huku kazi za ujenzi zikiwa zimefikia hatua ya upigaji wa sakafu.

Akizungumza na wananchi wakati wa ziara yake wilayani Mkuranga, leo Oktoba 18, 2026, Kihongosi ameipongeza CCM Kata ya Kimanzichana Kusini kwa juhudi za kujenga ofisi hiyo, akisema hatua hiyo inalenga kuimarisha shughuli za chama katika ngazi ya kata.

Aidha, amesema Wilaya ya Mkuranga imepiga hatua katika maendeleo ikilinganishwa na miaka ya nyuma, akitaja mabadiliko ya makazi ya wananchi na upatikanaji wa huduma za kijamii.

Amesema Serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya wananchi wa Mkuranga, ikiwemo huduma za umeme, maji na afya kupitia hospitali ya wilaya, vituo vya afya na zahanati.

“CCM itaendelea kuwa chama kinachoongoza kwa sababu ni chama kinachotekeleza ahadi zake. Kimeahidi kuleta maendeleo kwa wananchi na kimeendelea kuyatekeleza,” amesema Kihongosi.

Ameongeza kuwa maboresho katika sekta ya afya yamepunguza changamoto ambazo wananchi, hususan wanawake wajawazito, walikuwa wakikabiliana nazo walipokuwa wakitafuta huduma za kujifungua.














Top News