Na Seif Mangwangi, Michuzi TV Arusha

WANAFUNZI wanaofanya ubunifu wa matumizi ya teknolojia mbalimbali katika chuo cha ufundi Arusha (ATC), wametakiwa kusoma Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kuielewa na kuona fursa zilizopo ndani yake na kufanya bunifu zao kutokana na malengo ya dira hiyo.

Hayo yameelezwa Juni 19, 2026 na Mkuu wa chuo cha ufundi Arusha Profesa Musa Chacha katika hotuba yake ya kufungua wiki ya maonyesho ya ubunifu yanayoandaliwa kila mwaka chuoni hapo.

Profesa Chacha amesema dira ya Taifa 2050 imeainisha maeneo ambayo yanapaswa kuendelezwa kwaajili ya Maendeleo ya Watanzania hivyo wanafunzi wanaofanya bunifu chuoni hapo wanapaswa kuyasoma na kuyajua na kuyafanyia ubunifu.

Amesema kutokana na kazi nzuri ya ubunifu ambayo imekuwa ikifanywa na wanafunzi chuoni hapo, chuo kimepanga kujenga jengo maalum la ghorofa nne ambalo litatumika kwaajili ya shughuli za ubunifu.

“ Kwa kushirikiana na Serikali ya Italia hivi karibuni tunatarajia kujenga jengo kubwa la ghorofa nne ambalo litatumika kwaajili ya shughuli za ubunifu( innovation), hapa chuoni hatutaki hivi vipaji vyenu vipotee,” amesema.

Aidha Profesa Chacha amesema chuo kinaendelea na ujenzi wa karakana ( industrial workshop), ambayo itatumika kutengeneza mitambo bunifu itakayokuwa ikigunduliwa na wanafunzi chuoni hapo kwaajili ya kuuzwa na kwamba tayari mashine zitakazotumika katika karakana hiyo zipo njiani kufika chuoni hapo.

“ Hivi sasa tumeamua kuendeleza bunifu zote zitakazobuniwa na wanafunzi Kwa kuzizalisha na kuziingiza sokoni, tutakuwa na kiwanda hapa hapa chuoni na wote mnaofanya ugunduzi huu tutaendelea kuwafuatilia na kuona namna mnafaidika na bunifu zenu, tutawashika mkono popote mtakapoenda,” amesema Profesa Chacha.

Aidha amesema chuo kinakamilisha jengo la hospitali itakayokuwa ikitibia wanafunzi chuoni hapo lakini pia chuo kipi kwenye mikakati ya kujenga jengo litakalojulikana kama innovation center ambalo litakuwa maalum kwaajili ya ugunduzi na uzalishaji wa vifaa tiba vya hospitalini ( biomedical engineering).

Awali akimkaribisha mgeni rasmi Makamu mkuu wa chuo, Dkt Yusuph Mhando alisema katika maonyesho ya mwaka huu ambayo ni awamu ya tatu tangu kuanzishwa, jumla ya bunifu 75 ziliingia kwenye ushindani.

Amesema kati ya bunifu hizo, bunifu 20 zilihusiana na teknolojia ya habari na mawasiliano(Tehama), umeme 15, mitambo na magari 19, sayansi timizi 8, ujenzi na barabara13 na kwamba baada ya majaji kupitia bunifu hizo jumla ya bunifu 19 pekee ziliweza kuingia fainali.

Amesema mshindi wa kwanza ametoka katika fani ya mitambo aliyegundua mashine inayojulikana kama ( Energy trauma kit), akifuatiwa na Tehama ambaye amegundua mashine ya kupima uoni wa macho ( VR acute test),

Aidha amesema maonyesho hayo ni muhimu Kwa Taifa Kwa kuwa yamekuwa yakikuza ujuzi wa wanafunzi chuoni hapo Kwa kuweza kuonyesha Kwa vitendo kile ambacho wamekuwa wakifundishwa darasani.

“ Katika bunifu hizi, Kuna vijana wametengeneza mfumo wa kupiga kura wakati wa uchaguzi ukiwa nyumbani, teknolojia hii ikiweza kuboresha itaweza kusaidia sana katika eneo hili,” amesema.

Amesema ni tegemeo la chuo kuwa bunifu hizo zitafikia jamii na kutatua kero mbalimbali inazizikabili na hivyo chuo kitaendelea kuimarisha na kuendeleza vipaji vya wanafunzi hao.



 

Tume ya Ushindani (FCC) imesema imeanza mpango wa kuanzisha klabu za elimu ya ushindani, ulinzi wa mlaji na udhibiti wa bidhaa bandia katika shule za msingi, sekondari na taasisi za elimu ya juu ili kujenga kizazi chenye uelewa wa masuala hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari Juni 20, 2026, katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea jijini Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa FCC, Bi. Roberta Feruzi, amesema mpango huo utatekelezwa kupitia klabu zitakazojulikana kama Ushindani School Club. 

Amesema lengo la mpango huo ni kuwafikia wanafunzi mapema na kuwajengea uelewa kuhusu ushindani, haki za mlaji na namna ya kufanya maamuzi sahihi wanaponunua bidhaa au kupata huduma.

Feruzi amesema elimu hiyo itawasaidia wananchi kutambua bidhaa bandia, kulinda soko dhidi ya udanganyifu na kuwawezesha watumiaji kuchagua bidhaa salama na zenye ubora.

Ameeleza kuwa uelewa wa masuala ya ushindani na ulinzi wa mlaji utasaidia wananchi kufanya uchaguzi bora wa bidhaa na huduma, huku sekta binafsi ikiendelea kuchangia katika uzalishaji na ukuaji wa uchumi.

Aidha, amesema utoaji wa elimu hiyo utaendelea kupitia ofisi za kanda za FCC zilizopo Mwanza, Arusha, Mbeya, Dodoma na Dar es Salaam kwa lengo la kuhakikisha wananchi katika mikoa yote ya Tanzania Bara wanapata elimu hiyo.




Katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 inayolenga kuhakikisha wananchi wanapata makazi bora na ya gharama nafuu, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umeendelea kutekeleza mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu ili kuwawezesha wananchi, hususan vijana, kumudu kumiliki makazi.

Akizungumza katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa TBA, Bi. Amina Lumuli, amesema kuwa TBA tayari imeanza kutekeleza miradi ya nyumba za gharama nafuu katika mkoa wa Dar es Salaam.

Bi. Lumuli ametaja Mradi wa Temeke Kota kuwa ni miongoni mwa miradi hiyo, akibainisha kuwa utekelezaji wa mpango huo utaendelea katika maeneo mbalimbali nchini.

"Tunawakaribisha wawekezaji kuja kushirikiana nasi ili kwa pamoja tuweze kufanikisha lengo la Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 la kuhakikisha wananchi wanapata makazi bora na ya gharama nafuu," amesema Bi. Lumuli.

Aidha, Bi. Lumuli amesema utekelezaji wa mradi huu unatokana na dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha wananchi wanapata makazi bora na yenye gharama nafuu.

Amesema TBA itaendelea kuhakikisha makundi yote, yakiwemo makundi maalum, yanafikiwa na kunufaika na programu hii ya nyumba za gharama nafuu.

Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) imeeleza kuwa uzalishaji wa pareto nchini bado haujakidhi mahitaji ya viwanda vya ndani, huku Tanzania ikizalisha wastani wa tani 4,000 za maua makavu kwa mwaka dhidi ya mahitaji ya tani 9,000, hali hiyo imeacha upungufu wa tani 5,000, sawa na zaidi ya nusu ya mahitaji yaliyopo.

Akizungumza Juni 20, 2026,  katika maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea jijini Dodoma, Afisa Kilimo Mwandamizi wa COPRA, Sikitu Mwakeja, alisema kuna fursa kubwa kwa wakulima, vijana na wawekezaji wa sekta binafsi kuingia katika kilimo cha pareto kutokana na soko la uhakika lililopo nchini.

Mwakeja alibainisha kuwa bei ya maua makavu ya pareto imeendelea kuwa ya kuvutia, ikifikia kati ya Sh4,000 na Sh5,000 kwa kilogramu kulingana na kiwango cha ubora, ameongeza kuwa kwa kufuata mbinu bora za kilimo, ekari moja inaweza kutoa hadi kilogramu 500 za maua makavu kwa msimu, hivyo kulifanya zao hilo kuwa miongoni mwa mazao yenye tija kwa wakulima.

Kwa sasa, uzalishaji mkubwa wa pareto unafanyika katika mikoa ya Mbeya, Songwe, Njombe, Iringa, Manyara, Arusha na Kilimanjaro, COPRA imewahimiza wadau mbalimbali kutumia fursa ya mahitaji makubwa yaliyopo sokoni ili kuongeza uzalishaji, kupunguza pengo lililopo na kuimarisha mchango wa zao hilo katika ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia mnyororo wake wa thamani.



Leo tumefungua rasmi ziara ya Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuanza katika Jimbo la Kibamba.

Akizungumza na viongozi wa Kata na Matawi, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Dar es Salaam, Khadija Ally, amewashukuru kwa moyo wa kujitolea, uzalendo, mshikamano na ushiriki wao wa hali na mali katika kufanikisha shughuli za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

“Uzalendo wenu, mshikamano wenu, kujitolea kwenu na imani yenu kwa Chama Cha Mapinduzi vimechangia kwa kiwango kikubwa mafanikio ya chama na ushindi uliopatikana.”

Ziara hii inalenga kuwashukuru viongozi na wanachama wetu, kuimarisha umoja na mshikamano, pamoja na kuhamasisha ari ya utendaji kazi katika kuendelea kuijenga Jumuiya ya Wazazi na Chama Cha Mapinduzi kwa maendeleo ya Taifa letu.
Katika ziara hii, Kamati ya Utekelezaji ya Mkoa wa Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake Khadija Ally itatembelea Kata zote 102 za Mkoa wa Dar es Salaam na kugawa tuzo za pongezi na shukrani kwa viongozi wa Kata kwa mchango wao mkubwa katika kuimarisha chama.

Tunawathamini, tunawapenda, na tunaamini kuwa nguvu ya Chama Cha Mapinduzi ipo kwa wanachama wake wenye uzalendo, uaminifu, mshikamano na imani thabiti kwa chama chao.

#JumuiyaYaWazaziDSM
#UmojaMshikamanoNaMaendeleo
#CCMKaziIendelee
#ZiaraYaShukrani2026



 









no image

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umesema umeendelea kutekeleza jukumu lake la kuwaunganisha wananchi na huduma muhimu za kijamii pamoja na fursa za kiuchumi kupitia ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya barabara na madaraja nchini.

Akizungumza katika maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma Jijini Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma wa TARURA, Catherine Sungura, alisema lengo kuu la wakala huo ni kuwafungulia wananchi njia za kufikia huduma mbalimbali za kijamii, masoko na kuchochea ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Alisema hadi sasa TARURA imefanikiwa kujenga zaidi ya madaraja ya mawe 490 katika maeneo mbalimbali nchini, hatua iliyochangia kuboresha mawasiliano na usafiri kwa wananchi.

Aidha, Sungura alisema wakala huo umefanikiwa kurejesha kwa zaidi ya asilimia 70 mawasiliano ya barabara katika maeneo yaliyoathiriwa na mvua za El Nino zilizochangia mafuriko na kusababisha uharibifu wa miundombinu.

Aliongeza kuwa mafanikio hayo yamewezekana baada ya Serikali kupata ufadhili kutoka Benki ya Dunia, ambao umewezesha utekelezaji wa miradi ya kurejesha miundombinu na mawasiliano ya barabara kutoka ngazi ya vijiji hadi taifa kwa ujumla.

Na Janeth Raphael MichuziTv.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Abdulmajid Nsekela, amesema benki hiyo imejipanga kikamilifu kuhakikisha Watanzania wananufaika na fursa za kiuchumi zitakazotokana na mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 yatakayofanyika Tanzania, Kenya na Uganda.

Akizungumza katika Bunge Grand Bonanza lililofanyika jijini Dodoma, Dkt. Nsekela amesema CRDB itaendelea kutoa mitaji na huduma mbalimbali za kifedha zitakazowawezesha wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji kutumia kikamilifu fursa zitakazotokana na mashindano hayo.

Amesema AFCON si tukio la michezo pekee bali ni jukwaa muhimu la kiuchumi litakalovutia wageni wengi kutoka ndani na nje ya Afrika, hivyo kuongeza mahitaji ya huduma mbalimbali zikiwemo malazi, usafiri, chakula na biashara nyingine ndogondogo na za kati.

"AFCON ina fursa nyingi za kiuchumi. Huu si wakati wa kusherehekea michezo pekee, bali ni fursa ya kukuza biashara, kuongeza ajira na kuinua uchumi wa wananchi. CRDB imejipanga kuhakikisha Watanzania wanapata mitaji na huduma zitakazowawezesha kunufaika na fursa hizo," alisema Dkt. Nsekela.

Aidha, aliipongeza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa ya kutunga sheria zinazochochea maendeleo ya Taifa na kuimarisha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini.

Pia alimpongeza Waziri wa Fedha kwa kuwasilisha bajeti ya Serikali ambayo alisema itaendelea kuboresha maisha ya Watanzania na kuchochea ukuaji wa uchumi, huku akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa maono yake ya maendeleo yanayoendelea kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi nchini.

Dkt. Nsekela amesema uwepo wa mabalozi wa nchi mbalimbali katika bonanza hilo ni ishara ya mahusiano mazuri ya kidiplomasia na kibiashara ambayo Tanzania imeendelea kujenga na kuyaimarisha kwa miaka mingi.

Amesema michezo ni chombo muhimu cha kuimarisha mshikamano, urafiki na ushirikiano miongoni mwa watu wa mataifa tofauti, huku akisisitiza kuwa ushiriki wa wadau mbalimbali katika bonanza hilo unaonesha namna michezo inavyoweza kuunganisha jamii.

Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa CRDB imekuwa mshirika wa maendeleo kwa zaidi ya miongo mitatu na imeendelea kuwa zaidi ya benki kwa kusaidia ukuaji wa biashara, uwekezaji na ajira nchini.

Amengeza kuwa benki hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na Bunge katika kuhakikisha Tanzania inanufaika kikamilifu na fursa za kiuchumi zinazotokana na matukio makubwa ya kimataifa.

Katika hatua nyingine, Dkt. Nsekela ametoa shukrani kwa uongozi wa Bunge kwa kuendelea kuiamini CRDB na kuipa nafasi ya kuwa mdau mkuu wa Bunge Bonanza, akiahidi kuwa benki hiyo itaendelea kuunga mkono jitihada za maendeleo ya Taifa kupitia sekta za michezo, biashara na uchumi.

Bunge Grand Bonanza lilihusisha ushiriki wa wabunge, watumishi wa Bunge, taasisi mbalimbali za umma na binafsi pamoja na mabalozi wa nchi rafiki, ambapo washiriki walishiriki michezo mbalimbali kwa lengo la kuimarisha afya, mshikamano na ushirikiano.







Na Janeth Raphael MichuziTv 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania na Namibia zimejipanga kuimarisha zaidi ushirikiano wa kiuchumi kwa lengo la kuongeza kiwango cha biashara na uwekezaji kati ya mataifa hayo mawili. 

Amesema hatua hiyo inalenga kufungua fursa mpya za maendeleo kwa sekta binafsi na wananchi kwa ujumla.

Akizungumza katika Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Namibia lililofanyika jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesema licha ya uhusiano wa muda mrefu wa kidiplomasia kati ya nchi hizo, bado kiwango cha biashara hakijafikia uwezo unaolingana na fursa zilizopo pande zote mbili.

Amesema viongozi wa Tanzania na Namibia wamekubaliana kuharakisha utekelezaji wa makubaliano mbalimbali ya ushirikiano, ikiwemo Hati ya Makubaliano (MoU) inayolenga kuimarisha biashara na kukuza sekta ya biashara ndogo, za kati na ndogo kabisa ili kuimarisha uchumi jumuishi.

Rais Samia amebainisha kuwa Tanzania inaendelea kuwa moja ya nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi barani Afrika, na ina nafasi ya kipekee kama lango la biashara kwa nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini. Amesema hali hiyo inatoa fursa kubwa kwa Namibia na wawekezaji wake kutumia Tanzania kama kituo muhimu cha usafirishaji na uwekezaji.

Katika kuimarisha mazingira ya biashara, Rais Samia amesema Serikali ya Tanzania imeendelea kufanya maboresho mbalimbali ikiwemo kurahisisha usajili wa kampuni, ambapo sasa mchakato huo unakamilika ndani ya saa 24, hatua inayolenga kuvutia wawekezaji zaidi wa ndani na nje ya nchi.

Aidha, amezitaja sekta za usafirishaji na huduma za bandari kuwa miongoni mwa maeneo yenye fursa kubwa za ushirikiano, akibainisha kuwa maboresho yanaendelea katika Bandari ya Dar es Salaam huku mipango ya kuendeleza Bandari ya Bagamoyo na bandari nyingine ikiendelea ili kuongeza ufanisi wa biashara za kikanda.

Katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi, Rais Samia amesema Tanzania ina ardhi kubwa na rasilimali nyingi, huku Namibia ikiwa na uzoefu mkubwa katika sekta ya mifugo na uvuvi, jambo linalofungua nafasi ya ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote mbili.

Pia amesisitiza umuhimu wa sekta ya mafuta na gesi kama eneo jingine la kimkakati lenye fursa kubwa za uwekezaji, akieleza kuwa mataifa hayo yote mawili yana rasilimali hizo na yanahitaji ushirikiano katika teknolojia, uwekezaji na uendelezaji wa sekta hiyo.

Hata hivyo Rais Samia amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuboresha mazingira rafiki ya uwekezaji kwa kuhakikisha kunakuwa na utulivu, uwazi na sera imara zitakazowezesha kuvutia mitaji ya muda mrefu kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania na Namibia.