Michu!
Kuna mtu katika blog yako anataka kujua maana ya maneno tajwa hapo juu, hii ndio maana yake.

MAANA YA VIMBWETTE, ACADEMIC BRIDGE NA M-DEGREE NI HIVI:

***Jina Vimbwette linatokana na Profesa Tolly S.A. Mbwette aliyekuwa programme Manager miaka ya nyuma, na ndiye aliyetoa wazo la kutengeneza viti vile vya saruji baada ya chuo kuwa na uhaba wa viti vya kukalia. Hivi sasa Profesa Mbwette ni mkuu wa chuo huria cha Tanzania (OUT).
***Academic Bridge ni hilo daraja la njano ambalo michuzi kalipiga picha, ni kiungo kati ya madarasa, utawala na mabweni ya wanafunzi. Inadadikika kuwa kama mtu hajapita katika daraja hilo akiwa anasoma hapo UDSM basi huyo hakusoma hapo, kwani kwa namna yoyote ile lazima upite hapo, ukiwa unaenda utawala,ofisi za DARUSO, mabwenini, posta ama katika baa na migahawa ambayo ipo karibu na posta ya pale chuo.
***M-degree ni ule mti mkubwa ulio karibu na ukumbi wa Nkrumah, kama unatoka katika jengo la utawala. Ni mti maarufu sana kwa wanafunzi, kwa sababu wengi wao hupata kivuli hapo wakati wa jua kali na hata wakati wa kujisome usiku. Prospectus zote hutolewa pale, pamoja na vitambulisho, kwa hito na wenyewe inasadikika kuwa kama mtu hajagusa katika m-degree basi hakusoma hapo (imani hizi ni tata kidogo, tunaweza kusahihishana. Kwa aliyesoma UDSM nadhani anatambua sana maana ya maneno hayo niliyoyataja hapo juu. Ndhani wewe uliyehitaji kujua maana ya maneno hayo utakuwa umepata mwanga kidogo!
Karibu tujadiliane
mheshimiwa_2000@yahoo.com

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 11 mpaka sasa

  1. nashukuru sana kwa ufafanuzi. Ila naomba kufahamu maana ya neno NGWINI hapo udsm.

    ReplyDelete
  2. Kaka Michuzi huyo Prof Mbwette jamaa ni kichwa alikua foe maji na akawa ndio meneja wa mradi wa kuongeza wanafunzi chuo kikuu jamaa alijitahidi sana kwa kweli nasikia yuko Chuo kikuu huria kama mkuu wa chuo nchi inataka wataalamu kama hao ili iendelee vijana wadogo lakini kazi zao tunazikubali

    ReplyDelete
  3. Serikali yashinikizwa kuwarejesha wanafunzi
    * CUF, TLP, LHRC wasema ilikurupuka
    * Serikali za wanafunzi zatishia mgomo nchi nzima

    Na Waandishi Wetu

    VYAMA vya siasa, taasisi za kijamii na Umoja wa Serikali za Wanafunzi wa Vyuo vikuu nchini wameitaka Serikali kuwarudisha mara moja na bila masharti yoyote wananfunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na vyuo vyake vishiriki waliofukuwa juzi.

    Vyama vitatu vya upinzani nchini vya Chama cha Wananchi (CUF), Tanzania Labour Party (TLP) na NCCR- Mageuzi vimeitaka serikali kusikiliza na kuyapatia ufumbuzi madhubuti matatizo yanayowakabili wanafunzi wa UDSN ndani ya siku 21 kuanzia jana.

    Ndani ya muda huo vyama hivyo pia vimeutaka uongozi wa chuo hicho kuwarejesha masomoni wanafunzi wote waliosimamishwa na wakati huo huo, serikali iwe inaufanyia marekebisho utaratibu unaotumika sasa wa wanafunzi wa elimu ya juu kuchangia masomo yao kwa asilimia 40.

    Kwa mujibu wa tamko lao la pamoja, vyama hivyo wameitahadharisha serikali kuwa vinakusudia kuchukua hatua za kisheria na za kisiasa dhidi yake, endapo itashindwa kuupatia ufumbuzi mgogoro wake na wanafunzi wa elimu ya juu nchini.

    "Sisi vyama vyote vitatu tunatoa siku 21 kwa serikali kumaliza mgogoro huo baada ya hapo tutachukua hatua za kisheria na kisiasa kuishinikiza." alisema James Mbatia, mwenyekiti wa NCCR Mageuzi.

    Alifafanua kuwa katika hatua za kisiasa, vyama hivyo vinakusudia kuuhamasisha umma hasa wafanyakazi katika taasisi za umma na binafsi kugoma kufanya kazi kwa muda usiojulikana hadi hapo serikali itakapoboresha utaratibu wa upatikanaji wa elimu ya juu nchini.

    Alisema kitendo cha serikali kuwataka wanafunzi wa elimu ya juu kuchangia gharama za masomo yao kwa asilimia 100 kinakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 11, Ibara ndogo za (2) na (3) inayozungumzia waziwazi haki ya raia wa Tanzania kupata elimu ya juu kwa gharama za walipakodi wa nchi yake.

    Katika tamko hilo, vyama hivyo vimeitaka serikali kusikiliza madai ya wanafuzi hao ya kutaka iwafadhili masomo yao kwa asilimia 100 na kuchukua hatua za haraka kuwarejesha masomoni wanafunzi wote waliosimamishwa bila masharti yoyote.

    Kwa mujibu wa tamko hilo, utaratibu wa serikali kuwataka wanafunzi hao kuchangia asilimia 40 ya masomo yao huku ikitenga kiasi kikubwa cha bajeti yake kugharamia mambo yasiyowasaidia wananchi wa kawaida, ni kuwasaliti wapigakura wake na taifa kwa ujumla.

    Tamko hilo limeongeza kuwa serikali inapaswa kuelekeza nguvu zake katika kufadhili elimu badala ya kuendelea kutwika mzigo wananchi kugharamia elimu ambayo ni haki yao kuipata bure.

    "Tatizo ni kwamba kuna baadhi ya wanasiasa wanaingiza siasa kweny elimu, utaratibu wa kujiunga na chuo kikuu kwa mfano unamtaka yeyote aliyepata kuanzia points 4.5, lakini serikali inasema tunafadhili waliopata madaraja ya kwanza na pili, sijui utaratibu huu wameutoa wapi,"alihoji Mbatia.

    Akizungumza katika mkutano huo, Mhadhiri wa Kitivo cha Sheria, UDSM Dk Edmund Mvungi aliuponda uamuzi wa chuo hicho kukifunga, kama njia ya kumaliza mgomo kuwa siyo sahihi.

    Alisema ufumbuzi wa matatizo ya vyuo vikuu hauwezi kutokana na uamuzi wa kukifunga chuo bali vikao vya pamoja baina ya wanafunzi kupitia serikali yao na uongozi wa chuo.

    Mvungi ambaye alidai kuwa anazungumza kama msomi na siyo kiongozi wa chuo hicho, alisema kuwa uongozi wa chuo kikuu cha Dar es Salaam unatakiwa kulinda haki za wanafunzi katika maamuzi yake badala ya kutoa maamuzi yenye mwelekeo wa kujipendekeza kwa serikali.

    Nao Umoja wa Serikali za Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya juu nchini (TAHLISO) umeitaka Serikali kuwarudisha wanafunzi wote waliofukuzwa ndani ya wiki moja lasivyo wataitisha mgomo wa kitaifa.

    Akitoa tamko hilo jana kwenye ofisi za Serikali ya Wanafunzi wa Chuo cha Biashara (CBE), Mwenyekiti wa TAHLISO, Bruno Mpinga alisema Serikali inapaswa kuwarudisha wanafunzi hao bila sharti lolote kwa kuwa walikuwa wanatetea haki yao ya msingi.

    Alisema hakukuwa na sababu ya wanafunzi hao kufukuzwa kwani Serikali yenyewe imekuwa ikishindwa kutekeleza madai ya msingi ya wanafunzi mpaka wanapogoma.

    Bruno alisema kwa hatua iliyofikia sasa wanataka kuonana na Rais Jakaya Kikwete uso kwa uso ili wamweleze namna wasivyoridhishwa na Serikali hasa inavyopouuza madai yao yenye maslahi kwa taifa.

    Mwenyekiti huyo alisema kwamba wanafunzi wamechoshwa na Waziri wa elimu ya juu, sayansi na teknolojia, Profesa Peter Msolla kwa madai kwamba si mtekelezaji wa matatizo yao bali ni mtu wa maneno bila vitendo.

    Bruno alitahadharisha kwamba endapo suala hilo halitashughulikiwa mapema TAHLISO itaitisha mgomo wa wanafunzi wa vyuo vyote (52 ) vya elimu ya juu nchini.

    Alisema haiingii akilini kuona kwamba Serikali inafanya jitihada kubwa kujenga shule za sekondari na msingi huku ikiwafungia mlango wanafunzi wanaohitimu wasiendelee na elimu ya chuo kikuu.

    Nacho Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimesema hatua ya Serikali ya kuwasimamisha wanafunzi wote wa shahada za awali katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam imekurupuka kwa kutumia ubabe, badala yake ingetumia busara kutatua madai yao.

    Akizungumza ofisini kwake jana, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo hicho, Harold Sungusia, alisema Serikali inatakiwa kutafiti chanzo cha mgomo pamoja na matizo mengine ya wanafunzi ili kumaliza kabisa matatizo hayo.

    Sungusia alisema kitendo cha Serikali kuamua kutumia ubabe na nguvu ni ishara kwamba imeshindwa kutumia njia za kidiplomasia kutatua matatizo yanayowahusu watu wake na alishauri iache kutumia njia kwa sababu zinalitia taifa hasara pamoja na kupoteza malengo ya wasomi.

    Alisema hatua hiyo, haiendani na mpango wa Shirikisho la Afrika Mashariki kwani mara kwa mara Serikali imekukuwa ikisisitiza watu wasome ili waweze kuingia katika ushindani ndani shirikisho hilo.

    "Ukiangalia idadi ya wanafunzi wanaomaliza elimu ya juu katika nchi za Uganda na Kenya iko juu sana ukilinganisha na Tanzania. Hapa kwetu wanafunzi wanaomaliza elimu ya juu ni ndogo sana licha kuwa Tanzania ina idadi kubwa ya watu kuliko nchi hizo," alisema Sungusia.

    Akizungumzia madai ya msingi ya wanafunzi hao, Kaimu Mkurugenzi huyo, alisema kuwa si kweli kwamba Serikali inashindwa kuwasomesha wanafunzi hao bali ni uzumbe wa kutokuwa na mikakati ya muda mrefu ya kuwekeza katika elimu.

    Alisema kama Serikali ingelikuwa inachukua hatua kali kwa watendaji ambao si makini isingelikuwa na upungufu wa fedha za kuwasomesha wanafunzi hao.

    SOURCE: www.mwananchi.co.tz

    ReplyDelete
  4. Mashangingi yaitafuna serikali Tanzania
    *Yatumia Sh33bilioni kwa mwaka

    Na Ramadhan Semtawa

    WAKATI matumizi ya Serikali yakiwa yamezidi bajeti kwa Sh 900 bilioni, imebainika gharama kubwa za kuendesha magari ya kifahari maarufu kama mashangingi ni moja ya chanzo kinachochangia hali hiyo.

    Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kwamba, mashangingi yanayotumiwa na viongozi wa serikali yapo 800 yanatumia zaidi ya Sh33 bilioni kwa mwaka ikiwa ni matumizi ya mafuta na gharama za kuyafanyia mategenezo.

    Kwa mujibu wa takwimu zilizopatikana, magari hayo yanatumia wastani wa lita 300 kila moja kwa wiki, hivyo hutumia lita za mafuta 240,000 kwa kipindi hicho kwa magari yote hayo.

    Kwa wastani bei ya sasa ya mafuta ya diseli ni sh 1200 kwa lita hivyo magari hayo yanatumia Sh1.152 bilioni kwa mwezi. Uchunguzi umegundua kuwa gharama za kulifanyia mategenezo kwa mwezi ni Sh2 milioni kila gari hivyo gharama za kuhudumia magari hayo kwa mwezi ni Sh1.6 bilioni.

    Ukijumlisha gharama za mafuta na mategenezo kwa mwezi ni Sh 2.752 bilioni na kwa mwaka ni kiasi cha Sh33 bilioni. Kiasi hicho cha matumizi kingepungua iwapo baadhi ya viongozi ukiachia rais, waziri mkuu na makamu wa rais wangetumia magari ya kawaida.

    Kati ya magari hayo, 540 ni ya viongozi wa Serikali Kuu wakiwamo ofisi ya rais, ofisi ya waziri mkuu, makamu wa rais, mawaziri, manaibu mawaziri, makatibu wakuu.

    Orodha hiyo ya serikali kuu imezingatia, makatibu wakuu 27, manaibu wao 27, maafisa utumishi (Ma Dap) 27, na wakurugenzi wanne kila wizara na sehemu nyingine wakurugenzi wasaidizi, huku Ikulu, ofisi ya makamu wa rais na ya waziri mkuu, kwa pamoja zikiwa na magri hayo yasiyopungua 40.

    Mengine hutumiwa na watendaji wakuu wa mashirika na taasisi za serikali, wakati kwa upande wa Tamisemi ni kuanzia wakuu wa mikoa 22, makatibu tawala wa mikoa 22, makatibu tawala wa wilaya, wakurugenzi watendaji wa wilaya na wakuu wa wilaya 104.

    Wakati gharama hizo zikionekana kuwa mzigo kwa walipa kodi, Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, ameliambia Mwananchi: "Tena naomba uninukuu vizuri, mawaziri wataendelea kutumia magari yanayoendana na hadhi yao, waziri hawezi kutembelea Vokswagen (Bito)".

    Uchunguzi umebaini kuwa gharama hizo zimekuwa zikiongezeka maradufu katika siku za hivi karibuni kutokana mawaziri, manaibu mawaziri, wakuu wa mikoa, wilaya, makatibu tawala wa mikoa na wilaya kutotulia ofisini kutokana na ziara wanazofanya katika maeneo mbalimali.

    Pia imebainika kwamba, gharama za kuendesha magari hayo zimekuwa ni mzigo kwa walipa kodi kutokana na baadhi ya mawaziri kutofanya kazi vizuri huku baadhi ya magari yakionekana kuranda randa kwenye mabaa nyakati za usiku na mwisho wa wiki.

    Akizungumzia zaidi kuhusu magari hayo, Chenge alisema serikali haijafikia uamuzi wowote wa kupiga marufuku magari hayo ya kifahari ambayo yeye anayaita kuwa ni ya kawaida.

    "Kwanza si magari ya kifahari, wewe ndiye unayeyaita hivyo, ni kwa sababu ya umasikini wetu tu, lakini lazima waziri atembelee gari lenye hadhi yake," alisisitiza Chenge.

    Hata hivyo, aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo kabla ya Chenge, Basil Mramba aliwahi kukaririwa na gazeti hili kuwa mashangingi ni mzigo mkubwa kwa serikali na kwamba inafanya mipango ya kusitisha ununuzi wa magari hayo.

    Alipoulizwa haoni huo umasikini wa nchi yetu ndiyo ambao ulitupasa kuacha kununua magari hayo, alijibu, " kwanza, matumizi ya serikali hayawezi kuzidi kwa ajili ya magari haya", na kuhoji:

    "Hivi siku za nyuma katika serikali zilizopita mafuta yalikuwa yakitolewa lita 50 kwa wiki, nchi yetu ilipiga hatua gani kubwa katika nyanja za maendeleo?"

    Chenge alipoelezwa mfano, wa serikali ya Mwalimu Nyerere kwamba iliweza kujenga viwanda na mashirika makubwa ambavyo watawala wa sasa wanayauza ovyo, alijibu tena, " wewe sikia, haya mafuta ya magari hayawezi kukuza uchumi, cha msingi watu fanyeni kazi kwa bidii, tushirikiane kutekeleza ilani ya chama na mipango ya maendeleo ya serikali."

    Hata hivyo, Chenge alisema serikali itachukua hatua kwa wale watakaobainika kutumia magari hayo katika mabaa na nyakati zisizo za kazi.

    Wakati huo huo; Shirika la Fedha Duniani (IMF) limeishauri Serikali ya Tanzania kubana matumizi yake kwa kuyaelekeza fedha kwenye vipaumbele muhimu vya nchi kama afya, miundombinu, elimu na maji.

    Ushauri huo ulitolewa jana na Mwakilishi Mkazi Mwandamizi wa IMF nchini, Dk David Robinson, alipokuwa akijitambulisha kwa wanahabari jijini Dar es Salaam, katika ofisi ya shirika hilo.

    "Siwezi kulitolea maoni kwa undani kwani nahitaji muda wa kujifunza zaidi, lakini ni muhimu Serikali ikadhibiti matumizi yake ya fedha na kuzielekeza katika sekta muhimu kama afya, miundombinu, elimu na maji," alishauri Mwakilishi huyo wa IMF.

    Dk Robinson alisema hayo wakati akijibu hoja ya wanahabari juu ya ripoti ya IMF kuhusu hali ya uchumi wa Tanzania, ambayo imeifagilia Serikali kuwa iko makini katika udhibiti wa fedha, wakati ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imeonyesha kuwepo kwa mushkeli katika matumizi.

    Ripoti hiyo ya CAG ya hivi karibuni inaonesha kwamba Serikali imekuwa na matumizi makubwa kwa kutumia ziada ya sh900 bilioni miezi minne kabla ya kuisha kwa mwaka wa fedha.

    Taarifa ya CAG kwa mwaka 2005/06, inaonesha kuongezeka kwa matumizi ya kawaida kutoka Sh2,138,860,343,786 mwaka 2004/05 hadi Sh2,732,455,841,323 mwaka 2005/06.

    Taarifa hiyo inasema, fedha za matumizi ya miradi ya maendeleo zimepungua kutoka Sh850,533,139,955 mwaka 2004/05 hadi Sh844,103,204,420, huku deni la taifa la nje likikua hadi kutokaSh5,548,446,077 hadi Sh5,772,620,992 katika kipindi hicho na kumfanya Rais Jakaya Kikwete kuitisha mkutano na watendaji waandamizi wa serikali kuijadili katika kikao hicho kilichofanyika Dodoma, ambapo aliwatahadharisha watendaji watakaorudia makosa hayo watatimuliwa kazini.

    Takwimu zilizotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Machi mwaka huu, zinaonesha tayari katika matumizi hayo kuna ongezeko la asilimia 5.6 ya pato la taifa, badala ya asilimia 5.1 ya pato la taifa kama ilivyokuwa imekadiriwa kwenye bajeti ya mwaka 2006/07.

    Kutokana na kuongezeka kwa matumizi hayo, taarifa ya hiyo ya BoT inaonyesha mpaka Februari mwaka huu, tayari kumekuwa na pengo la Sh978.8 bilioni.

    Akizungumza zaidi, Dk. Robinson alieleza kwamba kwa sasa jumuiya ya nchi wahisani imekuwa ikielekeza zaidi misaada yake ya fedha kwenye bajeti kuu za Serikali ili ziwe na uhuru wa kupanga vipaumbele vyake badala ya kuamuliwa.

    Kwa mujibu wa ripoti ya shirika hilo ya Februari mwaka huu Bodi tendaji ya IMF imeridhia kuipa Tanzanai fedha zaidi baada ya kuridhishwa na inavyotekeleza Mkakati wake wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umasikini (MKUKUTA) katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita .

    Kwa hali hiyo Tanzania imefunzu kupewa dola za kimarekani 4.2 milioni kwa ajili ya kuendeleza jitihada hizo. Kiasi hivyo kinafanya jumla ya fedha ambazo Serikali ya Tanzania itazipata kwa ajili ya mpango huo kufikia dola za kimarekani 29.4 milioni.

    Lengo la wahisani hao ni kuona kwamba uchumi wa Tanzania unakuwa hasa katika kujenga uwezo wa matumizi bora ya fedha, kuimarisha mchango wa sekta ya fedha katika maendeleo, kuwa na sera za fedha zinazotekelezeka na mazingira bora ya biashara.

    Ripoti hiyo imeonesha kwamba katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Uchumi wa Tanzania umekuwa ukikuwa vizuri na kufanikiwa kushusha mfumko wa bei pamoja na kujiwekea hakiba kubwa ya fedha.

    source: www.mwananchi.co.tz

    ReplyDelete
  5. Ufumbuzi wa migomo uko ndani ya uwezo wa serikali

    BARAZA la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam juzi alasiri lilikifunga Chuo Kikuu sehemu ya Mlimani pamoja na vyuo vingine vinne vishiriki - UCLAS, DUCE, MUCE na IJMC- baada ya kuwasimamisha wanafunzi wote wa shahada za awali.

    Hatua hiyo, ambayo inaungwa mkono na Serikali ilichukuliwa na Baraza hilo baada ya wanafunzi wa vyuo hivyo kuendelea na mgomo wao kwa siku mbili mfululizo wakipinga sera ya kuchangia asilimia 40 katika elimu ya juu.

    Mgomo huo ambao ulianza Jumatatu uliandaliwa mapema kwa lengo la kuishinikiza Serikali irejeshe utaratibu wa kulipa posho ya Sh 6,000 kwa kutwa kwa ajili ya mafunzo ya vitendo badala ya Sh 3,600 kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza.

    Kiasi hicho cha Sh 3,600 kinachotolewa na Serikali ni asilimia 60 ya posho, hivyo kiasi kingine cha Sh 2,400 sawa na asilimia 40 kinatakiwa kitolewe na mwanachuo. Ingawa asilimia 40 inaonekana kuwa ndogo kwa kutwa, malipo yanapofanyika kwa miezi miwili ya mafunzo yao ni kiasi kikubwa na mzigo kwa wanafunzi au familia zisizo na uwezo.

    Kiasi hicho ndicho mwanachuo anatakiwa kutumia kwa chakula, kulipia pango na usafiri katika muda wote wa mafunzo.

    Ikiwa Sh 3000 haziwatoshi wanapokuwa chuoni, Sh 3,600 zitawezaje kutosha wakati wanatakiwa kujigharimia kila kitu?

    Ni kutokana na msingi huo kwamba tunaunga mkono madai ya wanafunzi kwa sababu asilimia 40 ni mzigo mkubwa kwa familia masikini. Wanafunzi waliopo vyuoni wapo hapo kwa sababu ya uwezo wao wa akili darasani si uwezo kifedha, wapo masikini na elimu wanayopata ndiyo inatarajiwa kutumiwa kwa ajili ya kujiletea maisha bora.

    Msingi wa hoja za wanafunzi ni kutokana na Serikali yenyewe kujikanganya katika kupima uwezo halisi wa wazazi kuchangia gharama za masomo. Awali ada ya masomo katika shule za sekondari ilikuwa Sh 60,000, lakini ilishushwa hadi Sh 20,000 baada ya kuona kuwa ni kikwazo kwa baadhi ya wazazi.

    Lakini mwanafunzi huyo anapofaulu na kujiunga na elimu ya juu, Serikali hiyo hiyo inabadilika na kumpangia mzazi aliyeshindwa kulipa Sh 60,000 sekondari alipe kiwango kikubwa zaidi ikiwa ni asilimia 40.

    Serikali inatakiwa kukaa chini na kutafakari kwa makini badala ya kutumia nguvu kama ilivyofanya kwa kufunga vyuo na kuwaondoa kama wahalifu.

    Walipoandamana kwa amani hadi viwanja vya Jangwani mapema mwaka huu wakiomba Serikali ifute asilimia 40 anayotakiwa kuchangia mzazi, Rais Jakaya Kikwete aliahidi wakati wa mkutano wa chama tawala (CCM) kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee kulifanyia kazi suala hilo na akawataka wavute subira.

    Hadi wanaandaa mgomo na maandamano wiki hii Rais bado alikuwa hajatoa ufumbuzi wowote wala kutoa rai. Ukimya huo ni ishara kwamba ama ile ilikuwa ahadi hewa au ombi la wanafunzi hao limepuuzwa.

    Kwa kuwa hatua ya kuwasimamisha wanafunzi hawa ni ufumbuzi wa muda, watarudi na kuendelea na masomo yao, na kwa kuwa wanafunzi wameapa kuendelea na mgomo huo watakaporejea ni vyema ikatafuta suluhisho la kudumu sasa ambao limo ndani ya serikali yenyewe.

    Tunaishauri Serikali itoe mikopo kwa asilimia 100 na iimarishe utaratibu wa kukusanya fedha kutoka kwa watu wote waliokopa. Bodi ya Mikopo iandae mtandao utakaofika katika kila sekta kuwabana wakopaji.

    source: www.mwananchi.co.tz

    ReplyDelete
  6. Mtu hajawahi kuniboa hivi. Sasa nanai ana haja ya kuyajua hayo yote?? Ndo yale yale ya kumaliza digirii bila ufahamu wowote mnacho jua ni mdigirii, academic bridge na pumbaffff. Be sensible we mtoa maoni. Hizo hadithi za Abunuasi hatuna haja nazo.

    ReplyDelete
  7. Point of correction:

    sio wote ambao wamepokea prospectus chini ya mdegree. Ni vijana wa siku za hivi karibuni ndio wamepokea hapo. Wazee wa zamani kutokana na uchache wetu tulipokea kati ya Nkurumah Hall au ofisi za admission. Wakati mwingine zilikuwa zinatolewa ofisi za faculty mbali mbali.

    ReplyDelete
  8. Nakubaliana na wewe kwa 100% kwani uliyoyatoa hapa ni exactly niliyochangia mimi katika maoni ya picha na pale jamaa alipouliza. Mimi huyu prof T, Mwete kanifundisha pale FOE mwaka 2000, ni mtaalamu wa maji taka. Lakini aliweza ku manage vizuri kitengo chake na ndio maana leo hii kuna mabibo hostel na kijitonyama hostel, na new lecture theatres 1&2, zote moja ya maandalizi ya ofisi yake ya kulindika wanafunzi chuo kikuu

    ReplyDelete
  9. kabwa ya kupachikwa jina vimbwete tulikuwa tunaviita 'vislabu', then baadae vikawa vimbwete kufuatia jina la jamaa na jinsi alivyokuwa anatetea hoja yake ya kuongeza idadi ya wanafunzi bila kuongeza teaching facilities

    ReplyDelete
  10. cv ya mbwette inapatikana hapa http://www.udsm.ac.tz/faculty/foe/wetlands/MbwetteCV.pdf

    ReplyDelete
  11. MI nadhani mambo ya M-degree na vimbwete msichanganye watu!
    Si kweli kwamba ambaye hakupitia hapo basi hajasoma UDSM. Huyu Mbwete kaja juzi tu, je wale wa zamani waliosoma UDSM kabla ya Mbwete unawaweka kwenye kundi gani.

    Lakini pia, kwa uzoefu wangu, wanafunzi weng wa hapa UDSM ambao wanasomea kwenye M-Degree au Vimbwete ni wale wa kuunga-unga. Ninaposema hivi nina maana wale ambao huwa mara nyingi hawatumii akili zao bali wanategemea discussion na kufundishwa na wenzao. Watu wote serious hawajawahi kukanyaga wala kusomea kwenye hivyo vimbwete au m-degree kama mtoa hoja anavyotaka tuamini.

    Hapo utawakuta wale wanaotegemewa kuwa wana-sheria, waalimu na several NGWINI degrees. Kwani kundi hili la wanafunzi pale UDSM ni lile ambalo halihitaji nguvu wala akili kuweza kuelewa shule zao. Porojo zinatosha kufaulu mtihani. Ndo maana m-degree na vimbwete kwao ni a MUST.

    Ni lazima mtoa hoja aelewe kuwa wote tumesoma UDSM lakini hatuko daraja moja! Duniani nzima pia iko hivi hivi. Ndiyo maana Eistein au MARIE CURIE huwezi kuwafananisha na Che Guevera!. Haitatokea.

    Natoa Hoja.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...