mwandishi mwandamizi wa deliniuzi alfred ngotezi akisoma gazeti la spia. anasema hii ni nyenzo iliyosaidia sana kumpa mtu tizi la kiinglishi enzi hizo tofauti na sasa ambapo majarida kama haya ni adimu. ngotezi alikuwa mgombea ubunge jimbo la buchosa, sengerema, mwanza na leo kachafua magazeti kwa habari hii


Mbunge Chitalilo aburuzwa mahakamani

Na Mwandishi wetu,

Hatimaye mbunge machachari wa Buchosa mkoani Mwanza Samuel Mchele Chitalilo amefikishwa mahakamani na wananchi wa jimbo hilo kwa tuhuma za kugushi vyeti na kudanganya kuhusu elimu yake katika chaguzi za 2000 na 2005.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na mlalamikaji wa kwanza katika suala hilo, Henriko Msheleja, kesi hiyo imefunguliwa katika Mahakama Kuu mjini Mwanza na kupewa namba za usajili 25 ya 2007.

Mlalamikaji wa pili katika suala hilo ni Alfred Ngotezi ambaye ndiye aliyefungua jalada na. SEN/IR/104/2006 la uchunguzi kuhusu elimu ya Chitalilo,mapema mwaka jana mjini Sengerema mkoani Mwanza.

Msheleja aliliambia gazeti hili jana kwa njia ya simu kutoka Mwanza kuwa wamepeleka maombi rasmi Mahakama Kuu ili waruhusiwe kumshitaki Chitalilo kwa utaratibu wa uendeshaji mashtaka binafsi (Private Prosecution) chini ya kifungu cha 99 cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Mwezi uliopita Msheleja alikuja jijini Dar es Salaam akiwa na mpiga kura mwenzie Ramadhani Amani wakiwa na majina na sahihi za wapiga kura wengine 184 wa jimbo la Buchosa wakiomba msaada wa kisheria ili kumshitaki Chitalilo kwa kughushi vyeti na kudanganya kuhusu elimu yake.

Hatua hiyo ilifuatia Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai DCI Robert Manumba kuthibitisha mapema mwezi Februari kuwa ni kweli mbunge huyo alikuwa ameghusi vyeti katika chaguzi za 2000 na 2005 lakini akasema hawawezi kumshitaki kwa madai kuwa hakuvunja sheria ya uchaguzi.

Msheleja alibainisha kuwa wao wanamshtaki mbunge huyo kwa kuvunja sheria dhidi ya kughushi ingawa hakutaka kutaja vifungu watakavyotumia kumshitaki akisema bado ni mapema mno. Hata hiyo baadhi ya wanasheria walioulizwa kuhusu suala hilo waliliambia gazeti hili majuzi kuwa Chitalilo anaweza kushtakiwa kwa kifungu 333 au 335 cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Msheleja alieleza kuwa wamefanikiwa kufanya hivyo baada ya kupata msaada wa kisheria kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kilichoko mjini Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Kituo hicho Hellen Kijo-Bisimba alilithibitishia gazeti hili jana kuwa wanawasaidia wananchi hao wa Buchosa kutafuta haki mahakamani kwa kumfungulia mashtaka mbunge huyo.

Kwa kawaida, masuala yote ya jinai hushughulikiwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), isipokuwa pale inapobidi kufanya kinyume ambapo ruhusa maalumu inaweza kutolewa na Mahakama Kuu kwa kutumia kifungu cha 99 cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Hati ya kiapo iliyowakilishwa mahakamani jana Jijini Mwanza ambayo gazetil hili limepata nakala yake imeorodhesha hoja 13 na viambatanisho sita katika maombi hayo ya kutaka Chitalilo ashtakiwe kwa utaratibu wa binafsi.

Hati hiyo inadai kuwa Chitalilo alighushi vyeti na kujipatia sifa zisizokuwa zake na kuwa alifanya makosa hayo katika chaguzi za 2000 na 2005. Inaongeza kuwa aliwadanganya wapiga kura kwa kutoa vipeperushi akionyesha kuwa alimaliza kidato cha nne kwenye Shule ya sekondari ya Bupandagila mkoani Shinyanga kati ya 1985 hadi 1990, na kuwa alisoma Sekondari ya Katikamu nchini Uganda kati ya 1990 na 1991.

Walalamikaji wanadai pia katika hati hiyo kuwa Baraza la Mitihani la Uganda na Shule ya Katikamu wametoa nyaraka kukanusha kuwa Chitalilo aliwahi kusoma huko. Wanadai pia kuwa wamewasilisha malalamiko yao katika ngazi mbali za utawala lakini bila mafanikio yoyote.

Hati pia inadai kuwa walalamikaji walimwandikia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Spika wa Bunge la Jamhuri kuhusu tatizo hilo lakini wanadai hakuna kilichofanyika. Wameongeza kuwa wanatafuta haki katika suala hilo ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye mwenendo kama huo.

Wamesema kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) alithibitsha bayana Machi 4 mwaka huu kuwa baada ya uchunguzi wao, Polisi walibaini kuwa Mbunge huyo alikuwa ametenda kosa la Jinai kwa kughushi vyeti.

Wameongeza kuwa pindi Polisi walipoanza kuchunguza elimu yake alibadilisha wasifu aliokuwa ameweka kwenye Tovuti ya Bunge, mabadiriko ambayo hata hivyo wanadai yanaonyesha kuwa hakumaliza kidato cha pili kwenye sekondari ya Bupandagila mwaka 1991, sembuse kuingia kidato cha tano mwaka huo huo wa 1991. Katika mabadiriko hayo Chitalilo anakiri wazi katika tovuti hiyo kuwa hakumaliza shule popote pale isipokwa shule ya msingi ya Nguduluguru.

Ngotezi alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema wamefikia uamuzi huo baada ya kuvuta subira ya muda mrefu bila hatua zozote kuchukuliwa dhidi ya mbunge huyo. Alisema kuwa sasa muda wa kulifanya suala la Chitalilo la kisiasa umekwisha; “ tuache sheria ichukue mkondo wake,” alisema.










Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 9 mpaka sasa

  1. Michuzi safi hiyo! najua ni wachache sana ambao wanamjua huyo `spia`.Majarida ya wakati huo hata leo ukiliona unalitamani kulisoma.Nimekuelewa mtu wangu

    ReplyDelete
  2. Eehh bana eeh unajua haya magazeti bado bomba; hivi wapi mtu anaweza kupata ya kununua kwa kumbukumbu? na lile jingine BOOM (Mtu wa porini alikuwa akitamba na Tembo) ... AkD

    ReplyDelete
  3. Mbona watakua wengi waliofodge hivyo vyeti huko bungeni. Ndio maana hata speaker wa bunge aliminyia huyu mtu....Who knows....

    Michuzi mbona page counter yako inarudi chini badaya ya kwenda juu? Ni baby Y2K nini? manake miminilikua nasubiria tuingie million mbili tufanye party mara naona tunamba tuko hivi...Ouch

    ReplyDelete
  4. Ngotezi aligombea ubunge kwa chama gani?

    Nawasilisha.

    ReplyDelete
  5. annoy wa 10:17 umeuliza swali zuri. hivi ni wapi mtu unaweza kuyapata haya na kuyanunua ili kuwaonyesha watoto wetu tulichokuwa tukisoma zamani? kwa hakika ningependa kumsoma tena The Spear, Captain Victor, Sonia, Rabon Zollo, Devil, bwana mdogo Lemmy na wengineo....

    ReplyDelete
  6. Ahsante sana Bw. Michuzi kwa kunikumbusha mbali. Enzi hizo nilikuwa sikosi gazeti hili. Namkumbuka Lance Spearman akiwa na mpambe wake Sonia wakimbana vikali na Rabon Zorro na wafuasi wake. Haya ni vigumu kuyapata nadhani hata series zenyewe zilikwisha. Vipi Michuzi inawezekana kwenye Archives za Daily News?

    ReplyDelete
  7. Nimejibiwa na Ngotezi mwenyewe jioni hii kuwa, yeye alikuwa tayari kugombea pia kwa tiketi ya CCM pamoja na Bw. Chitalilo.

    Haya na tuone huko mbele itakuwaje maana mahakama ndiyo mwamuzi wa mwisho.

    Nawasilisha.

    ReplyDelete
  8. Jamaa wa www.youngafrican.com wamelijadili sana hii issue za degree fake mpaka kutaja nani mwenye nazo na shule husika - waziri mdogo mmoja chuo chake fake kilichompa degree fake kiliwahi kuto degree kwa mbwa anayeitwa "Wally"!?

    Tatizo ni kwamba serikali imekaa kimya kuhusu hizi masters na Phds fake kwani nchini Marekani zinasema wazi kuwa hauwezi kutumia degree kama hizi ili upate promotion, au kugombea ofisi au kujiendeleza kikazi yaani career advancement. Sasa iweje mawaziri wadogo wengi watumie kupata ubunge na uwaziri udogo? Labda serikali yetu inakubali hizi degree fake kama degree zingine. Iseme basi na kuweka bayana swala hili.

    Vilevile, pale SUA ma lecturer woooooote mpaka mkuu wa chuo wanazo hizi fake Phd zilizotolewa na chuo kilekile kilichompa Agustino Mrema degree - Pacific Western University.

    Haya, tutaendelea kuangalia kama kweli tusome tu au tununue degree na kuukwea ubunge na labda uwaziri.

    ReplyDelete
  9. Hapo ilikuwa sehemu mojawapo ya Story ya "Power maddy tycoon" kati ya sehemu tano. Jambazi moja la kimataifa linaloitwa Keaton lilitaka kutawala dunia. Mbali ya kuwa na mabomu matano ya nyukilia alikuwa na nyambizi yake mwenyewe. Serikali ilimtumia Spear kumtafuta huto jambazi ambaye alijificha katika kisiwa kisichojulikana. Spear aliweza kkukigundua hicho kisiwa lakini na yeye alikamatwa na watu akafikishwa kwa Keaton. Keaton akamwambia Spear plan yake ya kuanzisha vita vya dunia. Alimfungia Spear kwenye kastodi pamoja na mwanamke mmoja aliyekuwa Profesa hapo hapo. Akabonyeza batani ukutani akamwambia Spear baada ya dakika 45 kisiwa chote na yeye Spear watateketea na wkati huo atakuwa ameshafika kwenye nyambizi yake kwa ajili ya vita. Spear alimwamsha profesa na kumwambia plan za Keaton kuteketeza kisiwa. Profesa akasema yeye anajua namna ya kufanya azma hiyo isifanikiwe. Ndipo Spear akafungua chumba na kumfuatilia Keaton. Alipomfikia Keaton, Keaton alikuwa akikimbia bila kuangalia anakokwenda. Hatimaye akaiangukia fensi iliykuwa ina moto wa umeme na kufa papo hapo. Spear akashinda.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...