Mkurugenzi Mkuu wa NMB Ben Christiaansen akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya NMB juu ya mgomo wa wafanyakazi. Kulia ni Afisa Utumishi Mkuu wa benki hiyo Kabeho Solo. stori kamili ya hali ilivyo sasa hapo chini...
MAHAKAMA Kuu imesema mgomo wa wafanyakazi wa Benki ya Makabwela (NMB) ni haramu na batili na kuwataka wafanyakazi warejee kazini ifikapo saa mbili asubuhi hii, hatua iliyokubaliwa na wafanyakazi baada ya ushawishi wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwandani, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO).
Jaji Mfawidhi wa Divisheni ya Mahakama ya Kazi ya Mahakama Kuu, Ernest Mwaipopo akitoa uamuzi wake leo mchana alisema baada ya kusikiliza maelezo ya Menejimenti ya NMB na ya wafanyakazi, amebaini kuwa mgomo huo ulikuwa haramu, kwani ulikiuka baadhi ya vifungu vya sheria ya kazi na uhusiano kazini.
Wafanyakazi wa NMB walianza kugoma jana baada ya kutoa notisi ya saa 48 kwa menejimenti Ijumaa saa saa 10.55 jioni.
Waligoma ili kuishinikiza serikali kusaini makubaliano ya mwajiri wao wa zamani kuwalipa mafao na kuwauzia asilimia tano ya hisa za benki hiyo.
Jaji Mwaipopo alitoa uamuzi wake baada ya kusikiliza utetezi wa wakili wa wafanyakazi, Amour Khamis na hoja za Wakili wa menejimenti ya NMB, Rosan Mbwambo.
Katika uchambuzi wake wa kisheria, Jaji Mwaipopo alitaja mambo yanayosababisha mgomo huo uwe batili, la kwanza katika notisi ya kugoma ambayo wafanyakazi waliitoa Ijumaa ambayo inaeleza kuwa watagoma hadi pale serikali itakapokubali kutia saini.
“Hapa najiuliza mgomvi wa mfanyakazi ni mwajiri au ni serikali, kama ni serikali iweje wamgomee mwajiri? Au kama mwajiri na serikali wote wana ugomvi na mfanyakazi kwa hali hiyo ni vyema notisi hiyo ikarekebishwa na waonyeshe kwamba wafanyakazi wana ugomvi na mwajiri,” alisema.
Jaji Mwaipopo pia alisema sababu nyingine inayobatilisha mgomo huo ni muda wa notisi uliotolewa na wafanyakazi.
Alisema saa 48 zilizotolewa kwa sheria za nchi, siku ya Jumapili ambayo ni ya mapumziko hazihesabiki hivyo ni wazi kuwa saa 48 ingemalizika Jumatatu saa 10.30 na sio Jumapili saa 10.30.
“Saa 48 katika sheria za kazi haikusema inahesabika kuanzia lini, lakini sheria za nchi zinatambua kuwepo kwa siku za kazi na siku za mapumziko, hivyo ni jukumu la mahakama kutoa tafsiri sahihi katika kipengele hiki,” alisema Jaji Mwaipopo.
Lakini akichambua zaidi juu ya saa za kazi, alisema iwapo notisi hiyo ingekuwa inatoa fursa ya menejimenti kujitetea kwa saa za kazi, basi notisi hiyo ingemalizika Jumanne na mgomo ungeanza kesho (Jumatano, leo).
Kipengele kingine alichotaja ambacho alisema kinaonyesha mgomo huo ni haramu ni kile kinachoeleza ukomo wa mgomo ambacho katika notisi, kipengele hicho kinasisitiza kuwa wafanyakazi hawatarudi kazini hadi pale serikali itakapotia saini rasimu ya makubaliano ya kulipa mafao yao.
“Kutokana na sababu hizi mahakama imeridhika kwamba mgomo huu ni batili na inautengua, hivyo hautakiwi kutekelezwa au kufuatwa na mwajiriwa wa NMB.
“Naamuru wafanyakazi wa NMB wawe wamerudi kazini ndani ya saa tatu kuanzia sasa….menejimenti ya NMB iwapokee bila ubaguzi wala masharti na waendelee na kazi zao za kila siku kama kawaida,” alisema.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 9 mpaka sasa

  1. Sasa mahakama unaamuru kurudi kazini wewe kama nani, mahakama ilibidi ipendekeze wafanyakazi kurudi kazini si kuamuru, kwa vile wafanyakazi hawapo chini ya ya mahakama ilichotakiwa ni kupendekeza, kuna uatata hapa wa hukumu hii, ukisoma saNA HUKUMU YENYEWE UTAONA INA KASORO KIBAO. vyama vya wafanyakazi vya nchi za kiafrika vinashinda sana katika kusaidia wafanya kazi kutokana na mfumu mzima wa vyama hivyo na serikali za nchi za kiafrika. vyama vya wafanyakazi vinatakiwa kuwa huru wala visibanwa na sheria yoyote ili.

    ReplyDelete
  2. Jamani huu ni onevu na unyanyasaji wa wafanyakazi TZ, kwani pamoja na mahakama kuamuru wafanyakazi kurudi kazini mara moja, sikusikia Jaji akizungumzia suala la msingi lililowafanya wafanyakazi wagome na utatuzi wake ni nini!!!!!!!!!! jamani serikali hii mbona hivi, mgomo wa walimu nao wanukia tena, migomo migomo mpaka lini haki za wanyonge zinapotea pasi na utetezi, inasikitisha sana namna hii.

    ReplyDelete
  3. nmb imebinafsishwa wakati ilikuwa na superprofit. jamani tumeuzwa kiaina sijui tutakimbilia wapi

    ReplyDelete
  4. Huyo aliyesema vyama vya wafanyakazi viwe huru na visibanwe na sheria yeyote anachekesha sana, umeona wapi kitu kisiwe na ukomo wa sheria? Mahakama imeamuru coz jamaa wamemgomea muajiri wao nmb wakati wanailalamikia serikali (kumbukeni hapa anayelalamikiwa ni serikali na siyo nmb), vilevile notisi imemuadres nmb na siyo mlalamikiwa serikali, notisi inatakiwa itolewa ndani ya masaa ya kazi tofauti na wao wametoa notisi weekend na notisi haikuwa na muda wa mgomo jambo ambalo ni kinyume na sheria. Khwahiyo mgomo ni batili, Mahakama imeamuru warudi kazini na uongozi usiwachukulie hatua yeyote kwa mfanyakazi atake rudi kazini kwa muda uliopangwa, huku wakiendelea kushugulikia matatizo yao kwa njia sahihi...Kilichotokea mahakamani ni kutafsiri sheria ya mgomo kama nani ana haki, ndio wafanyakazi wana haki lakini hawakufata taratibu za kisheria that's it.Kwahiyo badala ya kusema vyama vya wafayakazi vipewe nguvu na visiguwe na sheria, ningeomba viongozi wetu wa vyama ivi wawe wanafahamu sheria za kazi na utekelezaji wake ile waepushe usumbufu kwa siku za usoni.
    Watanzania wengi huwa tunakosa haki zetu kwa kutojua sheria, nani alaumiwe???

    ReplyDelete
  5. Hawa wafanyakazi wa nmb na hiyo TUICO hawana wana sheria?Kwa nini hawakuona haya madhaifu mapema.Sitapenda kuiingilia mahakama.

    ReplyDelete
  6. Oh, I know that guy...

    ReplyDelete
  7. Kaka napenda kuliona wazo la mahakama kama liko sahihi, na halina tatizo, kama waliona mgomo ndio njia pekee ya kupata haki zao basi wanapaswa kufuata taratibu za kisheria. Ila wahusika wanapaswa kujifunza kitu kutoka hapo. Mwisho mi nahisi UDSM wapo wengi hapo wadau au mnasemaje wazee wa KUNJI, Tungekuwa wote kama wafanyakazi wa NMB Ufisadi kwisha, na ole wako usipost michuzi

    ReplyDelete
  8. Tabia ya kugoma sasa naona inakuwa kama mchezo Tanzania.
    nafikiri kuwepo na sheria kali kwamba watu wa sehemu muhimu kama hospitali, benki na usafirishaji , wakigoma basi uwezekano wa kufukuzwa kazi pia uwepo.
    Huwezi anzisha mgomo wa sehemu hizi muhimu na kutegemea kwamba humuumizi mtu wa kawaida moja kwa moja.
    wasomi wengi wanasubiri kazi , hivyo migomo kama hii huwa ni kuwafukuza wafanyakazi na kuajiri wapya.

    ReplyDelete
  9. Sheria za kazi za Tanzania ni za kikale, kwa mfano wanaposema siku za kazi jumapili hatuhesabu, ni kwa vipi ni pale tu swala hilo linapomwangukia mwajiri lakini likimwangukia mwajiriwa huwa zinahesabiwa, mfano mdogo tu mbona mwajiriwa anapoenda likizo huwa zinahesabiwa, mbona mama aliyejifungua mtoto anapoenda likizo ya maternity zinahesabiwa, mbona mishahara inakuwa-determined by 30 days that including sundays and saturdays, hilo lingekuwa sahihi nchi kama UK kwa wale watu wanaolipwa kwa masaa tu. pia vyama vya wafanyakazi vinatakiwa kuwa huru na kama hivitakuwa huru hakuna ya haja ya kuwepo, na kazi kubwa ya vyama hivyo ni kulinda na kutetea maslahi ya wanachama wao ambao ni wafanyakazi, pia kugoma ni haki ya msngi ya mfanyakazi pale maslahi yake hayaendi vizuri, wanafanya kazi kwa ajili ya maslahi yao wao si charity organisations. mahali popote pale duniani hasa kwenye nchi za kidemokrasia wanachofanya ni kuwa wanatoa taarifa kuwa sisi tunamatatizo haya na wewe usipotutatulia ama tusipoongea na kufikia makubaliano yoyote yale yenye maslahi pande zote mbili basi tarehe fulani hatutafanya kazi na wala hutosikia serikali inasema lolote hutokea mara chungu nzi huku UK na USA kwenye utawala wa haki na sheria.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...