Mkuu wa Wilaya ya Nanii na Balozi wa kudumu wa ile kampuni;
mojawapo ya mashairi yangu yaliyopendwa sana ni hili la "Kinu kimevunja Mchi" ambalo nililiandika mwaka 2004 (miaka minne kamili leo angalia http://www.zanzinet.org/poems/2004/kinu_kimevunjika.html).
Natumaini itakuwa ni burudani tosha katika siku hizi za wasiwasi. Nimefanya mabadiliko kidogo tu kulileta tena kwa wadau katika jitihada ha kuinua lugha yetu.

1. Habari tena Michuzi, mdau nimesharudi,
Suala lanipa simanzi, nashikwa na ubaridi,
Wadau wenye ujuzi, watwangao kama jadi,
Kinu kimevunja mchi, kutwanga hakutwangiki!

2. Ndugu zangu sikieni, ninatafuta shauri,
Wataalamu changieni, mniepushie shari,
Wenye Elimu ya dini, na hata madakitari,
Kinu kimevunja mchi, kutwanga hakutwangiki!!
3. Nina nafaka ghalani, za mahindi na mpunga,
Na nyingi ziko shambani, katika vyangu viunga,
Ninahitaji maoni, mnaojua kutunga,
Kinu kimevunja mchi, kutwanga hakutwangiki!!
4. Ni mgumu si laini, hivi leo umepinda,
Sijui nifanye nini, mchi wangu naupenda,
Nitumie mbinu gani, kwa upya nikauunda,
Kinu kimevunja mchi, kutwanga hakutwangiki!!
5. Tatizo hili ni geni, halikuanza zamani,
Na kinu hiki si duni, ni changu hapa nyumbani,
Natwangia kwa makini, asubuhi na jioni,
Kinu kimevunja mchi, kutwanga hakutwangiki!!
6. Kinu hiki kina nini, au tatizo ni mchi,
Ni njama yake jirani, nikamkatie pochi,
Kutwanga ninatamani, hilo mimi siwafichi,
Kinu kimevunja mchi, kutwanga hakutwangiki!!
7. Maji kidogo kinuni, kutwanga kuwe rahisi,
Tatizo lake ni nini, nimepatwa wasiwasi,
Au hili jini gani, au ni yule chunusi,
Kinu kimevunja mchi, kutwanga hakutwangiki!

8. Nifanye nini watani, niokoe mchi wangu,
Asije naye jirani, kutwanga kwa kinu changu,
Nimpelekee nani, niokoe mchi wangu,
Kinu kimevunja mchi, kutwanga hakutwangiki!

9. Shime shime wa jamani, mnijibu kwa makini,
Mazao yalo ghalani, kutwanga ninatamani,
Mniondolee soni, nirudishie imani,
Kinu kimevunja mchi, kutwanga hakutwangiki!!
-Mzee Mwanakijiji
--------------------------------------
1. Mwanakijiji mzee, ujumbeo umefika,
Hata kama ni mzee, haujawa takataka,
Wala usiuchezee, ukadhania dhihaka,
Pole kwayo maswahiba, yaliyokutia shaka.
2. Pole kwayo maswahiba, yaliyokutia shaka,
Umeshachomwa na mwiba, shurti upate wahaka,
Uwe mama ama baba, lazima kuhuzunika,
Pole kwayo maswahiba, yaliyokutia shaka.
3. Pamoja na hayo yote, tufae ufafanuzi,
Kwani yako ni ya wote, walimu kwa wanafunzi,
Ukweli hapa ulete, tukupunguze simanzi,
Pole kwayo maswahiba, yaliyokutia shaka.
4. Iweje uvunje mchi, ndani ya shimo la kinu,
Sijawahi ona mchi, uliozidiwa mbinu,
Waajabu huo mchi, twaomba tupe fununu,
Pole kwayo maswahiba, yaliyokutia shaka.
5. Wadau wa hii globu, kweli wameshapagawa,
Wamegeuka mabubu, wa keko hadi kipawa,
Na wala si kwa ulabu, kama inavyokuwa,
Pole kwayo maswahiba, yaliyokutia shaka.
6. Wape mji wakishindwa, wasomi nao malenga,
Usiwacheke kushindwa, kwani hapo umelenga,
Mwanakijiji mpendwa, fafanua hilo janga,
Pole kwayo maswahiba, yaliyokutia shaka.
7. Sioni alo makini, ya mchi kufafanua,
Haingii akilini, la kinu kulitatua,
Manyanga twabwaga chini, ubingwa twakupatia,
Pole kwayo maswahiba, yaliyokutia shaka.
8. Acha niishie hapa, zinatosha beti nane,
Hakika kweli naapa, usiku huu wa manane,
Wengi tumetoka kapa, na tungojee mwingine,
Pole kwayo maswahiba, yaliyokutia shaka.
9. Mwisho kabisa naomba, walio malenga ka wewe,
Njoni hapa kutamba, msipatwe na kiwewe,
Wala hapataki namba, wala hapana mwenyewe,
Pole kwayo maswahiba, yaliyokutia shaka.
-michuzi

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 20 mpaka sasa

  1. Hapo Zamani mwanakijiji ulikuwa unanifuraisha kweli kweli, ulikuwa unaweka jina lako la kweli na kwenye mabano unaandika mwanakijiji. Unaondoa utamu wa shairi lote ukiweka hilo jina. Michuzi mimi naomba tuanzishe mashindano ya nani zaidi kwenye mashairi hii itakuza kwa kiasi fulani kiswahili chetu.

    ReplyDelete
  2. Mwanakijiji jamani, ni koku ndani ya nyumba
    kwetu huku kijijini, hasa walima mashamba
    tabia hii singeni, leo nimeshakukumba
    acha uhadhimishaji, mwichi utwange kimoja

    kaishazoea Nunu, kuja kuazima mwichi
    makwao wanachokinu, ila tatizo ni mwichi
    tangu enzi zake Tanu, wanaazimisha mwichi
    ACHA UAZIMISHAJI, MWICHI UTWANGE KIMOJA,

    wataka mwichi udumu, leo rosa kesho jeni
    mwichi unalala zamu, mbagala si mtongani
    twauita mhudumu, baba huruma mjini

    ACHA UAZIMISHAJI, MWICHI UTWANGE KIMOJA.

    SEMA NAYE KOKUSIMA

    ReplyDelete
  3. Duu Wazee nimewavulia kofia..haya mashairi yananikumbusha mbali sana nyumbani jinsi lugha yetu ikitumia kitaalamu katika kuelimisha na kufundisha jamii. Inatia raha sana...natamani wengine wajitokeze kuendeleza hapa mlipo.

    ReplyDelete
  4. 1. MWANA KIJIJI.
    Ewe Mwana wa kijiji, Acha hizo zako mbwembwe.
    Siyo kupiga mashuti, Katika mechi bwelele.
    Mchi zamisha kwa kati, siyo kulenga kwa pembe.
    Kuvunjika wako mchi, Kinu kilishindwa ngebe.

    2. BALOZI MICHU.
    Beti umepangilia, Kwa vina nayo mizani.
    Vema kawa shahiria, Kamera weka gizani.
    Japo wengi kasirika, Kukosa osha vinywani.
    Libeneke si tu picha, Hata shahiri za fani.

    Mdau, Japanese.

    ReplyDelete
  5. Waheshimiwa mashairi yenu ya kisasa au tunayaita mashairi mamboleo kwani ni mazuri lakini yamekosa ile ladha ya lugha yetu tamu ya kiswahili. Hebu jaribuni kutumia vilahaja kuleta ladha. Sijui kama mnanielewa, mnaweza kupitia mashairi ya Malenga kama kina Andanenga na YOB wa Morogoro, na wengineo mtaona vilahaja humo vilivyotumika kuleta ladha fulani adimu katika mashairi ya zamani.

    Michuzi umejitahidi sana lakini unakuwa kama sio mtu wa pwani bwana, hebu angalia ubeti wa tano mstari wa kwanza, kina kinagoma, unaposema "wadau wa hii blogu" hiyo imekuwa kama sentensi ya kawaida tu na si ushairi hata nikitaka kuimba inakuwa kama nalazimisha.

    Mtanisamehe kwa kuyasema hayo "Malenga" wetu, maana malenga ni magwiji basi mtuonyeshe umalenga kweli kweli ili mashairi yanoge, yawe na ladha! Haya tunaomba na tenzi pia tufaidi mambo,

    ReplyDelete
  6. Mimi naona haya mashairi yanajaza nafasi tu humu. Kwanini michuzi usiweke link special kwa ajili ya malenga wetu?

    ReplyDelete
  7. BORA UENDE KWA BABU, MCHI TAKUOKOLEA.

    Haya leo maajabu, ya kinu kuvunja mchi,
    toka enzi za mababu, mabara na zote nchi,
    haijatokea nakabu, ya kinu kuvunja mchi,
    Bora uende kwa Babu, mchi takuokolea.

    Wasema kinu si duni, nichako hapo nyumbani,
    hapo naona uhuni, umefanya mwafulani,
    mchi kutwa vijumbani, hapo wategemeani?!
    Bora uende kwa Babu, mchi takuokolea.

    Mwanakijiji ajabu, kuazimisha mchiwe,
    hiyo ni kubwa sababu, ya mchi kungia ndewe,
    usilaumu "DHAHABU", kwani mkosa ni wewe,
    Bora uende kwa Babu, mchi takuokolea.

    Pengine umezeeka, wa kijiji usifiche,
    umetwangia nafaka, toka asubuhi kuche,
    jioni wahangaika, na kulaumu "kinuche"?!
    Bora uende kwa Babu, mchi takuokolea.

    Au mchi waugua, maradhi yameukumba,
    wadudu wameingia, sababu u-kumbakumba,
    mbio kwa babu kimbia, "afua" yako twaomba.
    Bora uende kwa Babu, mchi takuokolea.

    Bora uende kwa Babu, mchi takuokolea,
    usiende kwa tabibu, "HOGO" atakuwekea,
    itakuwa ni aibu, Babu siri tofichua,
    Bora uende kwa Babu, mchi takuokolea.

    ReplyDelete
  8. MTWANGIO WEWE TWANGA USICHOKE
    MTWANGIOEEEEEEEEEE
    TWANGA BILA WASI WASI WEWE MTWANGIO WANGU KINU KIMEKURIDHIA EEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEE

    ReplyDelete
  9. Yaani mimi nafurahi tu hapa I wish ningekuwa najua mashairi niwajibu ...lakini kiswahili chenu ni kigumu sana.

    ReplyDelete
  10. Kinu kuvunjika, ni mbaya bahati
    blender hutumika, nenda na nyakati
    maji ya kimwaika, kuyazoa valangati
    Mwichi umeisha kazi, karne ya leo

    Ni nyingi nafaka, unaandaa party?
    Kukoboa unataka, au kusaga boriti?
    mashine zimetapakaa,Mpanda na Babati
    Mwichi umeisha kazi, karne ya leo.

    Kuna blender kata, ngamba na bati,
    Mpingo wa Msata, Mninga Nyamisati
    Tafuta utazipata, tumia wakati,
    Mwichi umeisha kazi, karne ya leo

    Kuna blender nata,wewe tafuta Siti,
    Sio bora kupata, tafuta ilio fit
    Usicheze karata, ubora uudhibiti
    Michi umeisha kazi, karne ya leo

    Nenda hata Kipata, Mwanza au Kibiti
    Nyingi zimejikita, penda ilio smart
    Usingizini toka, technologia

    ReplyDelete
  11. mchi kufia kinuni,hilo jambo si geni,
    mwanzoni hukuuthamini,ukautumia vibaya chooni,
    wadau kuweni makini,msije dharaurika mitaani,
    msikawie msalani,mchi hautofia kinuni.

    ReplyDelete
  12. Tumia Viagra, Ili mchi uwe fiti,
    Huwezi weka papara, utaona huo mti,
    Utapa maraha, na hutaona tofauti,
    Mwanaume rijala, Hilo sio tatizo.

    ReplyDelete
  13. samahani malenga Mwana kijiji, mie nitakupa jibu bila kujali viina wala nini:
    jawabu ya mchi kuvunjwa na kinu ni jepesi,
    mwone mzee wa kimasai akusaidie kuchonga mchi mpya,
    yeye huchonga kwa kutumia kwa mkno wake na mchi unapokuwa tayari huupaka mkuyati A.K.A viagra ya kienyeji,
    kama mchi utashindwa kazi ya kutwanga kinuni,
    mzee yupo tayari kutafuta mbinu nyingine za kisasa kuhakikisha kazi yake inafanywa barabara!

    ReplyDelete
  14. ha ha haaaaa, hogo ataekewa? wacha nicheke mie, michuzi kumbe nawe umooo

    ReplyDelete
  15. kwa kweli mnatisha.

    ReplyDelete
  16. Kwa kweli Mwanakijiji, pole unastahili,
    Wadau wakufariji, wakutulize akili,
    Jibu la ulilohoji, ulilouliza swali,
    Tatizo lako la mchi, chanzo chake si kinucho

    Michi panapo msoto, kwenye kazi za misuli,
    Haiishi ja vifuto, vya kufutia penseli,
    Hutwanga kwenye fukuto, huimarika kwa kweli,
    Tatizo lako la mchi, chanzo chake si kinucho

    Usije twanga na mchi, ilhali kula huli,
    Jilie maparachichi, na karanga mabakuli,
    Mtwanga kula haachi, ni lazima ujijali,
    Tatizo lako la mchi, chanzo chake si kinucho.

    Yawezekana jirani, ni mtwangaji wa pili,
    Wa hapo kwako kinuni, amejigea kibali,
    Kwani siri za kinuni, hutoka kiubahili,
    Tatizo lako la mchi, chanzo chake si kinucho.

    Licha ya hayo lakini, wewe katu usijali,
    Usiwe majaribuni, kuazima ni aghali,
    Mazingara na majini, yakakufanya batili,
    Tatizo lako la mchi, chanzo chake si kinucho.

    Usitafute tabibu, kukusaidia hili,
    Kukupa atajaribu, tembe za rangi ya nili,
    Hivi tembe ni jawabu, la hiki kitendawili?
    Tatizo lako la mchi, chanzo chake si kinucho

    Mkuu bini Uyati, nguli wa maliasili,
    Mtafute hapo kati, afanye wake u-nguli,
    Mchio akarabati, uirudie asili,
    Tatizo lako la mchi, chanzo chake si kinucho

    ReplyDelete
  17. Mchi huu mchi gani,Mzee watutatiza,
    Bora uweke hewani,tupate nalo kukwaza,
    Bado tupo gizani,wa lukange na vigwaza,
    Mchi huu mchi gani, Mzee watutatiza

    Kukatika na kupinda,nilipi lilo kukuta,
    Kwa michuzi naye pinda,wote wajaa utata,
    Wa mbagala na kitunda,bado hatujakupata,
    Mchi huu mchi gani,Mzee watutatiza

    Hili kwetu ni ajabu,mchi wako kukatika,
    Bado sijapata jibu,hali hiyo kukufika,
    Lazima kuna sababu,hebu punguza wahaka
    Mchi huu mchi gani,Mzee watutatiza

    Wezekana uliruka,ukatwanga vya wenzako,
    Waka amua kuvuka,mpaka nyumbani mwako,
    Ili upate umbuka ,utwangapo kinu chako,
    Mchi huu mchi gani,Mzee watutatiza

    Au labda ni maradhi,mwilini yameingia,
    Muombe mola hafidhi,akujaaliye afua,
    Hapo tapata hifadhi,ya maradhi kufifia
    Mchi huu mchi gani,Mzee watutatiza,

    Nilipofika tamati,beti zimeniishia,
    Nakutakia bahati,si majuto kujutia,
    Uje pona kwa wakati,utimize yako nia
    Mchi huu mchi gani,Mzee watutatiza

    Mullah

    ReplyDelete
  18. YAKUBALI MATOKEO KUTWANGA HUWEZI TENA

    1. Hodi hodi we balozi, na mzee mwa-kijiji
    Nisije kuwa baguzi, kama mpanda Bajaji
    Japo mi si mchambuzi, najua mji si jiji
    Yakubali matokeo , kutwanga huwezi tena.

    2. Mchi ni kama pumzi, zina mwanzo pia mwisho
    Haihitaji ujuzi, kulipata suluhisho
    Usimtafute mwizi, bure utatokwa jasho
    Yakubali matokeo , kutwanga huwezi tena.

    3. Hauhitaji mhunzi, wala mchonga vinyago
    Watakujaza simanzi, pasi kuona kinyongo
    Utawona ni wezi, au wasema uongo
    Yakubali matokeo , kutwanga huwezi tena.

    4. Kutwanga huwezi tena, yakubali matokeo
    Usihisahau jana, ukang’nga’na na leo
    Umepitwa na ujana, japo bado una cheo
    Yakubali matokeo , kutwanga huwezi tena.

    5. Hayakuanzia leo, yalikuwepo awali
    Tumia wako upeo, kukabili hii hali
    Huitaji pembejeo, wala zile kemikali
    Yakubali matokeo , kutwanga huwezi tena.

    6. Yaliwakuta wahenga, wewe huwezi hepuka
    Usitumie mapanga, kuvifukua vichaka
    Muhimu ni kujipanga, uihepuke zihaka
    Yakubali matokeo , kutwanga huwezi tena.

    7. Kiweke bayana kinu, pia usione soni
    Zitumie zako mbinu, usiingie mitini
    Ipokee kama tunu, tena ukiwa yakini
    Yakubali matokeo , kutwanga huwezi tena.

    8. Usipokuwa makini, wajanja watafaidi
    Utaingizwa mjini, na hofu itakuzidi
    Utapokuja baini, utajiona fisadi
    Yakubali matokeo , kutwanga huwezi tena.

    9. Ata ukiwa makini, mchi budi uvunjike
    Hakitupwi lawamani, kinu kwa yake makeke
    Usijishushe thamani, kwa kushindwa libeneke
    Yakubali matokeo , kutwanga huwezi tena.

    10. Naweka kalamu chini, ili nipishe wengine
    Wenye mawazo makini, fikira zilizo nene
    Wasiotuacha chini, Kwenye giza lilo nene
    Yakubali matokeo , kutwanga huwezi tena.


    Mdau H.Q.

    ReplyDelete
  19. Wadau wote, wabeba maboksi na Wadanganyika nisaidieni mwenzenu
    **********************
    Ndugu zangu, nisaidieni
    Mchi wangu,nihurumieni
    Nguvu zangu, zapunguani
    Mara moja yaja haraka, ya pili mboni taabu?

    Nawauliza wadau,hivi ndivyo ilivyo
    Niifaidi pilau, lakini si kihivyo
    Kutwanga wangu, nikawie vilivyo
    Mara moja yaja haraka, ya pili mboni taabu?

    Sitaki kukatiza, nisaidieni jamani
    Nipate himiza, purukushani kinuni
    Tamati nimefikiza,nisaidieni jamani
    Mara moja yaja haraka, ya pili mboni taabu?

    Malenga jr

    ReplyDelete
  20. heeeeeeeeeeeee,,,hahahahaaaaaa
    jamani watu mna fikra za "uroda na ngono"
    michu weee michu wee una balaa,me sio mpenzi wa ushairi ivi bt niliposoma hii kitu nimechoka kabisa nyie wadau haaaaaaa
    ama kweli vitukoeti viagra hahahaaa

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...