JK akiwa na Mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika Mh. Jean Ping
Heko JK, huu ndio utawala wa sheria
(Tahariri ya gazeti la Kulikoni la November 28, 2008)

MOJA ya sifa kubwa za Rais Jakaya Kikwete ni kutoonesha papara wala jazba katika maamuzi yake. Umakini na msimamo wake juu ya uongozi wenye kuzingatia utawala bora na sheria za nchi ulianza kuonekana wazi pale alipounda tume maalum ya Jaji Mussa Kipenka kuchunguza mauaji ya wafanyabiashara wanne wa madini.

Mauaji hayo yanadaiwa kufanywa na Polisi kwa amri ya aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Zombe. Rais Kikwete hakuchelewa; baada ya kukabidhiwa ripoti ile na Jaji Kipenka, siku chache baadaye watuhumiwa wakatiwa mbaroni, akiwemo Zombe aliye rumande Gereza la Keko hadi leo akishtakiwa kwa mauaji.

Kama ofisa wa jeshi mstaafu, Rais Kikwete bado anakumbuka fika kwamba katika vita au mapambano yoyote kuna kushinda na kushindwa. Anafahamu fika kwamba kama ofisa wa jeshi wapiganaji anaowaongoza wanahitaji kuwa na ujuzi wa aina kuu mbili: Mikakati ya Mapambano (Military Strategies) na Mbinu za Medani au Stadi za Kivita (Military Manoeuvres).

Juu ya yote, anajua kwamba askari mzuri anatakiwa kuwa na afya njema, elimu na maarifa lakini katika mapambano kitu muhimu zaidi ni uvumilivu na subira. Katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake (2006-2008), Rais Kikwete ameonesha dhahiri tabia yake halisi ya uvumilivu na subira wakati akipanga mikakati ya kutekeleza mambo muhimu.

Mfano halisi ni jinsi alivyotoa matokeo ya ripoti ya ukaguzi wa hesabu za fedha za Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu Februari mwaka huu. Ukaguzi huo ulifanywa na kampuni ya Ernst & Young kwa niaba ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali na ripoti yake alikabidhiwa Rais.

Alikuwa na hiari ya kuitangaza au kuificha au kuibadili. Lakini aliamuru vyombo vya dola viwashughulikie wanasiasa, wafanyabiashara na maofisa waandamizi wa Benki Kuu waliohusika katika ufisadi ambao kampuni 22 zilichotewa bilioni 113/- za walipa kodi kwa wizi wa kughushi mwaka 2005 / 06.

Alisisimua umma wa Watanzania siku ya tangazo hilo lililoambatana na kufutwa kazi kwa Gavana wa Benki Kuu, Marehemu Daudi Ballali. Kwa niaba ya Rais JK, Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo alitangaza Februari 8, 2008 kwamba, Mwanasheria Mkuu Johnson Mwanyika, Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi Mwema, na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Edward Hoseah wameagizwa kuchunguza na kuchukua hatua sahihi za kisheria, kinidhamu na kiutawala dhidi ya wahusika wote wa wizi huo.

Malalamiko, tuhuma za kulindana na mizengwe vilifuata na kupata upeo kila muda uliposogea huku umma ukiwa na shauku ya kuona mafisadi wanatiwa adabu kisheria. Wako waliobeza kwa kusema: “Ah, JK anatafuta umaarufu tu hakuna kigogo atakayeshtakiwa, mambo yataisha hivi hivi, tutasahau...”Lakini Rais wetu hakusahau mafunzo ya kijeshi sambamba na utawala bora. Alizingatia uvumilivu na subira.

Hata alipokwenda kuhutubia Bunge Agosti 21 mwaka huu alisema serikali imetoa hadi Oktoba 31 wezi wa EPA wawe wamerejesha fedha walizoiba. Alikuwa anavuta subira kuhakikisha kuwa wezi wanashtakiwa baada ya kurejesha mali walizoiba.Kiswahili kina methali zisemazo: “Mvumilivu hula mbivu” ; “Subira yavuta kheri”; “Kawia ufike” na “Heri kenda nenda, kuliko kumi nenda rudi”.

Hizo tatu za awali zinahimiza sana uvumilivu na subira ili kufanikiwa, lakini hiyo methali ya mwisho inahimiza zaidi uharaka katika maamuzi na utekelezaji, unapobaini uvumilivu na subira havina tija au vitaleta hasara.Rais JK alitumia busara hiyo.

Majalada ya watuhumiwa wa wizi wa EPA yalipelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka, na hatimaye Novemba 5 mwaka huu washtakiwa wa kwanza wa wizi huo wa kutisha wakafikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya jinai. Kila mwananchi makini sasa anajua faida ya uvumilivu na subira katika suala la EPA.

wamba asilimia 76.7 ya fedha zilizoibiwa zimerejeshwa na watuhumiwa wanapewa adabu inayostahili kisheria! Huo ndio utawala wa sheria unaozingatia umakini na busara.

Iwapo Rais Kikwete angekuwa na papara na kusikiliza shinikizo lenye jazba la kutaka wahusika wafikishwe mahakamani haraka, kiasi hicho kikubwa cha fedha zilizoibwa kamwe kisingepatikana.

Serikali nyingi duniani zimejikuta zikipoteza kiasi kikubwa cha fedha kutokana na hamaki ya kuwashtaki watuhumiwa na hatimaye kutiwa hatiani bila serikali kuambulia chochote. Wakati watuhumiwa wa wizi EPA wakiendelea kunaswa, Serikali ya Rais Kikwete haikubweteka kwa furaha na sifa kutoka kwa walipa-kodi na wapiga-kura wanaovuja jasho kila siku.

Jumanne ya Novemba 25 mawaziri wawili waandamizi katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Basil Mramba na Daniel Yona, walipandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka 13 ya jinai kwa matumizi mabaya ya madaraka na ofisi.Mramba alikuwa Waziri wa Fedha wakati Yona alikuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati wa muhula wa pili wa utawala wa Rais Benjamin Mkapa.

Wawili hao, kwa nyakati tofauti wakiwa madarakani, wanadaiwa kutumia vibaya madaraka yao kinyume na Ibara ya 96 (1) ya Sheria ya Makosa ya Jinai, Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, hivyo kuikosesha serikali kiasi cha 11,752,350,148/- kutoka kwenye kodi.Kupelekwa kwa mawaziri hao mahakamani kulivuta hisia za Umma huku wengi wakisema msururu wa viongozi wote waliotumia vibaya madaraka yao ufikishwe mahakamani.

Lakini bado busara ya Serikali makini na Rais JK haziwezi kuruhusu papara katika maamuzi muhimu ya kisheria.Watuhumiwa wote wamepelekwa rumande baada ya kushindwa kulipa fedha taslimu bilioni 3.9/- taslimu kila mmoja. Kesi hiyo itatajwa tena Desemba 2, 2008, na upelelezi bado haujakamilika.

KULIKONI tunasema sasa umefika wakati umma wote umpongeze Rais Kikwete na serikali yake kwa hatua nzuri walizochukua na kumwombea kwa Mungu awaongezee busara wasisahau uvumilivu, subira, mkondo wa sheria, maadili ya uongozi, haki za binadamu na misingi ya utawala bora.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 7 mpaka sasa

  1. mimi nampongeza kwa kweli, lakini viongozi wengine wote ukiondoa Magufuli wanafanya kazi kwa mazoea sana,

    ReplyDelete
  2. Kula TANO....mhariri nimegundua JK atakuwa the best presidaa in Tz since Uhuru.Time will tell....Ila kuna issue yetu(wabeba mabox) baba rais....Dual citizenship we're still waiting.
    CONGRATULATIONS MR.PRESIDENT.
    Cha Chandu - UK

    ReplyDelete
  3. Here we go again kutukuzana wakati ukweli wa mambo raisi ni mwajiriwa wa wanananchi.
    Hakuna haja ya kumwagiana misifa wakati kosa limetokea. Serikali ni lazima iwajibike kwa wananchi wake badala ya kuwa na kazi ya kujisafisha na kashfa.
    How did it happen at the first place anyway na serikali haikuwa makini mpaka wananchi na baadhi ya wabunge wa upinzani na ccm yenyewe walipolivalia njuga masuala haya ya ufisadi ndio serikali ya JK inakurupuka na kuanza kutoana kafara.
    It just dont get in my head that we can applaude scandals being invastigated while we still have corrupt leaders running the goverment.

    ReplyDelete

  4. Anafahamu fika kwamba kama ofisa wa jeshi wapiganaji anaowaongoza wanahitaji kuwa na ujuzi wa aina kuu mbili: Mikakati ya Mapambano (Military Strategies) na Mbinu za Medani au Stadi za Kivita (Military Manoeuvres).


    mwandishi umekosea: wanajeshi wanatakiwa wajue fieldcraft na military tactics. Siyo strategies na maneuvres kama unavyodai

    ReplyDelete
  5. Mungu mbariki Kikwete Mungu ibariki Tanzania na watu wake.Sasa viongozi na wale wote waliokO madarakani mjuwe kuwa unapopewa kazi ya kutumikia wananchi watumikie kwa uadilifu.

    JK KUMBE SI WA KUCHEZEA AISEE.DOOOOOOOOOOOOOOH!SIAMINI.

    ReplyDelete
  6. Watanzania tuelewe kuwa nchi haijengwi na Jk peke yake huku sisi tukitizama kusubiri kukosoa na kupiga kelele kwa vitu tusivyoelewa.

    Rais ameonyesha njia tumuunge mkono aliyoahidi kafanya na tunaona tusiwasikilize maaduwi wa maendeleo wasioona jema lolote hata jema wanalibadili kuwa baya wameumbwa hivyo tunao na hatuwezi kuwakataa.

    JK TUKO PAMOJA BABA NAKUPA SHAVU MIMI MBEBA MABOX NIMESHAONA WEWE NI MZARENDO ASILIA.

    ReplyDelete
  7. dang JK got style,wow kama anapiga cartwalk.suit ya nguvuuuuuu,wazaramo hoyeeeeeeee.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...