TAARIFA YA SERIKALI KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU KUSUDIO LA WALIMU LA KUTAKA KUGOMA
1. Tarehe 13 Oktoba, 2008 Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi ilitoa amri ya kusitisha mgomo usiokuwa na ukomo wa walimu uliokuwa umekusudiwa kuanza tarehe 15 Oktoba, 2008 na kuendelea, ili kutoa fursa kwa majadiliano yaliyokuwa yanaendelea kati ya Serikali na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kufikia ufumbuzi. CWT hawakuridhika na uamuzi huo hivyo walipeleka maombi yao ya marejeo ya uamuzi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi kwenye Mahakama ya Rufani. Katika maombi yao hayo, walidai kuwa Mahakama Kuu ilisikiliza shauri ambalo lilikuwa limepelekwa mbele ya Mahakama ile chini ya Kifungu kisichokuwa sahihi kulingana na maombi husika.
2. Mahakama ya Rufani, katika uamuzi wake kuhusu suala hilo ulioandaliwa tarehe 11 Novemba, 2008 na kusomwa tarehe 13 Novemba, 2008, ilikataa maombi ya CWT ya kutaka kurejewa kwa uamuzi wa Mahakama Kuu na kuelekeza kuwa walipaswa kukata rufaa badala ya kuomba marejeo.
3. Hata hivyo, Mahakama ya Rufani, kwa kutumia mamlaka yake yenyewe iliamua pia kuwa maombi ya Serikali yaliyowasilishwa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi, yalikuwa yamewasilishwa kupitia Kifungu cha Sheria kisicho sahihi. Kwa sababu hiyo, Mahakama ya Rufani ilifuta mwenendo wote pamoja na maamuzi juu ya shauri lile.
4. Ni vema isisitizwe hapa kwamba Mahakama ya Rufani haikutamka kwamba mgomo usio na kikomo uliokusudiwa kuanzishwa na CWT ulikuwa halali na wala haikuruhusu kufanyika kwa mgomo huo.
Baada ya uamuzi huo wa Mahakama ya Rufani, Serikali imepata taarifa ya Tamko la CWT la tarehe 14 Novemba, 2008 lililotolewa na Mwal. Gratian Mukoba, Rais wa CWT kupitia vyombo vya habari kwamba, pamoja na mengineyo, wanachama wa CWT wataanza mgomo wao usio na kikomo siku ya Jumatatu tarehe 17 Novemba, 2008.
Pia katika tamko lao, CWT wametoa mapendekezo ya namna ya kuboresha zoezi la uhakiki wa madai ya madeni yao linaloendelea ambayo wanaitaka Serikali kuyafanyia kazi.
Serikali kwa upande wake imeendelea kulipa madai mbalimbali ya walimu na watumishi wengine kwa mujibu wa taratibu zilizopo. Aidha, Mheshimiwa Rais katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi kwa Taifa ya tarehe 31 Oktoba 2008, alielekeza na kuahidi kuwa Serikali italipa madeni yote ya walimu yaliyohakikiwa. Maelekezo ya Mhe. Rais yalirejewa tena na Mhe. Waziri Mkuu tarehe 7 Novemba, 2008 alipokuwa akitoa hoja ya kuahirisha Mkutano wa 13 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuahidi kwamba Serikali itakamilisha uhakiki huo mapema iwezekanavyo. Serikali hivi sasa inakamilisha zoezi la uhakiki wa madeni ya walimu na italipa madeni yote yaliyohakikiwa ifikapo tarehe 30 Novemba 2008. Kuanzia tarehe 17 Novemba, 2008, Wizara ya Fedha na Uchumi itaanza kupeleka fedha kwenye Halmashauri zote 133 tayari kwa malipo. Kwa hiyo, Serikali inawataka walimu kuwa na subira kwani kwa hatua hizi zinazochukuliwa na Serikali hatuoni busara ya walimu kugoma.
Walimu ni watumishi wa umma, na kama ilivyo kwa watumishi wote wa umma, masuala yahusuyo mgomo lazima kwanza yawe yameshughulikiwa na kukamilika chini ya Sheria ya Majadiliano ya Pamoja Katika Utumishi wa Umma Na. 19 ya mwaka 2003 ambayo imeweka masharti yanayohitaji kutimizwa kabla ya watumishi kugoma. Katika kusudio la walimu la kutaka kugoma, baadhi ya masharti hayakutimizwa na ndio maana Serikali inapinga mgomo batili usio na kikomo unaokusudiwa.
Tayari Serikali imekwishawasilisha katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi Maombi Anuai Na. 21 ya 2008 kuiomba Mahakama Kuu izuie mgomo usio na kikomo unaokusudiwa. Aidha, CWT wamepelekewa samansi ya kuitwa Mahakamani kwa ajili ya shauri hilo la maombi anuai ambalo limepangwa kusikilizwa tarehe 17 Novemba, 2008.
Kutokana na hatua hizi zinazoendelea kuchukuliwa, Serikali inakitaka Chama cha Walimu kufanya yafuatayo:-
Kusitisha mgomo wao usio na ukomo unaokusudiwa kuanza tarehe 17 Novemba 2008, kwa kuwa tayari Serikali inashughulikia kwa ukamilifu madai ya madeni yao.
Serikali inawashauri CWT wawasilishe rasmi Serikalini mapendekezo yaliyo kwenye tamko lao, kuhusu namna ya kuboresha zoezi la uhakiki wa madai ya madeni ya walimu, na Serikali iko tayari kuyafanyia kazi. Serikali inaamini kwamba iwapo mgomo utaendelea, utainyima fursa ya kushughulikia mapendekezo ya CWT yaliyo katika tamko lao.
Kwa kuwa mgomo unaokusudiwa haukutimiza masharti yote yaliyotajwa katika Sheria ya Majadiliano ya Pamoja katika Utumishi wa Umma, mgomo huo machoni mwa Serikali kama mwajiri ni batili na walimu watakaoshiriki kwenye mgomo huo wanaweza kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria hiyo. Aidha, kwa mujibu wa Sheria ya Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004 mtumishi atakayeshiriki kwenye mgomo batili, hatalipwa mshahara na Serikali, kama mwajiri kwa kipindi chote cha mgomo. Itabidi mshahara wake ulipwe na aliyeitisha mgomo huo.
10. Ikumbukwe kuwa tayari suala hili liko Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi, hivyo walimu hawapaswi kugoma kwa sababu kufanya hivyo ni kuishinikiza mahakama kutoa maamuzi ambayo walimu wanayataka, kitendo kinachoingilia uhuru wa mahakama. Mgomo huo hauna maslahi kwa umma na hata kwa walimu wenyewe kwa sababu unakusudiwa kufanyika katika kipindi ambacho wanafunzi wanapaswa kufanya mitihani yao ya kuvuka madarasa au vidato.
Hivyo, kwa kuwa Serikali inayafanyia kazi madai ya madeni ya walimu, na kwa kuwa mgomo unaokusudiwa kufanyika ni batili na usio na maslahi yoyote kwa Taifa, Serikali inawataka CWT kusitisha kusudio lao la kufanya mgomo usio na kikomo uliopangwa kuanza tarehe 17 Novemba, 2008 na kuwataka walimu wote kuendelea na kazi zao kama kawaida.
(Phillemon L. Luhanjo)
KATIBU MKUU KIONGOZI NA
MKUU WA UTUMISHI WA UMMA
15 Novemba, 2008


Unawatishia nyau na ahadi hewa! Ilitakiwa waanza kulipwa week hii iliyoisha kabla ya maamuzi ya mahakama. Hapa ndipo penye utamu! Tuone Jumatatu sasa.
ReplyDeletewao serekali wangejadiliana na walimu meza moja sio kuja kwa waandishi na kutoa vitisho,serikali nyingi za africa zina ukaidi mkubwa hasa kwa wanachi wao madai ya walimu niya siku nyingi, wapewe haki yao mbona hela ya rada na ndege zilikuwepo bila mizengwe tuweke priorty jamani elimu muhimu wauze ndege ile wawalipe walimu haha aha ngedere wakubwa yaani (nyani)
ReplyDeleteTHIS IS POLITICALLY INCORRECT, JUST BLAH BLAH POLITICS, LAWS AND REGULATIONS OF TRADE UNIONS IN TANZANIA SHOULD BE CHANGED, THEY ARE STILL IN COMMUNISM FACE, UJAMAA NA KUJITEGEMEA, DEMOCRACY SHOULD BE IN THERE, THE FIRST PRIOROTY WHEN HANDLING WORKERS' MATTERS, NOT SOCIALSM POLITICS. TRADE UNIONS SHOULD BE GIVEN FULL AUTONOMY POWERS WHEN COMES TO WORKERS' RIGHTS
ReplyDeleteInasikitisha kuona Katibu mkuu kiongozi anatoka kauli kama hii, kwanza anaonyesha wazi kuwa, serikali inaomba walimu wasigome lakini anatumia lugha ya kibabe? Mimi namshauri angewaomba tu smahani Walimu wetu wapendwa pengine wangemuelewa. Sasa hata usipowapa mishahara watu wenyewe wanategemea zaidi Michingo yao, kwa mishahara huwa wanapata after six month unfikiri ndo utawatisha? hapo ni sawa na Kumnyima Masai samaki? Tafadhali walimu mtofundishie watoto wetu, tunawaoma kwa kuwa kina Luhanjo na wenzoa watoto wao wapo Ulaya na Marekani wanasoma huko so athari hawataziona. Sisi tunawaahidi kuwa mwaka 2010 tutkuwa pamoja kutafuta mtu atakayewasilikiza walimu na watumishi wengine. lakini ikiwa mtaamua kugoma pia nawaunga mkono.
ReplyDeleteNawatakia kila raheri katika kipindi hiki kigumu cha vitisho ya serikali ya kina Luhanjo.
Walimu nawapongeza sana kwa hatua mliyoifikia katika kudai haki yenu.Wizara ya elimu na serikali ya CCM imejaa ukiritimba, urasimu na vitisho kama ilivyo kwa katibu mkuu kiongozi.
ReplyDeleteWalimu toachane na kaugonjwa ketu ka uoga.Kazi ya ualimu si wito kama tulivyokuwa tukidanganya nyakati zilizopita. Ualimu ni kazi kama kazi nyingine yeyote ile.Serikali inapaswa kuelewa wazi kuwa haki na wajibu ni pande mbili za sarafu moja. Walimu ni kioo cha jamii, hivyo fundisho watakalotoa ni dhahiri itawapa uelewa hata wananchi wa kawaida kuielewa serikali CCM pamoja na madhaifu inayoyakumbatia.
Walimu ni sehemu kubwa ya wafanyakazi wa serikali. Hivyo tukiwa makini basi tutapewa haki yetu bila masharti na vitisho.
Tusimame imara tuingoe serikali ya CCM kwenye madaraka na hatimaye maisha bora yatawekena kwa kila mtanzania.
Safi kabisa. Tamko hilo la Serikali liko wazi na limeeleza vizuri hali ilivyo. Mimi kama mzazi nawaomba CWT watumie hekima na busara na waache kuhujumu watoto wa taifa hili. SErikali imeahidi kuwa ifikapo Novemba 30 watalipwa. Zimebaki siku 15 tu mgomo wa nini? Kwangu mimi hii serikali ni sikivu. CWT unless wana agenda nyingine na bila ya hska ya kisiasa basi waendelee kugoma. Lakini watuambie wanagoma kwa kutumia bendera ya chama kipi. Waache ghiliba.
ReplyDeleteHii serikali imezidi usanii, wanategemea hawa walimu wasomeshe nini watoto wao na kama kuna aliye chuo kikuu serikali inataka achangie kwanza ndiyo asajiliwe ila wao kutoa hela ya watu hawataki. DAWA ndiyo hiyo! Mbona richmond hawakukopwa? Itabidi na taasisi nyingine waunge mkono walimu.
ReplyDeletemchangiaji ulopita inaonekana kabisa hujaelewa nini maana ya mgomo, ni wazi kwamba serikali ya jk wanataka kuturudisha miaka ile ya ubabe kwamba hawawezi kushughulikia matatizo ya waajiriwa wake mpaka kwa bakora. ni aibu kubwa kwa raisi ambaye wananchi walikuwa na high expectation naye na issue ya kawaida kama paychec ya mwalimu wa kawaida ina kutoa jasho. kwanini issue kama hii inasubiriwa mpaka dakika ya 89 ndio goal geta anaingia wakati tuo nyuma kwa magoli mawili. unategemea muujiza gani ufanyike kupata muafaka hapo.
ReplyDeleteWewe Melkiory Matilya. CCM inahusiaka nini na CWT? Kama CWT ni chama cha siasa sawa. Hata hivyo kosa la Luhanjo ni nini? Mbona wao CWT wamepitia vyombo vya habari sasa ulitaka wajibiwe kupitia wapi? Mimi naishauri serikali CWT wakigoma Rais wao MKoba na akina Oluoch wafunguliwe mashitaka. Wahujumu wakubwa hao!!!
ReplyDeletehakuna muda wa kupoteza,acha wagome kwani madai haya sio ya mwezi huu wala mwaka huu,ni yakipindi kirefu,kwani serikali haikujua kuwa inadaiwa kipindi chote hicho au kutotilia maanani na kuwadharau walimu.acha watoe machungu yao.na hii ni changamoto kwa serikali,madai ni mengi wengine hawajapandishwa madaraja n.k sasa nani anahusika juu ya kupandisha madaraja yao mpaka wao walalamike hivi hakuna wa kutunza kumbukumbu za wafanyakazi na kujua nani anatakiwa kupandishwa daraja,huu ni uzembe kwa watendaji wake.sasa inatakiwa ijipange upya juu ya utendaje wake kwani baadhi ya sehemu ni ubabaishaji tu.
ReplyDeletehuyo anayesema wanagoma kwa kupitia bendera ipi ...poinless kabisa.Wewe ni fisadi nini? Unajua jinsi watu wanavyoteseka alafu unawaambia wasubiri siku 15. Kwani sirikali haikujua kuwa watu hao wanatakiwa kulipwa ...mpka watake kugoma ndio serikali iwaambie subirini.....Kwanza tumbo linasubora?
ReplyDeleteMimi nawaunga mkono....kama walivyosema hapo juu ualimu sio wito na mnahitaji kula na pia hawa wakubwa watoto wao wako nje ya nchi wanajizomea lakini no matter what watoto wetu watago through....you guys have to do what you got to do......msiogope vitisho wana nini simameni pamoja na mtafika
Mimi binafsi naunga mkono mgomo wa waalimu! Serikari yetu imekuwa ya kibabaishaji! inachanganya akili za watu. sasa walikimbilia mahakamani, na waalimu rufaa wameshinda, serikali inakwenda tena mahakama ya kazi sijui, huu ni ubabaishaji! mabilioni ya Epa kwanini wasiwalipe walimu? eti wameyaweka kwa Kilimo, unadhani pesa hiyo itatumika kwa Kilimo kweli? wangewalipa walimu tungeona mojakwa moja kuwa pesa hiyo imatumika! Pesa hiyo itarudi mifukoni mwao!
ReplyDeleteTanzania tumefikia pabaya sana na nionavyo mimi CCM haitufai tena, pamoja na kuwa ninaimani itarudi madarakani 2010, kwani ufisadi wote wanao, na wizi wote wanao! lbda yatokee mapinduzi, tusimame pamoja, kama Slobodan mirosvici alivyotolewa!
Sina hata hamu ya kuona Picha ya rais wetu! sitaki hata kusikia Hotuba zake! sababu anadanganya watu waliompigia kura! Lakini "mambo haya yana mwisho"
Mimi nawaunga mkono walimu, wagome tu, Serikari imekuwa kiziwi mpaka mgomo ndiyo unaweza kuwafanya wasikilize na kutekeleza mambo. Inashangaza kuona kwamba vitu vingine hawachelewi kutekeleza kama mikataba mibovu, Mimi nayapongeza sana majimbo ambayo yameweza kukiondoa chama cha mapinduzi madarakani (Chama cha mapinduzi sijui mapinduzi gani wakati huu), ni chama cha zama zileeeeeeee. Mambo yamebadilika sasa. Jamani tubadilike na kuangalia upande wa pili wa shilingi sio kila siku CCM na wakati wanaendelea kutufanyia mbaya. Nakwambia CCM 2010 haipati kitu, watu wamechoka. Mdau
ReplyDeleteHapa Tanzania kuna mwalimu anayelipwa mshahara na marupurupu makubwa kuliko walimu na maprofesa wa vyuo vikuu vyote Tanzania. Hacheleweshewi mishahara yake. kapangiwa jumba la kifahari. Kapewa gari nzuri. hualikwa kwenye dhifa kubwa kubwa za kiselikali na kibinafsi. Wanafunzi wake hawapasi mitihani wala hana vipimo vyovyote vya kudhibitisha uwezo wao wala uwezo wa mwalimu mwenyewe.
ReplyDeleteUnamfahamu mwalimu huyo?
Kama humfahamu ngoja nikufahamishe. Mwalimu huyo ni mwalimu wa timu ya taifa ya mpira wa miguu Marcio Maximo.
Ikiwa kama unafikiri haya niliyoandika ni uzushi tafuta data za mkataba wake; uone mshahara, marupurupu, bei ya pango (house rent), gari anayotumia na mengineyo. Halafu linganisha au wianisha na mikataba ya walimu na wahadhiri wa vyuo vyuo vikuu Tanzania.