Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 5 mpaka sasa

  1. Serikali yaogopa moto wa Dowans

    2008-12-18 12:34:48
    Na Mwandishi Wetu


    Hatimaye serikali imesalimu amri kwa Bunge na kuamua kusitisha uamuzi wake wa kutaka kununua mitambo ya kampuni ya kufua umeme ya Dowans.

    Awali, serikali iliamua kuziba masikio na kuendelea na mazungumzo ya siri na Dowans kwa ajili ya kutekeleza mpango huo, licha ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kutoa ushauri wa kutoutekeleza mpango huo.

    Kutokana na shinikizo la Kamati hiyo ya Bunge, serikali ilitangaza rasmi kuusitisha mpango huo kwa maelezo kuwa imezingatia maoni ya Bunge.

    Ingawa serikali imetangaza kusitisha uamuzi huo, hata hivyo imesema kuwa hata kama mitambo hiyo imekwisha kutumika, lakini isingekuwa jambo geni kuinunua kwani nchi mbalimbali zinafanya hivyo.

    Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alisema nia ya serikali kutaka kununua mitambo hiyo ilikuwa kukidhi mahitaji ya umeme, ambayo kwa sasa ni makubwa kuliko uwezo wa uzalishaji.

    Ngelaja ambaye mara kadhaa amekuwa mwepesi kukwepa kuzungumzia kwa kina mpango huo kila alipokuwa akibanwa na vyombo vya habari, alisema dharura inayoikabili Tanzania kwa sasa kuhusu upatikanaji umeme haitokani na upungufu wa maji, bali kasi kubwa ya ongezeko la mahitaji ya umeme kwa wastani wa MW 70 kwa mwaka.

    Alisema kadri uchumi unavyokua mahitaji ya umeme nayo yanaongezeka kila mwaka hivyo mitambo hiyo ingeokoa jahazi.

    Alisema serikali haikuchagua kuagiza mitambo mipya nje ya nchi kwa kuwa mchakato huo huchukua muda mrefu na si muafaka katika hali ya dharura.

    ``Mitambo kama ile unapoagiza siyo kwamba inakuwa tayari sokoni, unatoa oda unatengenezewa sasa katika mazingira ya dharura haifai kwa kuwa mchakato kama huo unaweza kuchukua miaka miwili au zaidi,`` alisema Ngeleja na kuongeza:

    ``Mbona watu wananunua ndege na meli zilizokwishatumika, isingekuwa ajabu kwetu kununua mitambo ya Dowans,`` alisisitiza.

    Ngeleja alisema serikali imetafakari maoni ya Kamati ya Bunge na imejiridhisha kwamba ni vyema Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) isishiriki kwenye zabuni ya ununuzi wa mtambo wa Dowans na tayari ilishaliagiza shirika hilo lisishiriki kwenye zabuni hiyo.

    Alisema serikali imeamua kusitisha ununuzi huo ili kuepusha malumbano kati yake na Bunge, hali ambayo alisema ingewachanganya wananchi.

    Serikali ilitaka kuinunua mitambo hiyo kwa Sh. bilioni 70 kutoka Dowans, ambayo ilirithi zabuni tata ya Kampuni hewa ya Richmond ya Marekani, baada ya kushindwa kufua umeme wa dharura.

    Kukiukwa kwa taratibu zilizosababisha kuipa Richmond zabuni hiyo kulisababisha Bunge kuunda Kamati Teule ya kuchunguza mchakato wa zabuni hiyo Septemba mwaka jana, iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe.

    Ripoti ya uchunguzi iliwasilishwa bungeni mapema Februari mwaka huu na kubainisha kukiukwa kwa taratibu na kuwalazimisha mawaziri watatu kujiuzulu.

    Mawaziri hao ni aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, aliyekuwa Waziri wa Madini na Nishati, Nazir Karamagi na aliyekuwa Waziri wa Afrika Mashariki, Dk. Ibrahim Msabaha.

    Ngeleja alisema serikali inatarajia kuanza kuagiza mitambo mipya nje ya nchi ambayo kwa gharama isiyo halisi alikadiria kuwa inaweza kufikia Sh. bilioni 100.

    Alisema Wizara yake ina imani na Kamati ya Bunge na aliishukuru kwa kuitikia wito wa kikao cha dharura kilichoitishwa na wizara yake na kutoa maoni yao kuhusu suala hilo.

    Alisema wizara yake ilifanya mawasiliano na Wizara ya Katiba na Sheria lengo likiwa ni kupata ushauri kama Sheria ya Umeme ya mwaka 2008 inaruhusu Tanesco kushiriki katika ununuzi wa mitambo hiyo iliyokuwa imeletwa katika hali ya dharura.

    Alisema Wizara ya Katiba iliwaruhusu kuingia katika mchakato wa ununuzi wa mitambo hiyo kwa kuzingatia Sheria na taratibu za manunuzi zilizopo.

    Alisema Wizara iliona ni busara kuishirikisha Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ili kushauriana kuhusu suala hilo na ilifanya hivyo kwa nia njema na kwa kutambua umuhimu wa dhana shirikishi kati ya Serikali na Bunge hasa kwenye maamuzi muhimu na nyeti yanayohusu maslahi ya Taifa.

    Ngeleja alisema wizara yake ilimwomba Spika wa Bunge, Samuel Sitta, idhini ya kuitisha kikao cha dharura kati ya Wizara ya Nishati na Madini, Tanesco pamoja na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini.

    Alisema kikao hicho kilifanyika Desemba14, ambapo serikali ilielezea faida za kutaka kuiruhusu Tanesco kununua mitambo ya Dowans.

    Ngeleja alisema kuwepo kwa mitambo ya Dowans ambayo tayari ina uwezo wa kufanyakazi ni fursa muhimu ya kuwezesha kuziba pengo la uhaba wa umeme hivyo ingekuwa vyema serikali ikaliwezesha Tanesco kununua mitambo hiyo.

    Alisema mtambo wa Dowans wenye uwezo wa kuzalisha umeme wa Mw 112.5 ni sawa na mbadala wa umeme wote unaozalishwa na mabwawa ya Mtera (MW 80), (Hale 21) na Nyumba ya Mungu (MW08).

    Ngeleja alitaja faida nyingine kuwa ni kupunguza gharama za kununua umeme kama kampuni binafsi itanunua mitambo hiyo na kuiuzia Tanesco umeme kwa utaratibu wa capacit charge.

    Alisema mitambo ya Dowans ilikuwa inafanya kazi hivyo haihitaji kuunganishwa au kufungwa kama ambavyo ingefanyika kwa mitambo inayoletwa kwa mara ya kwanza.

    Jumatatu wiki hii, Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, William Shellukindo, aliweka mambo yote hadharani mbele ya waandishi wa habari kuwa serikali imefikia uwamuzi wa kununua mitambo hiyo kwa gharama za Sh. bilioni 70.

    Alieleza kuwa kamati yake juzi iliitwa na Ngeleja na kuelezwa uamuzi huo wa serikali na kutakiwa kutoa maoni yake.

    Hata hivyo, Shellukindo alisema kamati yake imeieleza wazi serikali kuwa haikubaliani na uamuzi huo kwa kile alichoeleza kuwa unakwenda kinyume cha Azimio la Bunge ambalo linataka mapendekezo yote yaliyotolewa na Kamati Teule ya Bunge iliyokuwa ikichunguza mchakato wa mkataba wa kampuni ya Richmond ambayo iliuza mitambo hiyo Dowans kwanza yatekelezwe kabla ya kufikiwa uamuzi wowote wa kuinunua mitambo hiyo.

    ``Jumapili kamati iliitwa kwenye kikao cha dharura na Waziri wa Nishati na Madini kuelezwa uamuzi wa serikali kutaka kununua mitambo ya Dowans na tukatakiwa kutoa maoni yetu, sisi kama Wabunge tumekataa kushirikishwa katika uamuzi huo kwa sababu kwanza kanuni za Bunge haziruhusu, jambo lililokwisha pitishwa na Bunge kujadiliwa upya na pili Sheria ya Manunuzi ya Umma hairuhusu serikali kununua vifaa au mitambo chakavu,`` alisema Shellukindo.

    Shelukindo alionyesha kukerwa na uamuzi huo wa serikali, ambao alisema ni dharau kwa Bunge.

    Alifafanua kuwa moja ya mapendekezo yaliyotolewa na Kamati Teule ya Bunge iliyokuwa ikichunguza mkataba wa Richmond ni kutaka watu wote waliohusika kupitisha mkataba huo wachukuliwe hatua za kisheria, lakini kamati yake ikashangazwa kuona kuwa kabla ya hatua hizo kuchukuliwa serikali imechukuwa uamuzi wa kutaka kununua mitambo hiyo iliyoleta matatizo makubwa.

    ``Tulitarajia tumeitwa ili tuelezwe utekelezaji wa maazimio ya Kamati Teule ya Bunge iliyokuwa ikichunguza mkataba wa Richmond na si kuibua tena suala la Dowans, kuihusisha kamati ya Bunge katika maamuzi haya ni kinyume cha taratibu kwa sababu ilishaamuliwa na Bunge kwa hiyo kuridhia itakuwa ni kuleta mgogoro kati ya Bunge na serikali,`` alisema.

    ``Hii ni sawa umemkamata mwizi wa mali yako na baada ya kumkamata mnakaa kuzungumza ili akuuzie mali aliyokuibua,`` alisema.

    Alieleza kuwa kama serikali iliona kuna umuhimu wa kuchukua uamuzi huo, kwanza ilitakiwa kujenga hoja ya msingi badala ya kulifanya jambo hilo kuwa siri na kisha kuwashtukiza wabunge kutaka ushauri wao.

    Mwenyekiti huyo alisema si busara kwa serikali kununua mitambo iliyokwishatumika ambayo alisema ni chakuvu, kwani hata sheria za manunuzi nchini haziruhusu kufanya hivyo.

    SOURCE: Nipashe

    ReplyDelete
  2. Gado muhuni.

    Unaona hapo Waandishi wa Habari wote HAWANA VIATU.

    Kwa hiyo siku hizi watakuwa wanaambiwa wavue viatu waviache nje kwanza KAMA MSIKITINI vile!

    Teheh teh tee

    ReplyDelete
  3. Hiyo ya kuwavua viatu haisaidii. Si watakauwa na Camera, Kalamu, notebooks, labtops, simu, n.k. Zote hizo ni siraha. Cha muhimu tu viongozi wetu hususan marais wasijikusanyie maadui kila mahali mpaka waandishi wa habari. Haya yamkini yanaweza kutokea hata hapa Africa mfano Rais Kibaki akipitisha mswaada unaompa uwezo waziri wa habari kukifungia chombo chochote cha habari wakati wowote nchini Kenya, basi waandishi wa habari kuna siku watamrushia viatu au kamare. Huu ni mfano mdogo tu lakini kuna mingine mingi tu.
    Mdau

    ReplyDelete
  4. anony 4:31pm, orodha inaendelea na miwani, saa, mikanda, funguo, mabegi/vipochi, viti na hata mate. wahenga walisema/waliimba,"bubu hutaka kusema, mambo yanapomzidia".
    iraq mbona mbali, tumeyaona na kuyasikia hapahapa tanzania kwa msafara kutupiwa mawe na mawaziri kuzomewa.

    ReplyDelete
  5. wadau apo list inaendelea;
    mapazia,doormats,glass za juice/maji,sahani watazolia,kofia,penseli,ushungi kumkabia nk
    hahahaaaaaaa
    MICHU KUNA KATUNI MOJA ULIIPOST APA YA MCHORAJI WA KATUNI INAYOONYESHA ZUMA ANABAKA SHERIA (mwanamke) NA UKU WEZIE WAKIMSHIKILIZIA CHINI JAMAA AKIFUNGUA MKANDA,,,aisee CARTOONIST YULE KASHTAKIWA ADAIWA MILLIONS OF MONEY (hii ni BBC news last week ithink)nimeisikia live

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...