JK akimkabidhi kombe Angelaambaye aliibuka kuwa mmoja wa wanafunzi waliofunika katika kula nondozz ya IT wakati wa mahafali ya kwanza ya Chuo Kikuu cha St.Joseph College of Engineering and Technology huko Luguruni, Mbezi, Dar. Kati s Arch-bishop Norbert Mtega wa Arch-Diocese of Songea

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. Wadau wa Bulogu hii haya maneno Ya mheshimiwa katika mahafali haya yamenigusa nikaona niyafikishe kwenu mnisaidie kimawazo mnayaonaje.
    Jamani tuepuke usenene, au lugha za kuchafua bali tuiangalie hoja ya Rais Kuhusu
    1. Ulevi wa Wasomi,
    2. Mikopo na Uwezo wa Serikali
    3. Ushiriki wa wasomi katika shughuli za kiuchumi.(Vikundi,Ubunifu,nk-Kuajiriwa au kujiajiri)

    Mdau Joseph

    Dk.JK awashukia wasomi walevi

    2009-02-15 12:55:22
    Na Abdallah Bawazir

    Rais Jakaya Kikwete amewataka wasomi wanaohitimu masomo ya fani mbalimbali nchini kujiendeleza zaidi kielimu na kuitumia elimu waliyoipata kufanya shughuli za maendeleo, badala ya kujikita katika ulevi.

    Amesema wapo baadhi ya wasomi ambao wanapohitimu masomo yao hujikita kwenye unywaji wa pombe kupita kiasi, kiasi kwamba wanashindwa kutumia vizuri elimu waliyoipata kwa maendeleo yao na taifa.

    Rais Kikwete alisema hayo kwenye Mahafali ya Kwanza ya Chuo cha Uhandisi na Teknolojia cha St. Joseph, wakati akizungumza na wahitimu wa kozi za uhandisi, wazazi na wageni mbalimbali waalikwa, jijini Dar es Salaam jana.

    Aliwaasa wahitimu hao kuacha kuingia katika mkumbo huo wa ulevi, akisema kuwa unywaji wa pombe kupita kiasi umeangamiza wataalamu wengi nchini.

    `Mkitoka hapa mwendelee kusoma na kujifunza zaidi siyo kunywa pombe kupita kiasi, maana staili ya maisha ya wengine bwana inashangaza yaani ili mtu aonekane ana uwezo kila siku jioni anaenda baa au klabu akanywe pombe`.

    ``Mtu akinywa pombe kupita kiasi baada ya siku mbili tatu mikono itaanza kutetemeka, hivi kweli mhandisi utaweza kuchora michoro ya majengo huku mikono inateteneka!, kuna uhandisi tena hapo?`` alihoji Rais Kikwete na kufanya watu waliohudhuria mahafali hayo kuangua kicheko.

    Rais Kikwete pia aliwaasa wahitimu hao kuzingatia maadili ya kazi zao walizosomea watakapoanza kufanyakazi, ili taifa liweze kuwa na wataalamu wa kiwango cha juu.

    ``Tumieni vizuri elimu yenu kwenye shughuli za maendeleo na si tu kwenye ujenzi wa barabara, bali pia kutengeneza vifaa vya kisayansi kama vile kompyuta,`` aliwaambia wahitimu hao wa kozi za uhandisi.

    Katika hotuba yake, Rais Kikwete, pia alizungumzia malalamiko ya baadhi ya wasomi wa vyuo vya elimu ya juu ambao wanaitaka serikali itoe mikopo kwa asilimia mia kwa wanafunzi wote tofauti na utaratibu wa sasa wa kuwagawa katika madaraja.

    Alirudia kauli yake kuwa serikali kwa sasa haina uwezo wa kutoa mikopo hiyo kwa asilimia 100 kwa wanafunzi wote, kwani uwezo wake wa kifedha bado ni mdogo.

    Hata hivyo, alisema serikali itaendelea kutoa mikopo kwa utaratibu wa sasa lakini kwa misingi ya haki bila ya kumuonea mtu.

    ``Hatutaki mtu apendelewe wala kuonewa katika upataji wa elimu nchini,`` alisisitiza.

    Alitoa wito kwa taasisi za fedha nchini kuanzisha utaratibu wa kutoa mikopo ya elimu ya juu ili kusaidia wanafunzi wanaohitaji.

    ``Naziomba taasisi za fedha nchini zitoe mikopo ya elimu na huu utakuwa msaada mkubwa kwa serikali kwani kwa sasa haiwezi kutoa mikopo kwa asilimia mia moja,`` alisema.

    Rais Kikwete pia aliwataka wahitimu wa fani mbalimbali nchini kujiunga katika vikundi kulingana na fani zao na kisha kuanzisha shughuli inayoendana na elimu waliyosomea ili serikali iweze kuwasaidia kijendeleza.

    ``Mara nyingi tumekuwa tukitoa wito kwa wasomi kujiunga katika vikundi na kuanzisha shughuli walizosomea lakini mpaka sasa hakuna muitikio, sasa ninawaomba nyinyi msituangushe, muwe mfano,`` aliwaasa wahimu hao.

    Awali, Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Methodus Kilaini, alitoa pongezi kwa Rais Kikwete, kuwa katika kipindi cha miaka minne aliyokaa madarakani, uongozi wake umetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya elimu nchini.

    ``Katika kipindi cha miaka minne ya urais wako, moja ya michango mikubwa uliyotoa ambao utakufanya uendelee kukumbukwa katika historia ya Tanzania ni kuendeleza elimu, Chuo Kikuu cha Dodoma kitabaki kuwa kumbukumbu ya utawala wako na utaratibu wa utoaji mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu vya umma na binafsi ni mfano wa kipekee katika nchi zote za Afrika Mashariki``, alisema Askofu Kilaini.

    Hata hivyo, alitoa changamoto kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini kuboresha utaratibu wa kutoa mikopo hiyo ili wanafunzi wote wanaostahili hasa masikini wapate mikopo hiyo bila ya matatizo.

    Akizungumza kwenye mahafali hayo, Mwenyekiti wa chuo hicho, Mchungaji Arul Raj, alisema jumla ya wahimu 126 wamehitimu fani mbalimbali za uhandisi na kati yao 80 walitunukiwa cheti ngazi ya shahada na 46 stashahada.

    ReplyDelete
  2. Hahaha,tungi muhimu bwana alimuradi usipate summary dismisal tu kwa job..
    Tatizo ukimaliza chuo baada ya kitabu kigumu unasema ngoja nivute mama niweke ndani,balaa linakuja kama mama mwenyewe asiwe yule uliekua ukimfikiria akili mwako, mwisho unaishia kuikimbia nyumba na kuona kwamba bar ndio tulizo lako.
    Hapo ndio mwanzo wa kupenda tungi, ukifika nyumbani unalala tu hata kelele huzisikii,asubuhi kazini jioni kama kawa pale pale break point! na wewe unajifanya papaa

    ReplyDelete
  3. ilipendeza sana kwa kweli..hongereni sana kwa kitabu kile cha wahindi?kweli mmefanya kazi jamani Mungu awajalie mpate kazi mliohitimu

    ReplyDelete
  4. Prezidaa tungi ni muhimu ... mi nina tatizo la asthma nisipokunywa pombe basi lazima ninywe dawa kabla ya kulala vinginevyo lazima mishale ya saa nane-tisa usiku niamke kuugulia kifua kinabana ...
    Lakini nikinywa beer(bia) nalala mpaka asubuhi bila kuumwa katikati ya usiku hivyo kwangu mimi tungi inaniepusha na matatumizi ya dawa kila siku.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...