Mwibaji na watwana, mlifi ni mwungwana
(sehemu ya kwanza)

Hizi lawama tutatupiana mpaka lini? Umahiri wa kusemana umekuwa ndiyo utamuduni wetu sasa na haswa kwenye duru la siasa. Baya zaidi hakuna yeyote kati ya hawa wasemaji anakuwa muelimishaji, bali, anakuwa mkosoaji ama mlalamikaji ambaye huongeza na kurudia kauli mbiu “Nchi itafikia ama inaelekea pahali pabaya”, ama kweli sumu ya neno ni neno.

Mara zote panapotokea jambo ambalo linahitaji marekebisho ama mtazamo chanya wa kuboresha hilo jambo, basi ada ya mja ni kunena na siyo kulaumu, kukashifu, ama kudhalilisha na kuwafanya wengine waonekane si bora na labda wapo kwenye nyadhifa walizokabidhiwa na umma kimakosa!!! Kamwe huu si uungwana!!! Ninaandika haya makala kwa makusudi ya kulenga na kukemea tabia mpya ambayo imejitokeza hivi karibuni ya “malumbano bayana” kwa staili ya kuwaita waandishi wa habari ama kuitishia kongamano - na hili linajiri hasa kwa viongozi wa juu wa serikali waliyopo madarakani na wale ambao kwa nyakati fulani walikuwa viongozi katika serikali hii hii.

Kwa matatizo ya kisiasa na kiuchumi ambayo yanamgusa kila mtanzania hayana haja ya yote haya bali zaidi yanahitaji kutafutiwa ufumbuzi na siyo malumbano ambayo mara nyingine watu wameyafananiisha na mtindo maarufu wa nyimbo za mafumbo yaani “Taarab”. Sasa haya mafumbo tumamfumbia nani wakati watanzania takriban wote hivi sasa ni waerevu!!! Kw kurudia lugha yeti ya mtaani ningesema huu si wakati wa “longolongo” kinachotakiwa na kuyanusuru maisha ya watanzania wengi ambao mpaka leo hii wanasuasua katika kujikimu ki-maisha.

Uongozi wa aina yeyote ile huwa mgumu, na siku zote hapatakuwa na asilimia 100 ya makubaliano ama kutokubaliana kwa maamuzi katika uongozi. Hayumkiniki kukubali kwamba yale ya makubaliano ndiyo yenye mafanikio na yasiyo makubaliano ndiyo mapungufu. Awamu zote tatu za Serikali ya Muungano, Tanzania, zilitenda mema mengi na mapungufu hayakukosekana. Sasa bado tungali kwenye awamu ya nne ambayo bado ipo madarakani na kwa hakika nayo ipo katika mchanganuo huo huo wa kuyatazma mema ambayo imetenda na mapungufu yanayojitokeza. Ni ukweli usiyopingika kwamba awamu zote hizi nne zimekuwa na madhumuni ya makusudi ya kuendeleza na kufanya mambo mema kabisa kwa ajili ya wananchi wake maana awamu zote hizi na wananchi wake hawana desturi ama tabia ya kujipaa makaa wenyewe kama pweza.

Katika makala haya nisingependa nami nijitiye katika umahiri wa kusema na kuwa sawa na hao wasemaji wengi ambao sasa ndiyo wamekuwa vichwa vya habari na wahamasishaji wa habari kwa kutenga muda na kuwaita waandishi wa habari wasikilize yaliyotangia mawazoni mwao kana kwamba ni jambo geni na jipya kusikika na dhahiri wanakuwa mithili ya bata akili kwa watoto, ilihali wakijuwa wazi kabisa linalojiri ni yarabi nafsi yangu – (ubinafsi). Kama kweli tunakubali na kusema kwamba penye wazee haliharibiki neno, basi nina hakika kwamba bado tuna wazee ndani ya uongozi na hata nje ya uongozi sasa lipi linaloshindikana kuweza weka mambo sahihi? Kusema tu isitoshe maana tonga si sawa na tui na si kila mwenye makucha huwa simba. La muhimu zaidi ambalo ndiyo pungufu kwetu sisi watanzania ni UZALENDO!! Ni kweli upo UZALENDO lakini si UZALENDO wa tamaa ya kuwa na maendeleo ya kiujumla kiuchumi na kisiasa na mara zote painamapo ndipo painukapo.

Ukitazama kwa uyakinifu katika mambo yote ambayo yanaleta malumbano bayana, utaona kwamba kubwa zaidi linaloelekezwa kwetu sisi wananchi ni katiak kuambiwa kwamba serikali iliyopo madarakani ina matatiozo ya uongozi na ndiyo maana ya matatizo mengi ambayo yamejiri katika nchi hivi sasa.

Hakika, kila awamu ya serikali ilikuwa na mambo yake ambayo yalitukuzwa na kuonekana bora nay ale ambayo yalekebehi ni kuonekana si bora. Inahitaji muda mrefu kuandika makala ambayo ingechambua awamu za serikali zote zilizopita mpaka kufika sasa, lakini kwa makusudi y aujumbe wa makala hii nitarahisisha kwa mifano michache ambayo yote ikiashiria namna gain demokrasia ilivyo ongeza wigo wa uhuru kwetu sisi watanzania.

Ilikuwa si jambo rahisi katika awamu ya serikali ya kwanza ya kizalendo Tanzania watu kusema lolote lile ambalo lingeonekana kama ni jambo kinyume na uongozi wa wakati ule na yeyote yule aliyethubutu kufanya amd kusema kinyume basi aliitwa “Muhaini” na adhabu yake ilikuwa kutiwa kuzuizini na wlae ambao walikuwa na uwezo kidogo waliponyoka kwenye adha hii na kukimbilia kusihi nje ya nchi ama hata nje ya bara la Africa. Watu hawa ambao walikimbia nje walitengenezewa mazingira ambayo yaliwaweka pahala pagumu hata kujitetea maana tukingali wadogo nyakati zile tulifundishwa hat anyimbo za kuimba za kuwadhalilisha hawa “mahaini” na hata kufikia kusema kama atatokea basi “mchinje”!!!! Na hizi hasa ndzio zilikuwa mbinu za propaganda za kisiasa wakati huo ambazo kwlei zilifana na hasa kwa matumizi ya vyombo vya habari na njia zote za mawasiliano ambazo zilikuwa zote zipo mikononi mwa serikali tawala.

Awamu hii ilipita na tukaona hata wale “wahaini” na waliyokuwa kizuizini wamerudi na wakaingia tena katika duru la siasa ambapo hawakufua dafu maana tayari walikuwa wamechoka sana ama kwa umri ama maradhi ama taabu zingine zozote za kutokuwa karibu na jumuiya ambayo wangependa kuchangia japo kidogo walichokuwa nacho!!! Haya yote yalikuwa ni mateso na bugudha ambazo baadhi ya watu walizipata kutoka kwenye serikali ya kipindi hicho, na hata waliporejea hapakuwa na kushitakiwa ama kusukumwa sukumwa tena maana tayari walikuwa wanaonekana tofauti ndani ya jamii ambayo waliipoteza takriban zaidi ya miaka ishirini na zaidi!!.

Demokrasia ikwa kidogo sasa inapenya baada ya ruhusa ya kuwaingiza “wahaini” na kuwafutia makosa wale waliyotiwa kizuizini kwa kutofautiana na uongozi wa juu wa serikali ya kipindi hicho.

Awamu ya pili ikafungua ukurasa mpya ambao ulikuja kuzaa uhuru wa biashara na kuweka na uwezo mwingi tu wa baadhi ya wananchi kujiweka pahala panono ki mapato, jambo ambalo lili zaa kauli mbio “RUKSA”. Kweli baadhi ya wananchi wakapat “ruksa” ya kuwa matajiri na hata wawekezaji ama wabia. Ilikuwa furaha isiyo kifani na hapa ndipo utajiri uliyo zaa ubinafsi ulipoanzia.

Ikumbukwe kwamba hii awamu ya pili nayo iliingia na staili yake ya uongozi na viongozi ambao walikuwa ndiyo chaguo la awamu hiyo.

Ndipo hapa tulipoanza kuwa na kipima joto cha uongozi maana sasa tunalo jingine la kufananisha. Mambo mengi yakasemwa kuhusu awamu ya kwanza na ugumu wa maisha ambao ulionekana kuwepo katika serikali ya awamu ya kwanza, sasa tumepewa “RUKSA” hivyo ilikuwa ni umahiri wako wewe mwananchi kwamba ni kiasi gani unaweza “kujichanganya”, “Bongo” imezaliwa.


Awamu ya pili ikapita kwa vishindo na visa vingi tuu na hata pakatokea kwamba uongozi wa awamu ya mwanzo kuwa na “malumbano bayana pekee” ninaposema malumbano bayana pekee nina maananisha kwamba haya malumbano yaliweza kutolewa upande mmoja tuu na upande ambao unashambuliwa ulikuwa butu kujibu haya labda kwa hofu ile ya kwamba unaweza kuwekwa “kizuizini” ama kuitwa “muhaini”, maana bado uongozi wa awamu ya kwanza ulikuwa bado na wafuasi wake wngi ambao bado walikuwa watendaji sehemu nyeti za serikali ya awamu ya pili!!!! Lakini pakatokea njia na namna ya kuwaopunguzia makali hawa viongozi waliyokuja toka awamu ya mwanzo nayo ilikuwa ni kuyabatilisha baadhi ya maamuzi na maazimo muhimu yaliyopitishwa awamu ya mwanzo.!!!!

Awamu hii ya pili tulisikia watu wakibezwa kuendesha nchi kwa kuwasikiliza wake zao na wengine waliitwa “wahuni” basi ili mradi kuna jambo la kukosoa lilipenyeza, nab ado watu wakastahimili na kukaa kimya bila ya majibu na mambo yakawa swhari maana ilikuwa “RUKSA”.

usikose kesho (inshaallah panapo majaaliwa) sehemu ya pili na ya mwisho ya hoja nya haja hii



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 14 mpaka sasa

  1. Kutokana na uliyokwisha kuongea tayari naweza kuhisi unaelekea wapi no problem na kwa vile naona bado unashuka vizuri tu nakusubiri sana kesho nione utakavyomalizia and then nita-comment.

    Thanks brother!

    ReplyDelete
  2. Mimi kutokana na ulivyoanza tayari nishajua unataka kumaliziaje,hivyo naona niongee na ya kesho hapa hapa kwa kutumia aya yako ya kwanza na pili:
    KWAMBA, nakushukuru kwa Kiswahili japo kina misamiati mingi isiyolingana na wakati, na wenda wewe huendi na wakati ndio maana unataka kutunyamazisha.

    NDIYO, unataka kutunyamazisha bila kujua huwezi kwa umenena bila ama kukosoa, kushukuru, kutukana n.k. Huko pia ni kunena... Kumradhi, ni heri kunena hata kwa kutukana ilimradi una sababu kuliko kukaa kimya...

    KWAMBA, ukiishi maisha kwa kufanya makosa ni bora kuliko ukiishi bila kufanya chochote! Yani hata nchi ikiporwa ukae kimya kwa kuogopa utaitwa mlalamishi? Aka!

    ETI, hata ukiona mambo ya MEREMETA, Twin Towers za BOT, EPA, TANESCO na kashfa nyingine nyingi zinakuwa kimya kimya usipaze sauti kuchokonoa kujua kunani? Yaani hata usihimize vyuo na mitaala ya elimu itilie mkazo kwenye kilimo ili dhana ya 'kilimo kwanza' iwe endelevu... ebo! Wewe vipi, au umetumwa!

    Hatudanganyiki

    Chaster

    ReplyDelete
  3. Swadakta, au tawire kwa asili yetu waafrika, mwandishi umenena, na mpaka hapo ujumbe tayari umefika ingawa bado hujamaliza.

    Tatizo wao wanafikiri sisi wananchi hatuelewi kinachoendelea, tunawaelewa sana na tulijifunza mengi sana wakati wa awamu ya pili, na hata awamu ya tatu tuliona hali ilivyobadilika kutoka kupeana lawama na kuhamia kupeana misifa, huku uchumi ukiteketea na watu wakijilimbikizia mimali. Lakini hao hao wanaopiga kelele leo wakati mambo yakiharibika awamu ya tau walikuwa kimya kama waliomeza vyura midomoni. Sasa sijui kwa sababu walikuwa wanaogopa kuitwa wahaini au sijui kwa sababu gani, maana usisahau wengine mpaka walivuliwa uraia wao ikabaki kidogo tu wafukuzwe. Sasa vile vyura vimetemwa, labda amekuja mtu ambaye tuseme tuwe wazi sasa tumeshachoka na kelele zao kwa kuwa wanafanana dini zao basi kelele zimekuwa nyingi. Hakuna haja ya kufichana sasa tunaweka mambo wazi angekuwa JK ni mkristo usingesikia makelele yote hayo hata kama angekuwa anahujumu nchi wazi wazi, lakini kwa kuwa ni muislam basi kila atakalolifanya kwao ni baya! Kwani yeye ni second rate citizen hana haki ya kuwa Rais, ingawa watanzania wote bila kujali dini zao walimchagu awe Rais wao lakini kundi hilo unalolisema limegubikwa na udini mkubwa! Tushawachoka sasa wanyamaze tu kimya, yao yamekwishapita wakae chini watulie. Hatukatai critism lakini iwe fair critisicm sio hiyo ya kwao naweza sema ni ya KITOTO!

    Natambua wana wafuasi wengi wenye mtazamo kama wao lakini hilo pia nalo kwa sasa halitutishi maana mbwa ukishamjua jina hakupi shida! Wataloloma humu, watatukana humu, lakini katu kwetu haitupi shida, kwani tunawatambua shida yao ni nini.

    Mswahili

    ReplyDelete
  4. naungana na mdau hapo juu,huyu alivyoongea tu anaonyesha anakwenda wapi na ana msimano gani,na mimi namsubiri amalize tutoe maoni kamili

    ReplyDelete
  5. Ndugu mzalendo uko sahihi kabisa katika hoja yako kwamba
    "Awamu zote tatu za Serikali ya Muungano, Tanzania, zilitenda mema mengi na mapungufu hayakukosekana." Wakati huo huo hatuna budi tukumbuke kuwa dhana ya 'awamu' ni mazingira tofauti ya kisiasa, kijamii, na hata kiuchumi na kila awamu inakabiliwa na changamoto tofauti na awamu zilizotangulia. Pia tunatarajia ubora zaidi kadiri tunavyotoka awamu moja kwenda nyingine.
    Watu wanaokabidhiwa madaraka ya kutawala huwa wanaomba wenyewe na tunawalipa vizuri sana (hawajitolei) ili watende mema (sio mapungufu). Ni kweli kila awamu imetenda mema na mapungufu. Walipa kodi wana haki ya kuwapongeza wanapotenda mema (ndio maana wanalipwa vizuri) na hali kadhalika wana haki ya kuwalaumu na kuwanyooshea kidole wanapovurunda. Mapungufu yaliyotendwa awamu iliyotangulia hayalalishi mapungufu ya awamu iliyopo! Kwa hiyo basi kila awamu inapimwa kwa kiasi gani imefanikiwa kuweka mazingira bora ya kuwatoa watanzania wote katika dimbwi la ufukara!

    ReplyDelete
  6. Muungwana tumia hata 'pseudo-name' ili tuweze kufuatilia hoja zako kama vile pweza anavyoji fumbata na kaa la moto.
    Mdau
    Mgeninani DSM

    ReplyDelete
  7. Watanzania, bwana. Eti maandamano ya kuunga mkono. Nadhani hawa ndo JK mwenyewe alisema 70% wanaofuata upepo tu. Yaani Rais akijamba wanaandama kumuunga mkono kwa kujamba. Asipojamba pia wataandama kumuunga mkono kwa kutokujamba. Haya mambo yamepitwa na wkt. Na Mwalimu mwenyewe ndiye alikuwa mkosoaji namba 1. Alimkosoa Mzee Mwinyi wazi wazi. Akawaita Malecela na Kolimba wahuni. Akawatungia na kitabu. Leo eti yanayosemwa na Mwalimu Nyerere Foundation yanaitwa wivu. Nchi hii labda aje Yesu Kristo ndio itakombolewa. Binadamu tu hawezi. Watu wanaokombolewa ni wale wanaojua kuwa wanahitaji ukombozi. Tatizo la Wabongo hawajui kama wanahitaji ukombozi au la! hao ndio kuna kazi.

    ReplyDelete
  8. Rais anayeweza kubadili au kuzamisha maisha yetu ni huyu wa sasa. Yule mwaka 80, 90, au 2000 hawezi kutusadia sasa. Na hata kama yule wa miaka hiyo alifanya makosa, huyu wa sasa hawezi kutimia makosa ya 80 au 90 kutetea makosa ya sasa. Two wrongs do not make a right! Watanzania tuamke sasa.

    ReplyDelete
  9. We mswahili kweli u mswahili. 'Mwehu' Salim Ahmed Salim ni mkristu? Badilisha mindset yako ndio utaweza kuona ukweli, vinginevyo utakalia hilo giza!

    ReplyDelete
  10. Ninyi mnaotetea uovu pia nanyi ni waovu. Kumbukeni demokrasia ya sasa ni tofauti na demokrasia ya nyakati na awamu zilizopita. Mh. Rais anastahili kupewa hayo yanayoitwa ni wivu kwani huo ni wivu chanya unaomuamsha ili aendelee kufanya vizuri zaidi. Nchi hii inaendeshwa kwa misingi ya iliyoridhiwa ya uongozi bora yaani uongozi unaozingatia sheria, uwazi, uwajibikaji n.k.
    Nami namshangaa Rais wetu kujiingiza ktk makundi ya waswahili kusikiliza umbea wa kwamba ati akina fulani wanasema hivi na vile. Kwa kuwa akina fulani si kundi lake basi Mh. naye anaweka kisasi. Ni vyema Rais akasikiliza hoja zao, na hoja hizo yawezekana kabisa ndizo kilio cha wengi.Hivyo hawa ni watu wa msaada kwako sio wa kukudhalilisha.
    Nakubali kuwa mh. amekuwa akijitahidi kutoa ahadi za kushughulikia kero za wananchi, sasa ni muda mwafuaka kuona juhudi hizo zinazaa matunda, tuone kesi moja baada ya nyingine inahukumiwa, lawama za kutowajika na upendeleo usio na tija unapungua n.k. Na kuhitimisha Rais usiwe kama MBWA KIBOGOYO unaishia kubweka tuu hung'ati!!!!. Ushauri wa BURE siku hizi kuna teknohama tumia nafasi ya maendeleo ya Teknologia na MANO UTAPATA.

    ReplyDelete
  11. Kuhalalisha mapungufu ya sasa kwa kutumia mapungufu ya awamu ya 1, 2 na ya 3 ni kuwatania Watanzania. Kwa hiyo kwa sababu Nyerere nk nk walikuwa na mapungufu, basi Marais watakaokuja waendeleze tu mapungufu mpaka mwisho wa dunia? Hebu tuache utani sasa. Tuondoe ufisadi tujenge nchi. Aliyekutuma haitakii Tanzania mema. Hatuwezi kuwa nchi ya "Ndiyo Mzee" tena.

    ReplyDelete
  12. ok tunasubiri umalize iyo kesho
    tujibu kiakili zaidi,sawa???

    ole wako michu ubane comments zetu,sii umeruhusu huu mjadala?tunataka tuone mwanga wa jua tunapopeana AKILI umu ndani thr this article

    sawa??

    ReplyDelete
  13. Watanzania bwan wale watu waiokuwa wkijita ma G5 sijui six si wale waliopewa madraka waka jilimbikizia mali na leo wapo mahakamani kwa kutumia madaraka yao vibaya, kuiba pesa mali zaserikali na kiajili kwa memo... sasa mtanzania ukikaa kimya nani atasema haya?? semeni watanzania hadi machafu yote yaishe. Rais aliyepo ndo anayweza kurekebisha makosa yote yake na yawenzake.
    Mwanzilishi wa mada hii ni kada katumwa huyo..

    Idumu siasa ya azimio la Arusha!

    The 2015 Minister of Science and Technology

    usiniweke kapuni wewe jamaa wa nanihii...

    ReplyDelete
  14. Nakubaliana na wewe "Chaster"
    HATUDANGANYIKI!!!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...