Mwibaji na watwana, mlifi ni mwungwana
(sehemu ya pili na ya mwisho)
Ilipopita awamu ya pili ikajiri awamu ya tatu (Awamu kati). Hii kwa hakika ilikuwa awamu ambayo iliingia katikati na kuyaangalia mapungufu na mafanikio ya awamu ya kwanza na awamu ya pili.
Awamu hii ikarudia pale pale kwenye awamu ya kwanza kuhusu swala la demokrasia, na kwamba viongozi wake wakawa wakali kwamba wanataka kurudisha tabia ile ile ya kuogopa watu wasisemeseme hovyo. Hakika viongozi wa awamu ta tatu walikuwa wakali sana na wakatengeza uga ambao ilikuwa si rahisi tu kupenyeza rupia hata penye udhia.

Awamu hii ilisheheni sifa za kujenga uchumi na kwamba pato la taifa likawa limedhibitiwa na ule uholela baada ya “RUKSA” haukuwepo tena, na zaidi ubinafsi sasa ukarudi na kujilimbikiza kwa hao viongozi wa awamu ya tatu. Kauli mbio hapa ilikuwa na “Uongozi Bora”. Hakika ulikuwa uongozi bora maana matokeo yake yalikuwa kwamba baadhi ya viongozi walikuwa bora haswaa katika kujizatiti ki-uchumi na kimaendeleo binafsi na siyo kwa kila mwananchi!.

Mengi yamesemwa na bado yataendelea kusemwa kuhusu maazimio yenye madhumini endelezi ya awamu zote tatu na hapatakosa kujiri kasoro zake ambazo baadhi nimezigusia hapo juu.

Haya sasa tupo kwenye awamu ya nne ambayo ilipokelewa kwa vishindo, shangwe na nderemo nah ii kweli iliingia kwa staili yake tofauti kabisa na awamu zote japo ikizingatia kabisa misingi muhimu iliyowekwa na awamu zote ambazo zilizopita. Hapa tukapata utawala wa kwanza kabisa wa uongozi wote wa juu kuwa na safu kubwa ya vijana ambayo wengi waliitafsiri kwa lugha ya kigeni “boys to men”. Hakika pailikuwa na faraja kubwa na hasa kwa vijana ambao ndiyo tumaini kubwa la maendeleo yeyote katika nchi yeyote.

Hapa pakatokea demokrasia ya uga mpana kabisa kwamba unaweza kusme chochote na hata jambo ambalo si zuri kulisema kwa kumtaja kiongozi yeyote yule wa kitaifa na bado hutafanywa lolote kama vile kupelekwa kuzuizini ama kuitwa muhaini.

Sasa ni hili ndilo limezaa yote haya ya watu kutumia vinywa vyao kusema yanayowakera binafsi na kuyafanya ya kitaifa, kujenga tabaka za makundi ya wafuasi wa kisiasa na mpaka kufikia kuleta makundi ambayo sasa ndiyo yamekuwa maarufu ndani ya serikali na vyama vyao vya kisiasa na hata mpaka kwenye dini!!!! Hakika chombo kinawenda mrama hapa!!!

Nani alisema kwamba unapokuwa na uhuru wa kusema basi unasimama kwenye majukwaa na kuanza kukashifu na kubeza viongozi wa kitafia eti tu kwa sababu nawe ulikuwa kiongozi wa nyadhifa fulani katika awamu zilizopita?
Mbona wapo ambao walikuwa na hata nyadhifa kubwa tu wamekaa kimya na ndiyo sasa wanatumika kama wapatanishi wa malumbano haya!!! Kwa nini hizi taasisi ambazo zina majina makubwa zisijitenge ili kujitofautisha na “taasisi shutumu” badala ya kuleta maneno ama makongamano ya kushutumu, kukashifu na kudhalilisha viongozi ziungane na waungwana ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuleta suluhu ya matatizo yanayojiri nchi yetu kisiasa na kiuchumi??
Bado ninadirki kusema serikali ya awamu ya nne ni shujaa maana imefungua milango yote ya uhuru na mpaka baadhi ya watu wanadirki sasa kufanya mashambulio ambayo dhahiri yanaonyesha kulenga mtu binafsi??? Kweli tumefikia hapo bila ya kujijua ama kwa makusudi?????


Tanzania, Tanzania, Nakupenda kwa moyo wote!!!!!!!!!!!!!!!!!!!

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 14 mpaka sasa

  1. ndugu yangu utakufa vibaya sikutishi ila pile inaelekea kuna aliyekutuma usifie uongozi wa amu ya tatu kwa akili yako unafikiri bado watanzania ni wajingaga kiasi hicho?kwa kifupi la hasha ndugu labda ujipange uje kivingine maana hii hailete maana yeyote ni pumba tupu. Japo ni mtazamo wako.

    ReplyDelete
  2. anaonekana alikuwa na kiu akakosa maji safi ya kunywa ikamlazimu kunywa maji ya chooni...inasikitisha kuona bado jamii yetu ina vibaraka kama hawa wanaotumwa na kununuliwa na wanaoudidimiza uchumi wa nchi yetu,huyu keshadaka posho yake anakuja kutumwagia pumba zake tu hapa na mwenye blogu nae sijui inakuwa vipi hadi anawapa nafasi watu kama hawa...yaani inakera inaudhi na inasikitisha natamani ningeiona sura yake huyu mwandishi ili nikimuona nimkalie mbali kama ukoma vile..hawa ndio watu wanaotakiwa kutokomezwa kwenye hii jamii yetu kwa nguvu zote kama kweli tumedhamiria kupambana na umaskini kwadhati kabisa.awamu hii ya nne ndio awamu iliojaa ubabaishaji kuliko awamu zoooote zilizowahi kutokea ya 3 na ya 4 ni ovyoo kabisa i hope hazitatokea tena awamu za ovyo kama hizi tanzania..

    ReplyDelete
  3. Duuh!! anon wa 11:40 AM naona umichemsha maana hapakusifiwa kwa mazuri hiyo awamu ya tatu .. pale kuna lugha mbaya kwamba hawa jamaa walikuwa "bora" kwa kujilimbikizia mali wao wenyewe.. yanasemwa na yameonekana bado tu kufikishwa kwa PILATO

    ReplyDelete
  4. Mambo unauma na kupuliza kama panya. Umeanza vizuri tu kupinga malumbano ya kukusoa tu, lakini mwisho umeshia kuisifu serikali ya awamu ya nne. Kwa kufanya hivyo unaonekana na wewe ni mtu wa malumbano tu.

    Kumbuka lakini siasi ni malumbano. Kwa hiyo kama utakuwa unakemea malumbano kwenye siasi basi utakuwa unakosea.

    ReplyDelete
  5. MBONA UMEZUNGUKA SANA NDUGU YANGU.

    KWA KUFUPISHA KABISA UNACHOKISEMA NI KWAMBA - AWAMU YA NNE IMETOA UHURU MKUBWA WA WATU KUJIELEZA NA KWAMBA SASA UHURU HUO UNATUMIWA VIBAYA.

    UMETUMWA NINI??

    SASA MBONA WEWE NDIYO UNATAKA TENA KUTURUDISHA HUKO KWENYE AWAMU YA KWANZA AMBAYO TAYARI UMEDAI ILIBANA UHURU WA WATU KUJIELEZA.

    HUELEWEKI.

    ReplyDelete
  6. Ndugu watanzania, kuweni makini na watu wa namna hii wanaokuja kwa mbwembwe nyingi za kuhalalosha maovu eti kwa sababu tu ni maoni yake. Haiingii akilini mtu huyu amesema halaumu mtu kisha anamalizia kwa kutupia taasisi ya mwalimu nyerere lawama eti inafanya kazi za kukosoa, ukome kabisa watanzania wa ndiyo mzee hazipo tena, unasema uongozi wa vijana wapi au kingunge, mramba, mungai na wengineo? hayo unayosifia kuwa ni uongozi wa vijana umeletwa baada ya hayo matunda ya kukosoana baada ya kutaka kulipa fadhila kwa wanamtandao,
    Mimi nadhani mwandishi wa makala hii unatakiwa kupewa miwani ya kuona karibu kwani una matatizo ya kutona karibu maana umeyaona vizuri sana ya mbali yaani ya awamu zote tangulizi lakini , awamu hii aidha umezeeka ama miwani yako imepungua nguvu.
    WATANZANIA JIHADHALINI NA WATU KAMA HAWA HANA TOFAUTI NA MAKAMBA

    ReplyDelete
  7. Mambo mengine yanatia kinyaa. Ndio maana unaficha jina lako.

    ReplyDelete
  8. Wewe Anon wa dec 18, 11:40:00 AM naona hiyo mada imekuuma maskini. Huyu katumia uhuru wake wa kutathmini awamu zote 4. Wewe badala ya kumsuta--japo nawe watumia uhuru wako- ungeleta hoja tofauti na yake baasi!! Lakini inaelekea umejaa hamaki hata kufikiri na kuchambua huwezi. Mimi nakubaliana naye kuwa awamu ya JK ni tofauti na hizo nyingine in form and content as well as character. Tofauti lazima iwepo kwa sababu jamii na serikali yenyewe kama vile maisha yalivyo is never static. Jamii by nature ni dynamic that is to say it is always in a state of mobility qualitatively wise. Enzi ya Awamu ya kwanza na ya pili tulikuwa bado enzi ya ujima na ujinga kiteknolojia na kisayansi. Enzi ya Awamu ya tatu na nne sisi ni sehemu ya utandawazi na ukweli na uwazi. Japo tofauti ni superlatively. Maana yangu Mkapa alihubiri zaidi hiyo sera lakini JK anaitekeleza kiujasiri. Mimi nampa thums up JK. Mwacheni amalize awamu zake mpaka 2015. Waje na wengine nao waendelee na yao.

    Kwa hiyo ndugu yangu acha ushabiki wa Kiyanga na Simba hapa. Be sensible in your arguments and discussion please.

    ReplyDelete
  9. Ukweli unauma, nawe umesema ukweli, subiri watakaoumwa na huu ukweli watakavyokurushia madongo kama vile yale yote yanayosemwa na hao wenye taasisi ni sehemu ya msahafu. Hili halikuanza leo ndugu yangu, limeanza miaka dahari, na bado watu hawauoni ukweli bali wamegubikwa na udini na ukabila na upuuzi wowote wanaoweza kufikiria. Kuwa wao ni mabwana na wengine ni watwana. Hata useme nini huwezi itoa hiyo sumu ndani ya nafsi zao ilishasemwa wazi kuwa "Hawatakupendeni hao mpaka mfuate mila zao" Sasa washangaa nini?

    Weye subiri tu humu wanaoumwa na ukweli uliusema jinsi ambavyo wataacha mada na kuanza kukujadili wewe! Na utawajua tu huyu ni nani na nani kwa maneni yao!

    Mswahili

    ReplyDelete
  10. mie nimesoma mistari miwili tu,nikaona huyu anapotezea wanaume muda tu.wewe kama mafisadi wamekutuma utakufa kifo kibaya sana,laana tupu.

    ReplyDelete
  11. Pumba tupu! Kama alivyosema Anyonymous hapo juu.

    ReplyDelete
  12. Hii nakala si pumba. Ina maana na mwandishi wake aheshimiwe vilevile. Vijana siku hizi wakienda shule kidogo tu basi ndio jeuri inazidi utafikiri ndio nini. Watu jeuri kama huyu anony wa 11.40am watakapopata nyadhifa serikalini ndio huwa wala rushwa na madikteta wasioheshimu raia. Kuenda shule sio uje utukane watu. Hongera mwandishi kwa kutoa maoni yako. Hawawezi kukujibu hawa. Wanaishia matusi na kashfa tu.

    ReplyDelete
  13. Muandishi wa habari hii anawakilisha mtazamo ambao unakataa maongezi.

    Kwanza muandishi uelewe kwamba awamu zote nne ni tofauti sana kwasababu moja kubwa: Muda haujasimama, maendeleo/matukio ya kisiasa na ya kijamii ni dynamic processes. Mengi yaliyotokea ndani ya nchi yetu hayakusababishwa na sisi wenyewe au viongozi wetu, yalisababishwa na misukumo mikubwa ya kimataifa ambayo viongozi wetu mara nyingi hawakuwa na uwezo wa kufanya lolote.

    Katika viongozi wote, Nyerere ndiye alipambana na nguvu za nje zaidi kuliko wote, na ndiye ambaye kusema ukweli alijua tunataka kwenda wapi na alijitahidi kivitendo kufanya hivyo. Alifanikiwa kiasi gani hilo ni swala jingine.

    Wakati wa Awamu ya kwanza tulikuwa ndio tumepata uhuru. Wasomi walikuwa wa kuhesabu, kulikuwa na vita baridi duniani, na huku Afrika ikafikia wengine kama Lumbumba na Nkhrumah wakapoteza maisha. Waliobaki ilibidi either uwe kama Nyerere au Mobutu! Sidhani kama unatamani kwenda kuishi Congo.

    Watu kama Nyerere ilibidi wafanye kazi ya ziada kuzuia kuwepo ndani ya nchi watu ambao wapo tayari kuuza nchi kama kina Mobutu. Pia alikuwa na kazi ya kusomesha watu wengi zaidi ili nchi isonge mbele.

    Awamu ya pili kubwa zaidi lililotokea duniani ni kuisha kwa vita baridi/kubadilika kwa mfumo wa uchumi sehemu nyingi kutoka usosialisti/ujamaa kwenda ubepari. WAKAJA WAGENI wakatuambia mengi(mfano economic adjustment programs). wakasema waacheni watu wafanye wanavyotaka ikiwemo biashara huria. Wapeni RUKSA. Uongozi wa nchi nyingi kama wetu ulibebwa na mawimbi ya mabadiliko hayo bila hata kupenda.

    Awamu Ya tatu WAKAJA TENA WAGENI wakatuambia sasa vunjeni mashirika yenu, mbinafsishe, ndio mtapata ufanisi na maendeleo. Lakini hawakututahadharisha(wala sisi hatukushtuka) kwamba tukiyavunja haraka na kubinafsisha nani atayanunua? Watu wetu wana uwezo si tu wa kifedha lakini pia wa kitaaluma? kama hawana nani atayanunua?. Nakumbuka Mtanzania mmoja alitaka kununua Kilimanjaro Hotel lakini bado tukawapa wageni!

    Awamu ya nne imekuja, imekuta tumetoka enzi za uhuru bila wasomi wala mashirika yoyote, mpaka kufikia nchi imejaa wasomi na mashirika mengi mpaka namashirika tumeuza yote. Lakini pia utandawazi umekuja, mawasiliano yameongezeka, na watu wengi zaidi wanauliza kulikoni nchi yetu?. Wanauliza mustakabali wa nchi uko vipi?. Utandawazi huu ukiwemo wa teknohama ndio unaotuwezesha hata sasa kujadili hapa. Hili halikuwepo awamu zilizopita na kuwepo kwake sasa kutaleta mabadiliko makubwa si hata nyumbani peke yake bali Dunia nzima.

    Kigoda cha Mwalimu/Taasisi ya mwalimu ni kiti cha kitaaluma cha watu WOTE wenye la kuongea wanakwenda kuongea na kutoa mawazo yao. Kama Mwalimu angekuwa Messiah au mwana muziki, basi kongamano lingejadili U-messiah au uwana muziki. Bahati mbaya kwa Mwandishi, Mwalimu alikuwa kiongozi mwenye MAADILI. Kwa hiyo ukienda pale unaongelea MAADILI YA UONGOZI.

    Kuma matatizo mengi nchi hii kwa sasa. Kuanzia IPTL(1996) mpaka Richmond(2007) bado tupo kizani. Ni mengi mno na jipya ni TRL

    Ndio maana wanapokutana watanzania kumkumbuka Mwalimu, inawabidi wakumbuke MAADILI pia. Na wanapozungumzia maadili huku wakikabiliwa na matatizo yote haya, sio ajabu wakazungumzia uongozi. Wakajiuliza hivi tunakwenda wapi? Tatizo liko wapi?

    Wanapofanya hivyo, inakuwa vigumu kuelewa mwandishi anaposema kwamba" wanaitisha makongamano ya kushutumu na kudhalilisha uongozi" Inasikitisha pia kuyaita malumbano. Mimi nadhani watanzania wanaongea: wanajadili wanasema kwanini tupo hapa tulipo?.
    Mimi nadhani badala ya kuwajadili wao, tujadili wanachokisema.

    ReplyDelete
  14. nafikiri Watanzania wengi wana matatizo ya kutokuwa huru katika kufikiri na kuwa na hisia zinazofanana na watu walio kanisani ambao huwa hawana nafasi ya kumuuliza swali mhubiri. Ndg yangu jifunze ukiwa na mtazamano unaouonesha hapo juu mwisho wa siku utashindwa kuendesha hata familia yako, itakuwa ni yenye maadili mabovu. huwezi kusifia kitu kwa ajili ya kumfurahisha mtu ilhali si hivyo, jifunze kusema ukweli bila kuangalia kama ukweli huo utakugharimu. wewe unaesema watu wenye mtazamo tofauti hawafai kuajiriwa serikalini, hakika wewe mwalimu wako amepata hasara, hufai kupewa kazi iyohusisha kufikiri, wewe nenda kwa wahidi wakupe ajira ili uwe unapokea order.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...