Rais wa zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Amani Abeid Karume,akimtunuku Raha Ahmada Ali, Shahada ya kwanza ya Elimu ya Sanaa ya Chuo kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) katika mahfali ya tano ya Chuo hicho yaliyofanyika, huko viwanja vya Victoria Garden Mjini Zanzibar leo.
Rais wa zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Amani Abeid Karume,akimtunuku Rashid Mohammed, Shahada ya kwanza ya Elimu ya Sayansi ya Chuo kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) katika mahfali ya tano ya Chuo hicho yaliyofanyika, huko viwanja vya Victoria Garden Mjini Zanzibar.
Rais wa zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Amani Abeid Karume,akimkabidhi zawadi ya mfanyakazi bora Hassan Simba,katika mahfali ya 5 ya chuo kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) yaliyofanyika, huko viwanja vya Victoria Garden Mjini Zanzibar.
Picha na mdau Ramadhani Othman wa Ikulu Zanzibar

HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI AMBAYE PIA NI MKUU WA CHUO KIKUU CHA TAIFA CHA ZANZIBAR , (SUZA)
MHESHIMIWA AMANI ABEID KARUME, KATIKA MAHAFALI YA TANO YA CHUO, JUMAMOSI, 12 DISEMBA 2009 VICTORIA GARDEN, ZANZIBAR

Mheshimiwa Waziri Kiongozi,

Mheshimiwa Naibu Waziri Kiongozi,

Mheshimiwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali,

Mheshimiwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar,

Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Wabunge,

Ndugu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar,

Ndugu Kaimu Manaibu Makamu Wakuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar,

Ndugu Wageni,

Ndugu Wanachuo,

Mabibi na Mabwana,


Assalamu Aleykum


Naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Hekima na Mjuzi wa Yote, kwa kutujaalia afya njema, uzima na kuweza kukutana tena hapa leo hii katika mahafali iliyojaa furaha na kheri.

Mimi binafsi na wananchi wa Zanzibar kwa jumla tuna wingi wa furaha leo kuadhimisha kuhitimu kwa vijana wetu katika fani mbali mbali. Furaha yangu zaidi ni kuona katika muda mfupi wa kuanzishwa chuo chetu hiki cha SUZA tumeweza kutoa wahitimu wa kwanza wa Shahada ya Sayansi ya Kompyuta. Pamoja na wao, kama tulivyokwishaelezwa, wapo wahitimu wengine wa daraja mbali mbali katika Sayansi ya Kompyuta. Hili ni jambo la sote kujivunia.

Kama tunavyofahamu, dunia ya leo ni ya Sayansi na Teknolojia. Mambo hayo mawili hayafanikiwi au kupatikana bila ya ujuzi wa fani ya Sayansi ya Kompyuta. Nchi zilizoendelea kama Marekani, Japani, Ujerumani, Ufaransa na Uingereza, miongoni mwa nchi nyingi, zimefika zilizopo kwa kutilia mkazo elimu ya Sayansi na Teknologia ikiwemo hii ya Sayansi ya Kompyuta kwa vijana wao tokea umri mdogo.

Kwa kufahamu hayo, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeitia elimu hiyo katika mitaala yake tokea skuli za msingi. Kwa jitihada zetu na ushirikiano wa wadau mbali mbali, somo la kompyuta sasa linaeleweka na watoto wetu kiasi kikubwa. Huo ni mwanzo mzuri ambao lazima tuuendeleze kuueneza na kuukuza.

Nachukua nafasi hii kukipongeza Chuo chetu cha SUZA kwa jitihada yao hata leo tukaweza kushuhudia kuhitimu wanafunzi kumi na moja ambao wametunukiwa shahada zao. Aidha, nawapongeza wahitimu hao na kuwashauri kutumia ujuzi na maarifa waliyopata katika shughuli za maendeleo ya nchi yetu, ambazo zinahitaji sana maarifa yao .

Pia ni jambo la faraja na la kuzidi kutafakari nalo kuwa hivi sasa chuo chetu kinaendelea kutoa wahitimu wa elimu ya sanaa na sayansi. Hao ndio askari miamvuli wa maendeleo ya elimu katika skuli na taasisi zetu mbali mbali. Nawapongeza wahitimu wote hao na walimu wao, pia nakipongeza chuo na uongozi wake pamoja na Baraza la Chuo lililomaliza muda wake kwa kufanikisha hatua hiyo ya maendeleo ya chuo.

Napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Mwenyekiti mpya wa Baraza la Chuo, Mzee Hassan Nassor Moyo na wajumbe wake. Nawatakia kheri na mafanikio katika dhamana zao nzito za kutoa uongozi kwa chuo ili kiendelee kupata mafanikio zaidi. Wakati huo huo, nashauri kuwepo ushirikiano mkubwa baina ya Baraza na uongozi wa chuo. Ushirikiano wao ndio utakaofanikisha ustawi na maendeleo ya chuo chetu.

Nampongeza na kumshukuru pia Waziri wetu wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mheshimiwa Haroun Ali Suleiman kwa juhudi zake binafsi katika maendeleo ya chuo hiki na elimu nchini kwa jumla. Nawapongeza pia watendaji wa wizara yake kwa juhudi zao.

Ushirikiano wa viongozi na watendaji ni muhimu sana katika kufanikisha maendeleo. Haya tunayashuhudia hapa chuoni na wizarani. Napenda kusisitiza jambo hili ili liwe ndio msingi wa utaratibu wetu wa maendeleo. Tukifanikiwa hivyo, itakuwa wepesi kuwashirikisha wananchi wenyewe katika kupeleka mbele maendeleo yao .

Tuelewe kwamba mipango yetu yote ya maendeleo tunayojipangia, haiwezi kufanikiwa bila ya ushirikiano kamili wa wananchi wetu. Hili ndilo lengo la juhudi ya serikali yenu na ni wajibu wa viongozi, watendaji na wananchi kwa pamoja kulitilia mkazo na kulishughulikia ipasavyo.

Ndugu Makamo Mkuu wa Chuo,
Katika kuendeleza mipango yetu ya maendeleo, kama Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini, ni lazima chuo kishiriki katika kutoa maarifa na mbinu kwa wananchi. Haya yatawezekana tukitilia mkazo mambo ya utafiti katika fani zote tunazotumilia. Utafiti hauna kiwango au maeneo fulani bali unawezekana kufanyika katika sekta zote ambazo tuna watu wenye maarifa kama wahitimu na wahadhiri wa chuo. Napenda kushauri chuo chetu, pamoja na mipango yake ya kujiimarisha na kujiendeleza, ipo haja zaidi ya kutilia maanani suala la utafiti. Tukiangalia nchi zilizoendelea, utafiti na matumizi ya matokeo yake ndio umekuwa chachu za maendeleo. Tusikubali kuwekwa nyuma au kuwa na dhana kwamba hatuwezi.

Natoa wito kwa wahitimu wote waliotunukiwa shahada zao hivi leo kuitumia vyema elimu waliyoipata kwa manufaa ya nchi, wananchi na hata familia zao kwa jumla.

Kwa kumalizia, natoa shukurani zangu kwa wale wote wanaojitokeza kukisaidia chuo chetu kwa njia moja au nyengine. Tunathamini sana michango yao na nawaomba waendelee kutuunga mkono.

Nachukua fursa hii pia kuwapongeza wanafunzi wa chuo chetu kwa kuwa na nidhamu wakati wote na ushirikiano na wakuu wao, wakiwemo wakufunzi, wahadhiri, watendaji na wafanyakazi wengine wa chuo. Naamini huku kunatokana na upendo wao wa chuo chao na kupenda kujinasibisha na maendeleo yake. Ni mfano mzuri wa kuigwa na taasisi zetu nyenginezo za elimu .

Sitawasahau wazazi, jamaa, marafiki na wahisani wa wanafunzi wetu kwa kujitolea kwao kwa hali na mali kuwasaidia vijana wetu kufaulu. Ni wajibu wa wanaorehemewa nao kurejesha rehema kwa waliowapa, yaani wazee na ndugu zao pamoja na nchi yao .

Nimalizie kwa kuwakumbusha maneno ya Shakespeare:
“The quality of mercy is not strained. It drops like rain from heaven. It is twice blessed. It blesses him that gives and him that receiveth”

Kwa kifupi ni kwamba sifa ya rehema ni kwamba inateremka kama mvua kutoka mbinguni. Inabarikiwa mara mbili. Inambariki yule anayetoa na inambariki yule anaepokea.

Basi wahitimu na wafadhili wa maendeleo tutafute baraka hizo.

Ahsanteni kwa kunisikiliza.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. HONGERENI WAHITIMU, ila mbaya kwenu huwa mnatukimbia eti mnadai hakuna maslahi, ooh serikali haiwajali, jamani kazeni buti fanya kazi nyumbani kuokoa TAIFA unazani litajengwa na nani? Safari ndefu huanza na hatua moja bwana.
    Junior Hyderabad.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...