SERIKALI YAWABANA WAHAMIAJI HARAMU

Na Veronica Kazimoto – MAELEZO)
Idara ya Uhamiaji imekamata wahamiaji haramu elfu tano ndani ya kipindi cha miaka miwili (2008 – 2010) wakitokea nchi za Burundi, Kenya, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Somalia na Ethiopia. Kati yao wahamiaji wapatao elfu tatu wamefukuzwa nchini.

Kwa mujibu wa taarifa ya msemaji wa Idara hiyo Bwana Abdi Ijimbo, wahamiaji wengine elfu mbili baadhi yao kesi zao ziko mahakamani kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria. Endapo watabainika kukiuka sheria za uhamihaji wanaweza kukabiliwa na kifungo, kurudishwa makwao au kutakiwa kuhalalisha ukaaji wao nchini.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa, wahamiaji wengi waliokamatwa na Idara hiyo wametokea nchi za Pembe ya Afrika, yaani Ethiopia na Somalia wakitumia nchi ya Tanzania kama kipenyo cha kuelekea nchi za kusini mwa Afrika.

Taarifa hiyo imeendelea kubainisha kuwa, katika kipindi cha 2007 hadi 2008, kulikuwa na wimbi kubwa la wahamiaji haramu waliongia nchini Tanzania kupitia Kenya na Uganda wakielekea nchi za kusini mwa Afrika. Wengi wao wahamiaji hao walikuwa wanaume wenye umri kati ya miaka 20 hadi 45.

Taarifa hiyo imezitaja sababu zinazopelekea kuwepo kwa wimbi kubwa la wahamiaji haramu kuwa ni pamoja na machafuko ya kisiasa yanayozikabili nchi za Somalia na Ethiopia. Sababu nyingine zinahusu matatizo ya kiuchumi yanayozikabili nchi hizo pamoja na imani waliyonayo vijana kuwa maisha mazuri hupatikana Afrika Kusini na nchi za ulaya.

Hata hivyo kutokana na wimbi hilo kubwa la wahamiaji haramu, Idara ya Uhamiaji imepanga mikakati ya kupambana na kutokomeza wahamiaji hao ambao baadhi yao hupitia Tanzania kwa ajili ya kufanya vitendo vya kihalifu.

Taarifa ya Msemaji wa Idara ya Uhamiaji imebainisha mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kuundwa kwa kitengo kinachohusika na sera, uratibu na usimamizi wa shughuli zinazohusiana na menejimenti ya mipaka na operesheni ya kukamata wahamiaji haramu.

Idara ya uhamiaji imeanzisha Chuo cha Uhamiaji kijulikanancho kama Tanzania Regional Immigration Training Academy (TRITA). Chuo hiki kitatoa mafunzo kwa watendaji wa Idara za Uhamiaji katika nchi zinazoizunguka Tanzania.

Mikakati mingine ni kuongeza wafanyakazi hasa askari wa doria. Kazi ya askari hawa itakuwa ni kuchunguza wageni wanaoingia nchini bila kufuata taratibu zilizowekwa na Idara hiyo pamoja na kuimarisha vikosi vya doria mipakani na ndani ya nchi ili kukabiliana na wimbi la wahamiaji haramu.

Idara ya Uhamiaji inawaomba wananchi kutoa ushirikiano katika kufichua wahamiaji haramu pindi wanapobainika ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria mapema iwezekanavyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Hivi mnajua kama Congo,Somalia na Ethiopia ni waafrica wenzenu na wanakuja hapo kwa sababu ya matatizo katika nchi zao na si kwamba Tanzania ni peponi. Na wengi wao wanapita tu hapo na sio kukaa.Sasa badala ya kuwasaidia waafrika wenzenu ambao wapo kwenye matatizo mnawasumbua.Najua watu wataniambia kwa nini wasiishi kihalali,mtu atakayeuliza hivyo hajui nini maana ya mkimbizi.Na je tujiulize tungekuwa sisi kwenye matatizo na wao wangetufanyia hivyo je tungefurahi? Ni hayo tu.Ankal usinibanie. Naomba watu tulichambue hili suala bila matusi kistaarabu

    ReplyDelete
  2. Any no.1,kwanza inaonekana sio mtanzania ,kwahiyo unajenga wigo wa kutofuatiliwa,haikatazwi uliowataja kuishi hapa Tanzania,lakini kuna sheria husika. Mie naomba contact ya Idara ya Uhamiji - emmail ili niwalipuwe wahamihaji haramu kibao waliopo hapa Tz. bila kufuata taratibu wapo wengi sana toka Malawi,Kenya ,Rwanda wanapiga mzigo tu bongo tambarare-uhamihaji wakija wanapokea rushwa watu wandunda- haswa Mkoa wa Dar-es salaam,ube waulizwe kesi ngapi walifuatilia na wakazimaliza nje ya mahakama bandia -rushwa,Takukuru muko wapi jamani?
    nasubiri emal active wawaungulumishie,uzuri wangekuwa na utu kama sisi lakini wana roho mbaya,makatili,kimbelembele maofisini,na kupenda mitelemko kima mahali-hofu yangu wengi sana watajiandikisha katika kupiga kura uchaguzi ujao,kwani wao hati ya kuandishwa upigaji kura basi wanakuwa wamemaliza kila kitu.Kwa ujirani wasubiri basi hiyo jumuia hianze kazi.
    Katika maswali kwa Rais Kikwete nilituma email kuhusu kero hii,lakini mpaka leo sijapata jibu?
    Mchukia wahamiaji Haramu sasa.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...