Na Veronica Kazimoto - MAELEZO
Maji yanayoingia kwenye matanki ya Shirika la maji safi na maji taka DAWASCO katika maeneo ya Kimara na Mlandizi yameongezeka kutoka mita za ujazo 500 kwa saa hadi kufikia 1000 kwa saa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Afisa Uhusiano wa DAWASCO Bi Mary Lyimo, kuongezeka kwa maji hayo kumesababishwa na zoezi la kuwaondoa wakazi wa maeneo hayo waliojiunganishia maji kiholela katika bomba kubwa la nchi 30 linalotoa maji katika chanzo cha Ruvu Juu.
Taarifa hiyo imesema kuwa bado Shirika hilo linaendelea na msako wa kuwaondoa wale wote waliojiunganishia maji kiholela ili kuboresha upatikanaji wa maji kwa wateja halali wanaotakiwa kupata huduma hiyo.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa tatizo la maji Kimara ni kubwa kwa sababu watu walikuwa wametoboa mabomba makubwa na kujiunganishia maji na hivyo kusababisha yasifike katika matanki yanayosambasa maji katika maeneo ya Kimara, Msewe, Ubungo, Kibangu, Kisukuru, Makuburi na Tabata.
Pamoja na jitihada zinazofanywa na DAWASCO za kuboresha miundombinu na kufunga maji kila nyumba, bado upatikanaji wa maji katika maeneo ya Kimara Kin’gongo, Bonyokwa, Golani, Temboni, Baruti na Bakery unasuasua.
Kusuasua kwa upatikanaji wa maji katika maeneo hayo unasababishwa na hali ya miinuko na presha ndogo ya maji yanayopita kwenye bomba siku za migao kufuatia kujiunganishia maji kwa baadhi ya wakazi wa Kimara.
Aidha taarifa hiyo imebainisha kuwa DAWASCO kupitia mamlaka ya maji safi na maji taka DAWASA imeandaa awamu ya kwanza ya mpango wa kuboresha hali ya maji kwa kuchimba visima 12 eneo la Kimbiji na vingine 8 Mpera vyenye uwezo wa kuzalisha maji mita za ujazo 260,000 kwa siku.
Uchimbaji wa visima hivyo unakwenda sambamba na upanuzi wa mitambo ya maji ya Ruvu Chini na Ruvu Juu. Mtambo wa Ruvu Chini utaongeza uwezo wa kuzalisha maji kutoka mita za ujazo 182,000 kwa siku hadi 270,000 kwa siku. Wakati mtambo wa Ruvu Juu utakuwa na uwezo wa kuzalisha maji kutoka mita za ujazo 82,000 kwa siku hadi 150,000 kwa siku.
Mwandikaji naomba ajirekebishe uandishi Inchi 30 na si nchi 30.
ReplyDeleteKwa maneno matamu tu hatujambo !!
ReplyDeleteKuna haja gani yakuendelea kuongeza uzalishaji wa maji wakati maji kibao yanapotea kwenye mabomba yaliyopasuka? Mfano pale ubungo karibu kabisa na wizara ya maji na umwagiliaji kwenye mataa kuna bomba limepasuka mwaka wa tatu sasa bila kuzibwa. Kila ukipita pale unakuta maji yanatirirka kuelekea mtoni. DAWASCO kuweni makini na kazi yenu,acheni longolongo...
ReplyDeleteTeh teh teh teh he heheeeee!Kama kweli vile.........
ReplyDeleteWaanzie kwa mawaziri na wakubwa serikalini..karibia wote wameunganishiwa kwa madili. Mtu anatakiwa alipe 150,000Tsh kwa mwezi lakini unakuta bill yake ni 3,000 Ths kwa mwezi
ReplyDelete