Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Wavu nchini Bw. Agustino Israel Agapa akimkabidhi vifaa mbalimbali vya michezo Katibu mkuu Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo Bw. Sethi Kamuhanda(kushoto) kusaidia Chuo cha Maendeleo ya Michezo Marya leo jijini Tanga. Vifaa vilivyokabidhiwa leo ni pamoja na mipira, jezi, vitabu na Cds zenye mafunzo mbalimbali kwa ajili ya kufundishia.
Katibu mkuu Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo Bw. Sethi Kamuhanda (wa pili kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Idara, Viongozi na wafanyakazi bora wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo mara baada ya kuwakabidhi vyeti na zawadi mbalimbali jijini Tanga.

======================
WAFANYAKAZI WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA BIDII.

Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
Changamoto imetolewa kwa Wafanyakazi nchini kufanya kazi kwa bidii ili kukuza pato la taifa.

Changamoto hiyo ilitolewa leo jijini Tanga na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari na Utamaduni Bw. Sethi Kamuhanda wakati akihitimisha mkutano wa sita wa baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo.
Alisema wafanyakazi wanao wajibu na jukumu kubwa la kutumia rasilimali na fursa walizonazo kuleta ufanisi mahali pa kazi sanjari na kuhakikisha kuwa michango ya huduma wanazozitoa zinawafikia walengwa husika katika jamii.

Alifafanua kuwa serikali kwa kutambua mchango wa wafanyakazi itaendelea kuboresha huduma mbalimbali za kiofisi zikiwemo nyenzo mbalimbali za kufanyia kufanyia kazi zikiwemo huduma za usafiri ili kuweka mazingira mahali pa kazi .

Aliongeza kuwa serikali kupitia sekta mbalimbali itaendelea kutoa fursa zaidi kwa wafanyakazi kupata nafasi za masomo kwa lengo la kuinua viwango vya elimu kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi na kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia nchini.

Awali akizungumza kuhusu mkutano Baraza la wafanyakazi Bw. Sethi Kamuhanda alisema mkutano huo umetoa changamoto na kuamsha ari kwa wafanyakazi kwa sababu umezishirikisha ngazi zote za uongozi huku akitoa wito kwa wafanyakazi kutekeleza yale waliyokubaliana katika mkutano huo.

Aidha Bw. Sethi Kamuhanda aliwapongeza baadhi ya wafanyakazi wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo waliopata bahati ya kuchaguliwa kuwa wafanyakazi bora na kusema kuwa wao ni mfano wa kuigwa.

“Kuchaguliwa kwenu kusiwafanye mbweteke bali kuwe kichocheo na kuwafanye kuongeza bidiikatika utendaji wa kazi za kila siku ndani ya wizara, napenda kuwasihi wafanyakazi wengine waogeze bidii ili tushirikiane katika kuleta tija na ufanisi mahali pa kazi” alisema.

Alisema Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo bado ni Wizara mpya maana iliundwa mwaka 2006 na kuongeza kuwa inalo jukumu kubwa sana kwa watanzania katika kusimamia sekta ya Michezo, Habari na Utamaduni.

Aliendelea kufafanua kuwa mbali na wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo inalo jukumu kubwa sana kuhakikisha kuwa sekta ya Habari, Utamaduni na Michezo inatoa huduma bora kwa watanzania pia ina mchango mkubwa katika kuhakikisha Jumuiya ya Afika Mashariki inapata ustawi mzuri.

Aidha alitoa wito kwa wafanyakazi wa wizara kujipanga kikamilifu katika nafasi zao ili waweze kukabiriana na ushindani utakaokuwepo kutokana na Tanzania kuwa miongoni mwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“ Tanzania ni Mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) naomba tujipange namna tutakavyokabiriana na ushindani kwani kuna maeneo ambayo tutalazimika kuyafanya ili tuendane na ushindani na hali itakayokuwepo” alisisitiza.

Kwa upande wake Bw. Rish Urio ambaye alishika nafasi ya kwanza kwa kuwa mfanyakazi bora kati ya wafanyakazi 9 wa Wizara hiyo waliopewa vyeti na zawadi mbalimbali aliushukuru uongozi wa Wizara kwa kutambua mchango wa wafanyakazi na kutoa wito kwa wafanyakazi wengine kutumia muda wao wawapo kazini kufanya kazi kwa bidii.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 27, 2010

    Kweli kabisa tufanye kazi kwa bidii jamani maana tumeshaambiwa hata tukigoma miaka kumi hatuongezewi mshahara na kama hatutaki bai tuache kazi. Au vipi jamani nyie mnaonaje si tupige kazi tu, maana soko la kazi kwa kina yakhe Bongo hapa bado ni la ridhaa sio la kulipwa jamani.

    ReplyDelete
  2. AnonymousMay 27, 2010

    Nadhani Aliyeturoga Tanzania alishagakufa miaka mingi iliyopita!! huwezi sasa kuilaumu serikali eti inaumwa kifafa nadhani hata wananchi sisi pia tuna kifafa kama ilivyo serikali yetu! huku ni kutaka kuchezea akili zetu na sisi tumo tu, jamani hatma yetu iko mikononi mwetu!! serikali hiihii ndio inalipa mishahara midogo sana, juzijuzi tu hapa mabavu yakawa-applied kwamba hata msiponipa kura zenu haitanidhuru nyie ni wachache sana. tumeshaambiwa mishahara ya kutuwezesha kuishi maisha yenye uhuru tuisahau na kwamba hailipiki!! leo hii watu hawahawa wanashika vipaza sauti wanatuambia tufanye kazi kwa bidii tujenge nchi!!! hahaha duh ama kweli michuzi alijisemea bongo tambarare, leo sasa ndo nang'amua maana halisi ya hili neno. anyway ningependa zaidi wanangu nikawazalie marekani, canada, Uk, Norway au Australia ili automatically wawe na passport za huko, halafu ndo niwalete Tanzania ili wasiwe wananibugudhi eti baba hii nchi mnayotuachia iko vipi, wakipiga tu kelele mi jibu langu litakuwa eebwanae acheni kunizingua kwani tanzania kwenu?? nyie kuweni mkishapata akili rudini kwenu mlikozaliwa huko ndo kwenu mambo mazuri tu haya mavumbi hapa niachieni mimi mzawa mwenye nchi niliyezaliwa na kifafa na ambaye nitakufa nacho, nyie niliwazalia nje ili msipatwe na hiki kifafa cha kudumu!!!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...