BALOZI WA TANZANIA KATIKA UMOJA WA MATAIFA, OMBENI SEFUE AKIZUNGUMZA WAKATI WA MKUTANO WA BARAZA KUU LA UMOJA WA MATAIFA ULIOKUWA UKIJADILI TAARIFA YA KAMATI MAALUM ILIYOCHUNGUZA VITENDO VYA UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU VINAVYOFANYWA NA ISRAEL DHIDI YA WANANCHI WA PALESTINA

NA MWANDISHI MAALUM
NEW YORK- Tanzania imepongeza juhudi zinazofanywa na serikali ya Marekani za kuanzisha tena mazungumzo ya kutafuta amani kati ya Israel na Palestina.
Pongezi hizo zimetolewa na Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Ombeni Sefue wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipokuwa likijadili taarifa ya Kamati Maalum iliyohusika na uchunguzaji wa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya wananchi wa Palestina unaofanywa na Israel.
“Tanzania tunaunga mkono hatua hii iliyochukuliwa na serikali ya Marekani ya kufufua mazungumzo haya. Tunaishukuru na tunaihimiza kuendelea na juhudi hizo na tunawatakiwa mafanikio mema ”.Anasema Balozi Sefue
Aidha mwakilishi huyo wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa ameeleza kwamba, Tanzania pia inapenda kutambua michakato mingine inayofanywa na Umoja wa Mataifa, Jumuia ya Ulaya, Urusi , Misri pamoja na wadau wengine katika kutafuta amani na muafaka wa kudumu kati ya Israel na Palestina.
Hata hivyo, pamoja na kuipongea Marekani na wadau wengine katika uendelezaji wa mchakato wa kutafuta amani ya kudumu kati ya mataifa hayo mawili. Balozi Sefue hakusita kuelezea msimamo wa Tanzania wa kuungana na nchi nyingine katika kuelezea masikitiko yake ya namna Israel inavyoendelea na harakati zake za ujenzi wa makazi katika eneo linalokaliwa isivyo kihalali na Israel, mipaka ya Palestine, eneo la Mashiriki ya Jerusalemu na maeneo mengine ya Kiarabu.
Akasema wazi kuwa Tanzania inasikitishwa sana na upanuzi wa makazi hayo, ubomoaji wa nyumba na kuondolewa kwa nguvu kwa watu kutoka Ukingo wa Magharibi likiwamo eneo la Mashariki ya Jerusalemu.
“Tanzania tunaona maendeleo haya na ujenzi kama kikwazo kikubwa katika mchakazo wa utafutaji wa amani ya kudumu. Ingawa tunatambua haki ya kiusalama ya watu wa Israel, lakini katika mtazamo huo huo tunasikitishwa na taarifa za utumiaji nguvu wa kupita kiasi dhidi ya wananchi na tunapinga matumizi hayo ya nguvu” anasisitiza Balozi Seufe.
Aidha Balozi Sefue ameueleza mkutano huo kwamba, Tanzania inaunga mkono juhudi za kumalizwa kwa mgogoro kati ya waarabu na waisrael kwa kuzingatia misingi ya sheria za kimataifa , maazimio mbalimbali ya Baraza Kuu la Usalama, hadidu za rejea za mkutano wa Madrid na mikakati mingine ya amani .
“ Tanzania pia inaunga mkono suala la kuwapo kwa mataifa mawili huru likiwamo la Palestine huru wakiishi sambamba katika mazingira ya amani na salama na taifa la Israel huku tukiunga mkono haki ya waisrael kuishi kwa amani”
Tanzania pia imesisitiza utekelezwaji wa azimio namba 1860 la mwaka 2009 la Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu kuheshimu sheria za kimataifa na kufunguliwa bila ya mashariti njia za kupitishia misaada ya kibinadamu, biashara na watu.
Kwa kuzingatia misingi hiyo Tanzania, anasema Balozi Sefue, inakaribisha juhudi za hivi karibuni zilizotangazwa na serikali ya Israel za kulegeza vikwazo katika Ukanda wa Magharibi na uingizaji wa bidhaa huko Gaza, na kusisitiza kuchukuliwa kwa hatua zaidi.
Katika hatua nyingine Mwakilishi wa Tanzania Katika Umoja wa Mataifa, anatamka bayana kwamba Tanzania inapenda kusisitiza msimamo wake wa kuwaunga mkono wananchi wa Palestina katika jitihada zao za kuwa taifa huru ikiwa ni pamoja na kuufanya mji wa jerusalem kuwa makao makuu yake.
Akasema ni maoni ya Tanzania kuwa kwa kutambua na kuwapatia haki hii wapalestina ni njia muafaka na sahihi na yenye manufaa kwa pande zote yaani waisrael na wapaletina kwani wote watanufaika na kuwapo kwa amani ya kudumu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Hello,
    Asante kwa news, Mtazamo wa Tanzania juu ya Israel na Palestina.

    Labda niseme siku palestina inafanikiwa Jerusalemu kuwa mji mkuu wake,basi utakuwa mwisho wa dunia maana ya Iraq,Hiroshima afadhali,patachimbika hapo Jerusalemu. Ijulikane waisrael ni watu wana msimamo mikali na imani yao yote imesamama pale na historia yao yote iko pale tangu mwanzo wa dunia.

    Kitu kingine historia inaeleza vizuri sana kuwa Jerusalemu ilikuwa ya waisrael kabla ya bablon, wapalestina walikuja baadae na Mtume aliwai kuabudu pale last moment. Hivyo Wapalestina wanadai kwa msingi huo. Lkn ukweli UN isipotoshe dunia, acha iseme ukweli na nani alikuwa mmiliki wa eneo lile mwanzo. Haiwezekani watu wanganinie swala ambalo linafichwa ukweli .

    Mimi naiomba tu Tanzania, we should not jumb to ship we dont know start and the end, lets back in history and work on fact bila ya ushawishi wa marekani na mataifa mengine ambayo yanasabisha dunia inazidi kuteketea mabomu na risasi.

    Binafsi kama Mtanzania sisupport mawazo ya UN, wenye kumaliza tatizo hili ni Israel na Palestina wenyewe. Hawa wengine ni ushabiki kama ulivyo ktk Iraq, Arfghastan walivyo fanya mataifa makubwa.

    Asanten. Usiibane Michuzi na Omben aione.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...