Waheshimiwa wadau,

Kwa heshima na taadhima natoa salamu za MWAKA MPYA wa 2011 kwa wadau wote popote mlipo ulimwenguni. Nitakuwa mtovu wa fadhila endapo kama sintosema kwamba bila ninyi Libeneke lisingenoga. Asanteni sana na nawashukuru kwa kampani mnayonipa na mliyonipa toka Septemba 5, 2005 nilipozindua rasmi Globu ya Jamii kule Helsinki, Finland, chini ya usimizi wa mdau mkuu kaka Ndesanjo Macha.

Leo tunauanza mwaka mpya tukiwa na kila aina ya matumani kwamba Mola atatujaalia si pumzi tu bali pia fanaka katika kila jambo la maendeleo wakati tukianza ngwe hii mpya ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Nina mengi ya kusema, ila endapo nitathubutu kufanya hivyo nahisi nitajaza ukurasa wote huu lakini bado nisiweze kueleza robo tu ya niliyonayo moyoni. Itoshe tu niseme asanteni wadau wote kwa kuendelea kuniunga mkono kwenye shida na raha, katika kukubaliana na katika kupingana bila kupigana. Asanteni sana, sana, sana wadau wa Globu hii ya Jamii.

Sina zaidi ya kuahidi kwa mwaka mpya zaidi ya kuendeleza Libeneke kama kawaida. Hivi sasa nimejipanga kuja na mpya kadhaa ikiwa ni pamoja na mahojiano na watu wanaotakiwa kutoa neno katika lolote linalosibu jamii katika wakati husika, ikiwa ni kwa maandishi na video. Nitakaribisha pia fursa ya wadau kudai nani wa kumhoji na juu ya nini katika mfumo huo mpya ambao Globu ya Jamii itakuja nao kwa jina la MASWALI KUMI KWA......

Napenda pia kukumbusha sera ya Globu ya Jamii ya kwamba ‘Kilicho chema kwa bata mzinga, si chema kwa kuku’ (what’s good for the goose, is bad for the hen) yaani si rahisi kumridhisha kila mmoja kati ya wadau milioni moja na nusu wanaotembelea Globu ya Jamii kwa siku. Hivyo nawataka radhi kabisa wale ambao nitakuwa siwaridhishi kwa namna moja ama nyingine, na kwamba hiyo si kwa makusidi bali ni hali halisi ya maisha. HAKUNA ALIYE MKAMILIFU ILA MOLA PEKEE. Kwa hiyo maoni yako yakitiwa kapuni ujue ni katika hilo. Nia ni ile ile ya kupashana bila kuwa na haja ya kujeruhi mtu ama watu kwa kuchafua hali ya hewa.

Wakati ni kweli kwamba mwaka 2011 una changamoto (challenges) kibao katika tasnia hii ya libeneke, lakini si uwongo kwamba kwa msaada wenu wadau hali inaweza kuboreshwa zaidi. Na hii itawezekana endapo kama sie sote tutatumia teknolijia hii ya habari kwa kuendeleza maendeleo ya nchi na si mtu binfasi ama kikundi Fulani cha dini, siasa ama jamii.

Katika hilo nafurahi na kuona fahari kubwa kwamba Globu ya Jamii imekuwa chachu ya kuanzishwa Libeneke nyingi nchini na nje ya nchi zenye kuwa na msimamo wa kupashana habari kwa njia ya kisasa. Ushahidi ni jinsi ambavyo Globu ya Jamii ilivyo mstari wa mbele katika kutangaza blog mpya zinazoanzishwa kila ikitokea hivyo.

Pamoja na yote hayo nina masikitiko makubwa kwamba blogu nyingi zinazoanzishwa zinakuwa ni zile zile tu, kama zetu za akina sie. Yaani kwa mtazamo wa wengi blogu ni kuwa na habari za kila mara ama kila siku, badala ya wanaoanzisha blogu kujikita katika fani ambazo wamebobea. Badala ya wote kujikita katka katika habari, tunahitaji blogu za Nyanja tofauti zaidi ya habari tu. Kwa mfano tunahitaji blogu za useremala, uashi, urembo ama hata muziki wa mipasho. Si kila aanzishaye blogu ajikite katika habari na kutaka kutunishana misuli na kina sie tulio ndani ya tasnia ya habari. Angalizo hapa ni kwamba copy & paste aghalabu hukimbiza wasomaji.

Mwisho napenda kutoa shukurani kwa wote walioifanya Globu ya Jamii ifike hapa ilipo leo. Ni ngumu kumtaja kila mmoja. Lakini si vibaya nikiwataja baadhi ambao wamenipa msukumo kuendeleza Libeneke.

Naomba nianze na mdau mkuu Ndesanjo Macha aliyenifungua macho na kuanza kublogu, wa pili ni kaka yangu mpendwa aliye huko Helsinki, Finland, Fidelis Tungaraza aka Mti Mkubwa (Fide nashukuru sana kwa ushauri wako wa kila mara) , Jeff Msangi wa Canada, Balozi Peter Kallaghe na Balozi Mwanaidi Maajar (Mama maajar alinialika London kutoa mada ya Libeneke katika Disapora II, asante sana mama Maajar kwa kutambua mchango wetu katika jamii, mwaliko wako London umenipa moyo sana kuendeleza Libeneke), Balozi Patrick Tsere, Maggid Mjengwa, Haki Ngowi, Francis Godwin (asante na hongera kwa kuendeleza Libeneke huko Iringa) wadogo zangu Ahmad na Othman Michuzi, Mh. Lazaro Nyalandu, Dk. Emmanuel Nchimbi, Mh. Amos Makalla, kak Gardol wa Reading, Da'Chemi Che-Mponda, Shamim Mwasha 'Zeze', Zubeir Masabo, Lau Shari wa Arise na juu ya yote mke wangu Ainde na Rais Jakaya Mrisho Kikwete (nashukuru sana mheshimiwa Rais kwa kunipa moyo wa kutembelea kwako blogu zetu mbalimbali kila siku, unatutia moyo sana kwa kweli).

Naomba pia niwashukuru wadhamini wakuu wa Globu ya Jamii wakiongozwa na Vodacom Tanzania, Tanzania Breweries Limited, CRDB, LUCUS, Hillview Family, TIB, Export Showroom, IOM ambao bila wao tusingekuwa hapa leo.

Mwisho na mwanzo ni MK Computer Tweaks ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kwamba tuna blogu zenye muonekano wa kimataifa, chini ya kaka Christopher Makwaia. Asante sana MK kwa yote uliyoifanyia Globu ya Jamii na unayoendelea kuifanyia. Mola akuzidishie!

HERI YA MWAKA MPYA MDAU POPOTE ULIPO

Muhidin Issa Michuzi

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 6 mpaka sasa

  1. Asante kwa salamu za mwaka mpya.Ankal michuzi umeongea kweli tupu inabidi watu wanaoanzisha blogu ambao si wanahabari basi BLOGU zao zijikite kwenye taaluma zao.

    Utakuta mtu anaanzisha blogu leo anapost habari then anakaa wiki 2 ndio anaposti habari nyingine.Halafu pia inaboa mtu ana blogu lakini kazi yake ni kukopi habari toka blogu tofauti ,mbaya zaidi ukifika blogu yake unakuta habari zote umeshazisoma.

    Ankal Michuzi inabidi nyie wana blogu ukitoa habari toka blogu yako lazima mwisho wa hiyo habari utaje source ya hiyo habari.

    Mwisho kabisa sikujua kuwa Ankal una mke!! hongera

    Mdau wa blogu

    ReplyDelete
  2. Michuzi

    Nafikiri unamaanisha Kilicho chema kwa bata wa kike, pia ni chema kwa bata wa kiume’ (what’s good for the goose, is good for the gander.)

    ReplyDelete
  3. Mdau wa MasakiJanuary 01, 2011

    Asante sana Braza Michuzi,

    Ninachukua nafasi hii kukutakia wewe pamoja na wapendwa wote wa familia yako Kheri na Baraka katika huu mwaka mpya wa 2011!

    Na Asante Sana kwa kazi yako nzuri kwenye masuala yote ya LIBENEKE!

    ReplyDelete
  4. kwanza hongera sana kaka michuzi kwa maana wengi tumejifunza kutoka kwako naamini mchango mkubwa sana ulioufanya katika jamii yetu na dunia nzima umeoonekana na unastahili pongezi kaka michuzi.Kwa mimi nimejifunza mengi sana kutoka kwako na kwa kaka yangu Haki Ngowi na nitaendelea kujifunza mengi sana kutoka kwenu kwa maana Bila wewe na Haki Ngowi Kaka Yangu wa Karibu Sana Nadhani nisingefika hapa msaada alionipa kaka Haki Ngowi na Niliyojifunza Kutoka Kwako Ni mchango tosha ambao hata mimi nisiposhukuru nitakuwa mkosefu wa fadhila.Mungu akubaliki na akuongezee katika kila utoacho.
    Na hongera Sana Kwa kuwa blogger namba moja kwa kuwa na wa2 zaidi ya milioni kumi sasa akifuatiwa nadhani na kaka yangu haki ngowi

    ReplyDelete
  5. Pat-magazetiJanuary 02, 2011

    Michuzi,
    Heri ya mwaka mpya. Kama nigekufananisha na mwedesha blog na nchi za ugaibuni kidogo una nikumbusha( David Plouff) kwenye Organizing for Obama 2006-2008. Lakini blog yako ni changamoto ya siasa, uchumi, michezo, na matokeo ya jamii. Sisi tuliopo nchi za magaharibi tunasoma blog hii Kama kupata update na matukio hapo Tanzania. Michuzi social media ni chombo muhimu sana kwa kuwasiliana na watu bila gharama kubwa. Kupunguza gharama za matangazo kwenye mawasiliano kwa umma wanaoishi mijini kwa nchi za kiafrika ususani Tanzania tujaribu kutumia social media kuwasiliana na umma.

    ReplyDelete
  6. Hongera Michuzi kila siku asubuhi kabla sijafanya kitu chochote huwa ni kuangalia hii blog what is the news hapa mjini nakupongeza sana mungu akutangulie

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...